Wednesday, April 4, 2012

Maelekezo ya Jinsi ya Kuutumia Mtandao


Na Sheikh: Hamed Ibn Abdullah El Aly

Imetafsiriwa na Abu Ammaar

Kwanza:

 

Muislamu anapoisikia adhana anatakiwa ainuke na kuhakikisha anaitikia mwito na kutoruhusu jambo lolote limzuie katika kuitika wito wa Allah Subhaanahu Wata’ala. Anaseme Allah Subhaanahu Wata’ala:” Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka”.

 

Hivyo utakaposikia adhana, achana na Mtandao na nenda Msikitini kwa ajili ya kuitikia wito wake Allah Subhaanahu Wata’ala. Kama upo nyumbani (Mwanamke) hakikisha pia unaondoka kwenye Mtandao na kuitika wito.

 

Pili

 

Mtandao ni njia ya mawasiliano ambayo ni kama msumeno. Inapoleta faida huwa ni zawadi nzuri na inapoleta maovu huwa mbaya na haifai. Kwa Muislamu ni kuhakikisha anautumia Mtandao kwa kuangalia upande wake mzuri tu ambao utamsaidia katika dini yake na maisha yake na si kuutumia katika maovu ambayo yatamuharibia dini yake na maisha yake.

 

Tatu

 

Ni muhimu kwa watumizi wa Mtandao kuhakikisha wanakinga macho yao kwa kutoangalia yaliyoharamishwa. Hii  ni njia mojawapo ya Shetani kuharibu maadili ya Muislamu kwa kumpandikiza raha za muda mchache kisha kumuachia hisia za majuto na masikitiko ya muda mrefu. Kuangalia mambo ambayo Allah Subhaanahu Wata’ala ameharamisha huondosha nuru kwenye nyoyo na kuleta kiza na uzito kwenye vifua mpaka Muislamu kuwa mzito katika kutekeleza Ibadah. Shetani huuchukua moyo wa mja na kuutawala na kuuchezea kama mtoto mdogo anavyocheza na mpira. Na mwishowe ni kupotoka. 

Nne

Usiuruhusu  Mtandao uchukue muda wako wenye thamani na juhudi zako bila ya faida. Haya hutokea pale unapotembelea tovuti tofauti zisizo na faida yoyote kwa dini na maisha yako. Au kujiunga na magrupu ya mtandaoni na humo kupoteza muda mwingi kuporoja au kubishana kusiko na faida. Ni muda huu ambao ulitakiwa ukae na familia yako, watoto wako, wazazi wako na jamaa zako na pai kwa kazi yako ambayo hukupatia rizki yako na wanaokutegemea.

Tano

Tembelea Tovuti za kiislamu mara kwa mara zinazokupa maarifa na elimu na kuongeza upeo wako katika dini. Jiepushe na tovuti ambazo zinalenga katika kukupotoa kiimani au kimaadili na zinazolenga katika kuleta fitna na malumbano hata katika mambo ya kidini. Malumbano yenye utata na yasiyokuwa na faida hayafai. Pia usijiingize katika mazungumzo na maadui wa kiislamu isipokuwa kama una upeo na elimu ya kutosha kuweza kukabiliana na kazi hii. Tafuta mwenye elimu kuifanya kazi hii.

 Sita

Chukua tahadhari na kujiunga na  tovuti/vikundi vya mazungumzo na porojo (chatting group sites). Huu ni mtego kwa waislamu wanaume na waislamu wanawake kuwaingiza katika mahusiano haramu na mwishowe kuwaacha katika maumivu yatakayoweza kuathiri maisha na imani yao.

Saba

Ni moja kati ya mawili; aidha Mtandao uutawale au ukutawale. Ukiweza kuutawala ndipo utakapoweza kufaidika nao na kujiweka mbali na ubaya wake. Na ukikutawala, macho yako hudanganyika na starehe za raha za muda mchache, pesa zako kuibiwa, muda wako kupotea na kushindwa kutekeleza majukumu yako katika maisha kwa familia na vipenzi vyako. Umetegwa bila ya mwenyewe kujijua. Ni wajibu wako kujitoa katika mtego kabla hujapotoka au mambo yamesharabika ukawa huwezi tena kuachana nao.  

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget