JE, ni kweli kuna aina mbili za sikukuu ya Iddi El-Fitri nchini? Kama hazipo mbona waumini wanaanza kuzozana?
Aina ya kwanza inatajwa kuwa ile inayotambuliwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, ya pili ni ile inayotajwa na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA).
Ndivyo ilivyokuwa kwenye sikukuu ya Iddi El-Fitri, Jumatano 31 Agosti 2011.
Bakwata lilitangaza tarehe 29 Agosti 2011, sawa na mfunguo Mosi mwaka 1432; hivyo kutokuwapo kwa taarifa za muandamo wa mwezi wa kuhitimisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Bakwata ilitangazia ulimwengu kuwa swala ya Iddi El-Fitri itafanywa Jumatano, 31 Agosti 2011 kwa kile ilichoita, “Kushindwa kuonekana mwandamo wa kumalizika mwezi wa Ramadhani siku ya Jumatatu.”
Hata hivyo, taarifa za muandamo wa mwezi zilipatikana nchini Jumatatu 29 Agosti 2011. Redio Imani, inayomilikiwa na moja ya taasisi za kiislamu nchini ilitangaza kuonekana muandamo wa mwezi katika shule ya sekondari Kibiti, wilayani Rufiji, mkoani Pwani. Mwezi ulionekana pia nchini Uganda.
Radio hiyo iliwanukuu wanafunzi 10 wa Kiislamu wa shule hiyo, pamoja na Mwalimu wao wa somo la Sayansi ya Kompyuta, Hussein Njali.
Ilikuwa hivi: Katika mahojiano yake na gazeti hili, Mwalimu Njali anasema, “Nikiwa nyumbani kwangu majira ya saa 2.30 usiku, baadhi ya wanafunzi walifika na kunieleza kuwa wameuona mwezi mwandamo bila mashaka yoyote.
Anasema, “Sikumeza taarifa hizo nzimanzima; badala yake nilitaka wanafunzi wale niwaapishe kama mafundisho ya Kiislamu yanavyotaka.”
Anasema, “Wanafunzi hao hawakusita. Wote 10 waliapa mbele yangu kuthibitisha ukweli wa taarifa za kuuona mwezi.”
“Baada ya kujiridhisha na taarifa za wanafunzi hao, nilimpigia simu Sheikh wa Jimbo la Kibiti, Mustapha Doga, kumwarifu kuhusu kuonekana kwa mwezi pamoja na kiapo walichokula wanafunzi kuthibitisha taarifa hizo.”
Anasema baada ya kumueleza Sheikh Doga, naye alizikubali taarifa hizo na kuahidi kuijulisha kamati ya mwezi jijini Dar es Salaam.
Maelezo ya Mwalimu Njali yameungwa mkono na Sheikh Doga. Katika mahoajino na MwanaHALISI mwishoni mwa wiki, Sheikh Doga anasema, “Ni kweli nilipokea taarifa za mwandamo wa mwezi kutoka kwa Mwalimu Njau, baadaye niliwasilisha taarifa hizo Bakwata.”
Anamtaja Sheikh wa Bakwata mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Musa Salum Mahambe kuwa ndiye alimpa taarifa hizo.
Anasema mara baada ya kujulisha muandamo wa mwezi wa kuhitimisha mfungo wa Ramadhani, Sheikh Mahambe alimueleza, “Tayari tumefunga milango ya kupokea taarifa za kuandama kwa mwezi.”
Naye Amiri (kiongozi) wa wanafunzi wa Kiislamu shuleni hapo, Mohamed Adamu. Anasema mwezi ulionekana na kwamba “Taarifa zilizotangazwa na redio Imani kuhusu sisi kuuona mwezi, ni sahihi na zilitosha.”
Tarehe 29 Julai 2011, Sheikh Mahambe alilitangazia taifa, kwamba taarifa zozote za kuandama kwa mwezi, zingetolewa na Ofisi ya Mufti wa Tanzania na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar na si kwingineko. Alisisitiza, “Hiyo ndiyo nidhamu ya Uislamu.”
Sheikh Mahambe ndiye aliyeibukia televisheni ya taifa (TBC), majira ya saa nne usiku, kukanusha taarifa ya muandamo wa mwezi.
Alisema, “Waislamu wanatakiwa wakamilishe siku ya thelathini ya Ramadhani na kwamba mwezi haujaonekana.”
Sheikh huyo aliituhumu radio Imani kutangaza mwandamo wa mwezi. Akasema, “Mwenye mamlaka ya kutangaza mwezi ni Mufti, Sheikh Simba Shaban Simba, na wala siyo redio Imani na kwamba redio hiyo inawapotosha watu kwa kuwatangazia kuwa mwezi umeonekana.”
Sheikh Mahambe, ni mmoja wa wajumbe wa kamati ya mwezi chini ya Ofisi ya Mufti wa Tanzania na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar. Haya ndiyo Bakwata ilitenda.
Shekh aliyepewa dhamana na Kamati Kuu ya wanazuoni ya Bakwata kuwatangazia mwezi waislamu; ambayo ni ibada tukufu ya Iddi El-Fitri, ametenda kinyume na mafundisho yaliyo wazi na yasiyo ikhitilafu kwa wanachuoni wote.
Mwanazuoni Amir Said Amir aliyepata elimu ya dini ya Kiislamu nchini Libya kwa miaka saba anasema, sharia ya kiislamu juu ya mwandamo wa mwezi wa kuingia Mfungo Mosi inaeleza wazi, kwamba mwezi mwandamo utapoonekana na watu wawili au zaidi ambao ni waislamu, basi ni lazima waumini kufungulia wakati wowote watapopata taarifa.
Anasema, sharia ya Kiislamu inasema, “Ni haramu kufunga siku ya Eid, iwe ya Iddi El-Fitri au Iddi Alhajj, na kwa mujibu wa sharia ya kiislamu, mara waumini wanapopata taarifa ya kuandama kwa mwezi, hata kama taarifa hiyo imepatikana jioni, basi sharti wafungue.
Anataja Hadithi (Sunanu ibn Maajah, Juzuu ya Pili, chapa ya Daarul Fikri Beirut, Hadithi Na. 1653 iliyosahihishwa na gwiji la hadithi, Imam Albany, kwamba maswahaba walishindwa kuuona mwezi kwa sababu ya kutanda kwa mawingu. Wakakamilisha kufunga siku ya thelathini.
Anasema, “Lakini baada ya kufika muda wa Alasiri ukaja msafara wa watu, wakatoa ushahidi kwa mtume (S.AW), kwamba wao jana wameuona mwezi mwandamo. Haraka mtume akaamrisha maswahaba wafungulie wakati uleule, na kwakuwa swala ya Idd El-Fitri inaswaliwa kabla ya Adhuhuri, basi akaagiza kesho yake waswali Iddi El-Fitri," anaeleza.
Anahoji, “Kama haya ndiyo mafundisho ya mtume, Alhaji Mahambe amepata wapi mamlaka ya kufunga habari za mwezi saa nne usiku? Ametoa wapi mafunzo haya? Je, yeye ni bora kuliko Mtume Mohammad S.A.W?”
Anasema kutoka Dar es Salaam mpaka Kibiti ni kilometa zisizozidi 80. Hivyo kama hakuamini waliotoa ushuhuda wa mwezi,” alipaswa kufunga safari kwenda kuonana na wahusika.
Anasema kutoka Dar es Salaam mpaka Kibiti ni kilometa zisizozidi 80. Hivyo kama hakuamini waliotoa ushuhuda wa mwezi,” alipaswa kufunga safari kwenda kuonana na wahusika.
Akiongea kwa taratibu, Amir anasema, hata hicho anachoita Sheikh Mahambe, “Mwenye mamlaka ya kutangaza mwandamo wa mwezi, ni Mufti mkuu wa Bakwata, si kweli.”
Anasema sharia ya kiislam, haimpi mamlaka Mufti ya kulazimisha Fatwa yake ifuatwe na waumini kwa lazima, pale ambapo kuna kauli nyingine ya kisheria inayoweza kufuatwa.
Anasema kutangaza kuwa Mufti ndiye mwenye mamlaka pekee ya kutangaza mwezi, ni kuipotosha jamii.
Anauliza, “Kwanza, ni nani aliyemchagua Mufti Simba? Huyu amechaguliwa na wanachama wa Bakwata tu. Sasa kama hivyo ndiyo, kwa nini awasemee hata wale ambao si wanachama wake?”
Anaituhumu serikali kwa kile alichoita “kuanzisha Bakwata” baada ya kuvunjwa kwa taasisi ya kiislamu ya Afrika Muslim (East African Muslim Welfare Society EAMWS).
Anasema chombo ambacho hakikuanzishwa na waislamu hakina haki kuwazungumzia waislamu.
Makala hii iliandikwa katika gazeti la MwanaHalisi
No comments:
Post a Comment