Hekima inasimama kama maarifa au elimu inayofungana na uwezo wa kuona au kupambana na uoni finyu wa shetani na wanafunzi wake ambao hekima kwao wao ni kuwa mabakhili katika matumizi ya mali zao na siku zote kuwa waroho wa kupata utajiri zaidi na zaidi pasi na kujali halali au haramu.
Watu wenye hekima kwao wao ni kutumia mali yao katika mambo ya heri baada ya kutumia mali hiyo kwa mambo muhimu na ya lazima kwa watu wao wa karibu. Kwa maneno mengine watu hawa hutoa ile ziada inayobaki baada ya matumizi ya lazima kwa wale wanaowategemea kimaisha. Maisha kwao hayamaliziki na kumalizika kwa dunia bali haya ni sehemu ndogo tu ya maisha ambayo binadamu atayaishi – dunia na akhera. Siku zote huchukua maisha ya dunia kama nyenzo ya maisha yajayo ya akhera ambayo ndiyo yanayopaswa kufanyiwa kazi kwani ni bora na ya kudumu.
Aya ya 270
Na chochote mtoacho au nadhiri muwekezo basi Allah anajua. Na madhalimu hawatakuwa na wasaidizi.
Tofauti na binadamu ambaye huhukumu mambo kwa dhahiri yake, Allah Yeye anaangalia nyuma ya kauli au tendo la kila mtu. Binadamu anatoa mali yake kwa nia zinazotofautiana: Anaweza kutoa mali kwa ajili ya kupata radhi za Allah, anaweza kutoa mali kwa kutaka utukufu, umaarufu au kupata mali zaidi kwa njia nyingine n.k. Kwa hivyo Allah atamlipa kila mtu kwa haangalii sura ya mtu au ya kitu bali anaangalia ndni ya nyoyo za wale wanaotenda.
Hali bado ni hiyo hiyo kwa upande wa nadhiri. Nadhiri ni namna fulani ya ahadi ambayo hutolewa au kuwekwa na mtu kwa Allah au miungu wengine kinyume na Allah, watukufu, masharifu, n.k kufanya jambo au kutoa kitu iwapo jambo lake fulani limetokea au kufanikishwa.
Nadhiri ni kitendo cha ibada na iwapo itawekwa kwa yeyote asiye Allah basi hiyo itakuwa ni shirk ambayo itastahili adhabu kali iwapo muhusika atafariki kabla ya kutubia. Ushahidi wa nadhiri kuwa ni ibada unapatikana katika aya ifuatayo:
Kisha (wakiwa hapo Makka) wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na waizunguke nyumba ya kale (Al-Ka’abah). (22:29)
Nadhiri ambayo imetolewa au kuwekwa kwa Allah pasipo na ushirikina basi ni lazima itekelezwe kwani hiyo ni ahadi anayoitoa mtu kwa Mola wake. Nadhiri ambazo zinatolewa kwenye mambo ya haramu hizi haziruhusiwi kutekelezwa na ni dhambi iwapo mtu atazitenda.
Hivyo nadhiri inayotakiwa kutekelezwa ni ile iliyotolewa kwa Allah pekee. Ziko aina nyingine za nadhiri ambazo Allah amezikataza kupitia Mtume wake kama anavyoelezea marehemu Sheikh Abdallah Saleh Farsy.
"Hii inaitwa Nadhrul Mujaazaa" ya kumlipa Mungu kwa kitendo alichokifanya. Unasema akinifanyia langu hili na mimi lake nitamfanyia na kama hakunifanyia na mimi simfanyii".
Basi Mtume kaikataza nadhiri hii na akasema kuwa nadhiri hii haileti kheri ial ni sababu ya bakhili kutoa ambacho asingetoa ila kwa kuwa yey enaye kapewa...
Nadhiri inayopendwa na sharia kuwa Mwenyezi Mungu analolitaka ukafanya jambo la kheri kwa kumshukuru neema hiyo aliyokuteremshia, sio kuagana naye mbele ukinifanyia nitakufanyia.
Ndani ya Qur’an tunapata mfano mmoja wa nadhiri nzuri ambayo haikuwa na sharti la nipe nikupe. Nadhiri hii tunaambiwa ilikuwa ni ya mke wa mzee Imrani:
(Kumbukeni) aliposema mke wa Imrani (baba yake Maryamu) "Mola wangu ! Nimeweka nadhiri kwkao iliyomo tumboni mwangu kuwa wakfu (wa kutumikia dini yako) basi nikubalie. Bila shaka Wewe ndiye usikiaye na ujuaye".
Basi alimpomzaa alisema: "Mola wangu! Nimemzaa mwanamke... Na mwanaume (niliyetaraji) si sawa na mwanamke (niliyemzaa). Na nimempa jina Maryamu, nami namkinga kwako, yeye ni kizazi chake (uwalinde) na shetani aliyetengwa na rehema zako". (3:35-36)
No comments:
Post a Comment