Saturday, April 21, 2012

Ukweli wa Pasaka

Pasaka ni mnyama anayechinjwa kukumbuka kukombolewa Waisraeli Misri, siyo 'kufa' kwa Yesu


KINYUME na ukweli wa mambo, hivi sasa sikukuu ya Pasaka imegeuzwa na Wakristo duniani kuwa ni siku ya kukumbuka "kufa na kufufuka kwa Nabii ama Yesu (a.s.)". Ambapo tangu kuasisiwa kwa dini ya Kikristo miaka michache baada ya Yesu (a.s.) kuondoka, dhana hii (ya kufa na kufufuka) imefanywa na Wakristo kuwa nguzo kubwa na ya msingi wanayoitegemea kusimamisha Ukristo. Fuatana nami ili uweze kuangalia kwa undani ukweli wa sikukuu hii (ya Pasaka) na dhana nzima ya kufa na kufufuka kwa Bwana Yesu (a.s.).


Ukweli wa Pasaka kama alivyofundisha Mungu
Kwa mujibu wa mafundisho ya Biblia, Pasaka ni mnyama ambaye wana wa Israeli waliamrishwa na Mungu wamchinje na wamle kwa kufuata utaratibu aliouelekeza Mungu na kwa lengo maalum. Maandiko yafuatayo yanathibitisha ukweli huu:
"Hapo ndipo Musa aliwaita wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana kondoo kama jamaa zenu zilivyo, mkamchinje Pasaka". (Kutoka 12:21),
"Nawe umchinjie Pasaka BWANA, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng'ombe, mahali atakapochagua BWANA apakalishe jina lake". (Kumbukumbu la Torati 16:2),
"Usimchinje Pasaka ndani ya malango yako yote akupayo BWANA, Mungu wako, ila mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja Pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri". (Kumbukumbu la Torati 16:5-6).
Kulingana na maandiko hayo juu, tunaona hapa Biblia inafundisha wazi kuwa Pasaka ni kondoo au ng'ombe ambaye Mungu aliwaamuru wana wa Israeli wamchinje kisha wamle. Aidha, maandiko hayo yanaonyesha wazi pia kuwa amri hiyo (ya kuchinja na kumla Pasaka) haikuwahusu watu wa mataifa mengine isipokuwa Waisraeli peke yao.


Utaratibu aliouweka Mungu wa kumla Pasaka
Pamoja na wana wa Israeli kuamriwa na Mungu kumchinja Pasaka, Mungu pia aliwawekea utaratibu (sheria) wa kumla (Pasaka) kama tunavyosoma katika maandiko yafuatayo:
"BWANA akamwambia Musa na Haruni, Amri ya Pasaka ni hii; mtu mgeni asimle; lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha, ukiisha kumtahiri, ndipo hapo atamla Pasaka. Akaaye kwenu hali ya ugeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle Pasaka. Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yoyote; wala msivunje mfupa wake uwao wote. Na wafanye jambo hili mkutano wa Israeli wote. Na mgeni atakapoketi pamoja nawe, na kupenda kumfanyia BWANA Pasaka, waume wake wote na watahiriwe, ndipo hapo akaribie na kufanya Pasaka, naye atakuwa mfano mmoja na mtu aliyezaliwa katika nchi; lakini mtu yeyote asiyetahiriwa asimle. Sheria ni hiyo moja kwa mtu aliyezaliwa kwenu, na kwa mgeni akaaye kati yenu ugenini. Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli wote; kama BWANA alivyowaagiza Musa na Haruni; ndivyo walivyofanya". (Kutoka 12:43-50)
"BWANA akanena na Musa, akamwambia, mtu wa kwenu, au vizazi vyenu, yeyote atakayekuwa na unajisi kwa ajili ya maiti, au akiwako mbali katika safari, na haya yote, ataishika Pasaka kwa BWANA; mwezi wa pili, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, wataishika watamla pamoja na mikate isiyotiwa chachu na mboga za uchungu; wasisaze kitu chake chochote hata asubuhi, wala wasimvunje mfupa wake, kama hiyo sheria yote ya Pasaka ilivyo ndivyo watakavyoishika. Lakini mtu aliyesafi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika Pasaka, mtu huyo atakataliwa mbali na watu wake; kwa sababu hakumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake. Na kama mgeni akiketi kati yenu ugenini, naye ataka kuishika Pasaka kwa BWANA; kama hiyo sheria ya Pasaka ilivyo, na kama amri yake ilivyo, ndivyo atakavyofanya; mtakuwa na sheria moja, kwa huyo aliye mgeni, na kwa huyo aliyezaliwa katika nchi". (Hisabu 9:9-14).
Kwa kifupi, kama maandiko hayo yanavyoeleza, huo ndio ulikuwa utaratibu wa kumla Pasaka, ambao Mungu aliwawekea wana wa Israeli. Aidha, maandiko hayo nayo pia bado yanatuonyesha kuwa Pasaka ni mnyama ambaye Mungu aliwaamuru wana wa Israeli (peke yao) wamchinje kisha wamle.


Siku na muda aliouweka Mungu wa kuchinja na kumla Pasaka
Pamoja na Mungu kuwatajia wana wa Israeli watu wanaoruhusiwa kumla Pasaka (kama tulivyoona katika maandiko yaliyotangulia), Mungu pia aliwapangia siku na muda maalum wa kuchinja na kumla Pasaka, kama maandiko yafuatayo yanavyoeleza:
"Kisha BWANA akanena na Musa katika bara la Sinai, mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya kutoka kwao katika nchi ya Misri, akamwambia, Tena wana wa Israeli na washike sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa. Siku ya kumi na nne kwa mwezi huu, wakati wa jioni, mtaishika kwa wakati wake ulioagizwa; kwa amri zake zote, na kama hukumu zake zote zilivyo, ndivyo mtakavyoishika. Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli kwamba waishike sikukuu ya Pasaka. Nao wakaishika Pasaka katika mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, katika bara ya Sinai, vile vile kama haya yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli". (Hesabu 9:1-5)
"Tena, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, ni Pasaka ya BWANA". (Hesabu 28:16)
"Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni Pasaka ya BWANA". (Mambo ya Walawi 23:5)
"Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo na mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchnija jioni". (Kutoka 12:5-6)
Kulingana na maandiko hayo juu, tunaona kwamba siku ya Pasaka ambayo Mungu aliwapangia wana wa Israeli kuishika ilikuwa ni kila ifikapo tarehe 14 mwezi wa kwanza wa mwaka wa kutoka kwao nchini Misri. Aidha, kama maandiko mengine ya Biblia yanavyofundisha (tazama Kumbukumbu la Torati 16:1) mwezi huo uliitwa "mwezi wa Abibu" ambao ulianza kuhesabiwa kabla hata Nabii Issa au Yesu (a.s.) hajazaliwa (B.C.). Ni wazi kuwa shuhuda hiyo peke yake inadhihirisha kuwa Pasaka kuwekwa tarehe 2 mwezi wa nne wa mwaka wa kuzaliwa Yesu (A.D.) kama wanavyofanya Wakristo leo, kwa kweli hiyo si katika mafundisho sahihi ya Mungu, bali ni uzushi mtupu uliobuniwa na wanaadamu!


Lengo sahihi la Mungu kuweka sikukuu ya Pasaka
Sambamba na Mungu kuwawekea wana wa Israeli utaratibu maalum wa jinsi ya kutekeleza amri yake ya kuchinja na kumla Pasaka, vile vile Mungu hakuacha kubainisha lengo hasa la kutoa amri hiyo kwa wana wa Israeli, kama maandiko yafuatayo yanavyobainisha hapa chini:
"Utunze mwezi wa Abibu, ukamfanyie Pasaka BWANA, Mungu wako, kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa Abibu alipokutoa Misri usiku BWANA; Mungu wako, Nawe umchinjie Pasaka BWANA, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng'ombe, mahali atakapochagua BWANA apakalishe jina lake. Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu; siku saba utakula naye mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso; kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka; ili upate kukumbuka siku uliyotoka nchi ya Misri, siku zote za maisha yako". (Kumbukumbu la Torati 16:1-3).
Kufuatana na maandiko hayo juu, tunaona kuwa lengo la Mungu kuwawekea wana wa Israeli sikukuu hiyo ya Pasaka, ilikuwa ni kwa ajili ya kukumbuka siku aliyowakomboa kuwatoa nchini Misri chini ya utawala ya Farao (Firauni). Ambapo maandiko ya Biblia yamearifu kuwa wana wa Israeli walikaa nchini Misri katika hali ya utumwa kwa muda usiopungua miaka 430 (tazama Kutoka 12:40-42)).
Aidha, maandiko hayo yanaonyesha lengo lingine la Mungu kuwawekea wana wa Israeli sikukuu hiyo (Pasaka) ilikuwa kama desturi yake kujenga uhusiano mzuri baina yake na wanaadamu endapo watatii amri zake.


Na Muhibu Said

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget