Thursday, April 5, 2012

Kuomba & kukubaliwa DUA


Enyi Waja wa Allah, viumbe vyote vinamuhitaji Mola wao katika kupata manufaa yao au kuzuia madhara ya siwafikiye, kwa lengo la maisha yao hapa Duniani na kesho siku ya mwisho. 
Na kila mja anapo jikurubisha kwa Allah, basi Allah anamuinuwa daraja na kumfanya mtukufu mbele ya viumbe vyake. Mwenyezi Mungu (SW) Anawapa mitihani viumbe vyake kwa  misukosuko mbali mbali ili waweze kurudi kwa Mola wao na kuomba msaada kwake katika kupambana na mitihani hio. 
 Mwenyezi Mungu (SW) anapenda kuombwa msaada na waja wake. na anapenda waja wake kurudi kwake pindi wanapo fikiwa na shida na misukosuko ya ulimwengu. Kufanya hivyo, ndio msingi wa ibada. Na makusidio makubwa ya sharia kuamrisha  kunyeyekea kwa Allah na kutaraji pamoja na kumtegemea Yeye peke yake kwa mambo yote.Imepokewa na Abi Dharri  katika hadith Qudsi: [ Asema Mwenyezi Mungu: Enyi waja wangu nyinyi wote ni wapotevu ila Yule nilio muongoza, basi niombeni uongofu wangu].
 Mwenyezi Mungu (SW) Amepanga kila kitu, na Akaweka sababu ya kila kitu. Ameweka sababu za kufaulu Mwanadamu na sababu za kutofaulu Mwanadamu. Ameumba sababu zote na athari ya hizo sababu, na hakuna kitu kitakua bila ya kutaka Allah (SW). Na lau angetaka Mwenyezi Mungu (SW) kuumba kitu bila sababu angefanya. Amesema Mwenyezi Mungu (SW):
 {{ Mwingi wa kutenda Alipendalo}}. Na Amesema Mwenyezi Mungu (SW):
وقال تعالى: {أَلاَ لَهُ الْخَلْقُ وَالأمْرُ تَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ}
{{ Fahamuni, kuumba ni kwake tu Mwenyezi Mungu, na amri zote ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote}}.

Hukumu ya Kuamrishwa kuomba Dua
Dua ni ibada bora mbele ya Mwenyezi Mungu. Ameamrisha kwa lengo la lakupata kheri na kuzuia shari. Dua ni sababu kubwa ya kupata kheri na Baraka za Mwenyezi Mungu. Na ni sababu kubwa ya kukinga madhara na shari zote. Na hakika Mwenyezi Mungu ameamrisha waja wake kumuomba Dua katika Aya  nyingi.  Amesema Mwenyezi Mungu (SW):
قال الله تعالى: {وَقَالَ رَبُّكُمْ ادْعُونِى أَسْتَجِبْ لَكُمْ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِى سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ داخِرِينَ}
{{ Na Mola wenu anasema ; Niombeni nitakujibuni. Kwahakika wale wajivunao kufanya ibada yangu, bila shaka wataingia Jahannam wadhalilike }}.

Uhakika  wa kuomba Dua
-       Kutukuza mapenzi ya mja kwa mola wake katika kuomba msaada wakutatuliwa matatizo ya ulimwenguni na matatizo ya Akhera.
-       Kuhakikisha ukweli wa kumuabudu Mola wa walimwengu wote. Kufanya hivyo, ni kufungamanisha moyo wa mja na Mola wake na kumtakasia ibada zote  Mwenyezi Mungu (SW), na kutotegemea mtu au kitu kingine pamoja na  Mwenyezi Mungu (SW).
-       Kuwa na yakini kamili yakuwa Allah ndie Mweza wa kila kitu, hakuna kitu kinacho mshinda, Mjuzi wa kila kitu, hakuna kitu kilicho fichika mbele ya Allah (SW).
-       Kudhihirisha mja unyonge wake mbele ya Muumba wake. Na kumhitaji Mwenyezi Mungu (SW) katika mambo yake yote. Na hii ndio Ukweli wa kumuabudu Mwenyezi Mungu (SW).

Fadhila za Dua:
1.    Dua ni Ibada. Amesema Mtume (SAW) : [ Dua ni Ibada] (Abu-Daaud).  Dua ni bongo ya ibada, kwasababu Dua imekusanya ibada zote; kunyeyekea, kutegemea, kutarajia, kuogopa, kuomba msaada, n.k.
2.    Dua ni Ibada tukufu kushinda ibada zote.  Amesema Mtume (SAW) : [ Hakuna ibada tukufu mbele ya Allah kushinda Dua] (Atirmidhi).
3.    Kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu kwa ulinzi wake na hifadhi yake. Amesema Mtume (SAW) katika hadith Qudsi : [ Mola Asema: Mimi niko pamoja na mja wangu pindi anapo elekea kwangu kwa maombi yake] (Bukharin a Muslim).

Nyakati za kukubaliwa Dua.
  1. Wakati wa kusujudu. Amesema Mtume (SAW) : [ Mja anakuwa karibu zaidi na Mola wake wakati akiwa katika sijida. Kwahivyo, ombeni Dua wa wingi]  (Muslim).
  2. Baada ya Adhaana. Amesema Mtume (SAW) : [ Dua hairejeshwi baaina ya Adhaana na Iqaama] ( Attirmidhi).
  3. Thuluthi ya mwisho wa usiku. Amesema Mtume (SAW) : [ Mola wetu ateremka kila usiku mapaka katika uwingu wa dunia wakati wa thuluthu ya mwisho wa usiku. Na Anasema: Naani mwenye kuniomba ni mkubalie dua yake] ( Bukhari).
  4. Siku ya Ijuma. Amesema Mtume (SAW) : [ Katika siku ya Ijuma kuna Saa, atakaye omba Dua. Mwenyezi Mungu hukubali dua yake] (Bukharin a Muslim).

Ndugu Waislamu, kukubaliwa Dua na Allah ni lazima yapatikane masharti yake. Na Mtume (SAW) Ametufundisha masharti ya kimsingi ya  kukabiliwa Dua.


Masharti ya kukubaliwa Dua:-
  1. Kumtakasia Mwenyezi Mungu (SW) na kumpwekesha Allah katika kuomba Dua. Amesema Allah (SW) :
قال الله تعالى: (فادعوا الله مخلصين له الدين ولو كره الكافرون)
{{ Basi muombeni Mwenyezi Mungu yeye tu ibada yenu, ingawa makafiri watachukia }}.
  1. Kujiepusha na haramu; Kula, kunywa na kuvaa mavazi ya haramu. Amesema Mtume (SAW) : [ Enyi watu, hakika Mwnyezi Mungu ni nzuru, na hakubali ila kitu kizuri. Kisha akataja mfano wa mtu anaye safiri safari ndefu hali akiwa amechoka, nywele zake zimejaa vumbi, aiunuwa mikono yake kuelekeza mbinguni huku akisema: Ewe Mola wangu, Ewe Mola wangu, na hali kwamba chakula chake ni cha haramu, Kinywaji chake cha haramu na mavazi yake ni ya haramu. Vipi Allah ataikubali Dua yake].
  2. Kuhudhurisha moyo wakati wakuomba Dua, na kuwa na matarajio ya ukweli kwa Allah (SW).  Amesema Mtume (SAW): [ Muombeni Allah hali mkiwa na hakika ya kukubaliwa Dua yenu. Na mjuwe Allah hakubali Dua ya moyo ulioghafilika ] (Attirmidhy).

Adaabu za Kuomba Dua:
  1. Usafi wa mwili. Kwasababu Dua ni Ibada, na Ibada haikubaliki bila ya usafi
  2. Kuinua mikono juu wakati wa kuomba Dua. Amesema Mtume (SAW) : “ Hakika Mola wenu anasifa ya haaya na ukarimu. Anaona haaya kumrejesha  mja wake anapo inua mikono yake kumuomba Dua”
  3. Kuomba Dua zilizo thibiti katika Qur’an na Sunna ya Mtume (SAW).

Mwisho
Ndugu Waislamu, kwa hakika Dua ni silaha ya Muislamu. Muislamu anaweza kutumia silaha hii kwa ajili ya kupambana na adui yoyote, sawa katika binadamu au katika majini.  Vilivile, Dua ni kinga ya Muislamu, ikiwa Muislamu ataitumia kinga hio kujilinda nayo. Ndugu Waislamu, tusisahau masharti ya kukubaliwa dua zetu, ni muhimu sana. Bila ya kukamilisha masharti hayo dau zetu hazikubaliwi na Allah (SW). Tunamuomba Allaha Atukubalie dua zetu, na Atuepushe na haram. Atupe uwezo wakutafuta halali. Na Atujaliye mwisho mwema, tukatane nayeye hali Akiwa radhi na sisi.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget