Utangulizi
Siku ile alipofukuzwa Peponi na kutolewa katika rehma ya Mwenyezi Mungu, Ibilisi aliapa kuwa atazifisidi ibada za wanadamu na kuwakalia juu ya kila njia iliyonyoka.
Mwenyezi Mungu Anasema:
قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ
“Akasema (Ibilisi); ‘Kwa kuwa umenihukumia upotofu (upotevu) basi nitawakalia (waja Wako) katika njia Yako iliyonyoka (ili niwapoteze).”
Al Aaraf – 16
Ibilisi hawaandami waliokwishapotoka, lakini moyo wake unaungulika kila anapowaona walio juu ya njia iliyonyoka wakiswali na kufanya ibada zao sawa kama walivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.
Ili kuzifisidi ibada zao, Ibilisi hutumia hila nyingi zikiwemo:-
1. Kuwatia wasi wasi.
1. Kuwafanya wahisi tabu au dhiki wanapoanza kufanya ibada.
2. Kuwapambia ibada za uzushi na kuwafanya waongeze au wapunguze.
Talbis Iblis
Katika kitabu chake kiitwacho ‘Talbis Iblis’ (Upambaji wa Ibilisi), mwanachuoni maarufu Sheikhul Islam Ibni Taymiyah anasema:
“Juwa ya kwamba mlango mkubwa anaopitia Iblisi katika kuwaharibia Waislam ibada zao ni mlango wa ‘ujinga katika dini’. Iblisi huwaingilia watu kwa kupenya kupitia mlango huo kwa raha zake huku akiwa amestarehe kabisa. Kwani Ibilisi keshawaharibia wengi miongoni mwa wafanyao ibada kwa ajili ya kutokujuwa kwao namna ya kumuabudu Mola wao kama anavyotaka kuabudiwa. Ama wale wenye kufahamu, Ibilisi huwaingilia kwa kuibia ibia tu.”
Mmoja katika maulamaa wakubwa aitwae Matraf bin Abdullah amesema:
“Fadhila ya elimu ni kubwa kupita fadhila ya ibada”.
Na hii ni kwa sababu elimu ni nuru inayomuongoza mja kuijuwa njia sahihi ya kumuabudu Mola wake bila kupunguza wala kuvuka mipaka. Na Mwenyezi Mungu amekwisha tuelimisha kupitia kwa Mtume wake (Swalla Llahu alayhi wa sallam), namna gani anatutaka tumuabudu.
Mwenyezi Mungu Anasema:
ثُمَّ جَعَلْنَاكَ عَلَى شَرِيعَةٍ مِّنَ الامْرِ فَاتَّبِعْهَا وَلا تَتَّبِعْ أَهْوَاء الَّذِينَ لا يَعْلَمُونَ
“Kisha tumekuweka juu ya Sharia ya amri yetu, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wale wasiojua (kitu).”
Al Jathiya – 18
Ibilisi pia humfisidia mtu ibada zake kwa kumtia wasi wasi akiwa ndani ya ibada na kumfanya ahisi kama kwamba hajaifanya vizuri, hajaikamilisha, ina kasoro, udhu wake haukutimia nk. Na kutokana na hayo humfanya aongeze katika Swala au katika udhu, akidhani kuwa hiyo ndiyo sahihi inayomridhisha Mola wake, bila kuelewa kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).
Waliokula hasara katika vitendo vyao
Ibada yoyote isiyokuwa na amri ya Mwenyezi Mungu au ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) haifai na haina uzito wowote juu ya mezani.
Mwenyezi Mungu Anasema:
قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُمْ بِالأخْسَرِينَ أَعْمَالا. الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا.
“Sema; ‘Je! Tukujulisheni wenye hasara katika vitendo (vyao)?. Hao ambao bidii zao (hapa duniani) zimepotea bure katika maisha ya dunia, nao wanafikiri kwamba wanafanya amali njema !”
Al Kahf – 103 – 104
Katika kuzifasiri aya hizi, anasema Ibni Kathiyr kuwa; Aliy bin Abi Talib (Radhiya Llahu anhu) amesema:
“Aya hii inamsibu kila mwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu kinyume na mafundisho ya Mtume wake (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na huyo anakuwa mbali na njia inayomridhisha Mwenyezi Mungu, akidhani kuwa amali yake hiyo inakubaliwa, wakati ukweli ni kuwa anafanya makosa, na amali zake hizo zinapotea bure.”
Mwenyezi Mungu pia Anasema:
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ
“Sema; ‘Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni; (hapo) Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakughufirieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira (na) Mwenye rehema”.
Aali Imran – 31
Kuvuka mipaka
Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala Anasema:
يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لاَ تَغْلُواْ فِي دِينِكُمْ وَلاَ تَقُولُواْ عَلَى اللّهِ إِلاَّ الْحَقِّ
“Enyi watu wa kitabu msipindukie mipaka katika dini yenu wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila yaliyo kweli”.
An Nisaa – 171
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametukataza kuvuka mipaka katika ibada na kuifanya iwe nzito, kwani yeye (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ameletwa ili kutuwepesishia na si kuyafanyia mambo kuwa magumu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Mumeletwa ili muwepesishe na hamkuletwa kuyafanya mambo yakawa magumu”
Bukhari – Attirmidhy – Al Bayhaqi – Annasaiy – Imam Ahmad
Na katika hadithi iliyopokelewa na Imam Ahmad na Annasai, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Msipindukie mipaka katika dini kwani kilichowaangamiza waliokuja kabla yenu ni kupindukia mipaka katika dini”.
Dalili juu ya ubaya wa kuzusha au kupindukia mipaka katika ibada imo katika hadithi ifuatayo iliyopokelewa na Bukhari na Muslim na kusimuliwa na Anas (Radhiya Llahu anhu) inayosema:
“Watu watatu walikwenda katika kila nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na kuwauliza wakeze (wakitaka kujuwa) namna gani Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akifanya ibada zake, na baada ya kujulishwa, mmoja wao akasema:
“Sisi wapi na Mtume wapi. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amekwisha samehewa madhambi yake yote yaliyotangulia na yanayokuja. Ama mimi nitakuwa nikiswali usiku kucha wala sitolala”.
Mwengine akasema:
“Na mimi nitafunga siku zote na wala sitokula mchana tena”.
Wa tatu akasema:
“Ama mimi sitofunga ndoa kabisa (ili niweze kufanya ibada zangu vizuri).”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliporudi na kuhadithiwa, alipanda juu ya membari akasema:
“Nimesikia kuwa watu wanasema hivi na vile. Ama yule anayemjuwa Mwenyezi Mungu zaidi na kumuogopa zaidi kuliko wote ni mimi. Lakini mimi ninafunga na ninakula. ninaamka usiku kuswali na (pia) ninalala, na ninaoa wanawake. Kwa hivyo yeyote atakayekwenda kinyume na mafundisho yangu basi huyo hayuko pamoja nami”.
Hadithi hii inatufundisha umuhimu wa kufuata na ubaya wa kuzusha. Umuhimu wa kusahilisha na ubaya wa kuchupa mipaka katika ibada kwa kisingizio cha kujikurubisha zaidi kwa Mwenyezi Mungu, hata kama nia ni njema. Nia pekee haitoshi ikiwa ndani yake hamna muongozo wa mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), kwa sababu Mwenyezi Mungu haridhiki na ibada yoyote isipokuwa ile tu Aliyoitolea amri Yake.
Wasiwasi katika Udhu
Baadhi ya watu hawaridhiki wanapotawadha kwa kuosha viungo vyao mara tatu kama tulivyofundishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam). Ibilisi anawatia wasiwasi na utawaona wakizidisha idadi ya kuosha kwa kisingizio cha kuondoa wasiwasi, wakati ukweli ni kuwa huko kuongeza kwao ndio wasiwasi wenyewe.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amekataza kuyafanyia israfu maji.
Siku moja alipomuona mmoja katika Sahaba zake (Radhiya Llahu anhu) akitawadha, alimuuliza:
“Kwa nini unafanya israfu katika maji?”
Sahaba (Radhiya Llahu anhu) akauliza:
“Kwani hata katika maji pana israfu?”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamuambia:
“Ndiyo. Hata kama unatawadha penye mto wa maji yanayokwenda.”
Imam Ahmad
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliwahi kutawadha kwa kuosha viungo vyake mara moja moja, aliwahi pia kutawadha kwa kuviosha mara mbili mbili na mara tatu tatu. Kwenda kinyume na hayo ni kupindukia mipaka katika mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).
Mtu mmoja alimuuliza Imam Ahmad bin Hanbal:
“Ninaweza kuongeza zaidi ya mara tatu katika udhu?”
Imam akamjibu:
“La, huwezi. Hafanyi hivyo isipokuwa mwenye maradhi (ya wasi wasi).”
Imepokelea kutoka kwa Abu Daud kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Kutakuwa na watu katika umati wangu wanaopindukia mipaka katika kujitwahirisha na katika kuomba dua”
Na akasema:
“Hakika katika kutia udhu, pana shetani (mwenye kuwatia watu wasiwasi) anayeitwa Al Walahan, kwa hivyo jiepusheni na wasiwasi wa udhu”.
Attirmidhy
Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala Anasema:
إِنَّهُ لاَ يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ
“Yeye (Mwenyezi Mungu) hawapendi wapitao mipaka”.
Al Aaraf - 55
Kwa vile kuzidisha katika udhu wa mwenye wasiwasi ni katika uchupaji wa mipaka, basi huo unaingia katika zile ibada asizozipenda Mwenyezi Mungu.
Anasema Ibni Qudama, katika kitabu chake kiitwacho “Dhammi l Muwaswasiyn”:
“Ukimuuliza mwenye wasi wasi kwa nini unatawadha zaidi ya mara tatu?
Atakujibu: 'Akiba ya maneno, pengine nimekosea au nimepunguza idadi ya kuosha viungo vyangu.'
“Mtu anaweza kuipa sababu anayoitaka,” anaendelea kusema mwanachuoni huyo. “Lakini suali linakuja; “Je! Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) au Sahaba zake (Radhiya Llahu anhum) walikuwa wakifanya hivyo?"
Bila shaka jawabu itakuwa ;’La. Hawakuwa wakifanya hivyo’. Kwa sababu kusema kuwa walikuwa wakifanya hivyo, ni kuwazulia uongo."
Iwapo tutakiri kuwa hawakuwa wakifanya hivyo, basi itatulazimu na sisi kuacha mwenendo huo, kwani kuuendeleza ni kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam)”.
Kuvunjika kwa Udhu
Katika wasiwasi ni pale mtu anapokuwa ndani ya Swala akasikia mingurumo tumboni mwake, akadhani kuwa upepo umekwishamtoka, akaamua kuvunja Swala na kwenda kutawadha kwa dhana tu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametukataza kufanya hivyo aliposema:
“Mmoja wenu anaposikia sauti tumboni mwake akatia shaka, je kimetoka kitu (upepo) au hakijatoka? Basi asivunje Swala isipokuwa kama (ana hakika kuwa) amesikia sauti (ikitoka) au harufu”.
Muslim
Imepokelewa pia kuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kuwa; huwa anahisi kila anaposwali kama kwamba upepo unamtoka. Akajibiwa kuwa asivunje Swala mpaka asikie sauti au harufu.
Bukhari na Muslim
Katika Musnad ya Imam Ahmad na Sunan za Abu Daud, Imeelezwa na Abu Saeed Al Khodary (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Shetani humjia mtu katika Swala yake na kumfanya ahisi kama kwamba ametoa upepo, basi mtu asiivunje Swala yake mpaka asikie sauti au harufu”.
Na katika Sunan ya Abu Daud, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Shetani anapomjia mtu na kumwambia kuwa udhu wako umevunjia”. Basi naye asema (moyoni pake); “Muongo wewe”, isipokuwa pale anaposikia harufu kwa pua yake au sauti kwa sikio lake”.
Katika kitabu chake kiitwacho; “Dhammi l Muwaswasiyn” , anasema Ibni Qudama:
“Kwa ajili ya kuyapiga vita maradhi ya wasi wasi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) anatuamrisha kumkadhibisha shetani, juu ya kuwa kitendo hicho (cha kutoka upepo) kinaweza kuwa kimetokea kweli. Vipi basi mtu anakubali kumfuata shetani pale uongo wake unapokuwa dhahiri, pale anapoambiwa na shetani kuwa; “Hukutawadha vizuri au hukutia nia sawa nk., wakati anajuwa kuwa huo ni wasi wasi wa shetani tu, na kwamba anajaribu kumchezea”.
Kutia Nia
Katika kutia nia ya Swala, shetani hupata upenyo pia wa kuwachezea watu na kuwakosesha thawabu nyingi sana.
Utamuona mtu anafunga Swala kisha anaivunja. Na mwengine huendelea hivyo mpaka Imamu anaporukuu, hapo ndipo huifunga Swala kwa haraka na kurukuu pamoja naye.
Ameweza kuihudhurisha nia kwa haraka pale Imamu aliporukuu, wakati alishindwa kufanya hivyo tokea mwanzo wa Swala.
Hii ni njia moja wapo ya shetani kumkosesha thawabu nyingi kama anglifunga Swala pamoja na Imamu.
Wengine kabla ya kufunga swala utawasikia wakinyanyua sauti zao wakitamka maneno Fulani na kushadidia maneno hayo, kisha husema; “Allahu Akbar”, kisha huivunja Swala na kuanza kutamka tena maneno hayo akidhani kuwa amekosea kuyatamka, na akidhani pia kwamba maneno hayo yamepangwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na kwamba akiyakosea Swala yake inabatilika.
Utamuona akiendelea kukubali kuchezewa na shetani na kumkosesha thawabu nyingi za kujiunga na Imamu mapema.
Ukweli ni kuwa maneno hayo anayotamka, anayodhani kuwa ndiyo nia ya swala, hayajapata kutamkwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), wala na Sahaba zake watukufu (Radhiya Llahu anhum).
Anasema Ibnu l Qayim:
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa anapotaka kuswali husema:
“Allahu Akbar”, kisha hufunga Swala. Hakuwa akisema kitu kabla yake kama vile; “Uswaliy fardha sswalaati l Ishaa….” Au kauli zozote katika zile wanazozitamka watu hivi sasa. Hapana hadithi Sahihi wala hata dhaifu inayotujulisha kuwa kitendo hiki kimetendwa na Sahaba yeyote au Taabi'i au mmojawapo wa maimamu wanaojulikana kwa ucha Mungu wao. Hapana hata mmoja wao aliyewahi kutamka kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo kabla ya kufunga Swala….”
(Kitabu ‘ Al Qaulu l mubiyn fiy akhtaa l musalliyn)
Anasema Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa anapotaka kuswali huanza kwa kusema:
“Allahu Akbar.”
Muslim – 1/357 na 498
Kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu), anasema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipomuona mtu mmoja akikosea katika Swala alimuambia:
“Unapotaka kuswali, tia udhu kisha elekea kibla kisha sema; “Allahu akbar”, kisha soma utakachoweza kusoma katika Qurani”.
Bukhari na Muslim
Ama Abdillahi bin Umar bin Khataab (Radhiya Llahu anhu) alisema:
“Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akianza kuswali kwa kusema “Allahu akbar.”
Bukhari 2/221 na 738
Hizi ni dalili chache katika nyingi zinazotujulisha kuwa kitendo cha kuitamka nia hakikuwepo katika mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na kwa ajili hiyo tusimpe fursa shetani kutuingilia na kutufisidia Swala zetu au kutukosesha thawabu za kujiunga mapema na Imamu kwa kupitia mlango huo.
Imepokelewa kutoka kwa Ibni Aqiyl, kuwa siku moja aliulizwa na mmoja katika watu wenye maradhi haya ya wasiwasi:
“Mimi kila ninapotawadha, huhisi kama kwamba sijatawadha vizuri, na kila ninapofunga Swala huhisi kama sikuifunga vizuri, nifanye nini?”
Ibni Aqiyl akamjibu:
“Wacha kuswali, kwa sababu wewe huna lazima ya kuswali”.
Alipoulizwa kwa nini alijibu hivyo, alisema:
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
‘Haandikiwi dhambi wala thawabu mwendawazimu mpaka awe na akili …”, na mtu aliyetawadha akahisi kuwa bado hajatawadha, kisha akafunga Swala akahisi kuwa bado hajaifunga, huyo akili zake si sawa. Huyo ni mwendawazimu, na mwendawazimu halazimiki kuswali”.
(Talbis Iblis – Ibni Taimia Uk.169)
Na Muhammad Faraj Salem Al Saiy
No comments:
Post a Comment