Wednesday, April 4, 2012

Fitna na Namna ya Kukabiliana Nayo


Maana ya neno fitna katika Qur-aan

Fitna ni neno la kiarabu  فتنةَ) lenye maana pana.  Maana iliyo maarufu katika jamii yetu ni kama; mitihani, machafuko, majaribio na kutoelewana baina ya watu.

Neno fitna limetumika sana katika Qur-aan lenye makusudio tofauti. Miongoni wa hayo ni:

1.   Mtihani na majaribio: [Al-Ankabuut 29:2 - 3] Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)

 

 ((أَحَسِبَ ٱلنَّاسُ أَن يُتۡرَكُوٓاْ أَن يَقُولُوٓاْ ءَامَنَّا وَهُمۡ لَا يُفۡتَنُونَ))

Je, wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?

 

 ((وَلَقَدۡ فَتَنَّا ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِهِمۡ‌ۖ فَلَيَعۡلَمَنَّ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ صَدَقُواْ وَلَيَعۡلَمَنَّ ٱلۡكَـٰذِبِينَ))

Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo.

 

1.    Kugeuza na kuwekwa mbali na njia ya sawa :[Al-Maaidah5:49]

((وَٱحۡذَرۡهُمۡ أَن يَفۡتِنُوكَ عَنۢ بَعۡضِ مَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ إِلَيۡكَ‌ۖ))

Nawe jihadhari nao wasije kukugeuza (kukufitini) ukaacha baadhi ya aliyo kuteremshia Mwenyezi Mungu

 

2.    Mateso: [An-Nahl 16:10]

 

۬ ((ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ هَاجَرُواْ مِنۢ بَعۡدِ مَا فُتِنُواْ ثُمَّ جَـٰهَدُواْ وَصَبَرُوٓاْ إِنَّ رَبَّكَ مِنۢ بَعۡدِهَا لَغَفُورٌ۬ رَّحِيمٌ))

Kisha hakika Mola wako Mlezi, kwa wale walio hama makwao baada ya kuteswa, kisha wakapigania Dini na wakasubiri, bila ya shaka Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.

 

 

3.    Kutumbukia katika dhambi na ukafiri: [Al hadiyd 57:14]

يُنَادُونَہُمۡ أَلَمۡ نَكُن مَّعَكُمۡ‌ۖ قَالُواْ بَلَىٰ وَلَـٰكِنَّكُمۡ فَتَنتُمۡ أَنفُسَكُمۡ وَتَرَبَّصۡتُمۡ وَٱرۡتَبۡتُمۡ وَغَرَّتۡكُمُ ٱلۡأَمَانِىُّ حَتَّىٰ جَآءَ أَمۡرُ ٱللَّهِ وَغَرَّكُم بِٱللَّهِ ٱلۡغَرُورُ

(Wanafiki) Watawaita wawaambie: Kwani vile hatukuwa pamoja nanyi? (waislam) Watawaambia: Ndiyo, lakini mlijitia katika ukafiri (mlijifitini) wenyewe, na mkasitasita, na mkatia shaka, na matamanio ya nafsi zenu yakakudanganyeni. mpaka ilipo kuja amri ya Mwenyezi Mungu, na mdanganyifu akakudanganyeni msimfuate Mwenyezi Mungu

4.    Kupotoka, kwenda kinyume na sharia: [Al-Maaidah 5:41]

  ((وَمَن يُرِدِ ٱللَّهُ فِتۡنَتَهُ ۥ فَلَن تَمۡلِكَ لَهُ ۥ مِنَ ٱللَّهِ شَيۡـًٔا‌ۚ أُوْلَـٰٓٮِٕكَ ٱلَّذِينَ لَمۡ يُرِدِ ٱللَّهُ أَن يُطَهِّرَ قُلُوبَهُمۡ‌))

Na mtu ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumfitini huwezi kumpatia mbele ya Mwenyezi Mungu chochote. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao.

Kwa mtazamo wa Abu Hayaan [Al-Bahr al Muheet 4/262] Makusudio ya fitna katika aya hii ni  kupotoka.

 

5.    Tofauti baina ya watu na kutowafikiana: [At –Tawbah 9:47]

((لَوۡ خَرَجُواْ فِيكُم مَّا زَادُوكُمۡ إِلَّا خَبَالاً۬ وَلَأَوۡضَعُواْ خِلَـٰلَكُمۡ يَبۡغُونَڪُمُ ٱلۡفِتۡنَةَ وَفِيكُمۡ سَمَّـٰعُونَ لَهُم))

Kama wangekuwa pamoja nanyi wasingeli kuzidishieni ila mchafuko, na wange tanga tanga kati yenu kukutilieni fitna (kukugombanisheni). Na miongoni mwenu wapo wanao wasikiliza

Dunia ni Majaribio

Tuelewe kuwa maisha ya dunia ni makaazi ya mtihani, ni kujaribiwa kwa kila hali, na maisha ya akhera ni makaazi ya malipo kwa yale tuliyotahiniwa duniani, ima kufaulu au kufeli.

Katika kujaribiwa ndani yake kuna hikma na hakuna ajuaye kwa undani ila mwenyewe Allah Subhaanahu Wata’ala ambaye ametuwekewa mitihani.

Ushindi na mafaniko haupatikani isipokuwa kwa kujaribiwa ili ibainike ni wepi kati yetu wenye imani ya kweli na ni nani walioko kinyume wa hayo.  Suurat [Al-‘Imraan 3:179]

((مَّا كَانَ ٱللَّهُ لِيَذَرَ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ عَلَىٰ مَآ أَنتُمۡ عَلَيۡهِ حَتَّىٰ يَمِيزَ ٱلۡخَبِيثَ مِنَ ٱلطَّيِّبِ‌ۗ))

Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwaacha waislam katika hali mlio nayo mpaka apambanue wabaya katika wema.

Miongoni mwa mitihani ambayo Allaah Subhaanahu wa Ta’ala anawajaribu waja wake, Anatueleza katika Qur-aan [Suurat Al-Baqrah 2:155 -157]

  وَلَنَبۡلُوَنَّكُم بِشَىۡءٍ۬ مِّنَ ٱلۡخَوۡفِ وَٱلۡجُوعِ وَنَقۡصٍ۬ مِّنَ ٱلۡأَمۡوَٲلِ وَٱلۡأَنفُسِ وَٱلثَّمَرَٲتِ‌ۗ وَبَشِّرِ ٱلصَّـٰبِرِينَ (١٥٥) ٱلَّذِينَ إِذَآ أَصَـٰبَتۡهُم مُّصِيبَةٌ۬ قَالُوٓاْ إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّآ إِلَيۡهِ رَٲجِعُونَ (١٥٦) أُوْلَـٰٓٮِٕكَ عَلَيۡہِمۡ صَلَوَٲتٌ۬ مِّن رَّبِّهِمۡ وَرَحۡمَةٌ۬‌ۖ وَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡمُهۡتَدُونَ

Hapana shaka tutakujaribuni (kwa baadhi ya mambo) khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri. Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.

Hivyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) huwajaribu waja wake, na Huwapenda wale  wenye subira na kuvumilia mitihani itayowakuta, bishara njema na malipo mazuri juu yao.  Malipo ya pepo hayapatikani ila kwa kupasi mitihani hapa duniani.  Allaah anatueleza katika [Suurat Al-‘Imraan3:142]

((أَمۡ حَسِبۡتُمۡ أَن تَدۡخُلُواْ ٱلۡجَنَّةَ وَلَمَّا يَعۡلَمِ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ جَـٰهَدُواْ مِنكُمۡ وَيَعۡلَمَ ٱلصَّـٰبِرِينَ))

Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na kuwapambanua walio subiri

Tuelewe kuwa mali na watoto pia ni majaribio (mtihani) kwetu, ambavyo AllaahSubhaanahu wa Ta’ala Ametupa ili kupambanua ni nani atazitumia vizuri neema hizo kwa kuzishukuru na nani ni mwenye kuzikufuru.  [Suurat Al- Anfaal 8:28]

 ((وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّمَآ أَمۡوَٲلُڪُمۡ وَأَوۡلَـٰدُكُمۡ فِتۡنَةٌ۬ وَأَنَّ ٱللَّهَ عِندَهُ ۥۤ أَجۡرٌ عَظِيمٌ۬ ))

Na jueni ya kwamba mali zenu na watoto wenu ni Fitna (mtihani), na kwamba kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.

Vile vile Allaah ( Subhaanahu wa Ta’ala) Hutujaribu kwa kila hali;  mara hututia mitihani ya mabalaa, mswiba, maafa na janga, maradhi, na mara nyengine hututahini kwa kutubariki vizuri vizuri, utajiri, elimu, mali, swiha na mengineyo.  Hayo yote ni mtihani na siku ya kiama atatulipa kila mmoja kwa yale tunayostahikia.  [Al-Anbiyaa 21:35]

((كُلُّ نَفۡسٍ۬ ذَآٮِٕقَةُ ٱلۡمَوۡتِ‌ۗ وَنَبۡلُوكُم بِٱلشَّرِّ وَٱلۡخَيۡرِ فِتۡنَةً۬‌ۖ وَإِلَيۡنَا تُرۡجَعُونَ))

Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa.

 

Kwanini tunajaribiwa?

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ndie pekee mwenye kujua zaidi hikma ya kututahini, huwenda tukaona ni shari kumbe ndani yake mna kheri nyingi.

 Miongoni mwa hikma hizo ni:

1.    Kurudi kwa Allaah na kutubu Kwake:

Allaah Subhaanahu wa Ta’ala ni Mwenye rehma kwa waja wake, huwajaribu mara kadhaa ili wapate kutanabahi, kuyaacha yale yaliyokatazwa, kutubia, na kurudi kwake wakiwa wasafi. [At-Tawbah 9:126]

 ((أَوَلَا يَرَوۡنَ أَنَّهُمۡ يُفۡتَنُونَ فِى ڪُلِّ عَامٍ۬ مَّرَّةً أَوۡ مَرَّتَيۡنِ ثُمَّ لَا يَتُوبُونَ وَلَا هُمۡ يَذَّڪَّرُونَ))

Je! Hawaoni ya kwamba wanatiwa mtihanini kila mwaka mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu, wala hawakumbuki

 

2.    Kumtakasa na kumsafisha mja. [As-Sajidah 32:21]

 ((وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنَ ٱلۡعَذَابِ ٱلۡأَدۡنَىٰ دُونَ ٱلۡعَذَابِ ٱلۡأَكۡبَرِ لَعَلَّهُمۡ يَرۡجِعُونَ))

Na tutawaonjesha adhabu khafifu (duniani) kabla ya adhabu kubwa (huko Akhera), huenda labda watarejea

 

3.    Kufutiwa dhambi.

Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘Alayhi wa Sallam):

Hakuna mswiba au maradhi yanapomfika muislam, sio usumbufu wala huzuni hata kama ni kuchomwa mwiba, Allaah humfufutia dhambi kwa hilo. [Bukhaari 5641]

Pia hadithi nyengine iliyosimuliwa na Abu Hurayrah (Allaah awe radhi nae amesema);

Amesema Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi wa Sallam):

Mitihani itaendelea kuwafika waumini waume na wake, watoto na mali zao hadi wakutane na Allaah wakiwa hawana dhambi

[Tirmidhi 2399 na kusahihiswa na Albaani]

4.    Kumtambua Allah Subhaanahu Wata’ala na kukuza Iymaan;

Kufikwa na maafa na mitihani mbali mbali, humpelekea mja kuutambua udhaifu wa binaadamu kuwa yeye si lolote si chochote, na hakuna  mwenye uwezo ila Allaah Subhaanahu wa Ta’ala.  Humpelekea kujijua kuwa yeye ni masikini na ni mhitaji wa Mola wake kwa kila hali, hupelekea kumkumbuka, kumuomba na kumtukuza Alietukuka.

5.    Kuwasafisha walio wema na kuwaondoa walio wanafiki.

Unaweza kuona fitna na mtafaruku umeingia katika jamii, kumbe ikawa ni kheri ya kuwapambanua na kuwachuja wale wanafiki kati ya wale waislam wenye kuisimamia dini ya Allaah kwa dhati ili wasije wakaeneza machafuko zaidi. [Al-‘Imraan 3:141 – 142]

وَلِيُمَحِّصَ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَيَمۡحَقَ ٱلۡكَـٰفِرِينَ (١٤١) أَمۡ حَسِبۡتُمۡ أَن تَدۡخُلُواْ ٱلۡجَنَّةَ وَلَمَّا يَعۡلَمِ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ جَـٰهَدُواْ  ) ((مِنكُمۡ وَيَعۡلَمَ ٱلصَّـٰبِرِينَ

Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na awafutilie mbali makafiri. Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio subiri?

Pia katika suurat [At Tawbah 9:47]

((لَوۡ خَرَجُواْ فِيكُم مَّا زَادُوكُمۡ إِلَّا خَبَالاً۬ وَلَأَوۡضَعُواْ خِلَـٰلَكُمۡ يَبۡغُونَڪُمُ ٱلۡفِتۡنَةَ وَفِيكُمۡ سَمَّـٰعُونَ لَهُم))

Kama wangekuwa pamoja nanyi wasingeli kuzidishieni ila mchafuko, na wange tanga tanga kati yenu kukutilieni fitna (kukugombanisheni). Na miongoni mwenu wapo wanao wasikiliza.

6.    Kupandishwa darja.

Kutokana na hadithi aliyoisimulia Mama wa Waumini Aa’isha (Allaah awe radhi naye), kwamba Mtume (Swalla Llahu ‘Alayhi wa Sallam) amesema;

Muislamu hapatwi na dhara kwa kuchomwa na mwiba au kubwa yake, ila Allaah humnyanyua kwa hilo au humvutia dhambi. [Muslim 2572]

7.    Kujua thamani ya uzima, amani na utulivu

Kufikwa na misukosuko iwe ni ya maradhi, njaa au mengineyo inampelekea mja kuzidi kutambua neema alizojaaliwa na kuzithamini.  Pia kuwafikiria na wengine wanaopata maafa kama hayo.

Hautaweza kuingia peponi hadi ujaribiwe na uonje machungu ya dunia hii.  Hizi ni baadhi tu ya hekma za mitihani mbali mbali inayowaswibu wanadamu.  Zaidi ni Allaah pekee mjuzi wa yote.

Mambo ya kuzingatia kukabiliana na Fitna

1.    Istiqaama

Kwa ufupi neno Istiqaama lina maana ya kuwa sawa, kunyooka na kuwa imara bila ya kuyumba yumba. Cha msingi mja anapopata mtihani wa aina yoyote, hutakiwa awe na msimamo imara hasa katika kuchunga mipaka ya Allaah zaidi.  Tujue mtihani ni kipimo, wengi wanapokuwa shwari hakuna kinachowasumbua hutulia katika imani, lakini wakipata mtihani kidogo huyumba na kutumbukia katika kufuru. Suurat [Al-Hajj 22:11]

وَمِنَ ٱلنَّاسِ مَن يَعۡبُدُ ٱللَّهَ عَلَىٰ حَرۡفٍ۬‌ۖ فَإِنۡ أَصَابَهُ ۥ خَيۡرٌ ٱطۡمَأَنَّ بِهِۦ‌ۖ وَإِنۡ أَصَابَتۡهُ فِتۡنَةٌ ٱنقَلَبَ عَلَىٰ وَجۡهِهِۦ خَسِرَ ٱلدُّنۡيَا وَٱلۡأَخِرَةَ‌ۚ ذَٲلِكَ هُوَ ٱلۡخُسۡرَانُ ٱلۡمُبِينُ

Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ikimfikia fitna (msukosuko) hugeuza uso wake. Amepata hasara dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.

Tunatakiwa tuwe imara tukipatwa na mitihani bila kuvunjika moyo kwa kuacha matendo mema na kufuata hawaa za nafsi zetu na kuzidi kupotea na kusahau mazuri na neema zote tulizokuwa nazo wakati wa utulivu.

2.    Du’aa

Allaah Subhaanahu wa Ta’ala ndie tunaemtegemea kwa kila hali, Yeye ndie Anaetukadiria ya kheri na ya shari. Hutupa mitihani na Yeye ndie tunaemtegemea kutupa faraja.  Ameagiza Mwenyewe (Subhaanahu wa Taala) kuwa tumuombe nae atajibu maombi yetu. [Al-Ghaafir 40:60]

((وَقَالَ رَبُّڪُمُ ٱدۡعُونِىٓ أَسۡتَجِبۡ لَكُمۡۚ))

Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni.

Hivyo ni juu yetu kumuomba Allaah Subhaanahu wa Ta’ala sana atunusuru na kutulinda na kila ya fitna.

-      Kabla ya fitna:                     Atunusuru na kutuweka mbali nayo

-      Wakati wa fitna:                   Atupe subira na stahamala

-      Baada ya fitna:                    Atusamehe na kutukubalia amali zetu

 

 

3.    Kujiongezea Iymaan

Ni vyema mja kujitahidi katika mambo mema kwa kadiri awezavyo, kujibidiisha katika ibada, sala za usiku, sadaka kwa wingi na kila kitachomuongezea Iymaan.  Hii hupelekea kuwa karibu sana na Allaah Subhaanahu wa Ta’ala, kuhifadhi na kulinda mipaka yake; Mwenye kumhifadhi Mwenyezi Mungu nae Allaah Humhifadhi na kumpa faraja anapomhitaji. 

Katika riwaya ya At -tirmidhiy na kusimuliwa na Abdillaah Ibn Abbas (Allaah awe radhi nae yeye na baba yake) kwamba Mtume swalla Llahu ‘Alayhi wa Ssallam amesema

 

احْفَظِ اللهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللهَ تَجِدْهُ تُجاهَك،

Mhifadhi Allah nae Atakuhifadhi.  Mhifadhi Allah utamkuta mbele yako

Tunatakiwa tuwe na yaqini Kwake, kuwa ni yeye alietujaalia litufike na ni yeye ndie ataetuhifadhi na kutupa faraja juu ya misukosuko.

4.    Elimu

Kujiongezea elimu na maarifa ya dini kunapelekea kuitambua fitna na namna ya kukabiliana nayo, kwani dini yetu haikuacha kitu, kila kitu kimeelezwa katika Qur-aan na Sunnah.  Muislam ajitahidi sana kusoma na kujua angalau mambo muhimu ya dini yake.  Hii hupelekea kufaulu vizuri mtihani itayotukabili na kuzidi kumuogopa Subhaanahu wa Ta’ala na kumtii, kwani wenye kumuogopa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala hasa, ni wale wenye elimu na kuujua utukufu wake. [Faatwir 35:28]

((إِنَّمَا يَخۡشَى ٱللَّهَ مِنۡ عِبَادِهِ ٱلۡعُلَمَـٰٓؤُاْۗ))

Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wataalamu (wanazuoni)

 

5.    Kulingania wengine

Unapokuwa na elimu basi usitosheke pekee yako, ni vyema kuwalingania wengine, na kutanabahishana kila panapotokea mtafaruku.  Pasipo na mlinganiaji hasa wakati wa fitina madhara yake huwa ni makubwa zaidi.  Kuwepo watu miongoni mwa jamii wa kuweza kunaswihi, hapo ndipo jamii hiyo itakuwa bora na kutengenekea. [Aal ‘Imraan 3: 104]

 ((وَلۡتَكُن مِّنكُمۡ أُمَّةٌ۬ يَدۡعُونَ إِلَى ٱلۡخَيۡرِ وَيَأۡمُرُونَ بِٱلۡمَعۡرُوفِ وَيَنۡهَوۡنَ عَنِ ٱلۡمُنكَرِ‌ۚ وَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡمُفۡلِحُونَ))

“Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri Uislam na wanaoamrisha mema na wakakataza maovu. Na hao ndio watakaotengenekewa.”

6.    Subira

Subira ndio kitu kikubwa kinachohitajika wakati wa fitna.  Mbora kati ya mja ni Yule aliejaribiwa na akawa na subira kwa yaliomfika kwani Allaah yupo na wenye kusubiri. [Al-Baqarah2:153]

 ((يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱسۡتَعِينُواْ بِٱلصَّبۡرِ وَٱلصَّلَوٰةِ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ مَعَ ٱلصَّـٰبِرِينَ))

Enyi mlioamini! Takeni msaada kwa subira na Swalah. Hakika Allah Yu pamoja na wanaosubiri.

 

Hitimisho

Tujue kwamba tumeletwa ulimwenguni tufanyiwe mitihani ili tusafike vizuri kabla ya  kumaliza safari yetu na kwenda akhera.  Ni juu yetu kuvumilia na kushika yale tuliyoamrishwa na Allaah Subhaanahu wa Ta’ala na Mtume wake Swalla Llaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam hasa katika suala zima la majaribu. Tujue kuwa baada ya dhiki ni faraja. Tusikate tamaa, tupanie katika kujikinga na hizo balaa, zikitufika tustahamili na kuzidi kumuomba Allaah Subhaanahu wa Ta’ala. Zikiondoka tuwe na msimamo madhubuti katika dini ili tusije yumba wakati wa mitihani na majaribu.

Tumuombe Allaah Subhaanahu wa Ta’ala atupe mioyo isiyo na ukame, iwe ni ya kumkumbuka na kumtambua yeye kwa kila hali, atupe miili yenye kustahamili kila aina ya mikiki, na kutuepushia miswiba hasa katika dini yetu.

Amiyn

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget