Wednesday, April 4, 2012

NAFSI IMA NI NJIA AU KIKWAZO


Wanazuoni wamekubaliana kwamba nafsi, ima inakuwa kikwazo kati ya moyo wa mja na Allah (Subhaanahu Wata’ala) au ndio njia ya mwongozo wa moyo kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala).

Ibnul Qayyim anasema:

“Nafsi ni dhati moja tu ila hali yake hubadilika kutoka nafsi inayoamrisha maovu kwenda nafsi inayolaumu hadi kufikia nafsi iliyo na utulivu. Na hili ndio lengo la kufikia ukamilifu (wake)…”

 Nafsi inayolaumu ni nafsi ya muumini… Imetajwa pia kuwa na nafsi itakayojilaumu yenyewe siku ya kiama – kwani kila mtu hujilaumu mwenyewe kwa matendo yake ikiwa ni madhambi yake kama ni mtu wa kutenda madhambi au kwa upungufu katika kufanya mambo mema.Yote haya ni Salla Allahu ‘Alayhi Wasallama” (Madarij As saalikiin fi Manaazil iyyaaka naabudu Wa Iyyaaka  nastaiin,vol 1 pg 308)

Said Hawwaa yeye anasema:

Ikitegemea hali iliyo, nafsi inakuwa katika hali tofauti. Wakati inapokuwa tulivu kwa kumtii Allah(Subhaanahu Wata’ala) na kupinga matamanio ya nafsi yake. Nafsi hii hujulikana kama Nafsi iliyo na utulivu, ambayo imetajwa katika Quraan Suuratul fajr aya ya 27-28.

Lakini nafsi hii ikishindwa kujipatia utulivu na kuiachia kughilibiwa na matamanio;  hii hujulikana kama Nafsi inayolaumu kwa sababu  humlaumu mtu kwa kutokuwa na hadhari katika kumtii Allah(Subhaanahu Wata’ala) Suuratul Qiyaamah aya ya 2.

Na zaidi ikiwa nafsi itasalimu amri mbele ya matamanio na kumruhusu shetani aichezee basi nafsi hii ni Nafsi inayoamrisha maovu ambayo Allah (Subhaanahu Wata’ala) anaisimulia katika Quraan kisa cha mke wa mheshimiwa (Zulaykhah). Suuratu Yussuf aya ya 53.( Tarbiyatu  ruuhiyyah pg 38  Daru salaam  Cairo.)

Qatadah anasema:

Hii ni roho ya muumini wa kweli, Ikiwa tulivu kwa kuyajua majina ya Allah (Subhaanahu Wata’ala) na sifa zake na pia kwa yale iliyokuwa ikiyasema kuhusu Allah(Subhaanahu Wata’ala) na Mtume wake(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam). Na pamoja aliyoyasema kuhusu mambo yataipata nafsi baada ya kufa ,inapotoka roho,maisha ya Barzakh, matukio ya siku ya kiama . Nafsi inakuwa tulivu kiasi ambacho hata ataweza kuyaona haya kwa macho yake mwenyewe.hivyo anasikiliza maamrisho ya Allah (Subhaanahu Wata’ala) na kutii bila ya kuchoka wala kulalamika na imani yake kutetereka. Haifurahi (kupita kiasi) akipata mambo mazuri na wala majanga hayamfanyi avunjike moyo – kwani anajua tayari kwamba yameshaandikwa hata kabla ya kutokea, hata kabla ya yeye kuumbwa… ( Att Tabari : Jamiul Bayaan fi Tafsiiril Quraan vol 13 1323)  


NAFSI YA BINADAMU BAINA YA SHETANI NA MALAIKA

Kwa ujumla waja wamegawika katika makundi mawili.

Kundi la kwanza:

Ni wale ambao nafsi zao tayari zinawaongoza kwenye maangamizi. Watu hawa wamejikubalisha kutawaliwa na nafsi zao na kujikubalisha kuzifuata.

Kundi la pili:

 Ni wale waliozishinda nafsi zao na kuzifanya zikubaliane na matakwa yao

Makundi haya mawili kila mmoja lina kiongozi wake. Kundi la kwanza kiongozi wake ni shetani na la pili ni Malaika.

“Malaika”, anasema Imam Ghazali, “anamlinda kila kiumbe aliyeumbwa na Allah (Subhaanahu Wata’ala) na kukijaza elimu, ukweli, ahadi ya malipo na kuamrisha mema. Shetani anamsimamia kiumbe kwenda kinyume na yote haya…, wasiwasi dhidi ya ilham, shetani dhidi ya malaika, tawfiq dhidi ya hasara”

Hassan Al-Basry anasema:

“Nafsi hushughulishwa na nguvu mbili za fikra. Ya kwanza ni kutoka kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) na nyengine ni kutoka kwa adui. Allah (Subhaanahu Wata’ala) humrehemu mja anaeituliza nafsi yake kwa fikra zake. Huzipokea fikra hizi zitokazo kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) na wakati huo huo kupigana na za adui.

Vita hivi kati ya majeshi ya shetani na Malaika kila mmoja kutaka kuiteka nafsi ni vya kuendelea mpaka mmoja ashinde na kuweka bendera hapo. Na hapo siyo mwisho kwani lile jeshi lililoshindwa nalo huandaa mikakati madhubuti kuweza kuitwaa tena nafsi na kuvifanya vita hivi kuwa vuta nikuvute mpaka binadamu anaingia kaburini.

Nafsi nyingi hujikuta kuzidiwa zaidi na majeshi ya shetani. Kwani wana mikakati madhubuti kumfanya mtu kumili zaidi upande huo na kuzidi kuzitia wasiwasi wa kutaka kuifikiria akhera kwanza badala ya kufaidi matunda ya dunia ambayo wanayaona na nafasi ya kuyatumia pia ipo. Vitimbi vyao ni dhaifu kwani tayari Allah(Subhaanahu Wata’ala) anatufahamisha katika Quraan juu ya vitimbi na hila za shetani Annisaa /76

الَّذِينَ ءَامَنُواْ يُقَـتِلُونَ فِى سَبِيلِ اللَّهِ وَالَّذِينَ كَفَرُواْ يُقَـتِلُونَ فِى سَبِيلِ الطَّـغُوتِ                      

                       أَوْلِيَاءَ الشَّيْطَـنِ إِنَّ كَيْدَ الشَّيْطَـنِ كَانَ ضَعِيفاً  فَقَـتِلُواْ

 Walio amini wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio kufuru wanapigana katika njia ya upotofu. Basi piganeni na marafiki wa Shet'ani. Hakika hila za Shet'ani ni dhaifu.

Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema:

 “ Hakuna yoyote miongoni mwenu aliyekuwa hana shetani. Wakasema, ‘hata kwako wewe ewe Mjumbe wa Allah?’ Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akasema ,  ‘Hata kwangu mimi , ila Allah amenisaidia kuweza kumtawala na ananitii, hivyo haniamrishi lolote isipokuwa (huwa) zuri”

(Muslim)

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget