Saturday, April 7, 2012

Qur’ani Tukufu, kitabu kisichoweza kupotoshwa


Qur’ani Tukufu ambacho ndicho kitabu kikamilifu zaidi na cha mwisho cha Mwenyezi Mungu kina kanuni na sheria zinazooana kikamilifu na maumbile halisi ya mwanadamu na kinadhamini saada na ufanisi wa kiumbe huyo.
Qur’ani Tukufu ni kitabu cha Mwenyezi Mungu kinachotoa jibu kwa mahitaji ya mwanadamu na kilicholindwa na opotoshaji wa aina yoyote, kwani Mwenyezu Mungu Muweza ameahidi na kudhamini kukilinda kitabu hicho kitakatifu. Anasema:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ
“Hakika sisi tumeteremsha Qur’ani na Sisi ndio tutakaoilinda.” (al Hujr: 9)
Qur’ani Tukufu ambacho ndicho kitabu kikamilifu zaidi na cha mwisho cha Mwenyezi Mungu kina kanuni na sheria zinazooana kikamilifu na maumbile halisi ya mwanadamu na kinadhamini saada na ufanisi wa kiumbe huyo. Qur’ani pia ndio marejeo ya milele ya dini tukufu ya Kiislamu.
Vitabu vya mitume waliotangulia vilikumbwa na upotoshaji na mabadiliko na haviwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu wa zama hizi kutokana na upotoshaji huo. Hivyo basi zama za sasa zinahitajia kitabu kinachoweza kukidhi mahitaji ya kimaumbile na ambacho hakijapotoshwa au kufanyiwa mabadiliko ya aina yoyote.
Suala la kutumwa mitume na kuteremshwa vitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu lilihitimishwa kwa kuteremshwa Qur’ani na kudhihiri dini ya mwisho ya Uislamu. Hapa kunajitokeza swali kwamba je, Qur’ani kama vilivyokuwa vitabu vingine vya Mwenyezi Mungu, imekumbwa na opotoshaji na mbadiliko yaliyofanywa na mkono wa mwanadamu katika maandiko mengine matakatifu ya Mwenyezi Mungu au la?
Sisi kama Waislamu tunaamini kwamba kitabu cha Qur’ani Tukufu ndicho kitabu pekee cha Mwenyezi Mungu kilicholindwa na upotoshaji huo wa mwanadamu na kwamba Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliyechukua jukumu la kukilinda kitabu hicho. Aya ya 9 ya Suratul Hijr inasema: “Hakika sisi tumeteremsha kitabu hiki na hakika Sisi ndio tutakaokilinda.” Vilevile tunaamini kwamba kitabu hiki cha Qur’ani kilichoko mikononi mwa Waislamu ndicho kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu (SW) kwa Mtume wake wa mwisho Muhammad (saw) na kimelindwa na kuhifadhiwa na opotoshaji wa aina yoyote katika kipindi chote cha historia, kinyume kabisa na vilivyo vitabu vingine vilivyotangulia.
Kwa msingi huo uhakika kwamba Qur’ani ni ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ndio kitabu pekee ambacho hakijapotoshwa au kukumbwa na mabadiliko unakiweka kitabu hicho katika nafasi ya juu katika maisha ya Waislamu na kukipa utukufu wa aina yake kikilinganishwa na vitabu vingine.
Tabibu wa Kifaransa Morris Bokay ameandika: “Qur’ani ni ufunuo uliokuwa ukiteremshwa na Malaika Jibrail kwa Muhammad (saw) na kuandikwa papo na hapo na waumini ambao pia walihifadhi moyoni maandiko yake na kuyasoma katika sala hususan katika mwezi wa Ramadhani." Anaendelea kuandika: "Kinyume na ilivyokuwa katika dini ya Kiislamu, wahyi na ufunuo katika dini ya Kikristo unategemea nukuu na ushahidi tofauti na usiokuwa wa moja kwa moja, kwani kinyume na Wakristo wengine wanavyodhani, hatuna ushahidi wowote kutoka kwa mtu aliyemuona Yesu unaothibitisha kwamba maandiko haya tuliyonayo ni ufunuo." (Tazama kitabu cha "Ulinganisho Baina ya Torati, Injili, Qur'ani na Sayansi)
Pamoja na hayo inasikitisha kwamba kuna watu miongoni mwa Waislamu wanaodai kuwa Qur'ani imepotoshwa na wanaamini kwamba baadhi ya sehemu za kitabu hicho kitakatifu zimepotoshwa na hata kufutwa.
Dhana hiyo batili inaweka wazi udharura na umuhimu wa kuchunguza madai hayo. Japokuwa madai hayo yasiyokuwa na msingi yametolewa na idadi ndogo mno ya Waislamu, lakini hii leo Waislamu wa madhehebu ya Shia ndio wanaopachikwa tuhuma ya kuwa na imani kwamba Qur'ani Tukufu imepotoshwa.
Allamah Sayyid Murtadha Askari mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kishia wa zama hizi amenukuu kutoka kwa mwanazuoni mmoja wa India akisema: "Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran pekee vitabu mia mbili vimechapishwa nchini India kwa lugha tofauti vikiwatuhumu Waislamu wa madhehebu ya Shia kuwa wanaamini kwamba Qur'ani Tukufu imepotoshwa."
Inasikitisha kwamba tuhuma na uzushi huo umeenea sana katika maeneo mbalimbali na maadui wa Uislamu wanatumia fursa hiyo kuchapisha Qur'ani mpya waliyoiita 'Furqanul Haq' na kuisambaza katika baadhi ya nchi za Kiislamu. Kwa msingi huo kuna udharura wa kuchunguza mitazamo ya wanazuoni wa Kiislamu kuhusu suala hilo na kuweka wazi ukweli wa mambo kwa walinganiaji wa kweli wa Uislamu na kufichua njama zinazopangwa na maadui wa dini hii.
Maana ya neno 'tahrif' au upotoshaji
Neno tahrif katika lugha ya Kiarabu lina maana ya kuelekea upande mmoja, kupinda na kubadili kitu. Kufanya tahrifu katika maneno ni kuyafasiri visivyo, kuyaeleza vibaya na kuyafasiri kinyume na yalivyo. Vilevile kufanyia neno 'tahrifu' kuna maana ya kulibadilisha na kuweka jingine mahala pake.
Kwa msingi huo, neno 'tahrif" katika lugha ya Kiarabu lina maana ya kubadilisha neno au kubadilisha maana yake. (tazama vitabu vya lugha kama Lisanul Arab na Mufradatu Alfadhil Qur'ani)
Katika istilahi, neno hilo pia lina maana ya kubadili na kuweka kitu mahala pa kingine. Wataalamu wanasema tahrif ni ya aina mbili, tahrifu au upotoshaji wa lafdhi na maneno na upotoshaji wa maana.
Upotoshaji wa maneno ni ule wa kubadili neno ima kwa kuweka neno jingine mahala pake au kwa kuzidisha neno au sentensi nyingine katika maeneno hayo au kuyapunguza.
Na tahrifu au upotoshaji wa maana ni ule unaotimia kwa kubadili maana ya maneno na kuficha baadhi ya maana zake.
Tahrifu na upotoshaji katika Qur'ani
Kufanya tahrifu au upotoshaji katika Qur'ani ni kubadili herufi, maneno au baadhi ya maana ya aya zake. (Mufradat Alfadhil Qur'ani)
Qur'ani Tukufu pia imezungumzia maana zote mbili za tahrifu na upotoshaji wa maneno na maana. Upotoshaji wa maana umetajwa katika Qur'ani kuwa ni kufasiri aya za kitabu hicho kwa kutumia rai binafsi au kuzifasiri aya za Qur'ani Tukufu kwa kutegemea dhuku na matashi ya mtu binafsi bila ya kutilia maanani vigezo na ufahamu wa watu kuhusu maana ya kilugha ya neno linalofasiriwa. Aya ya 46 ya Suratu Nisaa inasema: مِّنَ الَّذِينَ هَادُواْ يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ
"Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno kuyatoa mahala pake…" Kwa mujibu wa aya hii, Mayahudi baada ya kuelewa vyema maana ya maandishi ya Torati walikuwa wakibadili maana yake ya wazi. Kwa mfano walikuwa wakisema: "Sentensi hii haina maana ya Mtume wa mwisho bali ina maana ya Malaika Jibrail" au walikuwa wakibadilisha maneno kwa kuyaondoa sehemu moja na kuyaweka sehemu nyingine.
Marehemu Tabarsi anasema katika kufasiri aya iliyotangulia: "Maana yake ni kuwa katika Mayahudi wako wanaobadilisha maneno na kuyaondoa sehemu yake yaani huyabadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu na sheria zake”. Mujahid pia anasema: “Maana “al kalim” yaani neno lililotajwa katika aya hii ni Taurati, kwa maana kwamba Mayahudi walikuwa wakificha na kupotosha maneno ya Taurati yanayozungumzia sifa za Mtume Muhammad (saw).” Tazama Majmaul Bayan.
Kitendo cha Mayahudi cha kupotosha jina na sifa za Mtume Muhammad (saw) katika Taurati ni upotoshaji katika maana, na kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu kwa kuzidisha au kuyapunguza ni upotoshaji katika maneno.
Baadhi wanaamini kwamba Qur’ani Tukufu imeashiria tu suala la upotoshaji katika maana. (Tazama: Siyanatul Qur’ani min Attahrif-Muhammad Hadi Maarifat). Hata hivyo, kutokana na aya hii na aya nyinginezo za Qur’ani tunaweza kutambua kwamba Mayahudi mbali na kufanya upotoshaji wa maana ya Taurati, walikuwa pia wakifanya upotoshaji wa maneno yake kwa maana ya kuyabadilisha kwa kuzidisha au kupunguza maneno ndani ya kitabu hicho.
Aina za upotoshaji wa maneno kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu
Upotoshaji wa maneno unaweza kufanyika kwa sura mbalimbali. Hata hivyo sura zinazoweza kutia dosari maandiko ya Qur’ani Tukufu ni hizi zifuatazo:
1- Kupunguza au kuzidisha herufi na harakati za Qur’ani. Mfano wake ni kama kubadilisha “‌حم عسق” na kuweka "‌حم سق" mahala pake.
2- Kupunguza au kuzidisha katika maneno ya Qur’ani Tukufu. Mfano wake ni kuweka neno: " و الذكر والأنثي " mahala pa neno"‌ و ماخلق الذكر والأنثي "
3- Kupunguza au kuzidisha aya na sura za Qur’ani Tukufu kama kusema: "Maneno fulani yalikuwa miongoni mwa aya za Qur’ani lakini yalifutwa au kusema aya fulani si sehemu ya Qur’ani Tukufu, au kusema baadhi ya sura au sehemu ya Qur’ani iliyopo hivi sasa haikuwa katika Qur’ani, au kusema Qur’ani hii ya sasa si Qur’ani kamili iliyoteremshwa kwa Mtume Muhammad (saw).(Tazama Siyanatul Qur’an min Attahrif)
Uchunguzi wa upotoshaji:
1- Upotoshaji wa maana
Hapana shaka kwamba kumefanyika upotoshaji katika maana ya baadhi ya aya za Qur’ani, kwani mtu yeyote anayefasiri Qur’ani kwa rai kwa maana tuliyoeleza hapo kabla huwa amepotosha maana ya Qur’ani. Hadithi za Mtume Muhammad (saw) na Maimamu watoharifu katika kizazi chake pia zimekemea na kulaani vikali upotoshaji wa aina hiyo.
2- Upotoshaji katika lafudhi
Vilevile hapana shaka kwamba kumekuwepo upotoshaji katika lafudhi na jinsi ya kutamka aya na maneno ya Qur'ani kwa maana ya kupunguza au kuzidisha herufi au harakati za Qur'ani Tukufu wakati wa kusoma aya za kitabu hicho sambamba na kulinda muhtawa na asili ya maneno yake. Suala hili ndilo linalozusha visomo na kiraa tofauti za Qur'ani. (Tazama al Bayan fi Tafsiril Qur'ani-al Khui)
Tunaamini kwamba Qur'ani iliyoteremshwa kwa Nabii Muhammad (saw) ilikuwa ikisomwa kwa kiraa moja tu ambayo ni kiraa ya Hafs kutoka kwa A'sim na tunatambua kwamba kiraa hiyo ndiyo yenye itibari. Kwani kiraa ya Hafs inaoana na hadithi sahihi na A'sim alipokea kiraa hiyo kutoka kwa mwalimu wake Abu Abdul Rahman ambaye pia alipokea kiraa hiyo kutoka kwa Amirul Muuminin Imam Ali bin Abi Twalib (as). Mtukufu huyo pia alikuwa akishikamana na kiraa cha Qur'ani kilichokuwa maarufu baina ya Waislamu wote na kilichoafikiana na maandiko asili ya wahyi na ufunuo. (Tazama: al Tamhid- Ayatullah Maarifat)
3- Upotoshaji wa maneno kwa maana na kuzidisha neno katika Qur'ani
Hakuna Muislamu hata mmoja anayeamini kuwepo upotoshaji wa maneno ya Qur’ani kwa maana ya kuzidisha aya au sura katika kitabu hicho kitukufu.
4- Upotoshaji kwa maana ya kupunguzwa au kufutwa neno, aya au Sura
Upotoshaji wa aina hii ndio unaochunguzwa zaidi katika vitabu vingi vinavyojadili maudhui ya Qur’ani Tukufu. Katika sehemu hii ya makala yetu pia tutajaribu kutupia jicho zaidi kadhia hiyo.
Mitazamo ya wanazuoni kuhusu kulindwa Kitabu cha Qur’ani
Kama tulivyosema hapo awali wanazuoni karibu wote wa Shia na Suni wamepinga vikali madai ya kupotoshwa maandiko ya kitabu kitakatifu cha Qur’ani. Hata hivyo kwa kutilia maanani umuhimu wa mtazamo wa madhehebu ya Shia kuhusu kadhia hii na uzushi na tuhuma zisizokuwa na msingi zinazodai kwamba Mashia wanaamini kuwa Qur’ani Tukufu imepotoshwa, tutatosheka hapa kwa kunukuu mitazamo ya baadhi ya wanazuoni wakubwa wa madhehebu hiyo ya Kiislamu tukimuusia msomaji arejee kwenye vitabu vingi vilivyoandikwa kuhusu maudhui hii ili kutambua kwa kina mitazamo ya wanazuoni wengine wa Shia na Suni kuhusu madai ya kupotoshwa maandiko ya kitabu hicho kitukufu. (Tazama vitabu vya Siyanatul Qur’ani cha Ayatullah Maarifat, al Bayan cha Ayatullah Sayyid al Khui, Manabiul Ijtihad Ayatullah Jannati, Tafsiri ya Ruhul Maani, Tafsirul Kabir na Manahilul Irfan fi Ulumil Qur’ani na kadhalika.)
Mitazamo ya Wanazuoni wa Kishia:
1- Mwanazuoni mkubwa na mashuhuri wa Kishia Sheikh Mufid (RA) 336-413 Hijria. Anasema: "Watu wenye kutegemewa na waaminifu wanasema kuwa halikupunguzwa neno, aya wala sura yoyote katika Qur’ani Tukufu… (Tazama Awailul Maqalat)
2- Sharif Sayyid Radhi, Ali bin Hussein Alamul Huda (355-436) Hijria. Anasema: "Maarifa na imani yetu kuhusu usahihi na ukamilifu wa kitabu cha Qur’ani ni kama elimu na maarifa yetu kuhusu miji, matukio makubwa, vitabu mashuhuri na mashairi ya Waarabu wa kale yaliyobakia hadi sasa. Zilifanyika jitihada kubwa za kulinda kitabu hicho na kukieneza kwa sababu ndio muujiza wa Bwana Mtume (saw) na chanzo na marejeo ya elimu na maarifa ya sheria." (Tazama: al Madkhal fi al Tafsir, Ayatullah Fadhil Lankarani)
3- Faqihi mashuhuri Sheikh Saduq, Mwenyezi Mungu amrehemu, anasema: "Tunaamini kwamba Qur’ani iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu (SW) kwa Mtume wake ndiyo hii hii iliyoko mikononi mwa Waislamu, na mtu yeyote anayedai kwamba sisi tunaamini kuwa ni pungufu, huyo ni kidhabu."
4- Mwanazuoni mashuhri na mkubwa wa Kishia Sheikh Tusi (385-460) Hijria, ambaye ndiye muasisi wa chuo cha kidini cha Najaf nchini Iraq. Sheikh Tusi ni maarufu kwa jina la Sheikhul Twaifa kwa maana ya Shekhe wa madhehebu ya Shia. Anasema: "Madai kuhusu kuzidishwa maneno katika Qur’ani au kupunguzwa hayafai kabisa. Waislamu wote wamekubaliana kwamba madai hayo ni batili. Vilevile kauli sahihi katika madhehebu yetu ambayo imepasishwa pia na al Murtadha na inayodhihiri katika hadithi nyingi ni kwamba Qur'ani Tukufu haijapotoshwa hata kidogo. Hadithi zote zilizopokelewa na pande mbili za Shia na Suni zikidai kuwepo upungufu katika kitabu hicho kitukufu zimepokelewa kwa njia ya ahadi (hadithi iliyopokewa na mtu mmoja mmoja katika mnyororo wa wapokezi wake) na haifidishi elimu wala yaqini. Hadithi kama hizo zinapaswa kupuuzwa. (Tazama utangulizi wa tafsiri ya al Tibyan)
5- Allamah Tabarsi, mwanazuoni na mfasiri mashuhuri wa Kishia (470-548) Hijria. Anasema: “Waislamu wamekubaliana kwamba hakuna ziada ya aina yoyote katika kitabu hicho. Hata hivyo kuna baadhi ya watu katika Shia na Suni ambao wametoa madai ya kuwepo upungufu katika kitabu hicho lakini kauli sahihi katika madhehebu yetu ni kinyume kabisa na madai hayo…" Tazama Majmaul Bayan.
6- Mwanazuoni mashuhuri wa Kishia Mulla Muhsin Faidh Kashani (1007-1091 Hijria. Anasema: "Iwapo tutasema kwamba kumetokea upungufu au ziada katika Qur'ani basi hakutabakia kitu chochote cha kutegemewa katika kitabu hicho. Maandishi yake hayatakuwa hujja na hayatakuwa tena na faida kwetu bali amri inayotutaka kushikamana na kitabu kama hicho haitakuwa na faida wala maana." Kisha Mulla Kashani anaashiria aya inayosisitiza kwamba Mwenyezi (sw) ameahidi kukilinda kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwa kusema: "Baada ya kauli hiyo ya Mwenyezi Mungu inawezekana vipi kuwepo upungufu au ziada katika kitabu hicho?" (Tazama Tafsiri ya al Safi."
Allamah Sayyid Sharafuddin al Musawi (1290-1377) Hijriaa. Anasema: "Kauli ya kupotoshwa Qur'ani Tukufu imenasibishwa kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Ninajikinga kwa Mwenyezi Mungu na kauli hiyo na kujitenga na wale wote wanaotoa madai kama hayo dhidi ya Shia. Qur'ani Tukufu, ikijumuisha aya, maneno na herufi zake zote, imepokelewa kwa njia ya mutawatiri na maelfu ya watu kutoka kwa Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) na hashuku katika hilo isipokuwa mwendawazimu. Maimamu wote wa kizazi cha Mtume wameinasibisha Qur'ani hii tuliyonayo kwa babu yao Mtume wa Mwenyezi Mungu na hilo ni jambo lisilokuwa na shaka ndani yake. (Tazama kitabu cha Masail Jarullah)
Hoja zinazothibisha Qur'ani haikuposhwa
Japokuwa ushahidi madhubuti unaonyesha kwamba hakuna upotoshaji wa aina yoyote uliofanyika ndani ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani lakini ili kuweka wazi zaidi suala hilo tunaashiria baadhi ya hoja zinazothibitisha usahihi na ukamilifu wa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu.
Kuna ushahidi wa aina tatu za kiakili, kihistoria, hadithi na aya za Qur'ani Tukufu zinazothitisha ukweli huo.
Hoja za kiakili:
Moja ya hoja za kiakili zinazothibitisha ukweli huo ni udharura wa kuwepo mitume. Kwa maelezo zaidi ni kuwa lengo la kuumbwa mwanadamu ni kufikia saada na ufanisi wa milele. Katika uwanja huo japokuwa akili ya mwanadamu inamwongoza katika njia ya kudhamini na kufikia ufanisi lakini akili ya mwanadamu pekee haitoshi na kiumbe huyo hawezi kufikia ukamilifu wake wa mwisho mwenyewe bila ya msaada wa Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo hekima ya Mola Muumba imekidhi kwamba kuna udharura wa kutumwa mitume na manabii waliokuwa na vitabu vya kuwaongoza wanadamu katika njia ya ukamilifu. Mitume hao wanapaswa kuwa na kitabu kamili kisichokuwa na upungufu la sivyo lengo la kumfikisha mwanadamu katika ukamilifu halitatimia.
Kwa msingi huo iwapo marejeo na chanzo pekee cha mwongozo wa mwanadamu kuelekea katika ufanisi na ukamilifu kitakumbwa na upotoshaji na upungufu, wanadamu hawatakuwa na njia nyingine ya kuwafikisha kwenye ukamilifu wao wa mwisho. Hivyo kuna udharura wa kitabu cha mwisho na marejeo ya milele ya wahyi na ufunuo wa Mwenyezi Mungu yabakie salama na bila ya upungufu wa aina yoyote ili mwanadamu aweze kufikia ukamilifu wa milele. (Tazama kitabu cha al Madkhal fi al Tafsiri cha Ayatullah Lankarani)
Hoja za kihistoria
Katika mtazamo wa kihistoria Qur'ani Tukufu imekuwa na nafasi na sifa makhsusi ambazo haziwezi kuruhusu kufanyika upotoshaji wa aina yoyote ndani ya kitabu hicho kitukufu. Baadhi ya sifa hizo makhsusi ni hizi zifiatazo:
1- Qur'ani Tukufu iliteremshwa ikiwa katika daraja ya juu kabisa ya balagha na ufasaha kiasi kwamba Waarabu wa zama hizo ambao walivutiwa mno na fani ya fasihi na balagha walikuwa wakianisika mno na mananeo ya kitabu hicho na kufanya jitihada kubwa za kulinda maandiko yake.
2- Qur'ani Tukufu ndiyo marejeo na mhimili wa dini ya Kiislamu na suala hilo lilikuwa sababu tosha ya kuwafanya Waislamu wakilinde na kukitilia maanani kitabu hicho.
3- Mtume Muhammad (saw) aliweka mikakati madhubuti ya kukilinda na kukihifadhi kitabu hicho ikiwa ni pamoja na kutayarisha waandishi makhsusi wa Qur'ani, kuwapa umuhimu makari na mahafidhi wa kitabu hicho na kuainisha thawabu na malipo makubwa ya watu wanaosoma na kuhifadhi Qur'ani Tukufu.
4- Tangu zama za awali za Uislamu, Waislamu walilipa umuhimu mkubwa suala la kulindwa Qur'ani na kuliona kuwa jambo nyeti mno.
5- Ahlul Bait na Maimamu watukufu kutoka katika Nyumba ya Mtume (saw) waliwakosoa mno makhalifa na watawala walioshika hatamu za uongozi baada ya Mtume (saw) lakini hawakushuhudiwa wakizungumzia suala la kupotoshwa Qur'ani katika vipindi vya tawala hizo na daima walikuwa wakiwahimiza na kuwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani iliyokuwa mikononi mwao.
Mambo yote hayo yanaonyesha kwamba Qur'ani iliyokuwa miongoni mwa Waislamu ilikuwa ikipewa umuhimu na kuchungwa kwa makini kiasi kwamba lau kungetokea upotoshaji wa kupunguzwa au kuwepo ziada katika aya na sura zake basi jambo hilo lingefichuka na kuwekwa wazi mara moja.
Haditi:
1- Hadithi ya Thaqalain
Maana ya hadithi hii ni kwamba Mtume Muhammad (saw) aliwaambia Waislamu wote kwamba anawaachia vitu viwili vyenye thamani kubwa ambavyo ni Qur'ani na Ahlul Bait wake na kwamba iwapo Waislamu watashikamana navyo basi kamwe hawatapotea. Hadithi hii imepokelewa katika vitabu mashuhuri vya wanazuoni wa Kiislamu kama vile kitabu cha Musnad Ahmad bin Hanbal, Sunanul Darimi, Kanzul Ummal na Biharul Anwar. Kwa msingi huo iwapo Qur'ani imepotoshwa itawezekana vipi kushikamana nayo. Na itakuwaje kwa Mtume (saw) kuwaamuru Waislamu washikamane na kitabu ambacho kitakuja kupotoshwa baada yake?
2- Hadithi za Mtume na Maimamu katika kizazi chake zinazowaamuru Waislamu warejee kwenye Qur'ani wakati wa fitina na mkanganyiko wa mambo. Maimamu wa Ahlulbait (as) wamenukuu kutoka kwa babu yao Mtume Muhammad (saw) akisema: "Fitina zitakapowakanganya kama vipande vya usiku wenye giza totoro basi shikamaneni na Qur'ani, ni shifaa inayoponya na anayeiweka mbele yake humuongoza, na anayeiweka nyuma yake humsukuma kuelekea kwenye moto. Ni mwongozo wa njia ya kheri na kitabu kinachobainisha ….." (Tazama: Wasailu al Shia na Usulul Kafi)
3- Hadithi inayosema kwamba Qur'ani ndiyo mizani ya kuainisha haki na batili na njia ya shetani na ya Mwenyezi Mungu. Amirul Muumin Ali bin Abi Twalib (as) anasema katika hotuba ya 176 ya Nahjul Balagha kwamba: "Eleweni kwamba Qur'ani ni mshauri asiyedanganya, kiongozi asiyepoteza watu wake na msemaji asiyeongopa…. "
4- Hadithi zinazowahimiza Waislamu kutadabari na kutafakari kwa kina aya za Qur'ani.
5- Hadithi zilizopokelewa kutoka kwa kwa watu wa Nyumba ya Mtume zinazowaambia Waislamu kwamba Qur'ani iliyopo baina ya Waislamu ndiyo ile ile iliyoteremshwa kwa Mtume Muhammad (saw).
6- Hadithi zinazowafundisha Waislamu jinsi ya kufaidika na kitabu hicho.
7- Hadithi zinazowahimiza Waislamu kupima kila jambo na kulioanisha na aya za Qur'ani Tukufu.
8- Kupokelewa Qur'ani kwa njia mutawatir, kwa maana ya kupokelewa na idadi kubwa ya watu tangu zama za Bwana Mtume (saw) hadi sasa kiasi kwamba ni muhali kudhani kwamba kumefanyika udanganyifu au upotoshaji ndani yake.
Hadithi zote hizo na nyinginezo nyingi ambazo hatuwezi kuzitaja katika makala moja, zina ujumbe muhimu kwamba Qur'ani ndiyo marejeo ya uongofu na ukamilifu wa mwanadamu. Vilevile iwapo kungefanyika opotoshaji wa aina yoyote katika kitabu hicho basi Watu wa Nyumba ya Mtume na Ahlul Bait waliokuwa karibu nacho zaidi wangeashiria suala hilo.
Qur'ani:
a- Miongoni mwa aya zinazotumiwa kuthibitisha kwamba kitabu hicho hakikupotoshwa ni ile inayosema: اِنّا نَحْنُ نَزَّلنَا الذكْرَ وَ اِنّا لَهُ لَحَـفظون "Hakika Sisi tumeteremsha kitabu hiki na Sisi ndio tutakaokilinda." (Hijr:9)
Maana ya aya hii ni kwamba:
1- Mwenyezi Mungu ameahidi kukilinda kitabu kitukufu cha Qur'ani.
2- Maana ya الذكْرَ iliyotajwa katika aya hiyo ni Qur'ani Tukufu.
3- Maana ya kulindwa Qur'ani ni kulindwa kitabu hicho kisitoweke, kusahaulika au kupotoshwa kwa njia yoyote ile ya ama kuzidishwa au kupunguzwa.
b- Aya za 41 na 42 za Suratu Fussilat zinasema:
لا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلا مِنْ خَلْفِهِ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ · إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ
Kwa hakika wanaoyakataa mawaidha haya (Qur'ani) yanapowajia (wataangamia), na haya (Qur'ani) bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
Aya hizo zinamaanisha kwamba:
1- Qur'ani haiwezi kupotoshwa na kupatwa na batili si katika aya wala hata maneno yake. Kwa maana nyingine ni kuwa mikono ya wapotoshaji haiwezi kukifikia kitabu hicho.
2- Maneno "hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake," yana maana kwamba Qur'ani imelindwa kutoka pande zote na wala haiwezi kupotoshwa kwa kuongeza au kupunguza maneno, aya na sura zake.
Kwa jumla ni kuwa wanazuoni wote wa Kiislamu wa madhehebu za Shia na Suni wanaamini kwamba Qur'ani Tukufu haijapotoshwa kwa maana ya kuongezwa au kupunguzwa chochote katika kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Hata hivyo kumejitokeza baadhi ya watu wachache mno katika madhehebu zote mbili wakidai kwamba kulitokea upotoshaji ndani ya kitabu hicho suala ambalo limepingwa vikali na kuvunjwa kwa hoja madhubuti za maulamaa wa Kiislamu. Vilevile hadithi nyingi zinazodai kupotoshwa baadhi ya maandiko ya Qur'ani zimepokelewa kupitia mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Sayyari ambaye wataalamu wa hadithi wanasema kuwa alikuwa kidhabu na mtu aliyepotea.
Wakati huo huo mas'hafu ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) inayozungumziwa katika baadhi ya hadithi za Kiislamu haitofautiani na Qur'ani ya sasa isipokuwa tu kwamba mas'hafu hiyo ilikuwa na maelezo na tafsiri zaidi ya aya za kitabu kitukufu cha Qur'ani kandokando ya aya za kitabu hicho kama inavyoelezwa katika vitabu vya taaluma ya Qur'ani na tafsiri.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget