Thursday, April 5, 2012

JIFUNZE UISLAMU


01.          DINI
Kila sikio la mwanadamu aliyewahi kuishi, anayeishi na atakayekuja kuishi katika ulimwengu huu limepata kulisikia, linasikia na litalisikia neno “dini” Neno hili “dini” neno fupi Kabisa, neno lenye herufi nne tu, d+i+n+I ni neon hai au tunaweza kusema ni neno linalobeba dhana hai iishiyo sambamba na mwanadamu. Ni sawasawa mwanadamu analitambua hilo au halitambui au anajitia kutokulitambua, kwani kule kutokuitambua kwake hakuondoshi/hakufuti ukweli kuwa yeye na dini ni washirika pacha katika maisha haya. Kwa hiyo basi neno hilo fupi na jepesi mno kutamka ulimini “dini” lina athari kubwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na ulimwengu wake kwa ujumla. Athari hiyo inaweza ama kuwa nzuri au mbaya kutegemeana na ufahamu/uelewa wa mwanadamu kuelekea dhana hii dini.
01:01- MAANA YA DINI:
Wanadamu kama viumbe waliotofautiana katika maumbile (sura), lugha, rangi, hali za kimaisha, fikra na kadhalika. Wameielewa “dhana dini” kwa maana mbalimbali. Maana hizi ukizingatia kwa fikra za haraka haraka, fikra za kijuu juu zisizochimba na kupenya ndani. Utaona kuwa zinatofautiana, lakini ukweli na hakika ni kwamba zinaona na kuhusiana kwa namna moja au nyingine hii ni kwa sababu zote zinachimbuka kutoka katika chemchem moja ambayo ni akili ya mwanadamu. Sasa basi ukizijumuisha na kuziunganisha pamoja maana hizo, hatimaye utatoka na natija ya mwisho kwamba kumbe dini kama aielewayo mwanadamu ni:
(Mfumo/utaratibu Fulani wa maisha unaofuatwa na jamii Fulani ya wanadamu).
Hili ndilo eleweko la dhana dini kupitia akili, fikra na mawazo ya binadamu. Sasa basi ili kuutambulisha kwa walimwengu mfumo wa maisha aufuatao mwanadamu akaamua kuupa jina mfumo wake huo aliojichagulia na kuufuata. Unaweza kuukuta mfumo huo chini ya majina kama mila/desturi/utamaduni, au ujamaa, ukomunisti, ubepari, kutoamini kuwepo kwa Munguu (Atheism), ushirikina (Polytheism) na kadhalika. Hii yote ni miongoni mwa mifumo hai ya maisha inayofutawa na matabaka Fulani ya watu wanaounda jamii ya wanadamu katika ulimwengu huu.
01:02- HISTORIA YA DINI:
Baada ya kuiangalia kwa mukhtasari dhana na maana ya dini, hebu sasa tujiulize dini imeanzia wapi? Tukiichukulia dini kwa maana ya aina Fulani ya mfumo wa maisha uliochaguliwa na kufuatawa na Jamii Fulani ya wanadamu. Tutagundua kwamba historia ya dini inaenda sambasamba na historia ya kuanza kuwepo kwa mwanadamu katika maisha ya ulimwengu huu. Hili ni dhahiri kwa sababu hakuna mwanadamu aliyepata kuishi, anayeishi au atakayeishi katika ulimwengu huu bila ya kufuata mfumo maalumu wa maisha. Iwe ni mfumo alio na khiyari nao mithili ya hizo mila/desturi, ujamaa, ubepari, ukomunisti na kadhalika. Au ule asio na khiyari nao mithili ya ule utaratibu mzima wa tangu kutungana kwa mimba, kuzaliwa mpaka kufa na yote yahitajikayo ili kuukamilisha utaratibu huu. Kwa mantiki hii basi huu unakuwa ni ushahidi wa kimazingira unaoonyesha kuwa dhana dini imeanza kuishi sambasamba na mwanzo wa kuwepo kwa mwanadamu katika ulimwengu huu.
01:03- KWA NINI DINI? (UMUHIMU WA DINI KATIKA MAISHA YA MWANADAMU)
Ingawa katika ulimwengu huu tuishimo kuna watu wanaoutaka ulimwengu uelewe kuwa mahitaji makuu ya msingi ya mwandamu ni maskani (nyumba), mavazi na chakula. Yaani ili mwanadamu aweze kuishi katika ulimwengu huu ni lazima apate vitu hivi. Ni sawa kwa kiwango Fulani kusema hivi lakini hili halizuii ukweli kwamba mwanadamu anaweza kuishi kwa muda Fulani bila ya vitu hivi vyote. Hata hivyo mwanadamu hana namna ya kuepa kuishi bila ya kufuata dini yeyote japo kwa sehemu ya sekunde. Ukweli huu unatokana na dhana hai kwamba hakuna mwanadamu anayeishi bila ya kufuata mfumo fulani wa maisha. Uwe mfumo huo ni ule uliobuniwa na wanadamu wenyewe kwa ajili ya jamii Fulani (mfumo binadamu). Au ni ule aliochaguliwa mwanadamu na Mungu Muumba wake. Kwa hivyo, tutaona kwamba mwanadamu ni kiumbe mwenye maumbile yanayomlazimisha kufuata mfumo fulani katika kuyaendea maisha yake ya kibinafsi sambamba na yale ya kijamii. Kwa mantiki hii hatuna namna ya kuepa kusema kuwa mwanadamu hawezi kuishi bilaya dini, bila ya kujali usahihi au ubatili wa dini hiyo.
01:04 – NI MFUMO GANI KHASA WA MAISHA (DINI)ANAOUHITAJIA MWANADAMU?
Tumekuishaona kwamba dini ni mfumo Fulani wa maisha unaofuatwa na binadamu. Sasa suala linalojitokeza ni je, ni mfumo upi wa maisha (dini) unaomfaa mwanadamu? Tuanze kulijibu swali hili kwa kuanza kusema kwamba tangu zama za kale mwandamu amekuwa katika harakati za kupigania kupata maisha ya furaha na amani. Si hivi tu bali pia kuunda jamii adilifu. Harakati hizi zinaaathiriwa kwa kiwango kikubwa na itikadi au mfumo maisha unaofuatwa na jamii husika.

Mfumo sahihi wa maisha au dini ya kweli inayomfaa mwanadamu na itakayokidhi kiu ya mwanadamu katika kupata maisha ya amani na furaha, ni lazima iwe:-
  1. Inalingana/inayokubaliana na maumbile ya mwanadamu na ulimwengu aishimo.
  2. Na itikadi inayokubali kuhojiwa na kuingia akilini.
  3. Inakidhi mahitaji asili ya kimaumbile ya mwanadamu kiroho na kimwili.
  4. Inaweza kujibu maswali ya mwanadamu kuhusiana na uumbwaji huu wa ulimwengu sambamba na yeye mwenyewe.
  5. Inaweza kumuonyesha mwanadamu nafasi lengo na wajibu wake katika maisha haya.
  6. Na uwezo wa kukidhi mahitaji ya kiakili, kimaono na kihaiba ya mwanadamu.
  7. Ni dini ya ulimwengu mzima kwa ajili ya walimwengu wote kwa zama zote.

Kwa kuzingatia nukta hizi kama kigezo/mizania ya dini/mfumo sahihi wa maisha unaomfaa mwanadamu. Tutaona kuwa hakuna mfumo unaoweza kuzigusa nukta zote hizi kwa ukamilifu zaidi ya ule Allah Mola Muumba aliowachagulia mwanadamu. Na huu si mwingine bali ni mfumo Islamu.


02.          UISLAMU.
Uislamu ndio dini ya maumbile bila ya makindano. Yaani Uislamu ndio mfumo wa maisha unaokwenda sambamba na maumbile ya mwanadamu na ulimwengu wake. Kwa mantiki hii tunaweza kusema kwa kinywa kipana kabisa kwamba Uislamu ndio dini ya jamii ya wanadamu. Uislamu haukuitwa dini ya jamii ya wanadamu kwa kuropoka tu au kwa hamasa na jazba. Imeitwa hivyo kwa sababu zifuatazo:-
  1. Imesheheni desturi zinazokubaliana na akili.
  2. Ina uongofu unaouangazia na kuupa nuru moyo.
  3. Inabeba maendeleo yanayofaa kwa hali, mahala na zama zote.
  4. Ina sheria inayokidhi hali na mahitaji yote ya jamii katika nyanja zote za maisha.
  5. Ina dhana ya usawa unaowaunganisha pamoja watu wote bila ya kujali lugha, rangi au hali zao za kimaisha.
  6. Sheria yake ina dhima ya kumpa mwanadamu maisha ya amani, utulivu, raha, furaha na heshima katika nafsi, mwili, akili na mali.
Haya na mengineyo ndiyo yanayoufanya Uislamu uwe ni dini inayokubaliwa na kuridhiwa na mwanadamu kwa kuwa inayogusa moja kwa moja maumbile yake.
02:01 – UISLAMU NI NINI?
Uislamu ni mfumo kamili na sahihi wa maisha unaozienea nyanja zote za maisha ya mwanadamu katika hali, mahala na zama zote. Mfumo uliofumwa na Allah Mola Muumba ulimwengu na walimwengu kwa ajili ya waja wake na akawaleta kupitia mitume wake. Tangu Nabii Adamu mwanadamu wa kwanza mpaka Nabii Muhamad Mtume wa mwisho. Ili uwe ni muongozo na katiba ya kukiendesha kila kipengele cha maisha yao katika maisha haya ya mpito ya ulimwengu huu yenye dhima ya kuwaandaa na maisha ya milele ya Akhera.
02:02 – KAULI MBIU YA UISLAMU.
Uislamu kama dini na mfumo sahihi na kamili wa maisha unalingana na kuhubiri juu ya kuwepo Mungu aliye Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo humo. Unawataka wanadamu wote waitakidi kuwa YEYE ni MUNGU MMOJA WA PEKEE ASIYE NA MSHIRIKA YEYE tu ndiye anayestahiki kukusudiwa na  viumbe wake wote kwa kumuabudu, kumuomba na kumtegemea. YEYE hakuzaa wala hakuzaliwa wala YEYE hana anayefanana naye hata mmoja. Hii ndio kauli mbiu ya Uislamu, dini ya jamii ya wanadamu.
Na akili isiyo lemavu haiwezi kupinga au kukanusha kuwepo kwa Mola Muumba wa ulimwengu na walimwengu kwani kanuni huru za kiakili zinasema kuwa (kila natija/matokeo yana sababu yake). Kwa kuichukua kanuni hii yenye mantiki kama mizani akili haitasita kukubali kuwa kila kiumbe kina Muumba. Kwa sababu kiumbe ni natija/matokeo yanayohitaji sababu na sababu hiyo ndiyo Muumba Mwenyewe. Maadam akili imetumika kumjua Muumba Mkuu, basi uadilifu wa kiakili unamsukuma mwanadamu kumuamini.
Kauli mbiu ya Uislamu inawafikia walimwengu kupitia ujumbe wa Allah Mola Muumba unaofikishwa kwao kwa njia ya Mjumbe (Mtume).
ALLAH (MOLA MUUMBA)

 
UJUMBE (Vitabu)
 
 
MJUMBE (Mtume)
  WALENGWA WA UJUMBE (Jamii ya wanadamu).
Huu ndio utaratibu kamili wa mawasiliano baiana ya Allah Mola Muumba na mwanadamu kiumbe muumbwa chini ya mfumo Islamu.
Uislamu ni AKIDA/ITIKADI na SHERIA
a.       AKIDA:       Ni ile Imani ya kumuamini Allah kuwa ni Mungu Mmoja Muumba ulimwengu asiye na Mshirika. Na kumuamini Muhammad kuwa ni Mtume wake kwa watu wote na kuwaamini Mitume wake kwa watu wote waliomtangulia katika kufikisha ujumbe wa Mola wake kwa nyumati zilizoutanguila umati huu wake. Akida pia inahusisha  kuiamini:-
  • Siku ya mwisho.
  • Kusimamisha swala
  • Kutoa zaka
  • Kufunga Ramadhani
  • Kuhiji Makah.
Mambo yote haya kwa ujumla wake ndio nguzo madhubuti na imara zinazolibeba jengo Uislamu. Akida hii ya UISLAMU ni ndugu baba moja mama mmoja na akida za mbinguni zilizotangulia kabla yake. Ambazo zote zina dhima ya kulingania kheri (wema) na kukemea mambo maovu na machafu. Uislamu umekuja kuikamilisha dhima hii. Hii ndio AKIDA ya Uislamu kupitia kitabu cha Uislamu (Qur-ani Tukufu).
“MTUME AMEAMINI YALIYOTEREMSHWA KWAKE KUTOKA KWA MOLA WAKE NA WAISLAMU (Pia wameamini hayo). WOTE WAMEMUAMINI ALLAH, NA MALAIKA WAKE, NA VITABU VYAKE, NA MITUME YAKE (nao husema) HATUBAGUI BAINA YA YOYOTE KATIKA MITUME YAKE (wote tunawaamini)………..” (2:285)
Na Uislamu haumlazimishi mtu kuifuata Akida yake hii kwa nguvu bali aingie Uislamu baada ya kukinaishwa na hoja zake. Hivi ndivyo tunavyosema katika kitabu cha Uislamu: “WAITE (watu) KATIKA NJIA YA MOLA KWAKO KWA HEKIMA NA MAUIDHA (nasaha) MEMA NA UJADILIANE NAO KWA NAMNA ILIYO BORA………..” (16:125)
“HAKUNA KULAZIMISHWA (mtu kuingia) KATIKA DINI. UONGOFU UMEKWISHA PAMBANUKA NA UPOTOFU………..” (2:256) Isitoshe Uislamu unawafundisha waislamu namna ya kujadiliana na watu wa dini nyingine.
“WALA MSIJADILIANE NA WATU WALIOPEWA KITABU (kabla yenu) ILA KWA YALE (majadiliano) YALIYO MAZURI……….” (29: 46)
          b./ SHERIA
Sheria ya kiislamu ni mkusanyiko wa maneno ya Allah Mola Mwenyezi (sheria mama) na maneno ya Mtume wake kama sheria shereheshi/fafanuzi. Sheria hii imezienea nyanja zote za maisha ya mwanadamu kuanzia yale ya kibinafsi mpaka ya kijamii. Inagusa matendeano ya kila siku baina ya watu, mahusiano ya watu wenyewe kwa wenyewe, watu wa viumbe wengine, watu na ulimwenguu wao na watu na Mola Muumba wao. Kama inavyogusa mfumo wa familia, mirathi, ndoa, mazishi na kadhalika.
02:03 – NIKITAKA KUWA MUISLAMU NIFANYE NINI?
Uislamu unaamini kwamba kila mtoto anazaliwa hali ya kuwa tayari ni muislamu tokea tumboni mwa mama yake. Anabakia na Uislamu wake huo wa kuzaliwa mpaka anapofikia umri wa utu uzima (baleghe) hali ya kuwa na akili timamu. Katika umri huu ndipo anapoweza kuitumia akili na khiyari aliyopewa na Mola wake:
“…………. BASI ANAYETAKA NA AAMINI (awe muislamu) NA ANAYETAKA NA AKUFURU (awe kafiri). HAKIKA TUMEWAANDALIA MADHALIMU (Makafiri) MOTO AMBAO KUTA ZAKE ZITAWAZUNGUKA …………” (18: 29).
Akaukana na kuuvua Uislamu ndio umbile aliloumbiwa: “BASI UELEKEZE USO WAKO KATIKA DINI ILIYO SAWA SAWA NDILO UMBILE ALLAH ALILOWAUMBIA WATU (yaani dini hii ya kiislamu inawafikiana barabara na umbo la binadamu). HAKUNA MABADILIKO KATIKA MAUMBILE YA VIUMBE VYA ALLAH. HIYO NDIYO DINI ILIYO YA HAKI, LAKINI WATU WENGI HAWAJUI” (30:30)
Kwa kufuata mfumo mwingine wa maisha (dini) ulio nje ya Uislamu ambapo atakuwa amejitia khasarani mwenyewe: “NA ANAYETAKA DINI ISIYOKUWA YA KIISLAMU BASI HAITAKUBALIWA KWAKE NAYE AKHERA ATAKUWA KATIKA WENYE KHASARA (kubwa kabisa)” (3:85).
Sasa muasi huyu anapotaka baada ya kuamua kwa khiyari yake kurudi katika umbile lake la asili (Uislamu) hahitaji kubatizwa. Kitu pekee anachotakwia kufanya ni kutamka hadharani shahada mbili na kuishi kwa mujibu wa shahada mbili hizo.

02:04 – SHAHADA MBILI NI NINI?
          Shahada mbili ni mkusanyiko wa matamko mawili ya ahadi anayoichukua kiumbe (mwanadamu) mbele ya Muumba wake na viumbe wenzake. Ambapo mtamkaji hula kiapo cha utii kwa Allah Mola Mwenyezi na Mtume wake katika maisha yake yote kwa kufuata maamrisho na makatazo yake.
1.     SHAHADA YA KWANZA – TAMKO LA UTII KWA ALLAH:
          Ni mtu kutamka kwa moyo na ulimi:-
          “ASH – HADU AN LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU”
Maana : “Ninakiri kwa moyo na kutamka kwa ulimi kwamba  hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila  Allah (Mola asiye na mshirika wala mwana)”
2.     SHAHADA YA PILI: TAMKO LA UTII KWA MTUME WA ALLAH.
          Ni mtu kutamka kwa moyo na ulimi:-
          “WA ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN ABDUHU WA RASUULUHU”
Maana: “Na ninakiri kwa moyo natamka kwa ulimi kwamba Muhammad ni mja na mjumbe wa Allah (kama alivyo Isa, Musa, Ibrahimu) Matamko mawili haya ya ahadi ndio tiketi ya kuingilia katika Uislamu baada ya mtu kujitoa mwenyewe. Mtu akiyatamka maneno haya tu tayari anakuwa muislamu tena na papo hapo anawajibika kuishi chini ya kivuli na mipaka ya shahada mbili hizo. Kwani kuishi kwa mujibu wa shahada mbili ndiko kutampa sifa ya kuwa muumini mbele ya Alah Mola Muumba wake na mbele ya viumbe (waumini) wenzake.
02:05 – NGUZO Z A DINI YA KIISLAMU.
Dini hii ya Kiislamu imejengwa juu ya nguzo tatu za msingi, ambazo ni:-
1.      UISLAMU, ambao huu umejengwa juu ya nguzo      tano kama zifuatavyo:-
  1. Shahada mbili
  2. Kusimamisha swala tano
  3. Kutoa zakah
  4. Saumu ya Ramadhani
  5. Kuhiji Makah (kwa mwenye uwezo).
2.      IMANI nguzo hii  ya pili ya dini ya Kiislamu inajengeka juu ya nguzo sita zifuatazo:-
  1. Kumuamini  Allah
  2. Kuwaamini malaika wa Allah.
  3. Kuviamini vitabu vya Allah.
  4. Kuwaamini mitume (wote ) wa Allah.
  5. Kuamini siku ya mwisho.
  6. Kuamini qadari ya Allah (ya kheri au ya shari) kuwa inatoka kwa Allah).

3.      IHSANI. Nguzo hii ya tatu inaundwa na nguzo hii:-
Kumuabudu Allah kama unamuona Kama humuoni yeye anakuona wewe.
Huu kwa muhtasari ndio Uislamu, dini na mfumo sahihi na kamili wa maisha kwa wanadamu wote waliochaguliwa na Allah Mola Muumba wao: |………LEO NIMEKUKAMILISHENI DINI YENU NA KUKUTIMIZIENI NEEMA YANGU NA NIMEKUPENDELEENI UISLAMU UWE DINI YENU ………….” (5:3) elewa na ufahamu kwamba kuishi nje ya dini hii ni kulikana umbile lako kwani UISLAMU NI HAKI YAKO YA KUZALIWA uliyopewa hadiya (zawadi) na Mola Muumba wako.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget