Thursday, April 12, 2012

Wajibu wa vijana

Mfasiri:
Abu Ahmad Hussein
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Jaribio la Kumfahamu
Kabla ya kufikia umri wa miaka kumi na mitano kwa kipindi kidogo, mwanadamu hukabiliana na kipindi muhimu na cha hatari katika uhai wake, nacho ni kipindi cha ujana (ubarobaro) ambacho huendelea nacho hadi kufikia umri wa miaka ishirini au ishirini na tano hivi.
Hiki ndicho kipindi cha ubarobaro (ushababi), nacho ni kipindi muhimu na cha hatari. Hebu tujiulize kwa nini kuwa ni muhimu na hatari?
Ni muhimu kwa kuwa huihukumu hali ya baadaye ya umma na mwisho wake. Vijana hawa wanaokua hivi leo bila shaka wao ndio umma wa kesho.
Umma huu ulioko hivi sasa utaondoka na pahali pao na vyeo vyao vitachukuliwa na hawa vijana. Naam, utawaachia pahali pake umma unaokuja, umma mpya. Nao huo umma mpya ni hawa vijana wa leo na mabarobaro wa sasa.
Kwa hakika ni kweli kabisa kwamba mwanachuoni wa leo wa kidini hatakuwa ndiye mwanachuoni wa kesho, bali hapana shaka yoyote kwamba pahali pake na cheo chake ataviacha kisha atakuja mtu mwingine miongoni mwa hawa vijana mabarobaro iIi achukue pahali pake.
Mkuu wa mkoa au wilaya wa leo hatakuwa ndiye mkuu wa mkoa au wilaya wa siku zijazo, bali hapana budi nafasi yake itafikia kikomo, atakufa na pahali pake patachukuliwa na mtu mwingine.
Vivyo hivyo, rais wa nchi wa leo, hakimu, amiri, waziri, kiongozi, n.k. watakufa na pahali pao patachukuliwa na vilana wa leo.
Hii ndiyo tabia ya uhai na tabia ya maumbile. Huu ndio mwenendo wake kwamba kizazi kimoja kinapoondoka badala yake huja kizazi kingine.
Je, hao watu wengine watakaochukua nafasi ya jamii ya sasa katika siku zijazo ni akina nani? Hakika wao ni hawa vijana wa leo, kwani wao ndio watakaounda jamil ya kesho.
Siku moja Imam Hasan bin Ali AS aliwakusanya watoto wake na kuwaambia: "Nyiny leo ni watu wadogo, mnatarajiwa kuwa watu wazima kwa wengine."
Vijana wetu wa leo ikiwa watalelewa vyema hadi wawe wema na wanyofu, tunaweza kubashiri kuwa umma wetu na jamii zetu bali na vizazi vyetu vijavyo vitakuwa na mustakbali mwema; lakini wasipokuwa wema au wasipofuata njia nyofu basi itamaanisha kuwa huenda mustakbali wao ukawa mwovu, mweusi na wenye giza.
Kipindi cha ushababu ni muhimu sana kwa sababu ndicho upeo wa mustakbali wa umma na mustakbali wa wananchi, na kutokana na sababu hii ndio mafundisho bayana ya dini yanatilia mkazo sana kukizangatia kipindi hiki kutokana na umuhimu wake.
Kwa mfano kauli ya Mtume Muhammad SAW aliposema: "Hakika nyayo za mja hazitaweza kunyanyuka katika siku ya Kiyama hadi aulizwe ameumaliza umri wake katika nila gani na ameutumia ujana wake katika nini."
Wakati kama huu ni wa hatari kwa kijana kwa kuwa huishi katika hali maalum inayoathirika kimwili, kifikra na kijamii.
Katika hali hii ya pekee anayoishi kijana katika kipindi cha ujana, inatakikana ama ajiimarishe katika mazingira yaliyo mema na maongozi yaliyo salama ili aweze kuvuka kipindi hiki akiwa ni kijana mwenye juhudi sana ambaye ataweza kuunufaisha umma kutokana na kuwepo kwake na harakati zake; au aondokee kuwa ni kijana aliyeharibika katika mazingira ya ufisadi na matokeo yake iwe ni kuibomoa nafsi yake na kuibomoa jamii yake.

Vipambanuzi vya Kipindi cha Ujana

Kipindi cha ubarobaro kinajipambanua kwa wingi wa sifa na vipawa. Sifa hizi na vipawa hivi hupatikana kwa wingi katika shakhsia ya barobaro katika pande zote za maisha yake.

Upande wa Kimwili:

Katika kipindi cha uvulana na ubarobaro, mwili wa mwanadamu hutangaza kuwasili kwake kwenye kilele cha kukomaa na kukamilika, kwani huchukua umbile lake halisi na nguvu zake hukamilika na kimo chake humuongezea urembo wa kitabia. Qur'ani Tukufu yaelezea kuwa wakati wa uvulana ndio wakati wa nguvu.
Mwenyezi Mungu amesema: "Mwenyezi Mungu (ndiye) ambaye amewaumba nyinyi kutoka unyonge kisha akajaalia baada ya unyonge nguvu, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge na uzee, Mwenyezi Mungu huumba anachokitaka na Yeye ndiye Mjuzi na Mwenye uwezo." (30:54)
Mwanadamu huja kwenye uhai akiwa yu mtoto mdogo dhaifu, hawezi hata kumwondoa nzi aliyetua usoni mwake, kisha hukipita kipindi hicho cha udhaifu (utoto) huenda katika kipindi cha uvulana, kipindi chenye nguvu na nishati; kisha unyonge humjia tena na kumtawala mara nyingine kwa jinsi ambayo huingia katika zama za uzee na ukongwe.
Vilevile katika wakati wa ujana, hisia za mwanadamu hulipuka na hisia za jinsia hazimpi nafasi. Kijana huishi katika hali ya zahama, dhiki na vurugu za kijinsia (shahawa) na huendelea katika hali hii. Hisia hizi huwa zinahitaji kushibishwa na kuondoshewa kiu yake.

Upande wa Kijamii:

Baada ya kukipita kipindi cha utoto alipokuwa mdogo akinyenyekea amri za wakubwa, akiwa hana rai wala hamiliki jambo lolote, sasa huona kuwa ni barobaro. Nafsini mwake anajihisi kuwa ana nguvu, na kifuani mwake amejawa na hisia ya kujamini dhati yake. Wakati huo hutafuta jukumu Ia kutekeleza katika jamii.
Sasa yeye si mtoto tena, bali hujihisi kuwa ni mtu mzima (mme) aliyekamilika uume (utu), na ni wajibu wake kufanya yale yanayofanywa na wakubwa.
Umekwisha ule wakati aliokuwa akitendewa kama mtoto mdogo, wakati alipokuwa akitii amri za wakubwa na kunyenyekea matakwa yao. Hivi sasa yeye amekuwa mkubwa si mdogo tena. Anayo rai anataka aitekeleze na anatafuta jukumu katika jamii alitekeleze ili aijaze hi faragha ya kinafsi aliyokuwa nayo muda mrefu.

Upande wa Kinafsi:

Katika kipindi hiki cha ubarobaro, ndani mwa nafsi ya ubarobaro huwemo matakwa ya kutaka kukataa kila jambo na roho ya kutaka kuasi, kama kulipizia kisasi kwa aliyofanyiwa alipokuwa mdogo, wakati alipokuwa akitii matakwa ya wazazi wake na vilevile kuzinyenyekea ada za jamii yake bila ya kuweza kupinga au kuhalifu na kujitenga.
Kijana anapokuwa mkubwa na mwenye nguvu hupendelea naye atekeleze haki yake katika kupinga au kukubali na kuwa na rai huru. Huu ndio wakati ambao hukua nafsini mwake roho ya kutaka kupinga na kuasi.
Tena hapa kuna sifa nyingine anayosifiwa barobaro kuwa nayo katika wakati huu wa uvulana na ujana, nayo ni ule upendo wake wa kujitolea na kuwa tayari kwake kujitoa mhanga.
Tabia ya binadamu na umbile lake kila anapoishi muda mrefu hapa duniani, tamaa na pupa lake Ia kutaka kubakia zaidi hapa duniani huzidi kuambatana naye.
Ama tunapomzingatia barobaro kwa kuwa ni chipukizi anayeanza kukua katika hii dunia, yeye hawi mwingi wa tamaa na pupa Ia kutaka kubakia hapa duniani kama anavyokuwa mzee mwenye umri mkubwa.
Mwenye kuyachunguza kwa makini matendo ya barobaro atagundua kuwa ana tabia ya kujiingiza kwenye hatari au kushikilia lilelile analolitaka, kupambana bila ya kujali kufa hasa anapojawa na hamasa. Ama mtu mkubwa wa umri, yeye hujihifadhi, tena huwa mwenye utulivu na husara katika matendo yake na shughuli zake. Kule kuwa kwake na majaribio humpa aina fulani ya kuwa na mizani na kujihifadhi, tena pupa lake Ia kubakia duniani halimkubalii kuwa na upendo wa kujiigiza katika mambo bila ya kuzingatia.
Hapa kuna mfano mwepesi kuhusu hakika hii. Hebu mpeleleze barobaro anapoendesha gari, kisha mpeleleze mtu wa makamo uendeshaji wake uko namna gani.
Imerekodiwa kwamba katika zama za khallfa wa Kiabbasi Harun Rashid, aliambiwa kuwa yuko mtu aliyeishi na Mtume Mtukufu na akasikia hadithi zake. Yeye ni sahaba aliyekuwa na umri mrefu ambaye aliishi tokea zama za Mtume Mtukufu hadi zama za Harun Rashid. Umri wake ulikaribia miaka mia moja na thelathini (130)
Kwa vile sahaba huyu ana heshima kuu, Harun Rashid alipendelea kukutana naye. Harun Rashid akaamuru aletwe na akaletwa kwake huku amebebwa. Harun Rashid akamwuliza:
"Je, wewe umekutana na Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Mzee akainamisha kichwa chake kama kuonyesha alama ya kujibu ndio.
“Je, umewahi kuyasikia mazungumzo (hadithi) ya Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
"Ndio.”
"Je, unakumbuka mazungumzo yoyote miongoni mwa mazungumzo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
"Ndio”
"Hebu nizungumzie iIe hadithi unayoikumbuka uliyoipokea kwa Mtume Mtukufu."
Mzee akasema kwa sauti dhaifu sana: "Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu siku moja akisema: 'Mwanadamu huzeeka na hubakia ndani mwake sifa mbili -tamaa na matumaini.”
Mzee akayakata mazungumzo huku akiwa hana uwezo wa kuendelea nayo.
Harun Rashid akaamuru apewe zawadi, nayo ilikuwa ni kiwango fulani cha mali, na iliwekwa juu ya kitanda chake. Kisha wakambeba ili kumrudisha nyumbani kwake.
Harun Rashid akahisi kwamba mdomo wa sahaba mzee ulikuwa ukichezacheza kana kwamba alikuwa akisema kitu. Akaamuru arejeshwe. Watumishi wakaja naye hadi ubavuni karibu na Harun Rashid. Akamwuliza: "Nimeiona mdomo wako ukichezacheza wakati ulipokuwa ukirudishwa kana kwamba ulikuwa ukisema kitu."
Mzee akasema: "Ndio, nilikuwa nikiwauliza waliokuwa wakinibeba: 'Je, huyu Harun Rashid ataifanya zawadi hii iwe ni ya kila mwaka, awe akinipa mfano wake ili niweze kumzuru mwanzo wa kila mwaka?'”
Harun Rashid akacheka, kisha akasema: "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema kweli kabisa katika ile hadithi uliyolsema hivi sasa kwamba: 'Mwanadamu huzeeka na hubakia ndani mwake sifa mbili - tamaa na matumaini.’”
Hivi ndivyo ilivyo. Tamaa ya mwanadamu na matumaini yake ya kutaka kuishi duniani huzidi kukua nafsini mwake kila umri wake unapozidi. Hubakia ana busara na hujihifadhi katika matendo yake na mambo yake yote, ambapo barobaro huwa yuko tayari kujitoa sadaka na kujiingiza katika mambo ya hatari bila ya kujali hatari zilizoko mbele yake.

Upande wa Kifikra:

Aghlabu vijana na barobaro katika kipindi hiki cha ujana huwa na faragha na udhaifu wa kiakili katika kufungamana kwao na watu.
Katika kipindi hiki cha ubarobaro akili ya binadamu hufumka na vipawa vyake hufunguka. Huanza kuyafikiria mambo kwa undani. Akilini mwake huchoreka maswali mengi kuhusu maisha yake na maisha ya jamii. Maswali ambayo hayana budi kujibiwa wazi.
Vilevile hujiona kwamba halazimiki tena kuzikubali fikra za watu wake na mazingira yao, madamu ameamini nafsini mwake kuiamini dhati yake, na kupendelea kufuata mtindo wa kukataa na kupinga kila jambo na kupondokea zaldi upande wa kubeba majukumu mazito mazito na ya hatari.
Kwa ajili hiyo, barobaro huwa yuko tayari kuipokea na kuifuata fikra yoyote mpya japo iwe ya hatari namna gani.
Ama mtu mkubwa yeye ana ukinaifu, imani na fikra anazoziamini na kuzitukuza miaka mingi. Yeye hana faragha ya kiakili wala hahisi kuwa na haja ya kuwa na itikadi nyingine mpya, bali yeye hayuko tayari kuiacha fikra aliyoiamini muda mrefu na kuitukuza miaka mingi.
Kwa ajili hiyo utaona kwamba kila ujumbe na mafunzo kutoka mbinguni yalisimama na kupata nguvu kutokana na mabarobaro (vijana) wale ambao kwamba wao huwa wepesi kuziamini hizo fikra mpya na huwa tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya kuzitetea.
Tuchukue mfano mmoja: Nabi Ibrahim AS alipowapelekea watu wake ujumbe wa kumpwekesha na kutomshirikisha Mwenyezi Mungu, ni nani aliyemwamini na kuukubali wito wake? Watu wake hawakuukubali ujumbe wake, isitoshe wakamtuhumu kwa kuwa aliaminiwa na kikundi cha vijana maskini, kama Qur'ani Tukufu inavyosema: "Na hatukuoni wamekufuata isipokuwa wale wanyonge katika sisi wenye fikra ya mwanzo." (11:27)
Naye Nabii wetu Muhammad SAW pia. Wale waliofanya upesi kumwamini na kuufuata ujumbe wake walikuwa ni kikundi cha mabarobaro, wadogo kwa umri, kama Ali bin Abu Talib AS, Bilal Mhabeshi na Ammar bin Yaasir, n.k.
Jambo hili liliwafanya wazee na viongozi wa Makureshi kumtuhumu Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba yeye amewaharibu vijana wao na wakayasema hayo hayo katika mashitaka yao waliyoyapeleka kwa ami yake, Abu Talib. Wakasema: "Hakika mwana wa nduguyo amewatusi miungu wetu, na amezipuuza ndoto zetu na amewaharibu mabarobaro wetu."
lli kuitilia nguvu hakika hii, Mtume Mtukufu amesema: "Nawausia kuwafanyia mabarobaro wema, kwani wao wana mioyo laini zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu amenituma mimi (niwe) mbashiri na mhofishaji, mabarobaro wakaapa kushikamana nami na wazee wakanihalifu... Na muda wao (wa kuishi duniani) ukawa mrefu na nyoyo zao zikasusuwaa (zikawa ngumu)."
Amirul Mu'miniyn Ali bin Abu Talib amesema: "Hakika moyo wa kijana ni kama ardhi isiyokuwa na kitu (isiyolimwa) chochote kinachoingizwa (kinacholimwa) ndani yake hukikubali."

Vipi Tufaidike katika Kipindi cha Ubarobaro

Hayo yote yaliyotangulia ndiyo mambo muhimu na sifa muhimu zinazompambanua barobaro zikiwemo sifa za machimbuko yaliyo hatari pia.
Kwa hivyo, imetubainikia kwamba ni kwa miongozo mema na taratibu zilizo salama tu, ndipo itamkinika kufaidika na hivi vipawa na kuvipatiliza katika kuujenga utu wa Kiislamu unaotakikana ili vijana wetu wawe ni mfano halisi wenye kufanana na maisha ya vijana wa Kiislamu waliopigana jihadi kama Ammar bin Yaasir, Mus'ab bin Umayr, Malik Ashtar na Al bin Husayn al-Akbar.
Ikiwa tutawapuuza vijana wetu na kutowajali katika wakati huu ulio hatari au tukawatendea vibaya katika sifa zao na vipawa vyao vya kifikra, huenda tukaonjwa kwa kupata umma mpya uliopotoka na kuharibika. Umma huu mpya utapotosha njia na lengo, na vilevile utaubomoa mustakbali wake mwema.
Swali Ietu hivi sasa ni hili: Ni kwa njia gani tutafaidika na wakati huu wa ubarobaro (uvulana)? Vipi tutavikuza vipawa vyake na kumpangia nyadhifa kwa ajili ya maslahi yake na kuujenga utu wake, ili aweze kuubeba wajibu wa ujumbe huu wa Kiislamu? Haya ni miongoni mwa yale yatakayomfanya kijana awe ni msingi mwema wenye utendaji katika maendeleo ya kijamii na kuuendeleza mbele ujumbe huu wa Kiislamu.
Hapa napendelea kuelezea kwa kirefu kila kipawa cha kipindi hiki cha uvulana, na kuyaelezea mambo yenye kumpangia wadhifa na kumwongoza kwa ajili ya kujenga viongozi miongoni mwa vijana na umma wa Kiislamu unaokuja. Hapo tutaona vipi tutaweza kufaidika na kila kipawa chake, miongoni mwa hizi sifa tulizozitaja wakati atalelewa na kukua katika maongozi sahihi.
Vikwazo vya Matamanio ni
Fursa Nzuri ya Kuimarisha Matakwa
Ikiwa vijana wa umma wanamiliki irada (matakwa) na nguvu ya nafsi iliyo thabiti ambayo inashinda matamanio ya nafsi, nia na Irada thabiti yenye kupambana na ghururi, hakika umma utakuwa umetukuka na kupata heshima kuu. Tena umma kama huu utakuwa una uwezo wa kukabiliana na maadui na kupambana na wakoloni. Hautaweza kurukuu na kuyaitikia matakwa ya wakoloni, na hautamnyenyekea dhalimu au kuridhia kuwa watumwa wa wadhalimu na wakoloni.
Umma ni muundo wa mkusanyiko wa watu. Ikiwa watu wanaounda umma ni watu waliopondokea kwenye uharibifu na maovu, na ni wenye tabia ya ghururi na shahawa, basi msimamo wa umma na muamala wao kwa maadui zao utakuwa ni baridi na wenye kukubaliana na maovu hayo na dhuluma hiyo.
Ama ikiwa watu wanamiliki irada (nia thabiti), nguvu ya nafsi na uwezo wa kupambana na vikwazo, hakika umma ukishikana na vijana wake unaweza kukabiliana, kupinga na kusimama kwa ushujaa dhidi ya tamaa za maadui na njama za madhalimu na wakoloni.
Wakati huu wa uvulana ni fursa nzuri yenye thamani ya kuikuza irada (matakwa) ya mtu katika umma. Sababu ni kwamba irada ya binadamu haipati nguvu mara moja kwa kuipa mawaidha au kuipa miongozo, bali hupata nguvu kwa kupitia ukinzani na kwa kupambana na ghururi na vikwazo vya kila aina.
Kwa mfano, mtu ambaye ataikuta nafsi yake imezingirwa na mambo yenye udanganyifu na hadaa zenye nguvu, tena ikawa nafsi imebanwa katika vikwazo vyenye shahawa kali, yamkinika kwake kuilelea nafsi yake kwa matendo, kwa kuwa mgumu wa kutoyatii matamanio yake, aikuze kwa kuiviza irada yake kwa majaribio ya kimatendo. Mtu kama huyu anaweza kupata ushindi, hasa pale atakapoitukuza nafsi yake na kuzidharau zile ghururi na shahawa na aikanye nafsi yake kuvinyenyekea vikwazo vya matamanio.
Vivyo hivyo, kipindi hiki cha ujana kwa vijana ni kipindi cha kuipa mazoezi irada na kuifanyia majaribio nafsi yake.
Kijana akipata miongozo iliyo salama na kupata mafunzo (elimu) sahihi yaliyojaa ubinadamu katika malezi yaliyo mema, ataweza kuyapita majaribio haya kwa ushindi mkubwa, na baada ya mtihani huu atakuwa mwenye irada yenye nguvu na ushujaa.
Hakika mara nyingi mabarobaro husumbuliwa na hisia kali za matamanio nafsini mwao, vilevile hupambana na ghururi (hadazi) za aina mbalimbali zenye nguvu, lakini huweza kupata ushindi upesi hasa anapoweza kuitawala nafsi yake, kuuhifadhi utu wake na heshima yake, akaweza kupambana na hadazi zote na akaweza kujiepusha na vitimbi vikubwa vya matamanio yenye kiwi, hasa katika hizi jamii zetu kunakopatikana kwa wingi upondokeaji kwenye uharibifu na ufisadi. Barobaro akiweza kuyashinda hayo yote, yamaanisha kwamba ameimiliki irada yake iliyo thabiti na amemiliki nafsi yenye kutoteteleka. Wakati ambapo umma utamiliki watu pamoja na vijana wa namna hi basi hapo utaweza kuwa na matumaini ya kuwa na mustakbali mwema.
Riwaya na hadithi tukufu zilizopokewa katika mafunzo matukufu ya Qur'ani zimeelezea kwamba barobaro anayo sifa tukufu ya kuyapa nyongo mambo yenye ghururi na ya haramu kwa kutubu, kwani toba inadhihirisha kujihifadhi kwake na kulingana kwake. Mtume Mtukufu amesema: "Toba ni nzuri, na kwa barobaro ni nzuri zaidi."
Pia imepokewa kwake kuwa amesema: "Hakuna kitu kizuri kinachopendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko kumwona barobaro mwenye kutubu."
Ni kwa nini kitendo hiki kinamfurahisha Mwenyezi Mungu? Sababu ni kwamba barobaro anapojiondoa kwenye maasi na kuyadhibiti matamanio yake huwa amefanya ukinzani mkubwa dhidi ya nafsi yake, vilevile huwa anailelea nafsi yake juu ya misingi ya kupania, kukakamia na kushikamana na imani yake.
Tunapoidurusu historia ya viongozi wakubwa wa historia ya binadamu, tunakuta kwamba aghlabu yao walikuwa na jitihada ya hali ya juu sana wakati wa ujana wao katika kuzijenga nafsi zao na kuzielekeza kwenye maongozi matukufu yenye utu na ukamilifu. Na sababu ni kwamba wao walishikamana na mkondo wa matukufu na kulazimiana nayo, na wakakataa kupomoka kwenye lindi Ia matamanio na upotevu wenye kutenganisha na haki, pamoja na kwamba kulikuweko hali zenye kusaidia kuwavuta kwenye matamanio na kuzama zaidi kwenye mambo ya ufisadi.
Hebu tujionee baadhi ya kumbukumbu za maisha ya baadhi ya viongozi wakuu ambao wamefaidika kwa kuziviza irada zao katika wakati wa ujana wao, wakazipa nguvu nafsi zao kwa kukakamia kujiepusha na shahawa za nafsi. Kutokana na kufuata njia hii, walizipa nafsi zao nafasi ya kwanza ya kuyavaa matukufu na kuvikwea vilele vya matukufu na ukamilifu.

  1. Hebu tuitazame historia ya Nabii wa Mwenyezi Mungu, Yusuf bin Yaakub AS akiwa ameyakosa malezi ya wazazi wake pamoja na huruma yao tokea udogoni mwake baada ya kumpoteza mama yake, ndugu zake walimlia njama na kumtupa kisimani, kisha akanunuliwa na mmoja wa misafara ya Misri kwa thamani ya chini ya dirhamu chache.

  2. Tazama ndugu msomaji, majaaliwa yalitaka aishi katika zama zake za ubarobaro ndani mwa nyumba ya Mfalme wa Misri pamoja na mkewe Zulaikha ambaye alivutwa vilivyo na uzuri wa Nabii Yusuf AS uliojulikana na uliokuwa ukipigiwa mfano. Ashiki ya kumpenda Yusuf ikavama moyoni mwa Zulaikha, na nyumba walimokuwa wakiishi haikuwa na yeyote mwenye kutia zahama, na hali haikuwa na pingamizi yoyote ya kuzuia kutekeleza hila za kishetani.
    Hebu sawirisha ewe kijana uliye barobaro, kuwa wewe umeingia kwenye mtego wa Nabli Yusuf AS. Pia chukulia kuwa uko katika mazingira yanayosaidia kupotoka, Je, ungefanya nini? Na wajibu wako ungekuwa ni nini katika hali kama hii?
    Naam, ukweli ni kwamba wengi wa barobaro wetu wa sasa, mara nyingi wanatatizwa na ghururi zilezile ambazo zilimtatiza huyu barobaro mtukufu Yusuf, vilevile wanaishi katika mazingara sampuli ileile aliyoishi.
    Kwa hivyo, ni juu ya vijana wetu kumfanya Nabii Yusuf AS kuwa ni kiongozi wao na kugizo chao, wamwige katika kupambana kwake na ghururi kama zile katika kukabiliana kwake na hali kama zile. Hebu tutazame msimamo wake ulikuwa namna gani?
    Qur'ani Tukufu yatusimulia kwa ufasaha mkubwa ikitumia njia yake ya kimbinguni. Yatutolea baadhi ya visa vinavyoelezea baadhi ya ile mikasa hatari aliyoipata Nabii Yusuf AS katika nyumba ya Mfalme wa Misri, pamoja na tukio Ia kurukiwa na Zulaikha. Mwenyezi Mungu asema:
    "Na akasema yule aliyemnunua huko Misri kumwambia mkewe: 'Mweke pahali pazuri huenda akatufaa au tukamfanya mwana. 'Na hivi ndivyo tulivyommakinisha Yusuf katika ardhi (nchi,) ili tumfundishe taawili (ufafanuzi) za hadithi na Mwenyezi Mungu ni Mshindi juu ya jambo Lake lakini watu wengi hawajui. Na alipofikia ukamilifu wake tukampa hukumu na elimu na vivi hivi huwalipa wonaofanya wema. Na akamtaka [Yusuf kutenda haramu] yule [Zulaikha] ambaye yeye yuko nyumbani kwake nafsi yake, na akafunga milango [ili asikimbie] na akasema: 'Ni toyari njoo [nimejitayarisho kwa ajili yako].' Akasema [Yusuf]: 'Namwogopa Mwenyezi Mungu, Yeye ni Mlezi wangu, ameyafanya mazuri makao yangu. Hakika madhalimu hawafuzu.' " (12:21-23)
    Qur'ani inaendelea kuyafafanua baadhi ya maelezo ya kisa chenyewe kutokana na umuhimu wake hadi pale ilipomdondoa Zulaikha akisema:
    Hakika nilimtaka nafsi yake akajizuia (akakataa) na ikiwa hatafanya ninayomwamuru, atafungwa na atakuwa katika wanyonge.' Akasema [Yusuf]: 'Mola wangu, jela ni boro zaidi kwangu kuliko yale wonayoniita kuyafanya, na ikiwa hutaniepusha na vitimbi vyao, nitapondokea kwao na nitakuwa miongoni mwa wajinga.' Basi Mola wake akamjibu, akamwepushia vitimbi vyao; hakika Yeye ni Mwenye kusikia na ni Mjuzi."(12:32-34)
    Vivi hivi Yusuf alimwomba Mwenyezi Mungu amsaidie katika kupambana na ghururi za matamanio na hali za upotofu. Naye Mwenyezi Mungu akayajibu maombi yake, na Nabii Yusuf akazishinda zile hali zote za uharibifu na ufisadi ingawa alistahamilia maovu na kwa muda mrefu alibaki jela kwa azma, nia thabiti na nafsi yenye ushujaa. Na hivi ndivyo inavyotakikana kijana mwema awe.

  3. Kuna kisa kingine chenye kuvutia na kustaajabisha kama kinachoelezwa katika historia. Kisa chenyewe kinamhusu Sayyid Mir Damad, aliyekuwa mwanachuoni mashuhuri sana nchini Iran.

  4. Yaelezewa kwamba Sayyid huyu alifikiwa na kisa hiki wakati akiwa kijana mbichi mwanzo wa kubalehe kwake, naye alikuwa ni mwanafunzi katika madrasa moja ya kidini katika jiji Ia Tehran. Katika usiku mmoja wakati binti wa Shah wa Iran katika zama hizo alipokuwa akitembea mitaani pamoja na vijakazi na watumishi wake, kwa ghafla kukanyesha mvua kubwa na kukavuma upepo mkali na kila mmoja miongoni mwa watumishi wa binti wa Shah akakimbia kutafuta mahali pa kujificha kibinafsi. Binti wa Shah akabakia peke yake mitaani katika lile janga Ienye kutisha na kuhofisha, ikawa naye hana budi kutafuta pahali pa kujificha. Katika kutazamatazama kwake huku na huko iIi angaa naye apate pahali pa kujificha na kujistiri, akauona mlango wa madrasa uko wazi, akaingia madrasani. Kwa bahati akagonga mlango wa chumba cha huyu Sayyid kijana na akamkuta yuko kando ya moto akijiota ili ajiondoshee baridi aliyokuwa nayo.
    Binti huyu akamwelezea huyu Sayyid kijana kisa chake, kwamba yeye ni msichana aliyepotea njia na anachohitaji ni msaada, pahali pa kulala na kujistiri usiku ule, hadi hali ya anga iwe tulivu na ipambazuke.
    Sayyid aliona hana budi kulijibu ombi lile Ia msichana, hivyo akamkaribisha chumbani mwake, yeye akakaa katika kipembe kimoja na msichana naye akakaa katika kipembe kingine.
    Baada ya kupita muda katika usiku huo, shetani akaanza kucheza mchezo wake mwovu katika hali kama hii, kama ilivyopokewa katika hadithi ikisema: "Mwanamume hakai faragha na mwanamke ila shetani anakuwa wa tatu wao."
    Shetani akawa anamshawishi Sayyid huyo kijana namna ya kuipatiliza hii fursa na kutenda haramu kwamba mambo yote yako sawa kwa kila njia, mlango umefungwa, wala msichana hana njia yoyote na kujikinga au kujitetea.
    Lakini vipi itakuwa? Kwani Sayyid huyo alikuwa ni kijana mwema na mwongofu, anayetambua hila na vitimbi vya Shetani. Akawa anafikiria njia ya kujiepusha kutokana na makucha haya ya shahawa na mtego huu wa Shetani. Mwishowe akafikia kwenye uamuzi mgumu. Akaamua kuitumia njia hii kwa ajili ya kupambana na shahawa zake na kuutatua wasiwasi wa shetani. Uamuzi wenyewe ukawa ni kuweka kidole chake juu ya kaa Ia moto, hadi ashughulishwe na uchungu wa kuchomeka ili asifikirie mambo ya haramu. Naam, aliendelea kujichoma hivihivi usiku kucha, huku akistahmilia uchungu na maumivu na huku akiihutubia nafsi yake: "Onja moto wa dunia ili uuogope moto wa Akhera!"

  5. Je, ndugu! Vijana wamewahi kukisikia kisa cha lbn Siriin ambaye alikuwa mwanachuoni mkubwa wa elimu ya nafsi na aliyejulikana kwa kufasiri ndoto?
Katika wakati wa ubarobaro wake Ibn Siriin alikuwa mwenye umbo jema, kiwiliwili kizuri, mwenye uso mwangavu na uzuri wa kitabia wenye kuvutia. Alikuwa akifanya kazi kwa mfanya biashara mmoja wa nguo. Siku moja alifika mwanamke dukani kununua vitambaa, alipomaliza kununua mahitaji yake, akamtaka yule mfanya biashara amtume mfanyakazi wake Ibn Siriin ili ambebee mizigo yake aliyonunua hadi nyumbani kwake, kisha ampe ujira. Ibn Siriin akabeba mizigo na kuandamana naye hadi nyumbani, walipoingia nyumbani mwanamke huyo akafunga milango, kisha akamtaka afanye naye kitendo cha haramu, lakini yeye akakataa. Mwanamke alipoona amekataliwa akazidi kutumia hila za kumlazimisha zaidi. Mwisho Ibn Siriin alijiona kuwa ametumbukia mtegoni, na hapana budi kufikiria njia ya kujisalimisha kutokana na mtego huo Alipoigundua hila yenyewe alimwomba huyo mwanamke amruhusu aende chooni kujisaidia. Mwanamke akamruhusu kufanya hivyo, naye alipoingia chooni tu alijipaka mavi mwili mzima, kisha akamtokea mwanamke yule akiwa katika hali kama hii ya kunuka. Mwanamke alipomwona katika hali kama ile, akamkimbia na kumfukuza nyumbani. Na kutokana na hila kama hii lbn Siriin alijiokoa kutoka mtego huu wa matamanio yaliyo na ghururi.
Wajibu wa Vijana katika Jamii
Vipawa vingi vya binadamu huchimbuka katika wakati huu wa ujana. Huwa na ukunjufu wa wakati na nafsi. Vilevile huwa anamiliki nguvu, uwezo na nishati. Hivi vyote vinampa nafasi nzuri na kumshajiisha kuwa na wadhifa maalum katika jamii.
Hapo mbeleni tuliwahi kuelezea juu ya matakwa ya kijana yenye kiwi ya kutaka kutekelezwa, na kupenda kwake kushiriki katika nyadhifa mbalimbali ili ahisi kwamba yuko huru na awathibitishie wengine uwezo wake na uume wake baada ya kuwa alikuwa mdogo akiishi katika hali ya kuwanyenyekea wengine na kupondokea kwenye matakwa yao. Baada ya kuwa alikuwa akitendewa kama mtoto mdogo, sasa ataka atendewe na jamii kama mtu mkubwa, mwenye heshima yake kamili na mwenye matakwa na irada.
Lau twampa nafasi kijana na kumuacha kutekeleza nyadhifa na wajibu anazoziweza katika jamii, na tukamwelekeza kufanya mambo mema Yenye faida na kumsaidia kuujenga utu wake na kuvikuza vipawa vyake, hakika tutakuwa tumefanya wema kwa kuyajua na kuya pambanua yale yanayoweza kumdanganya katika wakati wa ubarobaro. Na ikiwa hatutashughulika na masiala haya na ikawa hatutampa nafasi barobaro kutoa maoni yake na kutekeleza matakwa yake katika nyadhifa za kijamii kupitia maongozi mema, basi natija itakuwa moja kati ya mambo mawili:
Ima vipawa vya barobaro vitafifia, na vitazimika au vitakufa na matumaini yake yatazikika, au atajiingiza katika kutekeleza mambo yaliyopotoka na kufanya mambo maovu ya ufisadi. Na huu ndio mushkili unaoutatiza umma wetu wa Kiislamu.
Jamli nyingi hazijajua vipi zishirikiane na vijana wao katika upande huu. Wazee wengi pamoja na viongozi wale wanaoyatawalia mambo ya wananchi na kushikilia hatamu za uongozi, aghlabu yao hawako tayari kuwapa vijana wao fursa ya kutumia ujuzi wao na vipawa vyao, hawawapi nafasi yoyote ya kusimamia jambo lolote la kijamii, na hawawaamini, bali huwazingatia kuwa ni watoto wasiojua kitu na walio dhaifu.
Kutokana na sababu hii vijana wetu hukua huku wakiwa na juhudi chache sana na maarifa yao huwa ni ya daraja Ia chini. Hivyo, hupotoka na kuiacha njia ya utukufu yenye utengevu, hasa wanapochukuliwa na makundi mengine ya upotevu na kupewa nyanja za kuziamini nafsi zao na kupewa nyadhifa za kujishughulisha na mambo muhimu yaliyo hatari.
Kitabia, utamwona kijana akivutika kwa urahisi na kujiingiza katika lile kundi ambalo linashughulikia vyema na kumthamini kama mtu mwenye nguvu. Na utamwona mara moja anawaacha wale watu ambao wanaoshughulikiana naye kama mtoto mdogo au kijana dhaifu.
Tunasikitishwa sana kuona ya kwamba jamii yetu hadi sasa haijaacha kuwapima watu na kuwapa kima (hadhi na heshima) kupitia kipimo cha umri. Imekuwa kwamba kabla kijana hajakata masafa marefu ya umri, basi jamii ya watu wakubwa hawamwangalii kwa jicho Ia uaminifu na heshima, wala hawampi nafasi ya kutaharaki au kuwa na nishati yoyote.
Mtukufu Mtume ameitangaza wazi rai ya dini ya Kiislamu na akaelezea waziwazi juu ya kukataa kwake kipimo cha umri na miaka, na akafafanua kwamba kipimo cha pekee kilicho sahihi ni kipimo cha ujuzi na matendo, na kwamba kijana mwenye ujuzi na matendo anayestahili na ni bora zaidi na anayo haki ya kutangulizwa kuliko mwingine yeyote.
Mtume Mtukufu alimtawalisha Ittaab bin Usaid mjini Makka, juu ya kuwa umri wake wakati huo ulikuwa ni miaka Ishirini na moja. Akamwamuru kusalisha sala ya jamaa na kusimamia shughuli nyinginezo kwa niaba ya Mtume Mtukufu. Kijana huyo alikuwa ni amiri wa kwanza kusalisha jamaa mjini Makka baada ya kukombolewa mji huo. Mtume Mtukufu alimwambia: "Ewe Ittaab! Unajua nimekutanguliza kwa watu gani? Nimekutanguliza na kukufanya mwakilishi wangu kwa watu (waja) wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na lau ningekuwa namjua aliye mbora zaidi kukushinda wewe ningemteua."
Baadhi ya wakaazi wa Makka walipopinga uteuzi huo, Mtume Mtukufu alisema: "Mtu asihoji kwa hoja ya udogo wa umri wake, kwani ukubwa si ubora, bali ubora ndio ukubwa."

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget