Subira ni Wakati wa Pigo la Mwanzo
Binadamu anapofikwa na msiba anakuwa katika hali tofauti kuukubali.Misiba inapomfika mja huwa hana madaraka wala uwezo nayo kwani si miongoni mwa matendo yake bali ni mambo yanayomfika na yapo nje ya uwezo wake
Kuondokewa na vipenzi vyetu ghafla bila ya kutegemea , kuibiwa na kudhulumiwa mali mali zetu, kunyan’ganywa haki, amana na dhamana zetu, kupatwa na maradhi bila ya kutarajia , kuunguliwa majumba yetu ni baadhi ya masaibu ambayo mja huyapata si kwa matendo yake bali ni kwa mipangilio ya Allah Subhaanahu Wata’ala.
Kila mja katika ulimwengu huu huweza kupata masaibu katika hali tofauti ikiwa ni katika sura ya majaribu, mitihani na pia katika sura ya mabalaa kama anavyosema Allah Subhaahau Wata’ala katika Suuratul Mulk/2
الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلاً
Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi
Kimsingi mja anapofikwa na misiba huwa katika hali zifuatazo
1 Atasikitika na kuwa majonzi akiomboleza kuvuka mpaka
2 Atasubiri na kuvumilia
3 Ataridhia na kuikubali Qadr yake Allah Subhaanahu Wata’ala.
4 Atashukuru
1 Kusikitika kunakovuka mipaka
Nako kumegawika katika hali zifuatazo
· Kwa moyo
Nako ni kujenga hisia na tuhuma moyoni na kuzipeleka kwa mola muumba kana kwamba amedhulumiwa na kuonewa.
· Kwa mdomo
Kwa kuanza kulia kwa mayowe na kutamka maneno ambayo yanaweza kumuudhi Allah Subhaanahu Wata’ala.
· Kwa viungo
Kwa kujipiga mashavuni, kuzivuta nywele, kugaragara chini, kuchana nguo na mfano wake.
2 Kusubiri na kuvumilia
Ni kwenda dhidi ya hili la mwanzo kwani huizuia nafsi yake huku akiuchukia msiba na haupendelei utokee hata hivyo hatumii moyo wake kuanza kujenga dhana au mdomo wake kwa kutamka maneno yanayomuudhi Allah Subhaanahu Wata’ala na wala hatumii viungo vyake kuzidi kumkasirisha muumba.
3 Kuridhia
Kuwa katika hali ya kuukubali msiba bila ya kuuchukia na huku moyo wake ukiwa radhi kabisa na mipangilio yake Allah Subhaanahu Wata’ala na wala hakuna tofauti katika hali yake kabla na baada ya kufikwa na masaibu.
4 Kushukuru
Kurudi kwake Allah Subhaanahu Wata’ala na kushukuru . Hii ni darja ya juu zaidi ya kusubiri na kuridhia kwani mja humshukuru Allah Subhaanahu Wata’ala kwa sababu ya kuelewa malipo na jazaa ambayo ataipata katika msiba huu kuliko kuufikiria msiba wenyewe. Kwani Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alipokuwa akifikwa na jambo linalomchukiza huwa anasema:
في السلسلة الصحيحة وصححه الألباني الحمد لله على كل حال" أخرجه ابن ماجه
Ninamshukuru Allah kwa kila hali
Ibnu Majah na Sh Albani anasema ni Sahihi katika Assilsila Assahiyhah
Moja katika mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa kufikwa na masaib ni subira na uvumilivu kama anavyobainisha Allah Subhaanahu Wata’ala katika Quraan Suuratul Baqarah 155-157
وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوفْ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الأَمَوَالِ وَالأنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ{155} الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُواْ إِنَّا لِلّهِ وَإِنَّـا إِلَيْهِ رَاجِعونَ{156} أُولَـئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ وَأُولَـئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ
Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri
Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Allah, na kwake Yeye hakika tutarejea
Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao na rehema. Nao ndio wenye kuongoka
Na kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam
عجباً لأمر المؤمن إن أمره كله خير، وليس ذلك لأحد إلا للمؤمن: إن أصابته سراء شكر فكان خيراً له، وإن أصابته ضراء صبر فكان خيراً له. رواه مسلم
Ajabu ya mambo ya Muumin kwamba kila jambo lake lina kheir na hapati hayo isipokuwa kwa Muumin akifikwa na jambo zuri hushukuru na hilo ni kheri kwake na akifikwa na jambo la kumdhuru huwa na subira na hilo lina kheri kwake Muslim
Anasema Imam Al Qaraafiy, Allah amrehemu, kwamba masaibu yanayotukuta hutufutia madhambi ikiwa yatakwenda sambamba na ridhaa zetu au vyenginevyo. Ila kama yatakwenda na sambamba nasi tukiwa radhi na Allah Subhaanahu Wata’ala basi athari zake huwa kubwa kuliko tunapokuwa hatupo radhi. (Angalia Fat-hul Baari juzuu ya 11 ukurasa 242-243)
Pia kuna hadithi kadhaa kutoka kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam zinazothibitisha haya kama
ما يزال البلاء بالمؤمن والمؤمنة في نفسه وولده وماله, حتى يلقى الله تعالى وما عليه خطيئة
أخرجه الترمذي وصححه الألباني في الصحيحة
Mabalaa yataendelea kumfika muumini wa kiume na muumini wa kike katika nafsi yake na mtoto wake na mali yake mpaka atakutana na Allah ilhali hana tena madhambi.
Attirmidhiy na anasema Sh Albani ni sahihi katika Assilsilah Assahiyhah
Hata hivyo daraja ya subira na uvumilivu ambayo Allah anaiangalia katika nafsi ya mja ni pale pigo la mwanzo litakapomfika na jinsi atakvyoweza kujizua na kuonesha uvumilivu ili mja huyu kuweza kupata ujira uliokamilika kwa kusubiri kama anavyotufahamisha Mtume wetu Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam katika hadithi ifuatayo:
وعن أنس بن مالك رضي الله عنه قال: مر النبي صلى الله عليه وسلم بامرأة تبكي عند قبر فقال:"اتقي الله واصبري" قالت: إليك عني فإنك لم تصب بمصيبتي، ولم تعرفه! فقيل لها: إنه النبي صلى الله عليه وسلم فأتت باب النبي صلى الله عليه وسلم فلم تجد عنده بوابين، فقالت: لم أعرفك، فقال:"إنما الصبر عند الصدمة الأولى)
أخرجه البخاري في كتاب الجنائز
Kutoka kwa Anas Ibn Maalik, Allah amuwie radhi amesema: Alipita siku moja Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam sehemu yenye makaburi na akamkuta mama mmoja akilia kwenye kaburi na akamwambia; “Muogope Allah na uvumilie!” Akasema yule mama ; “ Niachie kwani hujafikwa na msiba ulionifika na wala huujui” Akaambiwa : “(Hakika) ni Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam”. Kisha akaja mama kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam na hakuwakuta walinzi mlangoni na kusema (kwa kuomba radhi): “ Sikukujua (kama ulikuwa Mtume)” Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akasema; “ Hakika subira ni wakati wa pigo la mwanzo”
Bukhari katika mlango wa Janaiz
Tumuombe Allah Subhanahu Wata’ala atupe msimamo wa kuikubali mipangilio na Qadr yake.
Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’ala atupe subira na uvumilivu tunapofikwa na misiba.
Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’ala atupe ujira katika masaibu yanayotufika
Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’ala atupe uwezo wa kuvumilia tokea tunapofikwa na Masaibu.
Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’ala atufutie madhambi yetu kwa ajili ya masaibu yanayotufika.
Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’ala atunyanyue daraja zetu kwa masaibu yote yatakayotufika.
Amiyn, Amiyn Amiyn
Wabillahi Atwafiyq.
No comments:
Post a Comment