Israi ni safari ya hapa hapa ardhini, kutoka Msikiti Mtukufu wa Makka mpaka Baytil Maqdis, kule Jerusalem. Na Miiraji ni safari ya mbinguni, kutoka Baitil Maqdis kwenda hadi anga za juu.
Wanazuoni wamehitalifiana juu ya safari mbili hizi. Wanazuoni wengi wamesema kuwa safari zote hizo mbili, Mtume (s.a.w) alizienda kwa roho na kiwili wili chake. Wako wanachuoni wachache waliosema kuwa Israi ndiyo aliyoenda kwa roho na kiwiliwili, lakini Miiraji alikuwa kwa roho tu pasi na kiwiliwili.
Lakini mwanzo wa karne hii, kilichomoza kipote cha watu wanaojinasibu na Uislamu, ambao wanadai kuwa safari zote hizo mbili zilikuwa ni njozi tu, ati hazikuwa safari za hakika.
Katika makala haya ninakusudia kutoa hoja na dalili zenye kuthibitisha kuwa Israi na Miiraji, zote zilikuwa ni kwa roho na kiwiliwili.
Kwanza, ingalikuwa safari hizo ni ndoto, basi makafiri wa Makka, wasingalimkadhibisha Mtume (s.a.w.) alipowaambia kuwa alikwenda safari hizo. Tokea lini mwenye kuota ndoto akapingwa? Usingizini mtu anaweza kuota chochote, hakuna ajabu. Lakini wao walimpinga kwa sababu walistaajabu vipi mtu aweze kutoka Makka kwenda Baitil Maqdis, Palestine na kurejea usiku huo huo, na wakati kulikuwa hakuna vyombo vya kusafiria kwa kasi, kama hivi tulivyo navyo hivi leo.
Ndiyo maana Mutiin bin Addiy akamwambia Mtume (s.a.w.), "Ama mambo yako kabla ya leo, yalikuwa yana afadhali, isipokuwa maneno yako yote kabla ya leo yamepindukia mipaka. Mimi nashuhudia yakuwa wewe ni mwongo. Sisi huchukua mwezi mzima kwenda Baytil Maqdis na mwezi mzima kurudi, wewe unadai umekwenda kwa usiku mmoja tu? Naapa kwa Lata na Uzza kwamba sikusadiki". Kama aliwaelezea habari ya ndoto aliyoiota palikuwa na sababu gani Mutiim bin Adiyy kumwona ni mwongo?
Pili, Mtume Muhammad (s.a.w.) hakudai asilani kuwa yeye mwenyewe ndiye aliyefanya safari hizo, bali ni Mwenyezi Mungu (s.w.) ndiye aliyempeleka. Ilikuwa ni miujiza. Ikiwa tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.) alimnusuru Nabii Ibrahimu (a.s.) asiungue na moto, kwa kuuambia moto uwe baridi na salama kwa Nabii Ibrahimu, na alimwambia Bibi Maryam achukue mimba ya Nabii Isa (s.a.) na akashika mimba hiyo na kumzaa Nabii Isa (s.a.) pasi kuingiliwa na mwanamume, kwanini Mungu huyo huyo ashindwe kumpeleka Mtume Muhammad (s.a.w.) Israi na Miiraji?
Muislamu anayetilia mashaka safari hizi ni kama anayetilia mashaka uwezo wa Mwenyezi Mungu (s.w.). Qur’an tukufu inasema mara kwa mara: Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu", kwa hivyo anayesema kuwa hakumpeleka Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa roho na kiwiliwili ni sawa na kusema Mungu apishe mbali, kuwa kuna baadhi ya mambo Mwenyezi Mungu (s.w.) hayawezi!
Tunaona kuwa aya inayoeleza kisa cha Israi imeanza na neno Subhana, ambalo maana yake ni kumtakasa Mwenyezi Mungu (s.w.) na kila aina ya upungufu. Neno hilo limetumika kuashiria kuwa kama watu watastaajabia juu ya safari hizo, lakini kwa vile aliyeziandaa ni Yeye aliye na uwezo wa kutenda lile linalodhaniwa kuwa haliwezi kutendwa basi kweli safari hizo zilifanyika. Laiti ingalikuwa safari hizo zingalikuwa ni ndoto balagha ya lugha ya Kiarabu isingalikubali kutumika kwa neno hilo.
Tatu, Qur’an tukufu haisemi kuwa Mwenyezi Mungu aliipelekea roho ya mja wake, bali inasema "alimpeleka mja wake" (Bani Israil 17:1). Neno mja hutumika kuonyesha roho pamoja na kiwiliwili na siyo roho peke yake. Pia Mtume (s.a.w.) amesema aliletewa kipando kiitwacho, Buraq, ndicho alichokipanda kwenda Baytil Maqdis na kumrejesha Makka. Kama alikwenda kwa roho, jee, roho inahitaji kipando?
Nne, kile kitendo cha Makureishi cha kumtaka Mtume (s.a.w.) awasifiye jengo la Baytil Maqdis ni ushahidi tosha kuwa Mtume (s.a.w.) alikwenda safari hiyo kwa roho na kiwili wili. Ni vigumu mtu kwenda pahali kwa muda mchache akaweza kuelezea mandhari yote ya eneo hilo pamoja na majengo kwa ufasaha mkubwa. Basi Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa uwezo wake na hekima yake, akauleta ule Msikiti mbele ya macho ya Mtume (s.w.) naye alikuwa akiutazama na kuwaelezea kitu kimoja kimoja kilichokuwapo katika jengo hilo. Wale miongoni mwa Makureishi waliowahi kufika huko, walikuwa wakimsikiliza kwa makini jinsi alivyokuwa akizielezea alama zote bila ya makosa. Wote wakakiri kwamba sifa zote amezipata, lakini wasimsadiki.
Tano, kule kumtaka Mtume Muhammad (s.a.w.) awape habari za misafara yao iliyokuwapo njiani naye akawapa habari hizo kwa ukamilifu ni dalili nyingine kuwa safari ilikuwa kwa kiwiliwili na roho.
Tatizo la wale wanaopinga safari hizo ni kutoangalia na kupima uwezo wa yule mwenye kutenda. Kwa mfano uambiwe kuna mama mmoja amempandisha mwanawe wa mikononi mlima Kilimanjaro, utazikubali habari hizo au utazikataa? Mbona kuna wanawake wengi tu walioupanda mlima huo. Basi kwa nini yule mwenye kitoto kichanga asiweze kumpandisha mwanawe kwa kumfunga katika mbeleko mgongoni mwake? Kitu muhimu cha kutazama. Je! Yule anayedaiwa kutenda kile kitendo ana uwezo wa kutenda kila kitendo au hana! Ungaliambiwa yule mtoto wa mikononi alipanda mlima Kilimanjaro mwenyewe hapo ulikuwa na haki ya kupinga, lakini umeambiwa amepandishwa na mama yake, ambaye ana uwezo huo wa kumpandisha. Basi kama tulivyotangulia kusema Mtume (s.a.w.) hakudai kuwa alifanya safari hizo yeye mwenyewe, isipokuwa Mwenyezi Mungu (s.w) ndiye aliyesema kuwa Yeye ndiye aliyempeleka!
Mimi ninaona safari za Israi na Miiraji zimethibitisha miujiza ya Qur’an tukufu na maneno ya Mtume Muhammad (s.a.w.) juu ya kitabu chake kitukufu Mwenyezi Mungu, "Haitakifikia batili mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye hekima, Ahidimiwaye". (Haa Miym Sajdah 41:42), na kuhusu Mtume Muhammad (s.a.w.), Mwenyezi Mungu (s.w.) anasema, "Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake). Hayakuwa haya (anayosema) ila ni ufunuo uliofunuliwa (kwake). (An-Najm 53:405)
Ukweli huo uliozungumzwa na Qur’an tukufu pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.) karibu karne 14 zilizopita leo umedhihirika. Katika zama hizo kulikuwa hakuna kipando cha kusafiria ardhini isipokuwa wanyama kama punda, farasi na ngamia, na hakuna chombo chochote kilichokuwapo cha kupaa kwenda juu. Ndiyo makafiri wa Makka wakampinga Mtume (s.a.w.), lakini hivi sasa jambo la kutoka sehemu moja ya ardhi na kwenda sehemu nyingine kwa kutumia vyombo kama ndege si ajabu tena. Na hivi vyombo vya leo vinazidiana kwa kasi, lakini hakuna chochote kilichopindukia kasi ya mwanga.
Mtume (s.a.w.) alieleza kuwa ile safari ya ardhini, kutoka Makka mpaka Jerusalemu, alipanda kipando kiitwacho Buraq. Watu walipotaka awaeleweshe kipando hicho kilikuwa cha aina gani aliwaambia alikuwa ni mnyama aliye baina ya farasi na nyumbu. Hivyo ni kwa sababu walikuwa hawaelewi vipando vingine isipokuwa hivyo. Lakini ili kuonyesha mwendo wa kasi wa kipando hicho aliwaambia mnyama huyo alikuwa na mbawa na hatua yake moja ilikuwa ikimalizikia pale linapokomea jicho lako. Inaonyesha mkazo wake aliuweka katika mwendo-kasi wa hicho kipando. Buraq hajawahi kuonekana na watu hapa ardhini, basi Mtume (s.a.w.) aliwaambia kuwa mnyama huyo alitoka mbinguni.
Nafikiri tusibishane juu ya huyo mnyama, lakini tuliangalie zaidi hilo neno Buraq neno hilo huenda likawa limetokana na neno la Kiarabu Barqun ambalo maana yake ni umeme (mwanga). Jee! Haiwezekani kuwa kipando hicho hakuwa mnyama hasa, bali ni chombo fulani ambacho mwendo-kasi wake ulifanana na kasi ya mwanga (light)?
Pili, Mtume (s.a.w.) alisema kuwa Buraq alitokea mbinguni, kwanini basi asingalimpanda mnyama huyo huyo katika safari yake ya kwenda huko mbinguni. Lakini badala yake amesema ameletewa chombo kingine cha kumpeleka huko mbinguni kiitwacho Miiraji. Hiyo Miiraji inatokana na neno la Kiarabu Yaajuju yaani kupanda kwenda juu, Kwa hivyo Miiraji ni chombo cha kwenda anga za juu. Sayansi leo imetuundia vyombo kama roketi ambazo safari zake haziendi ardhini kama ndege, bali zinaenda anga za juu tu, Mtume Muhammad (s.a.w.) hapana shaka alipandishwa chombo aina hiyo! Ingelikuwa ni ngazi kama tunavyoelezwa, nafikiri hadi hii leo ingalikuwa bado hajamaliza vidato vya kumpeleka juu seuze kuteremka! Mtume (s.a.w.) alikuwa akiwaeleza watu kwa mujibu wa fahamu zao na mazingira yao. Hivi leo sisi ndio tuliokuja kupambanukiwa na maneno ya Mtume (s.a.w.). Hakuna tena la ajabu.
Pia, Makureishi walipotaka Mtume (s.a.w.) awasifie ule Msikiti wa Baytil Maqdis ulikuwa vipi Mwenyezi Mungu (s.w) alimletea ule Msikiti mbele ya macho yake. Hiyo haina maana kuwa Mwenyezi Mungu aliuleta ule Msikiti wenyewe bali alimwonyesha Msikiti ule kama vile sisi leo tunavyoiangalia "White House" ya Marekani katika televisheni. Kwa hivyo ilikuwa ikiashiria kuwa kitu kilicho mbali kinaweza kufanywa kionekane sehemu nyingine, nazo ndizo hizi televisheni tulizo nazo.
Mwisho, juzi tu tulionyeshwa jinsi mwana anga mmoja mkongwe wa Marekani, John Glenn akifanyiwa matayarisho ya kwenda katika anga za juu kwa kutumia roketi. Na Mtume (s.a.w.) alisema kabla ya kupelekwa safari hizo alifanyiwa matayarisho na malaika wawili. Amesema walimpasua kifua chake wakamtoa moyo wake wakausafisha. Hiyo ilikuwa ni ishara kuwa mwanaadamu yumkini kufanyiwa upasuaji wa kuuondoa moyo wake kuusafisha na kuurejesha kama ulivyokuwa. Kisha Mtume (s.a.w.) akasema, akashonwa kifua chake wala hapakuonekana dalili ya kushonwa kwake. Leo utaalamu wa "Plastic surgery" umekuja kudhihirisha kuwa hili linawezekana.
Kwa kweli sisi tunaoishi katika hizi zama za sayansi na teknolojia ndiyo tunaoweza kuuthibitisha ukweli wa Israi na Miiraji kuliko hata wale waliokuwa wakiishi zama za Mtume (s.a.w.). Wale waliamini kutokana na nguvu za imani zao, lakini leo sisi yanatuthibitishia yale yaliyosemwa huko nyuma na tunayashuhudia kwa macho yetu. Basi mwenye kutaka kuamini na aamini na yule mwenye kutaka kukufuru basi na akufuru.
Mwandishi: Maalim Bassaleh
No comments:
Post a Comment