Ni Miongoni mwa Waislamu Walioisahau Quraan?
Umeshindwa kupata muda wa kuisoma au unaisoma lakini huoni athari yake katika nafsi yako? Kumbuka kauli ya Mtume Salla Llahu ‘Alayhi Wasallam aliposema kama ilivyotajwa katika Quraan Al Furqaan/30
وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا
Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu ! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur'aan ni kitu kilichoachwa
Fuatilia miongozo ifuatayo kwa karibu na InshaAllah utaweza kuwa karibu nayo na Qur’aan iwe karibu kwako.
1 Kabla ya kuikamata jiangalie moyo wako.
Jiulize ndani ya moyo wako kwanini unataka kuisoma. Ni kwa ajili ya kupoteza muda au kwa ajili ya kuzingatia yaliyomo ndani yake? Uko tayari kwa ajili ya amali hii ya kheri? Kumbuka Mtume Salla Llahu ‘Alayhi Wasallam alikwa akijulikana kama Qur’aan inayotembea Hakuwa akiisoma tu bali alikuwa akiishi na Qur’aan kama hadithi maarufu ya Ummul Muuminiina, Bibi Aisha, Allah amuwie radhi aliposema; Tabia yake ilikuwa Qur’aan.
2 Tia udhu kabla ya kuisoma.
Udhu kabla ya kusoma ni maandalizi muhimu ya kisaikolojia kwamba unachotaka kukisoma si kitabu cha kawaida. Unataka kufanya mawasiliano kati yako na Allah Subhaanahu Wata’aala, hivyo itakubidi uwe katika hali ya usafi kimwili na hali ya kuwa tayari kiakili kwa ajili ya mazungumzo ya ana kwa ana kati yako na Allah Subhaanu Wata’aala.
3 Elekea Qiblah .
Kusoma Quraan ni ibada hivyo unapoelekea Qiblah unajenga hisia kwamba jambo unalolifanya ni moja katika amali za kujikurubisha kwa Allah Subhaanahu Wata’aala.
4 Anza kidogo kidogo.
Wengi wetu hupenda kujilazimisha kuisoma Qur’aan kwa muda mrefu wakati muda mwingi tuliitupa. Ni vizuri kuanza mahusiano haya kidogo kidogo kwa kujiwekea muda mdogo kwa kuanzia kila siku kupata nafasi ya kuisoma. Hadi pale tumeshajenga mazoea ndipo wenyewe tutaweza kuongeza muda kwa mujibu wa nafasi zetu InshaAllah.
5 Jifunze maana yake
Unapoisoma Qur’aan, Allah Subhaanahu Wata’aala anazungumza na wewe hivyo ni vizuri ukafahamu nini anachokuambia, anachokuamrisha, anachokukataza, anachokuusia n.k. Hivyo ifahamu maana yake ili unufaike nayo na kuzingatia yaliyokuwemo.Kuna malipo ya ziada kwa wenye kuisoma na kuifahamu maana yake.
5 Soma na uisikilize (ikisomwa)
Tuna muda mwingi wa kuweza kunufaika kwa kuisikiliza Qur’aan ikisomwa pia. Alhamdulillah, maendeleo ya teknolojia yanatuwezesha kuisikiliza Qur’aan kwenye majumba yetu(Redio, Kompyuta, T.V , DVD) kwenye magari, kwenye mp3, i-pod, kwenye simu zetu za mikono n.k. Hivyo kwanza tuhakikishe tunaisoma sisi wenyewe na pia tukipata muda tuwe tunaisikiliza ikisomwa mara kwa mara ili kuimarisha mahusiano yetu na kitabu chake Allah Subhaanahu Wata’aala.
6 Usiitumie visivyo
Quraan ni kitabu chake Allah Subhaanahu Wata’ala ambacho kimeletwa kwetu kuwa ni muongozo wa kuifahamu dini yetu. Kuitumia kwake ni kwa jinsi ya mafundisho na maagizo yaliyokuwa kutoka kwake Allah Subhaanahu Wata’ala pamoja Mtume wetu Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Kuitumia kama ni khitma ni suala ambalo lina utata, kuitumia kama ni milio ya simu za viganjani (ringtones) katika simu zetu za mikono ni haramu, Kuitumia kwa kuwa tuna shida na kama ni kombe ambalo tunakunywa, sivyo Quraan inavyotakiwa kutumika haikuletwa inywewe bali izingatiwe na kutekelezwa.
7 Omba du’aa
Jitahidi kurudi kwake Allah Subhaanah Wata’aala akuongoze na kukuongoa katika kukisoma kitabu chake, kukifahamu na kuyatekeleza aliyokuagiza na kuyaacha aliyokukataza. Kuomba kwako msaada kwa Allah Subhaanah Wata’aala ni moja katika silaha utakazopaswa kuzitegemea katika kuifanya kazi hii Inshaallah.
8 Usivunjike moyo
Quraan ina tabia moja pekee ukiisahau nayo inakusahau .Hivyo usichoke katika kujikumbusha kuisoma na wala usikate tamaa kwa kutoijua. Tafuta mwalimu akusaidie (C.D, Internet, DVD ) kama kupiga goti na kusoma kwa mwalimu itakuwa vigumu.Kumbuka shetani amesimama kati yako na Qur’aan na hujaribu kukusahaulisha na kukuvunja moyo katika amali hii adhimu.(Kuna programu ya moja kwa moja hewani – live programme ya kujifunza Quraan kwa lugha ya Kiswahili kwenye tovuti yawww.alnoorcet.co.uk) Faidika nayo wakati uko nyumbani.
Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’aala atuepushe na wale aliowataja katika Quraan Muhammad/24
أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَى قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا
Je! Hawaizingatii hii Qur'aan? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli
No comments:
Post a Comment