Wednesday, April 4, 2012

Uislamu dhidi ya usekula katika suala la ukombozi wa mwanamke


ULIMWENGU na hasa nchi za Magharibi hivi sasa uko katika kampeni kamambe ya "kumkomboa mwanamke". Imeanzishwa mitandano na vyama makhsusi kwa ajili hiyo. Lakini ipo dalili kuwa mwanamke chini ya mitandao hii atakombolewa? Na je, Uislamu unasema nini juu ya mwanamke? Katika mada iliyowasilishwa katika semina ya kitaifa ya wanawake wa Kiislamu iliyofanyika jijini hivi karibuni, Mhadhiri wa masuala ya Diplomasia Bi. Riziki Shehari ameandika kama ifuatavyo:
AMA kwa hakika mada hii muhimu sana kwa wakati huu. Ni mada ambayo imekuwa ikijadiliwa na inayoendelea kujadiliwa na watu mbalimbali duniani kwa mitazamo mbalimbali. Wanaongoza katika mjadala huu ni watu wa Magharibi (wanaojulikana pia kuwa nchi zilizoendelea) ambao siku zote wanamwonesha mwanamke wa Kiislamu kama kigezo cha mwanamke ambaye bado hajapata nuru ya ukombozi.
Kwa mtazamo wao mwanamke wa Kiislamu bado hadi leo hii anakandamizwa na "mfumo dume" unaofuatwa na Uislamu. Wanauliza kwanini leo hii Uislamu unawafanya wanawake "wabaki nyuma" na "wawe watumwa".
Mtazamo huu wa watu wa Magharibi juu ya suala hili ni potofu na wao wenyewe wanaelewa hivyo. Lakini agenda yao kuu ni kuikejeli dini ya Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo, ni jambo lenye kutia moyo kuona kwamba Waislamu wengi kote ulimwenguni wana elewa na mtazamo mpya juu ya dini yao. Waislamu wengi hivi sasa wamepambanukiwa na ukweli kwamba Uislamu ni dini isiyoishia Msikitini tu bali inafika pia maofisini, madarasani na hata nyumbani. Kwa hiyo Waislamu wanaelewa vile vile kuwa masuala yote yanayohusu maisha yao yote yanahusu siasa (utawala), elimu, biashara, mahusiano katika jamii (nafasi ya mwanamke Vs mwanaume, mke Vs mume, mtoto Vs mzaz, jirani Vs ndugu) na mengi mengineyo yanaelezwa katika Uislamu na kwamba wao wanawajibika kuona katika mtazamo huo.
Alhamdulillah, ni dhahiri kuwa kazi iliyofanywa na wanazuoni na waharakati wetu kwa kipindi kirefu imetoa matunda yenye kuonekana. Kuanziashwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ushirikishwaji na wanawake katika nchi hiyo (kuanzia uongozi wa nchi, taasisi za elimu ya juu, vyombo vya kutungia sheria (Bunge) na sehemu nyingine bila shaka yoyote kumetoa mwanga mpya kwa Waislamu duniani kote na changamoto yenye kuumiza bongo za "Wasekula".


Mwanamke katika historia mbalimbali
Historia inaonesha kuwa jamii nyingine duniani kwa wakati huo na hata sawa zimekuwa zikimdhalilisha mwanamke. Mwanamke siku zote alishesabika kuwa ni kiumbe duni, asiyestahili yoyote isipokuwa majukumu tu.
Mifano inatolewa na Warumi (Romans) ambao kwao mwanamke alikuwa mtumwa tu na sehemu hasa ya miliki ya mume. Historia ikaungana na Ukristo na Uyahudi na kuzaa neno la "Kistaarabu" la "Mrs....., asili yake ni hiyo kwamba mwanamke alikuwa sehemu ya mali ya mume. Wagiriki wao mwanamke alikuwa bidhaa kama bidhaa nyingine na hivyo aliweza kuuzwa na kununuliwa kulingana na matakwa ya mwanamume (baba, kama, mume).
Hata Ukristo ulimwangalia mwanamke kama kishawishi kibaya (Ibilisi) na kwamba ndiyo wa kulaumiwa kwa makosa aliyoyafanya Adam (a.s.). Siku hizi kuna issue ya gender sensitivity kwenye Biblia.
Huko India tunaelezwa kuwa Wahindi walimuona mwanamke kuwa ni kiumbe kibaya kisicho mfano. Mwanamke wa Kihindu ni mbaya kuliko kifo, mnyama au hata moto (jahanamu). Maisha ya mke hayakuwa na maana yoyote na yaliisha pale maisha ya mume yalipoisha. Mke ilibidi atoswe (ajitose) kwenye moto anaochomwa mumewe aliyekufa, yaani alitakiwa afanye "sati" siku hizi sheria za nchi zinakataza hilo lakini hata hivyo mwanamke unafuu alioupata ni mdogo sana. Hivi ni kwamba mwanamke anapofiwa na mumewe hesabiwa kuwa ni mkosi/balaa kubwa na hivyo haruhusiwi kuolewa tena; hana ruhusa kuonekana hadharani, kuvaa mapambo au nguo za rangi. Kutoonekana hadharani ni pamoja na kutoruhusiwa kuhudhuria harusi za watoto wake mwenyewe! Katika jamii ya Wahindu wanawake wananyimwa haki nyingi za kijamii na kiuchumi.
Kwa mfano, haruhusiwi kudai talaka hata kama anateswa kupindukia na mumewe, hana haki ya kumiliki au kurithi, na kwenye masuala ya ndoa ni wazazi wa mke ndio wanatakiwa walipe "mahari" kwa "mume" na ndoa mchanganyiko haziruhusiwi lazima wawe na caste moja wenye nyota zenye kuendana na za mume.
Huko Arabuni nako kipindi cha Jahiliya, mwanamke alionekana kuwa chanzo cha huzuni. Alipozaliwa mtoto wa kike basi alizikwa akiwa hai ili kuficha aibu na kuondoa huzuni ndani ya nyumba!
Huko Ulaya ambako sasa hunaonekana kuwa chimbuko la haki za wanawake pia hakuna historia nzuri kuhusu mtazamo wao kwa mwanamke. Tunaambiwa kuwa mnamo mwaka 587 A.D. ulifanyika mkutano huko Ufaransa wa kuchunguza hadhi ya mwanamke ili kuamua kama kweli mwanamke naye alistahili kuhesabika kama binadamu au la! Huko Uingereza Mfalme Henry VIII aliyetawala mwaka 1491 - 1509 alipiga marufuku wanawake kusoma Biblia na zama zote za kati (Middle ages C 5th - C15th) Kanisa Katoliki lilimhesabu mwanamke kuwa raia wa daraja la pili.
Wanawake wa Uingereza hawakuwa wakihesabiwa kama raia kabla ya 1850, hawakuwa na haki zozote mpaka mwaka 1882. Hata katika vyuo vikuu vya Cambridge na Oxford wanafunzi wa kike na wa kiume hawakuwa na haki sawa mpaka mwaka 1964. Hata harakati za Women's Lib zilizoanza mwishoni mwa karne ya 17 na kufuatana na mapinduzi ya viwanda mwishoni mwa karne ya 18 havikusaidia kumkomboa mwanamke wa magharibi. Kinyume chake vilizidi kumnyonya mwanamke na kumtoa kwenye asili na hifadhi yake (nyumbani) na kupelekwa viwandani ambako alitumika kama mfanyakazi wa kima cha chini na nguvu kazi ya bei poa (Cheap labour).


Uislamu umemleta nini mwanamke?
Baada ya kuangalia maelezo haya mafupi kuhusu maisha ya mwanamke katika jamii mbalimbali, tuangalie sasa maisha na hadhi ya mwanamke katika jamii ya Kiislamu.
Uislamu umekuja kama baraka kwa mwanamke. Ni mfumo ambo umekuja kumpa mwanamke anavyostahili kwa kuweka bayana tangu chanzo/asili yake, maisha yake ya dunia (haki, majukumu) hadi akhera yake (malipo/adhabu) baada ya kifo. Yote hayo yameweka wazi kuwa mwanamke hakubaguliwa kwa misingi ya mambo yake.
Qur'an inasema asili ya mwanamke na mwanamume ni moja kwa hiyo hakuna shetani na mwanadamu katika hili.
Allah (s.w.) anasema: "Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili) moja. Na akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake wengi kutoka katika wawili hao". 4:1.
Na 49:13: "Enyi watu! Kwa hakika nimekuumbeni nyote kutokana na yule mwanaume mmoja (Adam) na yule yule mwanamke mmoja (Hawa)..."
Wafanyaji mema, wanaume au wanawake, hali ya kuwa ni Waislamu, tutawahusisha maisha mema, na tutawapa ujira wao (akhera) mkubwa kabisa kwa sababu ya yale mema waliyokuwa wakiyatenda". 16:97.
Pia katika Qur'an 33:35 Allah (s.w.) anatuambia kuwa: "Bila shaka wanaume wenye kufuata vizuri nguzo za Uislamu, na wanawake wanaozifuata vizuri nguzo za Uislamu na wanaume wanaoamini vizuri nguzo za imani, na wanawake wanaoamini vizuri nguzo za imani, na wanaume wanaotii na wanawake wanaotii na wanaume wanaosema kweli na wanawake wanaosema kweli na wanaume wanaosubiri na wanawake wanaosubiri, na wanaume wanaonyenyekea, na wanawake wanaonyenyekea, wanaume wanaotoa (zaka na sadaka) na wanawake wanaotoa ý(zaka na sadaka) na wanaume wanaofunga na wanawake wanaofunga na wanaume wanaojihifadhi tupu zao na wanawake wanaojihifadhi tupu zao na wanaume wanaomtaja Mungu kwa wingi na wanawake wanaomtaja Mungu kwa wingi, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.
Hadith za Mtume (s.a.w.) zikaelekeza daraja ya juu ambayo mwanamke wa Kiislamu amepewa. Katika hadithi hizo mwanamke ni Malkia, malaika kheri tupu awe mama, mke au binti (mtoto wa kike).
Mtume amesema: "Pepo ziko chini ya miguu ya mama zenu".
Alipoulizwa siku moja: "Nani anstahali matunzo mazuri/shukrani kutoka kwangu. Mama yako, mama yako, mama yako, halafu baba yako, na baadaye ndugu zako wa karibu".
Hotuba ya kuaga (Arafa) 10 AH = C 7th: "Enyi watu, wake zenu wana haki juu yenu nyinyi mna haki juu yao. Wafanyieni wema na kuweni na huruma kwao, kwa sababu ni wenzi wenu na wasaidizi wenu".
Akasema pia: "Mbora zaidi miongoni mwenu ni yule aliye mwema zaidi kwa mkewe".
"Atakayejaaliwa watoto wa kike akawale/kuwatunza vyema hadi akawapa waume basi atafufuliwa bega kwa bega na mimi".
Uislamu ukaweka bayana haki za mwanamke katika Qur'an na Hadith. Haki ambazo mwanamke hakuzipata kabla ya Uislamu. Uislamu umempa mwanamke haki ya kupata elimu, kumiliki, kurithi na kuendesha shughuli zozote halali kumpatia kipato katika mipaka ya Allah, haki ya kuchangia/kutoa ridhaa kwa mume mtarajiwa, kudai talaka iwapo inabidi, kupewa mahari (zawadi yake toka kwa mume), kuolewa tena anapofiwa na mumewe, na mengi mengineyo.
Pamoja na haki hizo Uislamu pia ukabainisha kwa Qur'an na Sunnah majukumu ya mwanamke katika jamii ya Kiislamu, majukumu hayo yanayojumuisha kuwa mlezi wa familia/watoto, kumtii mumewe, kuwa chanzo cha utulivu katika nyumba na jamii, kujihifadhi na kutunza mali ya mumewe anapokuwa hayupo na kadhalika.


Tatizo la nini basi?
Tatizo tulilonalo ni kuwa tunazungumzia moja katika mitazamo miwili tofauti na pia inayopingana. Wakati Uislamu ni mfumo wa maisha ambao unamweka Muumba na mfumo aliouletea juu ya kila jambo kwa mfano kuendesha maisha yote, usekula (secularism) ni kinyume chake usekula kwa kifupi makamusi mbalimbali yameuelezea kama "kipinga dini" Usekula unapinga Mwenyezi Mungu au dini kuwa ndio usukani wa kila jambo. Tatizo linaloongezeka pale upande mmoja (kwa kuwa na nguvu za Ibilisi) umetumia mbinu mbalimbali kuudhalilisha mwingine. Usekula ambao ni fikra za Kimagharibi siku zote umechukulia Uislamu kuwa ni adui mkubwa na hivyo katika wote (hata hizo za Roman Empire/Chatholic Church) lakini katika sura tofauti tofauti.
Kama historia iliyoonesha huko Magharibi kabla ya karne ya 17 hapakuwa na kitu kama haki za binadamu na hivyo za mwanamke. Ukweli ni kuwa ni wasomi wa Kiislamu ndio walioanzisha suala la haki za binadamu na kuliweka wazi kama suala la asili/maumbile (natural) na siyo mikataba tu (conversations), lakini vurugu zilizotokea karne ya 8 za kuingiliwa na wazungu kulivuruga kabisa kazi za wasomi hao wa Kiislamu.
Muda wote huo mwanamke wa huko Magharibi hakuruhusiwa kuwa na haki ya kumiliki mali kwa sababu alichukuliwa kama mtoto mdogo au mwendawazimu. Kwa ujumla, mpaka ilipofikia karne ya 19 bado ilikuwa nadra kwa mwanamke kuwa na haki ambazo mwanamume angepeswa kuzitii kisheria.
Swala la uhuru, usawa, ukombozi wa mwanamke ulikuja na mapinduzi ya viwanda ambayo yaliwatumia wanawake kama wafanyakazi wa malipo hafifu lakini waaminifu (sio waasi/rebellious) Karne ya 20 alipokuja masuala yakapamba moto na 1948 kukawa na Universal Declaration of HRs (Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu). Katika tamko hilo masuala yaliyotawala yakawa ni "huru" na "usawa".
Mambo hayo yalichukuliwa kuwa yanatosheleza harakati za haki za binadamu/ wanawake. Tatizo likawa matumizi potofu na ambayo ndiyo tunaendelea nayo hadi hivi sasa ambapo uhuru/ukombozi wa wanawake na wanaume. Harakati hizi zimeshindwa kuangalia masuala ya msingi kama ya kibaiologia pamoja na haki na majukumu ya watu tofauti (mke/mume) katika familia. Kupuuzwa kwa masuala haya muhimu ndiko kulikoleta balaa zaidi badala ya nafuu siyo tu kwa wanawake bali kwa jamii nzima.
Mwanamke ambaye kwa asili ni kiumbe mwenye huruma na kujali wngine akafanywa mbinafsi mwenye kujiangalia yeye tu. Mtu wa haya kwa asili na mwenye kupenda kujisitiri akavuliwa haya na kumfanya ajifaharishe kwenda uchi au kinyume cha maumbile yake.
Masuala ya maumbile kwa mfano kikomo cha uzito ambao mwanamke aliruhusiwa kuinua lilipunguzwa kabisa ikiwa ni pamoja na mahitaji na uwezo wa mwanamke. Yote ni "ukombozi" ulioleta "uhuru na usawa".
Uislamu unamtazama mwanamke kwa jicho tofauti kabisa. Hakuna kufanana kwa mwanamke na mwanaume ni kama falsafa ipatikanayo katika aya ya 40 ya suratul Yasin:
"Haliwi jua kufikia mwezi (wakati wa nguvu zake) wala usiku kuupita mchana (ukaja ghafla kabla ya wakati wake). Na vyote vinaogelea katika njia (zao). 3:40.
Mwanamke na mwanamume katika Uislamu ni nyota katika mizunguko tofauti (Orbit) wako sawa katika uwezo wao binafsi lakini hawafanani. Kwa hiyo basi waendelee na harakati zao katika mizunguko yao. Qur'an imesimamisha haki za wanawake zaid ya miaka 1400 iliyopita kabla hata magharibi hawajawa chochote kuhusu haki. Yaliyokuwepo katika zama za Jahiliya yalibadilika alipodhihiri Mtume (s.a.w.) na Uislamu. Mwanamke akarudishiwa hadhi yake na akawa mwanzo na nuru baada ya giza nene na kuleta matumaini kwa mwanamke kuwa ni wenye asili moja (4:1). Hakuna dalili yoyote katika Qur'an inayoashiria uduni wa umbile la mwanamke, tofauti na Biblia. Arafa (7:19-22) Adamu na Hawa wanaonekana sawa katika kosa.
Waislamu kwa ujumla wao na hususan viongozi wa wanawake wa Kiislamu kama ninyi mna jukumu kubwa mbele yenu la kuonesha na kupambana na haki na batili.
Tulipofikishwa na usekula ni pale ambapo wanawake wamevaa hijab, wasiozurura ovyo vilabuni, wasiozini ovyo (free - sex) na kadhalika wanahesabika kuwa watumwa, washamba na wasioendelea. Wanawake wa magharibi na wenye mtazamo kama wao ambao tabia zao hazitofautiani na malaya kwa mfano wanavaa ovyo, wanatembea uchi (urembo/modals) wanachanganyika na wanaume bila mipaka hao ndio wasasa, wamejikomboa na wana maendeleo (progressive).
Tunaendelea kuulizwa kwanini Uislamu unawafanya wanawake wabaki na wawe watumwa? Basi tuwaambie: "Uulizeni kwani nini Uislamu unamlinda mwanamke, unafanya heshima, stara na uhuru wa kweli? Huu ndio Uislamu.
Uhuru na ukombozi wa mwanamke katika Uislamu hauna maana ya kuleta zile mila za kihahiliya ambazo amekuja kuziondoa.
Uislamu umekwishampa mwanamke hadhi anayostahili na ukombozi wa kweli kutokana na kukandamizwa na kutumiwa kama chombo cha starehe na kitega uchumi cha wanaume. Na tuwaoneshe Ulaya na Amerika ambako mwanamke anadhalilishwa kwa kuuzwa/kujiuza mwili wake ili apate pesa. Iwe katika filamu, matangazo ya biashara, modelling na starehe. Nguvu hii imefika huku kwetu ambako tunao akina "mama hao" "Chroroquine" na kadhalika na ma Miss Tanzania/Aspen.
Dada zangu katika Uislamu, kazi kubwa na ngumu bado iko mbele yetu. Vurugu lililopo hivi lnawagusa/linawakumba hata ndugu zetu wa karibu. Ni juu yetu kutumia uwezo wetu tulionao kulikemea hilo. Tuondoe uovu uliopo katika jamii yetu kwa mikono yetu, ndimi zetu au hata chuki zetu. Tuufikishe ujumbe aliouacha Mtume (s.a.w.) kila tunapopata wasaa wa afya.
Mwisho wa yote nawausia pamoja na kuusia nafsi yangu kumcha Mwenyezi Mungu. Turejee kwa Allah (s.w.) ili tupate mwongozo, ulinzi na mafanikio. 


Kutoka An-Nuur

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget