Monday, April 2, 2012

“Ushahidi” wa Uungu wa Yesu


“Ushahidi” wa Uungu wa Yesu

Kuna baadhi ya mistari iliyotafsiriwa na makanisa ya Kikatoliki pamoja na Kiprotestanti kuwa ndio ushahidi wa uungu wa Yesu Kristo. Hata hivyo, kwa uchunguzi wa kina kuhusu mistari hiyo, imekuwa ni dhahiri kuwa, ama maneno yake ni tata, yanayoacha tafsiri nyingi tofauti tofauti, au imeongezwa na haikuwepo katika miswada ya mwanzo ya mapokeo ya Biblia. Ifuatayo ni baadhi ya mistari hiyo iliyotajwa sana:

1. Mwanzo na Mwisho

Katika kitabu cha Ufunuo 1:8, inadokezwa kuwa Yesu amesema yafuatayo kujihusu yeye mwenyewe: “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi”. Hizi ni sifa za Mungu. Kwa hiyo, hapa Yesu, kwa mujibu wa Wakristo wa mwanzo, anadai uungu. Hata hivyo, hayo maneno yalitajwa hapo juu ni kwa mujibu wa toleo la King James Version. Ama katika toleo la Revised Standard Version, wasomi wa Biblia wanarekebisha makosa ya kitafsiri na wameandika: “Mimi ni wa mwanzo na wa Mwishom” asema Bwana Mungu,..”.  Pia, marekebisho yalifanywa katika toleo la New American Bible iliyotayarishwa na Wakatoliki. Tafsri ya aya hiyo imerekebishwa ili iwekwe katika muktadha wake ulio sahihi kama ifuatavyo: “Bwana Mungu anasema: “Mimi ni wa mwanzo na wa Mwishom…” Ikiwa na marekebisho haya, inadhihirika kuwa, mstari huu ulikuwa ni maelezo ya Mungu na sio maelezo ya Mtume Yesu. 

2. Maisha ya kabla ya Kristo

Mstari mwingine unaotumiwa sana ili kuunga mkono uungu wa Yesu ni Yohana 8:58: “Yesu akawaambia, amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko. Mstari huu umechukuliwa na kuashiria kuwa Yesu alikuwepo kabla ya kudhihiri kwake duniani. Uamuzi uliofikiwa kutokana na mstari huo ni kuwa Yesu lazima awe Mungu, kwa kuwa kuwepo kwake kumetangulia tarehe ya kuzaliwa kwake duniani. Hata hivyo, dhana ya kuwepo kabla ya kudhihiri kwa mitume, na kwa watu wengine, ipo katila vitabu vyote viwili, Agano la Kale, vilevile katika Quran. Yeremia anajielezea mwenyewe katika Kitabu Cha Yeremia 1:4-5 kama ifuatavyo:
“Neno la BWANA lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”
Nabii Suleimani anaripotiwa katika Mithali 8:23-27, ya kuwa amesema, “Nalitukuka tokea milele, tangu awali, kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde, Wala chanzo cha mavumbi ya dunia; Alipozithibitisha mbingu nalikuwako…"
Kwa mujibu wa Ayubu 38:4 na 21, Mungu amemtambulisha Nabii Ayubu kama ifuatavyo: “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa unafahamu.”
Katika Quran, Sura ya  Al-A’aaraf, 7:172, Mungu anaeleza kuwa mwanadamu alikuwepo kiroho kabla ya kuumbwa ulimwengu wa kimwili.
"وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَى أَنفُسِهِمْ أَلَسْتَ بِرَبِّكُمْ قَالُواْ بَلَى شَهِدْنَا أَن تَقُولُواْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ."
"Na pale Mola wako Mlezi alipowaleta katika wanaadamu kutoka migongoni mwa kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo." Al-A’aaraf, 7:172
Kwa hiyo, maelezo ya Mtume Yesu, “Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko”. Hayawezi kutumiwa kuwa ni ushahidi wa uungu wake. Katika muktadha wa Yohana 8:54, Yesu amedaiwa kuwa ametamka kuhusu ujuzi wa Mungu kwa Mitume yake, ambayo inatangulia tarehe ya kuumbwa kwao katika ulimwengu huu.

3. Mwana wa Mungu

Ushahidi mwingine uliotumiwa kwa ajili ya uungu wa Yesu ni kule  kutumiwa sifa ya “Mwana wa Mungu” kwa Yesu. Hata hivyo, kuna sehemu nyingi katika Agano la Kale ilipotumiwa sifa hiyo kwa watu wengine.
Mungu alimwita Israeli (Nabii Yakubu) “Mwanawe” pale alipomuelekeza Mtume Musa aende kwa Firauni katika Kutoka 4:22-23, “Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia…”[1]
Katika 2 Samweli 7:13-14, Mungu anamwita Nabii Suleimani Mwanawe, "Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu…"
Mungu alimuahidi Nabii Daudi kumfanya mwanawe katika Zaburi 89:26-27: “Yeye ataniita, Wewe baba yangu, Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu. Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.”[2]
Malaika wanachukuliwa kuwa ni “wana wa Mungu” katika kitabu cha Ayubu 1:6, “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao.[3]
Katika Agano Jipya, kuna marejeo mengi ya “mwana wa Mungu” ya watu wengine wasio Yesu. Kwa mfano, pale mtunzi wa Injili kwa mujibu wa Luka amewaorodhesha wahenga wake hadi kwa Adamu, ameandika: Luka 3:38 “Wa Enoshi, wa Sethi, wa Adamu, wa Mungu”.[4]
Baadhi ya watu wanadai kuwa kile cha kipekee kilichopo kwa Yesu ni kuwa yeye ndiye mwana wa pekee wa kuzaliwa[5] Mwana wa Mungu, huku hao wengine ni “wana wa Mungu tu.” Hata hivyo, Mungu ananukuliwa akimwambia Mtume Daudi, katika Zaburi 2:7, “Nitaihubiri amri, BWANA aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.”
Pia inapaswa ijulikane kuwa hakuna hata sehemu moja katika Injili ambapo Yesu alijiita yeye mwenyewe kuwa yeye hasa ndiye “mwana wa Mungu”.[6] Badala yake, amenukuliwa kuwa amekariri kujiita “Mwana wa Adamu” (mfano Luka 9:22) kwa mara zisizohesabika. Na katika Luka 4:41, kwa hakika amekataa kuitwa “Mwana wa Mungu”: “Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo.”
Kwa kuwa Wayahudi wanaamini kuwa Mungu ni Mmoja, na hana mke wala mtoto kwa maana halisi yoyote ile, ni wazi kuwa ibara “mwana wa Mungu” kwa Wayahudi ina maana ya “Mtumishi wa Mungu tu” yaani mtu aliye karibu na Mungu, kwa sababu ya huduma yake ya kiimani, akiwa kama mtoto kwa baba yake. Wakristo waliokuja kutoka katika historia za kuwa walikuwa ni Wagiriki au Warumi, baadaye waliitumia vibaya istilahi hiyo. Kwani katika urithi wao, “mwana wa Mungu” inamaanisha mungu ana mwili au mtu aliyezaliwa kwa muungano wa kimwili kati ya mungu mwanamume na mwanamke.[7] Wakati Kanisa lilipoacha msingi wa Kiyahudi, lilitwaa dhana ya kipagani ya “mwana wa Mungu”, ambayo kwa ukamilifu, ilikuwa ni tofauti na matumizi ya Kiyahudi.[8]
Kwa hiyo, matumizi ya istilahi “mwana wa Mungu” inafaa ifahamike kuwa ni alama ya ufahamu ya kisemintiki yenye maana “mtumishi wa Mungu”, na sio katika ufahamu wa kipagani wa uhalisi wa kuwa kinda la Mungu. Katika Injili nne, Yesu anarekodiwa akisema: “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mathayo 5:9.[9]
Vivo hivyo, matumizi ya Yesu ya istilahi abba, “baba mpendwa” lazima ifahamike hivyo hivyo. Kuna ubishani miongoni mwa wasomi wa Agano Jipya juu ya nini maana ya abba kwa uhakika kabisa katika zama za Yesu na Wayahudi wa makundi mengine wa muongo huo huo walilitumia kwa upana gani.
Hivi karibuni kwa ukali kabisa, James Barr amedai kuwa hilo halikuonyesha wazi wazi ufahamu wa kuwa hilo lilikuwa linamuhusu yeye ila hilo kiwepesi kabisa linaashiria “baba” tu.[10] Ili kufikiria kuwa Mungu ni “Baba yetu wa mbinguni” haina maana mpya, kwa kuwa katika sala ya bwana amenukuliwa kuwa amewafundisha wanafunzi wake kumtambulisha Mungu katika njia hii hii.

4. Pamoja na Mungu

Wale wanaodai kuwa Yesu alikuwa Mungu, wanashikilia kuwa yeye hakuwa Mungu aliyetengeka, bali ni mmoja na ni Mungu yule yule mwenye mwili. Wao wanaunga mkono imani hii kutokana na mstari wa 30 wa Injili kwa mujibu wa Yohana, sura 10, ambayo ndani yake Yesu anaripotiwa kuwa amesema, “Mimi na Baba ni kitu kimoja.” Nje ya muktadha, mstari huu unaashiria uungu wa Yesu. Hata hivyo, pale Wayahudi walipomtuhumu kwa kudai uungu, kwa kutegemea sentesi hiyo, Yohana 10:34 “Yesu akawajibu, Je, haikuandikwa katika Torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu? Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu;"[11] Amewabainishia, kwa mfano wa maandiko unaojulikana sana kwao, kuwa yeye alikuwa anatumia lugha ya kistiari ya manabii ambayo haipaswi kufasiriwa kwa kujipachika uungu yeye mwenyewe au kwa mtu mwingine yoyote.
Ushahidi zaidi unachukuliwa kutoka katika mstari wa kumi na wa kumi na moja wa Injili kwa mujibu wa Yohana, sura ya 14, pale watu walipomtaka Yesu awaonyeshe Baba, naye inaaminiwa alisema: "Husadiki ya kwambi mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwambi mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe.”
Ibara hizi zingeashiria uungu wa Yesu, kama sehemu iliyobakia ya Injili hiyo hiyo inapuuzwa. Hata hivyo, aya tisa baadaye, katika Yohana 14:20, pia Yesu anarekodiwa akiwaambia wanafunzi wake, "Siku ile mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.” Kwa hiyo, kama maelezo ya Yesu "Mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; yanamaanisha kuwa yeye ni Mungu, basi vivyo hivyo iwe kwa wanafunzi wa Yesu. Hii sentensi ya kiishara inamaanisha umoja wa lengo na sio umoja wa asili. Tafsiri ya kiishara inasisitizwa zaidi katika Yohana 17:20-21, pale Yesu aliposema, "Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.”[12]

5. Amekubali kusujudiwa

Inadaiwa kuwa Yesu tangu aliporipotiwa kuwa amekubali kusujudiwa na baadhi ya wafuasi zake, lazima atakuwa ni Mungu. Hata hivyo, uchunguzi makini kuhusu andiko hilo unaashiria mambo mawili; tafsiri wasiwasi, na tafsiri potofu. Istilahi “kusujudu” inaweza kupatikana katika King Jemes Version na The Revised Standard Version yakielezea watu watatu wenye busara waliokuja kutokea mashariki. Wameripotiwa katika Mathayo 2:2, wakisema, "Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”[13] Hata hivyo, katika Biblia ya The New American Bible (Catholic Press, 1970), hilo andiko linasomeka: "Yu wapi mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa sasa? Tumeona nyota yake ikichomoza na tumekuja kutoa heshima kwake.”
Katika The Revised Standard Version, Yohana 9:37-38, "Yesu akawaambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye. Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia. [14] Hata hivyo, katika The American Biblke, wafasiri wasomi wameongeza tanbibihi inayosomeka: 9:38. Mstari huu, imefutwa kwa umuhimu wa MSS [miswada], unaweza kuwa ni nyongeza kwa liturujia ya ubatizo.
Mistari hii haipatikani katika miswada muhimu ya kale yenye Injili hii. Huenda ni nyongeza ya baadaye iliyowekwa na waandishi wa kanisa ili yatumike katika huduma ya ubatizo. Zaidi, kama alivyofafanua, mwenye mamlaka makuu na adhima katika Biblia na lugha zake za asili, George M. Lamsa, “Neno la Kiarama sagad, sujudu, pia lina maana ya kuinama au kupiga goti kwa watu wa mashariki wakati wa kusalimiana kwa kawaida ya kuinamisha kichwa au kuinama chini.[15] “Alimsujudia”  haiashirii kuwa yeye alimwabudu Yesu kama vile mtu alivyomwabudu Mungu. Tendo kama hilo lilitakiwa lichukuliwe ni la kukufuru na la uvunjaji wa Amri ya kwanza mbele ya macho ya Wayahudi, na huyo mtu angepigwa mawe. Lakini yeye alipiga magoti mbele yake kwa kutoa heshima na shukurani.”[16]
Kitabu cha mwisho, Quran, kinaeleza tukio la kuabudiwa au kutoabudiwa kwa Yesu, kwa kunukuu mazungumzo yatakayotokea baina ya Yesu na Mungu siku ya Kiama. Allah anaeleza katika Sura Al-Maa`idah, 5:116-117
"وَإِذْ قَالَ اللّهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـهَيْنِ مِن دُونِ اللّهِ...،  مَا قُلْتُ لَهُمْ إِلاَّ مَا أَمَرْتَنِي بِهِ أَنِ اعْبُدُواْ اللّهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ..."
"Na pale Mwenyezi Mungu atakaposema: Ewe Isa bin Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu?...,  (Na Isa) atasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu…, Sikuwaambia lolote ila uliyoniamrisha, nayo ni: Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi…" Al-Maa`idah, 5:116-117

6. "Hapo mwanzo kulikuwa na Neno"

Huenda ‘ushahidi’ wa uungu wa Yesu ulionukuliwa sana ni Yohana 1:1 na 14, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, na Neno alikuwa Mungu… Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Hata hivyo, maelezo haya hayakutolewa na Yesu Kristo, wala hayakuhusishwa naye na mtunzi wa Injili kwa mujibu wa Yohana. Hivyo, mistari hii haiundi ushahidi wa uungu wa Yesu, hasa hasa kuzingatia shaka inayoshikiliwa na wasomi wa Kikristo juu ya Injili ya Nne. Wasomi wa Biblia waliotunga Injili tano: “Picha mbili zilizochorwa na Yohana na muhtasari wa injili (yaani Injili ya Mathayo, Marko na Luka) zote mbili haziwezi kuwa ubainifu wa kihistoria.[17] Neno lilohusishwa na Yesu katika Injili ya Nne limeundwa na wainjilisti kwa sehemu kubwa, na linaakisi mwendelezo wa lugha ya jamii ya Wakristo wa Kiyohana.[18] Neno la Kigiriki lilotumiwa na mtunzi wa Injili ya Nne asiyejulikana kwa “neno” ni logos.[19] Kwa kufanya hivyo, huyo mtunzi anamtambulisha Yesu kwa logos la wanafalsa wapagani wa Kigiriki, neno ambalo lilikuwa na lengo takatifu na thabiti lililojitokeza ulimwenguni, huyo mtunzi akalipangilia neno hilo na kulipa mfumo na maana.[20]
Wazo la logos katika fikra za Kigiriki huenda linarejea nyuma, kwa uchache hadi kwa mwanafalsafa wa karne ya sita BC, Heracleitus, aliyependekeza kuwa, kulikuwa na logos ulimwenguni anayetenda kwa mwanadamu kulingana na nguvu ya hoja. Baadaye, Stoics[21] analitambulisha logos kuwa ni tendo, mantiki, na kanuni ya kiroho inayosambaa katika ukweli wote.[22] Mwanafalsafa wa Kiyahudi anayeongea Kigiriki, Judaeus Philo wa Alexandria (15 BC -45 CE), amefundisha kuwa logos alikuwa ni mpatanishi baina ya Mungu na ulimwengu, kwa kuwa na sifa mbili za uwakala wa Mungu na ulimwengu,  na kuwa na sifa mbili za uwakala wa viumbe na wakala wa ambaye kupitia kwake akili ya mwanadamu inaweza kumfahamu Mungu.[23] Maandiko ya Philo yalihifadhiwa na kutunzwa na kanisa, na kueneza ufunuo kwa mafundisho ya kistaarabu ya tiolojia ya kifalsafa ya Kikristo. Aliacha mafundisho ya fikra za Kipilato wakichukulia logos (Neno) na kuliita “mtoto wa kwanza wa kuzaliwa na Mungu.”[24]
Utambulisho wa Yesu kwa logos, uliendelezwa katika kanisa la kwanza ikiwa ni tokeo la majaribio yaliyofanywa na wanatiolojia wa kwanza wa Kikristo pamoja na watetezi kuielezea imani ya Kikristo kwa istilahi ambayo ingekuwa wazi kwa ulimwengu wa Wayunani. Zaidi ya hayo, ilikuwa ni kuwavutia wasikilizaji wao na mtazamo wao kuwa Ukristo ulikuwa unashinda, au mrithi wa wale wote waliokuwa wanafalsafa bora wa kipagani. Kwa hiyo, katika kazi zao za utetezi na ubishani, Mapadri wa Kikristo wa kwanza wameeleza kuwa Yesu alikuwa ni logos aliyekuwepo hapo kabla.[25]
Neno la Kigiriki lililotumika kwa maana ya ‘Mungu’ katika hiyo ibara ni “na Neno lilikuwa kwa Mungu,” lipo katika mtindo wa “definite form- yaani mtindo uliowazi, au unaofahamika” batheos, Linalomaanisha “Huyo Mungu, au Mungu maalum”. Hata hivyo, katika ibara ya pili “na Neno alikuwa Mungu”, neno la Kigiriki lililotumika kwa maana ya ‘Mungu’ katika ibara lipo katika mtindo wa “indefinite form- yaani mtindo usiowazi, au usiofahamika” tontheos, Linalomaanisha ‘mungu yoyote, yaani mungu asiyejulikana, au mungu yoyote asiye maalumu’.[26] Kwa hiyo, Yohana 1:1, kwa uwazi zaidi ilipaswa itafsiriwe, “Hapo Mwanzo kulikuwa na Neno, na hilo Neno lilikuwa kwa Mungu, na hilo Neno lilikuwa mungu mwingine.” Kwa hiyo, kama hilo neno lilikuwa mungu mwingine kwa ufahamu wa kifasihi, itamaanisha kuwa kulikuwa na miungu miwili na sio mmoja. Hata hivyo, katika lugha ya Kibiblia, neno ‘mungu – asiyefahamika’ linatumika kwa maana ya istiari ili kuashiria nguvu. Kwa mfano, Paulo alimtaja shetani kuwa ni ‘mungu – asiyefahamika’ katika 2 Wakorintho 4:4, "ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu." Pia, Musa alitajwa kama ni ‘mungu – asiyefahamika’ katika Kutoka 7:1, "BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruna atakuwa nabii wako.[27]

Mawazo ya kale

Kulikuwa na mgogoro mkubwa kati ya tafsiri ya Pauline na ya Jerusalem kuhusu Yesu na ujumbe wake. Mgogoro huo, baada ya kutokea pole pole kwa miaka mingi, hatimaye ulipelekea mpasuko kabisa, katika mpasuko huo, ulipelekea kuundwa Kanisa la Wakristo wa Pauline, kwa athari hiyo, dini mpya iliyojitenga kutoka Uyahudi. Kwa upande mwingine, Wanazareti wa Jerusalem hawakukata uhusiano wao na Uyahudi, bali walijizingatia kuwa wao ndio kiini cha kuutekeleza Uyahudi, watiifu wa Torati, pia walimwamini Yesu, umbo la Masihi mwanadamu.[28]
Wakati uasi wa Kiyahudi ulipopondwa pondwa na Warumi na mahekalu yao kuharibiwa mwaka 70 CE, Wakristo wa Kiyahudi walitawanyika, nguvu yao na mvuto wao wa kuwa wao ndio Kanisa Mama na kituo cha vuguvugu la Yesu zilifikia kikomo.[29] Vuguvugu la Wakristo wa Kipauline, vuguvugu ambalo mpaka mwaka 66 CE. Lilikuwa linapigania liendelee kuishi, dhidi ya kutokubaliwa huko Jerusalem, sasa lilianza kusonga mbele.
Kanisa la Jerusalem, chini ya uongozi wa James, kiasili lilijulikana kuwa ni la Wanazareti, baadaye likajulikana kwa jina la kupanga na la kuaibisha la Ebionites (Kwa kiyahudi evyonium, “watu maskini”), jina ambalo baadhi ya Wanazareti walilitwaa kwa ufahari wakilichukulia kuwa ni kikumbusho cha maneno ya Yesu yasemayo, “Wabarikiwe maskini.” Baada ya Kanisa la Graeco-Roman kushika hatamu, Wanazareti wakawa wanadharauliwa na kuonwa kuwa ni waasi, kwa sababu ya kukataa kwao mafundisho ya Paulo.[30]
Kwa mujibu wa historia ya kanisa la wahenga, Irenaeus (c. 185 CE,) hao watu maskini walimwamini Mungu mmoja, Muumba, aliyefundisha kuwa Yesu alikuwa ni masihi, kwa mujibu wa Mathayo, walitumia Injili tu, na kumpinga Paulo kwa kumwona kuwa ni muasi aliyeasi Sheria ya Kiyahudi.[31]
Hao watu maskini walijulikana kuwa waliishi mpaka katika karne ya nne. Baadhi yao walihama Palestina na wakaishi huko Transjordan na Syria na baadaye sehemu hiyo ikajulikana kuwa ni Asia ndogo, Misri na Roma [32].
Kwa mfumo wa kifalme,[33] vuguvugu la Wakristo wa Mataifa lilioendelezwa kipindi cha karne ya pili na ya tatu liliendelea kuwakilisha mtazamo wa kuamini Mungu mmoja uliokithiri na ule wa Waibionia ‘watu maskini’. Mtazamo huo ulishikilia kuwa Kristo alikuwa ni mtu, mimba yake ni ya kimuujiza, lakini alikuwa ni “mwana wa Mungu” wa pekee kwa kuwa amejazwa busara takatifu na nguvu. Mtazamo huu ulifundishwa huko Roma takriban mwishoni mwa karne ya pili na Theodotus, aliyetengwa na Papa Victor, na ulifundishwa sehemu Fulani hapo baadaye na Artemon, aliyetengwa na Papa Zephyrinus. Takriban mwaka 260 CE mtazamo huo ulifundishwa tena na Paulo wa Samosata,[34] Askofu mkuu wa Antokia huko Syria, ambaye alihubiri kiwazi wazi kuwa Yesu alikuwa ni mtu na kupitia kwake Mungu ameongea maneno yake (Logos), naye kwa nguvu kabisa amethibitisha upweke wa Mungu.
Kati ya mwaka 263 na 268 kwa uchache vikao vitatu vya baraza la kanisa viliitishwa huko Antokia ili kujadili usahihi wa Paulo. Kikao cha tatu kililaani mafundisho yake na kumvua madaraka. Hata hivyo, Paulo alifaidika na ulinzi wa Zenobia, malkia wa Palmyra, ambaye kwake yeye, Antokia ilikuwa ndio mada, na haikuwa ila mpaka mwaka 272 pale mfalme Aurelian alipomshinda Zenobia kwa kiwango ambacho madaraka halisi yakanyakuliwa.[35]
Mwishoni mwa karne ya tatu na mwanzoni mwa karne ya nne, Arius (b.c 250, Libya – 336 CE), kasisi wa Alexandria, Misri, pia amefundisha maumbile yenye mipaka ya Kristo upweke kabisa wa Mungu, jambo lililowavutia idadi kubwa ya wafuasi, mpaka alipotangazwa kuwa ni mzandiki na baraza la Nicaea mnamo Mei mwaka 325 CE. Wakati wa baraza hilo, alipinga kutia saini mfumo wa imani unaoeleza kuwa Kristo alikuwa na tabia ile ile kama Mungu. Hata hivyo, akiwa ameshawishiwa na wenzake wa Asia ndogo na kutoka Constantia, binti wa mfalme Constantine, alifanikiwa kushawishi kurejea kwa Arius kutoka uhamishoni na kurudi kanisani.[36] Vuguvugu alilodhaniwa kuwa amelianzisha, lakini kwa hakika lilikuwa ni kupanua imani ya Wakristo wa kiyahudi Wanazareti wa Jerusalem, Vuguvugu hilo lilijulikana kama Arianism na kuunda tisho kubwa ndani ya imani ya itikadi ya Wakristo wa Kipauline juu ya uungu wa Yesu.
Kutoka mwaka 337 hadi 350 CE, mfalme wa Magharibi, Constans, alionyesha huruma kwa Wakristo waoksodoksi, na Constantius wa pili, aliyekuwa mfalme wa Mashariki, aliwahurumia Waarians. Ushawaishi wa Arian ulikuwa mkubwa mno kiasi ambacho katika baraza la kanisa lililofanyika Antokia (341 CE), uthibitisho wa imani ulikuwa ndio jambo lililoondoa kifungu cha kuwa Yesu alikuwa na maumbile yale yale ya uungu kama Mungu”. Mwaka 350 CE Constantius wa pili akawa mtawala wa pekee wa himaya yote, na chini ya uongozi wake sehemu ya Nicene (Wakristo Waoksodoksi) waliangamizwa kwa kiasi kikubwa. Baada ya kifo cha Constantius wa pili mwaka 361 CE, Wakristo Waoksodoksi walio na wingi mkubwa huko Magharibi waliimarisha nafasi yao. Hata hivyo, utetezi wa kuwa na Mungu mpweke kabisa, na kukandamizwa kwa Wakristo Waoksodoksi, imani ya utatu iliendelea huko Mashariki chini ya mfalme Arian Valens (364-383 CE). Haikuwa ila mpaka pale Mfalme Theodosius wa kwanza (379-395 CE) alipotwaa ulinzi wa imani ya Arius, hata hivyo, imani hiyo iliendelea miongoni mwa makabila ya Kijerumani hadi mwishoni mwa karne ya saba.[37]

Mawazo ya kisasa

Leo hii, kuna wasomi wengi katika Ukristo wanaoshikilia kuwa Yesu Kristo hakuwa Mungu. Mwaka 1977, kikundi cha wasomi saba wa Biblia, akiwemo mwanatiolojia kiongozi wa Kianglikana na wasomi wengine wa Agano Jipya, walichapisha kitabu kiitwacho The Myth of God Icarnate, (Kisa cha kubuni cha Mungu mwenye mwili) kilichosababisha fujo kubwa kwa makutano makuu ya Kanisa la Uingereza. Katika utangulizi, mwandishi, John Hick, ameandika yafuatayo: “Waandishi wa kitabu hiki wamekinaishwa kuwa mwendelezo mkubwa wa kitiolojia uitishwe katika muda huu wa karne ya ishirini.
Dai linaibuka kutokana na kukuwa kwa maarifa ya asili ya Ukristo, na kuhusisha kutambua kuwa Yesu alikuwa ni (kama alivyowasilishwa katika matendo 2:21) ‘mtu aliyethibitishwa na Mungu’ kwa kazi maalum kwa lengo la kiungu, na kuwa dhana ya baadaye juu kumhusu yeye kama ni Mungu mwenye mwili, Nafsi ya Pili ya Utatu Mtakatifu inayoishi katika maisha ya kibinadamu, ni ngano ya kubuni au njia ya kishairi ya kuelezea umuhimu wake kwetu.”[38] Kuna makubaliano makubwa miongoni mwa wasomi wa Agano Jipya kuwa, kihistoria Yesu hajadai uungu ambao fikra ya Kikristo ilimfanyia; yeye hajajielewa kuwa yeye ni Mungu, wala Mungu Mwana, mwenye mwili [katika mwili].[39] Askofu mkuu wa hivi mwishoni Michael Ramsy, ambaye alikuwa ni msomi wa Agano Jipya, ameandika kuwa “Yesu hajadai uungu.”[40] Mwenzake wa zama moja, msomi wa Agano Jipya C.F.D. Moule. Amesema kuwa, “Kwa hali yeyote ile ya Elimu ya Ukristo ya hali ya juu inayotegemea usahihi wa madai ya Yesu mwenyewe, hasa hasa katika Injili ya Nne, kwa hakika atakuwa hatarini.”[41]
Katika utafiti mkubwa juu ya asili ya imani ya kuwa na mwili, James Dunn, anayethibitisha Elimu ya Ukristo wa Kioksodoksi, anahitimisha kuwa “hakuna ushahidi wa hakika katika mapokeo ya mwanzo ya Yesu kwa kile ambacho kwa uadilifu, kitaitwa ufahamu wa uungu.”[42] Tena, Brian Hebblethwaite, mtetezi kwa nguvu wa Elimu ya Ukristo ya mapokeo ya Nicene-Calcedonian, anakiri kuwa “haiwezekani tena kutetea uungu wa Yesu kwa kurejea katika madai ya Yesu.”[43] Hebblethwaite na Dunn, na wasomi wengine kama wao wanaoendelea kuamini uungu wa Yesu, wanadai kuwa licha ya kuwa Yesu hakujijua kuwa Yeye alikuwa Mungu mwenye mwili. Haya yalijulikana baada ya kufufuka kwake tu.
Wengine wengi miongoni mwa Maaskofu wakuu mashuhuri wa Kanisa la Uingereza, wanoshuku uungu wa Yesu, ni Kasisi asemaye wazi wazi Profesa David Jenkins, Askofu mkuu wa Durham Uingereza, ambaye anaeleza kwa uwazi kuwa Yesu hakuwa Mungu.[44]
Makala ifuatayo, ilitokoea katika The Daily News miaka iliyopita, kwa uwazi kabisa inaonyesha kiasi gani cha shaka miongoni mwa wakuu wa kidini kuhusu uungu wa Yesu.
Uchunguzi wa kushtusha wa Maaskofu wa Kianglikana

LONDON: Zaidi ya nusu ya Maaskofu Waingereza wa Kianglikana wanasema kuwa: “Wakristo hawalazimiki  kuamini kuwa Yesu Kristo ni Mungu, kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa leo.
Kura za maoni za Maaskofu Waingereza 31, miongoni mwa Maaskofu 39, zinaonesha kuwa, wengi wao wanaona kuwa, Miujiza ya Kristo, kuzaliwa na bikira na kufufuka huenda hayo hayajatokea kama ilivyoelezwa katika Biblia. Ni Maaskofu 11 tu, ndio waliosisitiza kuwa "Wakristo lazima wamchukulie Yesu Kristo kuwa ni Mungu mtu, huku 19 wakisema kuwa inatosha kumchukulia Yesu kama ni "Mwakilishi mkuu wa Mungu". Na mmoja alijizuia kutoa maoni yake.
Hiyo kura ya maoni iliendeshwa na London Weekend Television's weekly religion show, Credo.
"DAILY NEWS" 25/6/84



[1] Pia tazama, Hosea 1:10, ya King James Version.
[2] Katika Revised Standard Version, inasema: “Na mimi nitamfanya mzaliwa wangu wa kwanza, mkuu wa wafalme duniani.” Pia tazama Yeremia 31:9, “Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyooka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.”
[3] Pia tazama, Job 2:1 na 38:4-7. marejeo mengine ya wana wa Mungu pia unaweza kupatikana katika Mwanzo 6:2, Kumbukumbu la Torati 14:1 na Hosea 1:10.
[4] Luka 3:38.
[5] Neno “wa kuzaa” katika Kingereza cha Kale linamaanisha ‘kuzaliwa na baba’ na lilikuwa linatumiwa kutofautisha kati ya Yesu, aliyechukuliwa kuwa ni mwana halisi wa Mungu, na mfumo wa kistiari wa kutumia neno ‘mwana’ kwa “wana wa Mungu walioumbwa”.
[6] Katika kitabu cha Matendo cha Agano Jipya, kuna mihtasari ya hotuba za wanafunzi wa kwanza wa Yesu, maneno ya tarehe zinazoanzia mwaka 33 CE., takriban miaka arobaini kabla ya kuandikwa zile Injili nne. Katika moja ya hotuba hizi, Yesu anaaonyeshwa kwa bayana kuwa ni andra apo tou theou: “yaani, mtu kutoka kwa Mungu.” Matendo 2:22. Hakuna hata nara moja kuungama huku kwa mwanzo kwa imani ukitumia maelezo wios tou theous: “Mwana wa Mungu”, lakini wao wanaongea mara kadhaa kuwa Yesu ni mtumishi wa Mungu na ni mtume Matendo 3:13, 22, 23, 26. Maana ya hotuba hizi ni kuwa hotuba hizo kibarabara zinaakisi imani asilia na istilahi za wanafunzi wa Yesu, kabla ya kubadilishwa kwa imani na istilahi chini ya ushawishi wa Dini ya Warumi na Falsafa za Kigiriki. Wao wanaakisi mapokeo ambayo ni ya zamani kuliko yale yanayotumiwa na Injili Nne, ambapo Yesu havikwi uungu wala umwana wa Mungu. (Bible Studies From a Muslim Perspective, p. 12). 
[7] Tazama Matendo14:11-13. Katika mji wa Lystra (Uturuki), Paulo na Barnabas walihubiri, na wapagani walidai kuwa Paulo na Barnaba walikuwa ni miungu wenye miili. Walimwita Barnaba mungu wa Kirumi Zeus, na Paulo mungu wa Kirumi Hermes.
[8] Bible study from a Muslim Perspective, p. 15.
[9] Mathayo 5:9.
[10] Journal of Theological Studies, vol. 39 na Thewology, vol. 91, no. 741.
[11] Yesu ananukuu Zaburi 82:6 “Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.”
[12] Pia tazama Yohana 17:11.
[13] Pia tazama, Mathayo 2:8.
[14] Pia tazama Mathayo 28:9, "Na tazama, Yesu akakutana nao, akasema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia."
[15] Tazama, kwa mfano, 1 Samweli 25:23, "Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi."
[16] Gospel Light, (1936 ed.) p. 353, quoted in Jesus, p.21.
[17] Injili ya Yohana kimsingi inatofautiana na Injili nyingine tatu (Injili za muhtasari) kiasi cha kutilia shaka uhakika wake. Kwa mfano:
Injili za Ufupisho
Injili ya Yohana              
Mahubiri ya Yesu kwa umma yalikuwa ni mwaka mmoja
Mahubiri ya Yesu kwa umma yalikuwa ni miaka mitatu
Yesu aliongea kwa ufupi kiasi cha mstari mmoja hivi, na kwa mafumbo
Yesu aliongea kwa urefu na kwa mijadala ya kifalsafa.
Yesu amesema kidogo mno kujihusu yeye mwenyewe
Yesu aliakisi kwa upana zaidi juu ya kazi yake na haiba yake.
Kumtoa mbadilisha pesa nje ya hekalu ndio tukio lake la mwisho katika kazi yake duniani
Kumtoa mbadilisha pesa nje ya hekalu ndio tukio lake la kwanza katika kazi yake
Yesu alitetea maskini na wakandamizwaji
Yesu alikuwa na jukumu dogo au hakuwa na jukumu lolote kwa maskini na wakandamizwaji
Yesu ni mtoa pepo
Yesu hajatoa pepo
Yesu alisulubiwa mnamo 15 Nisan
Yesu alisulubiwa mnamo 15 Nisan, siku ya Pasaka ya muhanga wa Wayahudi.

[18] The Five Gospels, p. 10.
[19] Wingi wake ni logoi nalo pia linamaanisha “hoja” au “mpango”.
[20] Dhana inayotambulishwa na neno logos pia linapatikana kwa wanafalsafa wahindu, Wamisri, na Wairani na mifumo ya kitiolojia. (The New Encyclopaedia Britannica, vol. 7, p. 440)
[21] Stoics walikuwa ni wanafalsafa waliofuata mafundisho ya mtambuzi Zeno wa Citicum (karne ya 4-3 BC).
[22] Wao wanaliita logos majaaliwa ya Mungu, maumbile, mungu, na roho wa ulimwenguni.
[23] Kwa mujibu wa Philo na wanafalsafa wa The Middle Platonists, waliofasiri kwa istilahi za kidini mafundisho ya karne ya nne BC ya mwalimu wa falsafa wa Kigiriki Plato, logos alizaliwa duniani kama ni msingi na wakati huo huo akili ya kiungu ya hali ya juu. (The New Fncyclopaedia Britannica, vol. 7, p. 44o)
[24] The New Fncyclopaedia Britannica, vol. 9, p. 386.
[25] Ibid, vol. 7, p. 440.
[26] Kristo katika Uislamu, pp. 40 – 1.
[27] Hili ni kwa mujibu wa King James Version na the Authorized Version. Katika Revised Standard Version, tafsiri ya mstari huu ni rejesho, “Na Bwana alimwambia Musa, ‘Tazama, Ninakufanya uwe Mungu kwa Farao; na Aroni nduguyo atakuwa mtume wako.
[28] - The Myth-maker, p. 172.
[29]Miaka sabini baadaye Kanisa la Kikristo lilijengwa upya huko Jerusalem, baada ya huo mji kuharibiwa na Warumi kwa mara ya pili na kujengwa upya ukiwa ni mji wa Mataifa usio wa Wayahudi ukiitwa Aelia Caitolina. Hili kanisa Jipya la Kikristo halikuendeleza ‘Kanisa la Jerusalem’ lile la kwanza lililongozwa na James. Wafuasi wake walikuwa ni watu wa Mataifa, kama anavyothibitisha Eusebius, na imani yake ilikuwa ni ile ya Ukristo wa Kipauline. (Eusebius, Ecclesiastical History, III. V. 2-3, iliyonukuliwa katika The Myth-maker, p. 174)
[30] The Myth-maker, p. 175.
[31] The New Fncyclopaedia Britannica, vol. 4, p. 344.
[32] Ibid., vol 4, p. 344.
[33] Pia ilijulikana kwa jina la Dynamic au Adoptionst Monarchianism.
[34] The New Fncyclopaedia Britannica, vol. 8, p. 244.
[35] The New Fncyclopaedia Britannica, vol. 9, p. 208.
[36] Ibid., vol. 1, pp. 556-7.
[37] The New Fncyclopaedia Britannica, vol. 1, p. 549-50.
[38] The Myth of God Incarnate, p. ix.
[39] The Metaphor of God Incarnate, pp. 27-8.
[40] Jesus and the Living Past, p. 39.
[41] The Origin of Christology, p. 136.
[42] Christology in the Making, p. 60.
[43] The Incarnation, p. 74.
[44] The Economist, April 1, 1989, vol. 311, no. 7596, p. 19.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget