Thursday, April 5, 2012

Wagombea Urais: Sarkozy anawakamata Waislamu ili kuimarisha kampeni yake

Wapinzani wa Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy katika uchaguzi ujao wa Rais nchini humo wanamlaumu kiongozi huyo kwamba anatekeleza operesheni ya kuwakamata ovyo wanaharakati wa Kiislamu kama sehemu ya kampeni ya kujipigia debe kwa ajili ya uchaguzi huo zikiwa zimesalia siku 18 tu kabla ya kufanyika. 

Mgombea wa chama cha mrengo wa kati katika uchaguzi wa Rais wa Ufaransa Francois Bayrou amesema suala hilo la kuwatia nguvuni wanaharakati wa Kiislamu halipaswi kutumiwa kama sehemu ya kampeni za uchaguzi ujao wa Rais. Bayrou ameilaumu serikali ya Sarkozy kwa kutumia suala hilo katika kampeni za uchaguzi. 
Mgombea mwingine wa kiti cha Rais wa Ufaransa Francois Hollande ambaye ndiye anayeongoza katika uchunguzi wa maoni, pia amemlaumu Rais Sarkozy kwa kutumia vibaya suala la kuwatia nguvuni wanaharakati wa Kiislamu nchini Ufaransa katika kampeni za uchaguzi. Amesema Nicolas Sarkozy anatumia kamatakamata hiyo kwa malengo ya kisiasa na kwa ajili ya kampeni za uchaguzi wa Rais. 
Jana polisi ya Ufaransa iliendeleza operesheni ya kuwakamata ovyo Waislamu kwa kuwatia nguvuni watu 10 ambao inadai ni Waislamu wenye misimamo mikali baada ya kuvamia makazi yao katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. 
Operesheni hiyo ya kuwatia nguvuni wanaharakati wa Kiislamu nchini Ufaransa ambayo imezidisha kwa kiasi fulani umashuhuri wa Sarkozy katika kampeni za uchaguzi ujao, inaandamana na kuzuiwa wanazuoni wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali kuingia nchini Ufaransa.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget