Wednesday, April 4, 2012

Mazikoni si Matembezini


Kuhudhuria maziko na kuona jeneza hapa Uingereza ni jambo la nadra au kama wengine wanaliita ni jambo tunu. Ni mara chache kupata nafasi ya kwenda mazikoni kama ilivyo kawaida nyumbani tulipotoka.

 Anapofariki mtu haingii katika akili zetu kwamba labda mimi ndie nitakaefuatia kwani hudhani bado ni mapema mno kufariki na bado tunao wakati wa kufanya mengi katika maisha yetu. Moja katika mambo ya kuzingatia tunapokwenda mazikoni kuna muislamu mwenzetu amefariki na kutangulia mbele ya haki.

Hii pia ni ujumbe kwamba kifo chetu pia kinakaribia kama anavyosema Allah Subhaanahu Wata’ala katika Qur’aan 
                      كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ثُمَّ إِلَيْنَا تُرْجَعُونَ                      

Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu 
 Jambo muhimu la kukumbuka tukifikishiwa taarifa za kifo cha Muislamu kitu cha kwanza kukifanya ni al Istirjaa nayo ni kusema:   
           
         إِنَّا لِلّهِ وَإِنَّـا إِلَيْهِ رَاجِعونَ     
         
(Innaa lillahi Wainnaa ilayhi Raaji’uun) 
Hakika sisi tunatoka kwa Allah na kwake ndio marejeo yetu 

Hii ni ni alama ya kuikubali qadar- mipango - yake Allah Subhaanahu Wata’ala. 

Kifo kina mafundisho na mazingatio. Mazikoni ndipo tutakapoweza kuyapata mafundisho na mazingatio kwa vitendo hivyo tunahudhuria maziko ikiwa ni wanaume au wanawake, mawazo yetu, fikra zetu, dhana zetu pamoja na mustaqbal wetu ufikirie suala hili la mauti na jinsi sisi wenyewe tulivyojiandaa si vyenginevyo.
Hubahatika tunapohudhuria maziko kukutana na watu ambao hatujaonana nao miaka. Lakini hapo hapo tukumbuke je ni hilo lililotupeleka mazikoni? Jawabu lililotupeleka hapo ni kumsindikiza na kumuaga ndugu yetu aliyetangulia mbele ya haki. Hivyo tukizama kwenye mazungumzo ya kidunia wakati wa maziko kweli tutalipata lengo tulilolikusudia kuacha shughuli zetu, kazi zetu, kusafiri masafa ili kuyawahi maziko ya ndugu yetu muislamu? Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema :

 “Zidisheni kukumbuka kiondoshacho ladha (yaani mauti)”. Attirmidhiy 
Pia mazikoni ni sehemu muhimu ya kumuombea du’aa na maghfira marehemu. Sehemu hii huhudhuriwa na Malaika na kila tuombapo  huitikia “Aamiyn”. Muda wa kumuombea du’aa na maghfira marehemu ni muda wote mpaka anapopelekwa maiti kuzikwa. Je tunaohudhuria mazikoni tunautumia wakati huu kwa kumuombea du’aa na maghfira au kwa mazungumzo ya kidunia ambayo ndani yake hupatikana kusengenya, kusemana, kufitiniana na kusutana? Na hata tukikumbushwa hapo hapo tunarudia tena yale yale ambao si kwa ajili yake tupo hapo kwenye msiba? Na hapo hapo tunasema kwamba kuhudhuria maziko ni tunu? 

دخل رسول الله صلى الله عليه وسلم على أبي سلمة وقد شق بصره فأغمضه ثم قال إن الروح إذا قبض تبعه البصر فضج ناس من أهله فقال لا تدعوا على أنفسكم إلا بخير فإن الملائكة يؤمنون على ما تقولون ثم قال اللهم اغفر لأبي سلمة وارفع درجته في المهديين واخلفه في عقبة في الغابرين واغفر لنا وله يا رب العالمين وأفسح له في قبره ونور له فيه                                                                                                                    Mtume Muhammad Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam alikwenda nyumbani kwa Umm Salamah na kumkuta Abuu Salamah tayari amefariki na macho yake yakiwa wazi. Akayafunga kisha akasema: “hakika macho huifuata roho inapotolewa” Baadhi ya jamaa zake wakaanza kulia kwa sauti kubwa na mayowe. Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akasema: “Msijiombee kwenye nafsi zenu bali muombeeni kheri kwani Malaika huitikia Aamiyn kwa mnayoyasema” Ewe Mola wangu nnakuomba msamehe (madhambi yake) na umpandishe daraja awe pamoja na wale walio karibu na wewe, ishughulikie aila yake muda wote na tusamehe sisi na yeye. Ewe Bwana wa ulimwengu lifanye pana kaburi lake na umfanyie wepesi na umjaalie nuru ndani yake.”     Muslim. 

Sasa katika hali zetu za mazungumzo ya kidunia Malaika pia wataendelea kuitikia Aamiyn; lengo la kuwepo mazikoni liko wapi hapo? Tunasengenya Malaika wanaitikia “Aamiyn”, tunahadithiana mambo ya mipira Malaika wanaitikia “Aamiyn”, Tunafanya utani miongoni mwetu Malaika wanaitikia “Aamiyn”. Allahu Akbar! Hatuna kumuombea maghfira na kumuombea du’aa maiti na tukifanya mara moja tunaona tayari temetekeleza wajibu.  

Moja katika mambo yanayopendeza akifariki muislamu, wale wanaomjua vyema marehemu kuyataja mambo yake mazuri na tabia zake alipokuwa hai. Mazikoni ni sehemu ya kuyasikia mema na mazuri yaliyokuwa yakifanywa na marehemu si kwa lengo la kuyahesabu na kuyachambua bali kwa lengo la kuyajua na kuzingatia. Anasema Anas, Allah amuwie radhi kwamba: Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema:

 “Muislamu yeyote atakaefariki na katika miongoni mwa majirani zake wane wakashuhudia kuwa walimjua marehemu kwamba ni mja mwema, Allah Subhaanahu Wata’ala atasema: “nimeipokea shahada yenu na nitamsamehe kwa yale msiyoyajua (katika amali zake)”  Ahmad na kusahihishwa katika Ahkaamul Janaaiz. 

Sisi tufikapo mazikoni mawazo yetu zaidi ni kujaribu kuangalia nani atakuwa bingwa kwenye maziko haya kama labda kutasomwa khitma au hakutosomwa, Itafanyika Talqin hau haifanyiki, Madihi itasomwa au haisomwi. Hii ndiyo hali halisi ya maziko yetu na ni mwenendo wa hatari tunaoelekea. Tumesahau kwamba pale ni mazikoni si pahala pa ushindani au ubishani, si pahala pa kuonekana nani bingwa na nani pocho, si pahala pa kuonekana nani mahiri katika malumbano. Ni pahala pa kutekeleza taratibu za dini yetu kwa mujibu wa mafundisho ya dini yetu na mwenendo wa Mtume wetu Salla Allahu Alayhi Wasallam.

Ni pahala pa kukithirisha du’aa na maghfira. Amesema Mtume Salla Llahu ‘Alayhi Wasallam:

“Mja yeyote Muislamu atakayemuombea du’aa ndugu yake – Muislamu - kwa ikhlas, basi Malaika husema: ‘Nawe ALLAH akupe kama hayo”     (Muslim)
  
 Du’aa hii humnufaisha maiti na muombaji kwa mujibu wa hadithi hii. Ni fursa nzuri ya kuitumia kuomba kwa Allah Subhaanahu Wata’ala na kwa nini basi muislamu amehudhuria mazikoni anachoka kuomba du’aa? Du’aa inayomsaidia maiti na yeye mwenyewe huchosha kila  ikirudiwa rudiwa? !!  

Mwishowe Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam anatujuulisha ujira tutakaopata kwa kuhudhuria maziko ikiwa tulikwenda kwa nia hiyo huku tuna ikhlaas ndani ya nyoyo zetu na tukizingatia kila jambo linalohusiana na mauti katika hadithi iliyopokewa na Abu Hurayrah,Allah amuwie radhi:

 (من شهد الجنازة حتى يصلي فله قيراط، ومن شهد حتى تدفن كان له قيراطان). قيل:                                            وما القيراطان؟ قال: (مثل الجبلين العظيمين). 


Mtu ambae atashuhudia jeneza mpaka likasaliwa, basi atakuwa na mema kiasi cha Qiiraat na atakaeshuhudia mpaka kuzikwa basi atakuwa na mema kiasi cha Qiiraat mbili. Masahaba waliuliza: Ni zipi hizo Qiiraat mbili? Mtume akasema: Ni mithili ya milima miwili mikubwa”.  Bukhari

Na katika Riwaya iliyopokewa na Muslim kuna ziada:


 وكان بن عمر يصلى عليها ثم ينصرف فلما بلغه حديث أبي هريرة قال لقد ضيعنا  قراريط كثيرة     
                                               
Na alikuwa Ibn ‘Umar akimsalia tu maiti kisha huondoka na ilipomfikia hadithi ya Abu Hurayrah akasema: Tumekwishapoteza Qiiraat nyingi sana

Huu ndio ujira tulioandaliwa ikiwa tutahudhuria maziko si kwa sababu ni tunu tu au nadra au kuweza kukutana na watu tofauti bali kuweza  kumsaidia ndugu yetu aliyetangulia mbele ya haki kwa du’aa na maghfira na kuzingatia sisi wenyewe kuweza kujiandaa na safari hii isiyoepukika.

Abu Ammaar  

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget