Wednesday, April 4, 2012

Mtazamo wa Uislamu kuhusu siasa


WENGI wetu tumekuwa tukisikia viongozi, wasomi na watu mbalimbali wakizungumzia masuala ya dini na siasa. Ujumbe mkuu siku zote umekuwa kuvitenganisha viwili hivyo yaani visichanganywe. Katika sehemu mbalimbali duniani, kama ilivyo kwa masuala mengine yahusuyo maisha ya kila siku, Waislamu wamekuwa ama wakiaswa kutochanganya dini na siasa au wakilaumiwa kwa kuvichanganya viwili hivi. Chanzo cha nasaha na lawama hizo ni mtazamo Kimagharibi au Usekula ambao unadai kutenganisha dini na siasa (separation of the Church from politics). Wasekula wanadai kuwa viwili hivyo vikichanganywa basi vurugu itatawala katika jamii husika. Hata hivyo, jamii nyingi za huko Magharibi zinaendeshwa kwa taratibu za kinaswara (Kikristo) lakini bado zinadai kuwa zenyewe ni za Kisekula. Wasiwasi wao umekuwa kwa Uislamu ambao siku zote wanaona kama dini isiyojali au isiyofuata haki za binadamu. Mwandishi Mama Nasir anaelezea zaidi.
Nini Uislamu na siasa ni nini?
Uislamu ni dini au mfumo wa maisha ambao Allah (s.w.) amewaletea waja wake kupitia kwa Mitume wake. Sisi tuliopo sasa Uislamu umetufika kupitia kwa Mtume Muhammad (s.a.w.). Uislamu ni mfumo uliokamili, unaongoza kila kipengele kinachohusu maisha ya mwanadamu. Wanaoamua kuukubali au kuufuata Uislamu basi wanaamrishwa na Allah (s.w.) kufanya hivyo kwa ukamilifu na kama inavyopasa kuwa.
Allah (s.w.) anasema: "Enyi mlioamini! Ingieni kwa ukamilifu katika Uislamu. (Ingieni katika hukumu za Uislamu zote), wala msifuate nyayo za shetani. Kwa hakika yeye kwenu ni adui dhahiri". (2:208).


Allah (s.w.) akasisitiza kwa waumini: "Enyi mlioamini! Mcheni Allah kama ipasavyo kumcha, wala msife isipokuwa mmekwisha kuwa Waislamu kamili". (3:102)
Kutokana na aya hizi ni wazi kuwa Muislamu anawajibika kutekeleza masuala yote ya maisha yake kama ilivyoelekezwa na Uislamu (Qur'an na Sunnah).
Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI) imetafsiri neno "siasa" katika kamusi ya Kiswahili Sanifu kama ifuatavyo:
"Mfumo wa mawazo yaongozayo utawala wa serikali ya nchi.
"Itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha uchumi wake, utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii".


Uislamu na siasa
Pamoja na kwamba maadui wa Waislamu na dini yao wanatulazimisha kuvitenganisha viwili hivi, lakini kufuatana na maelezo ya hapo juu ni wazi kuwa Muislamu anayeamini na kuufuata Uislamu hawezi kuitoa siasa kwenye dini. Hii ni kwa sababu Uislamu kama unavyoelezwa kwenye Qur'an na Sunnah unagusa nyanja zote zinazohusu maisha ya mwanadamu ikiwemo siasa, na lengo lake kuu ni kusimamisha utawala wa Allah (s.w.) hapa duniani. Kwa hiyo ili lengo hili litimie ni lazima maagizo yote yafuatwe kwa ukamilifu na siyo kipande kipande kwa kutenganisha mambo mbalimbali yahusuyo maisha ya mwanadamu.


Katika Uislamu, dini na siasa ni viwili viwili vilivyopangana (vilivyoingiliana) na kwa hiyo ni kitu kimoja. Uislamu ni njia kamili ya maisha na siasa ni sehemu ya maisha hayo. Kama Uislamu ulivyofundisha swala, swaumu, zakah, hija na mengineyo, umefundisha pia jinsi ya kuendesha dola (State) na kuunda serikali (government)u, kuchagua viongozi na wawakilishi wetu, kuweka mikataba, kuendesha biashara na shughuli nyingine mbalimbali.


Uislamu ni mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu na kuwa lengo la mfumo huo ni kusimamisha ufalme wa Allah (s.w.) hapa duniani.
Mfumo wa siasa wa Kiislamu unasimama katika misingi ifuatayo:
Utukufu/ukuu (sovereignity) wa Allah (s.w.). Uislamu unafundisha kuwa chanzo cha nguvu zote na sheria zote ni Allah (s.w.). Hii imedhihirishwa katika sura na aya mbalimbali za Qur'an kama vile 25:2 na 67:1. Ni Mwenyezi Mungu ndiye anayejua kipi kizuri na kipi kibaya kwa viumbe vyake. Na Yeye ndiye mwamuzi wa mwisho.
Kazi ya dola yoyote hewa ni kusimamia utekelezaji wa sheria, kwa hiyo ni dola iweze kusimamia sheria ya Allah (s.w.) ni lazima nayo itoke huko huko kwa Allah (s.w.). Sheria zilizomo kwenye Qur'an (za kukata wezi mikono, kuchapa viboko/kupiga mawe wazinifu na kadhalika) ni amri za Allah na hivyo haziwezi kubadilishwa na mamlaka yoyote ya kibinadamu hata Umoja wa Mataifa badala yake inatakiwa zitekelezwe na waja wote. Kwa Waislamu kutekeleleza amri/sheria hizo kwa vitendo ndio kukamilisha Uislamu wetu. Kunapotokea mifumo ya siasa ambayo haitekelezi au haisimamishi amri za Allah (s.w.) ni wazi kuwa Uislamu unapata kasoro, na hapo ndipo ulazima wa kuwa na dola ya Kiislamu unapokuja.


Ukhalifa wa binadamu: Mwenyezi Mungu anasema wazi katika Qur'an kuwa mwanadamu ni khalifa (mwakilishi) wake hapa duniani. Kwa mantiki hii mwanadamu analazimika fanye alivyoamrishwa na Allah. Hata hivyo, mwanadamu amepewa uhuru wa kufuata au kuzikana amri za Allah (s.w.) na ndio maana kuna wanaadamu wengi ambao wametokea kuwa wasaliti wa Allah (s.w.). Badala ya kutekeleza alivyoamrishwa ili kuleta amani na utulivu duniani wameamua kumuasi Allah (s.w.) na kusababisha machafuko tunayoyashuhudia sehemu mbalimbali duniani hivi sasa.
Kutunga sheria kwa ushauri (Shura): Uislamu unafundisha kuendesha serikali, kutunga sheria na kufanya maamuzi kwa kuzingatia ushauri na ushirikishaji watu (raia) kama Qur'an inasema katika 3:159 na 42:38. Uislamu hauruhusu udikteta, rejea zake ni Qur'an na Sunnah.


Uwajibikaji wa serikali: Katika mfumo wa siasa unaondeshwa Kiislamu, mtawala na serikali lazima wawajibike kwanza kwa Allah (s.w.) na baadaye kwa raia. Mtawala huwa ni mtumishi wa raia na wote kwa pamoja ni makhalifa wa Allah. Wote watawajibika kwa Allah (s.w.) siku ya mwisho ingawa kwa viwango tofauti. Jukumu la mtawala ni zito zaidi.
Vile vile, katika mfumo wa siasa wa Kiislamu raia yeyote wa kawaida ana uhuru wa kuhoji chochote kuhusiana na mtawala na serikali yake mradi tu abaki katika mipaka ya Qur'an na Sunnah.


Uhuru wa mahakama na usawa mbele ya sheria: Hili linapatikana katika mfumo wa siasa wa Kiislamu ambapo mkuu wa nchi au kiongozi mwingine yeyote hawi juu ya sheria. Mojawapo ya kazi za dola ya Kiislamu ni kuhakikisha haki kwa raia wote. Kigezo cha kuwapambanua waja katika Uislamu ni taqwa (ucha Mungu) tu na si vinginevyo.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget