Wednesday, April 4, 2012

Umuhimu wa kutaja jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinja


NI muhimu kutaja jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinja mnyama kwa ajili ya kitoweo.
Kutaja jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinja kuna siri nzuri ambayo kila Muislamu inapasa aijue.
Katika Kitabu The Lawful and Prohibited in Islam mwanazuoni Yusuf al Qardawi ametaja sababu kadhaa kuonesha umuhimu wa mchinjaji kujiegemeza kwa Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa sababu hizo ni kuonesha shukrani kwani wanyama nao ni viumbe wa Mwenyezi Mungu na wana roho kama yeye lakini hawanayo fursa hiyo.
Kwanini mwanaadamu awazidi wanyama na kuwatoa roho zao, si kwa sababu nyingine ila kwa idhini ya Muumba wake yeye na wao na ambaye anamiliki kile kilichomo ardhini. Basi kutaja jina la Mola wake hapa ni kuonesha kwamba hafanyi jambo hili kwa sababu ya uadui juu ya viumbe hivi wala kuwa anawaonesha unyonge wao mbele yake, lakini anataka kuonesha kwa jina la Mwenyezi Mungu anachinja na kwa jina lake akiwinda na kwa jina lake anakula.
Umuhimu mwingine wa kutaja jina la Mwenyezi Mungu ni kwenda kinyume na wasio Waislamu.
Siri ya kuchinja kama inavyoonesha ni kutoa roho ya mnyama au ndege kwa upesi bila la ya kuadhibika sana, ndio maana ikashurutishwa itumiwe ala iliyo na makali inayokata mara moja na kutumiwa kwenye koo ambapo huwezesha roho kutoka mara moja. Imekatazwa kutumia vifaa visivyo na makali katika kuchinja kwani kufanya hivyo ni kumuadhibu mnyama. Na kwa hakika havikati sawa sawa bali hukaba koo na kuzuia pumzi ambako ni kumtesa mnyama.
Kwa ajili hii, Mtume (s.a.w.) ameamrisha visu vinolewe sawa sawa kwa kufanya hivyo itakuwa ni kuonesha wema.
Katika hadithi moja Mtume amekaririwa kusema: "Mkichinja chinjeni vyema, na atie makali kisu chake anayetaka kuchinja na amuondoshee adhabu mnyama wake.
Na imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas (r.a.) kuwa mtu alimlaza mbuzi na huku ananowa kisu chake. Akasema Mtume (s.a.w.): "Unataka kumuua mara chungu nzima? Kwanini hukunowa kisu chako kabla ya kumchinja?
Kwa hiyo makusudio hapa ni kuwafanyia wanyama upole na kujaribu kuwapunguzia maumivu kadri itakavyowezekana.
Kwa hiyo Waislamu wanaamrishwa kutaja jina la Mwenyezi Mungu wachinjapo wanyama kwa ajili ya kitoweo.


Iliandikwa na Na Mujahid Mwinyimvua (Gazeti la An-Nuur)

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget