Tuesday, April 2, 2013

KIJIJI CHA MISUKULE FEKI CHAFICHULIWA BAGAMOYOINATISHA na hofu kubwa imetanda katika Kijiji cha Kimange, Wilaya ya Bagamoyo  mkoani Pwani kufuatia baadhi ya viongozi  wa dini kuwatumia vijana wa hapo kama misukule ili wapelekwe kanisani.
Msukule.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa nia ya viongozi hao wa dini kuteua kijiji hicho na kuwatumia vijana wa hapo kama misukule ni kuwalaghai waumini kwamba wana uwezo wa kufufua watu wanaodaiwa kufa na kuchukuliwa kimazingara.
Gazeti hili limebaini kuwa viongozi hao wa dini wamekuwa wakifanya udanganyifu huo lengo lao likiwa ni kupata waumini wengi katika makanisa yao ambao wamekuwa wakiamini kwamba kweli misukule inarejeshwa katika maisha ya kawaida.
Habari kutoka kijijini hapo zinadai kwamba viongozi wa dini wanaofika katika kijiji hicho wamekuwa wakiwalipa watu wanaojitokeza kuwa misukule bandia kati ya shilingi 200,000  hadi 250,000  kwa kila mtu.
Msukule.
Imegundulika kuwa viongozi hao wa dini  hufanya zoezi hilo kwa siri kubwa na kuna  nyumba ya mchungaji mmoja, nje kidogo ya kijiji hicho ambapo misukule hao feki  hupewa mafunzo ya nini cha kufanya kabla ya kusafirishwa kuelekea Dar es Saalam.
Imeelezwa kuwa misukule husafirishwa kwenye magari yenye vioo vyeusi ‘tinted’ wakiwa wamepakwa matope mwili mzima  na kuvalishwa nguo zilizochanika.
“Wapo wachungaji waliofanya hivyo kwa kuwalaghai waumini wao kwamba wana uwezo wa kufufua watu huku wakijua kwamba lengo lao ni kuwavutia watu wajazane kwenye makanisa yao ili wapate  sadaka nyingi,” kilisema chanzo chetu.

 Uchunguzi  umebaini  kwamba  kuna makanisa  ambayo  yana wafuasi wengi wa kufanya mazingaombwe ya namna hiyo na wamekuwa wakijipatia fedha nyingi ambapo kwa Jumapili moja, hujikusanyia kati ya shilingi 7,000,000 hadi 7,500,000.
Aidha, ‘hukomba’ sadaka wakati wa maombi ya katikati ya wiki kwa kutumia mbinu mbalimbali za kuvuta waumini.
Baadhi ya vijana wa kijiji hicho ambao  waliwahi kurubuniwa na wachungaji baada ya kufuatwa kijijini hapo ni pamoja na Ziada Mlanga (33) na Shakila Ayubu (29).
Katika  mahojiano  na mwandishi wetu kijijini hapo, Ziada alikuwa na haya ya kusema:
“Machi 21, 2011 kaka mmoja (jina tunalihifadhi) anayeishi Kijiji cha Makore jirani na chetu, alinifuata na kunieleza kwamba anahitaji vijana wanne, wa kike  wawili na wa kiume wawili ili wajiunge katika shughuli za sanaa, yaani kuigiza.

“Hata hivyo, alifanikiwa kunipata mimi na Shakila, akatuahidi kutulipa shilingi 350,000 kila mmoja na wazazi wetu kupewa shilingi 100,000 kila mmoja.
“Tulikubali  kufanya hivyo, walituchukua kwa pikipiki hadi Kijiji cha Makore  nyumbani kwa mtu mmoja aliyemtaja kuwa ni mchungaji.

“Tulipofika huko walituweka katika chumba maalum katika nyumba ya huyo mchungaji  ambayo ipo porini, wakatueleza kwamba  tusubiri kuna watu wanakuja kutupa  mafunzo.
“Baada ya muda mfupi walifika watu ambao tulipoongea nao, walitueleza tuvue nguo zote tubaki na za ndani. Tulifanya hivyo, wakatupaka majivu, wakatuvuruga nywele  na kutuvalisha nguo chakavu na ilipofika saa moja usiku, walikuja watu wengine wakiwa kwenye gari yenye vioo vya tinted.
“Walitueleza kwamba tunaelekea jijini Dar es Salaam ambako tukifika tujifanye mazezeta. Tulifika usiku sana na kupelekwa katika kanisa moja (jina linahifadhiwa).

“Ndani ya gari lile kulikuwa na bastola, hatukujua ni ya nini, pale kanisani tulitengenezewa chai. Hata hivyo, tulikataa  kuinywa.
“Baadaye walitueleza kwamba wametufanya vile ili tuonekane kama watu  waliokuwa wamechukuliwa kimazingara na kufanywa misukule na sasa tumeokolewa na mchungaji wa kanisa hilo.
“Kesho yake ilikuwa Jumapili, tuliambiwa tutasimama mbele ya waumini kanisani na tusiseme kitu chochote ili tuje kuanza kuongea kidogo baada ya kuombewa na mchungaji.
 “Hata hivyo, tulipewa majina ya watu mashuhuri waliokufa lakini mimi nilikataa kwa kuwa aliyetajwa kuwa nijifanye ndiyo mimi alikuwa mtu maarufu.
 “Nilijiuliza ndugu zake wangenielewaje? Kitu cha pili ni kwamba nilikataa kwa kuwa fedha tulizokubaliana walikuwa hawajatupatia na tukaona kuwa huo ni udhalilishaji.

“Baada ya kuona tumekataa, walitusihi  tusitoe siri na baadaye tulipewa nguo  nyingine tukavaa na tukapewa shilingi elfu hamsini kila mmoja kama nauli ya kurudia kijijini kwetu Kimange.
“Tulipofika tuliwaeleza wazazi wetu  mambo tuliyofanyiwa wakaona tumedhalilishwa, ikabidi tuje nao Dar es Salaam  tukaenda hadi Kituo cha Polisi  Magomeni na kufungua  kesi.
  “Tuliwaambia polisi kuwa simu na nguo zetu ziko kwa watu hao lakini hadi leo kesi tuliyofungua hatujui ilipofikia na tuliambiwa polisi wamewasiliana na wenzao wa Mkoa wa Pwani.
“Polisi wa Pwani walikuja Dar na kutuchukua hadi Kibaha ambako tulitoa maelezo na tukaenda nao Kijiji cha Makore lakini  hatukumkuta mchungaji huyo, tukaambiwa kuwa alihama baada ya kupata habari kuwa anatafutwa na polisi,” alisema Ziada akiungwa mkono na Shakila.

BABA  WA  ZIADA
Baba wa Ziada aliyejitambulisha kwa jina la Sijali Musini Mlanga, alisema kwamba kitendo walichofanyiwa watoto hao ni cha udhalilishaji na anaiomba serikali kuchukua hatua.
“Hatuwezi kukubaliana na hali hiyo, huo ni utapeli na udhalilishaji mkubwa, hakuna dini  inayoweza kufanya mambo kama hayo, wahusika wachukuliwe hatua,” alisema Mlanga.

MWENYEKITI  WA  KIJIJI  
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimange, Juma Issa  Madinga amekiri kufahamu suala hilo na kukemea kitendo hicho.
“Hao wachungaji hawawezi kuachwa wakifanya mambo hayo na kusababisha kijiji kupakaziwa kuwa ni cha misukule, sasa wananchi wasilaghaiwe na matapeli hao, wakija tena watoe taarifa kwangu,” alisema  mwenyekiti huyo.

Chanzo: Uwazi (Global Publishers)

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget