Wednesday, April 4, 2012

Mufundisho ya Qur'an juu ya Qadari


Tunafahamu vyema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.) ni mjuzi, Mwenye Hekima na Uwezo usio na kikomo. Pia tunafahamu vyema kuwa Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.) Ndiye Muumbaji wa vyote vilivyomo mbinguni na ardhini na vitakavyokuwemo katika maisha ya Akhera ambayo hatuna shaka nayo. Kwa hiyo, inakubalika akilini mwetu, na ndio hasa ukweli, kuwa, Mwenyezi Mungu (s.w.). Aliye Fundi wa mafundi, ni lazima uumbaji wake nao kabla ya kuanza uwe umetanguliwa na fikra au haja ya kuumba, kisha mpango wa maumbile yote na utaratibu utakaofuatwa na kila kiumbe ili kufikia lengo. kwa maana nyingine, akili zetu zinatulazimisha tuone kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.) kabla ya kuanza kuumba alijua fika yafuatayo:

Kwa nini aumbe - lengo la kuumba kila alichokiumba.
Viumbe vyote atakavyoviumba - aina ya viumbe, na idadi ya kila aina ya kiumbe.
Namna ya kuumbwa kila kiumbe ili kiwe na sifa zitakazo kiwezesha kufikia lengo.
Mahali na wakati wa kutokea kila kiumbe, muda wa kuishi kwake na wakati wa mwisho wa kuwepo kwake.
Kanuni na sharia zitakazo miliki kutokea, kuwepo na kutoweka kwa maumbile yote na sharia zitakazotawala matukio yote.
Aya zifuatazo zinatupa picha juu ya Qadar ya Mwenyezi Mungu (s.w.):
"Na Mwenyezi Mungu Amekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha akakufanyeni wanaume na wanawake. Na mwanamke yeyote hachukui mimba wala hazai ila kwa ilimu yake (Mwenyezi Mungu). Na Mwenye kupewa umri hapewi umri (zaidi) wala hapunguziwi umri wake ila yako katika kitabu (cha Mwenyezi Mungu). Bila shaka haya ni sahali kwa Mwenyezi Mungu" (35:11).
Na hakuna mnyama yeyote (yaani kiumbe chochote) katika ardhi ila riziki yake iko juu ya Mwenyezi Mungu. Na anajua makao yake ya milele na mahali pake pa kupita tu (napo ni hapa duniani). Yote yamo katika kitabu kinachodhihirisha (kila kitu). (11:6).
"Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha andikwa katika kitabu (cha Mwenyezi Mungu) kabla hatujaumba. Kwa yakini hilo ni sahali kwa Mwenyezi Mungu". (57:22).
"Kwa hakika tunakiumba kila kitu kwa kiasi" (54"49).
"Mwenyezi Mungu ambaye ni wake (peke yake) Ufalme wa mbingu na ardhi wala hakuzaa mtoto wala hana mshirika katika ufalme (wake), na ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo (chake)" (25:2).
Aya hizi zinaashiria kuwa mpango mzima wa Mwenyezi Mungu (s.w.) umedhibitiwa katika kitabu chake maalumu.
Utekelezaji wa mpango Mkuu wa Mwenyezi Mungu (s.w.), hauko mikononi mwa yeyote isipokuwa Yeye mwenyewe pekee. Anaweka sharia madhubuti zinazotawala kila kitu hatua ya uumbaji, uondelezaji wa viumbe, na yote yatakayotokea kulingana na lengo alilokusudia.
Sheria zote za maumbile zinazofanya viumbe viendelee kama vilivyo au yatowe matukio mbali mbali kama yanavyotokea ziko katika utaratibu wa utekelezaji na mpango mkuu wa Mwenyezi mungu (s.w.). Yale yote yanayomtokea mwanaadamu nje ya uwezo wake hutokea kulingana na Qadar ya Mwenyezi Mungu (s.w.). Kwa mfano vipaji alivyonavyo mtu, bahati zinazompitia, fursa anazopata katika mambo mbali mbali, mazuri na mabaya yanayomsibu yote yako katika Qadar ya Mwenyezi Mungu (s.w.). 

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget