Wednesday, April 4, 2012

AINA ZA NAFSI



Baadhi ya Maulamaa wameigawa nafsi katika daraja saba tofauti ila Ijmaaul Ulamaa (makubaliano ya Maulamaa) kwa ujumla wameigawa nafsi katika hali tatu kama zilivyotajwa katika Quraan.(comments on the footnote Kuna kauli pia kwamba nafsi ni mbili tu nafsi inayoamrisha maovu na na nafsi inayolaumu. Ama nafsi iliyo na utulivu si miongoni mwa aina hizi za nafsi)

1             Nafsi inayoamrisha maovu.

2             Nafsi inayolaumu

3             Nafsi iliyo na utulivu.

1             NAFSI INAYOAMRISHA MAOVU

Nafsi hii ni ile yenye kuamrisha kila lenye kuelekea katika kufanya maasi, uchafu na uovu.

Huwa haina hisia ya kuwepo kitu chengine zaidi ya maovu na kila kitu kwa ufahamu wa nafsi hii ni Salla Allahu ‘Alayhi Wasallama tu kwa mja na hivyo hutenda mambo bila ya kujijua kwani huwa tayari imeshaathirika.

Kwa hivyo nafsi hii huwa maskani ya adhabu kwani tayari hujiadhibu wenyewe kwa kujiingiza katika mambo yote machafu yaliyoharamishwa na kukatazwa. Na hakuna mwenye uwezo wa kuiokoa nafsi hii isipokuwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) pekee kama anavyobainisha katika Quraan (kwenye kisa maarufu cha Mtume Yussuf (‘Alayhi Ssalaam) na yule mke wa mheshimiwa (Zulaykhah) na kutajwa katika Quraan) Suurat Yussuf /53.

وَمَآ أُبَرِّىءُ نَفْسِى إِنَّ النَّفْسَ لأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ إِلاَّ مَا رَحِمَ رَبِّى إِنَّ رَبِّى غَفُورٌ رَّحِيمٌ

 “Wala siitoi lawamani nafsi yangu, hakika nafsi (kazi yake) huamrisha maovu isipokuwa ile iliyorehemewa na mola wangu, hakika mola wangu mlezi ni msamehevu na mwenye kurehemu”

Aya hii inaeleza kwamba binadamu hana madaraka ya kuweza kuiepusha nafsi isielekee kwenye maovu isipokuwa hiyo ni rehema kutoka kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) pekee.

Ukiiangalia aya hii kwa undani zaidi utaona ubaya wa nafsi hii ulivyo ambayo haifahamu kitu chengine ila maovu, maasi, uchafu, ubaya na kadhalika. Fahamu hii hujengewa mazingira mazuri ya kumtia hamu mja kufanya maasi.

Tuchukue mfano wa tendo la zinaa.

Nafsi inaelewa kama tendo hili ni haramu. Hata hivyo nafsi inamfanya mja kuanza kusifu na kutamani baada ya kuona. Inaendelea kumuongoza mja katika mtiririko mzima wa kufuatilia nyendo za mhusika kuweza kujua vipi kuweza kumtia mhusika mikononi. Nafsi hii haimpi mja nafasi ya kujali kwamba tendo hilo na dhambi, haramu na njia iliyo mbaya kabisa, wala haijali kama kuna madhara makubwa katika kutenda tendo hilo. Maadam nafsi imeshamsemeza mja na kuitika bila ya kuiambia hapana inakua balaa tupu na hata haitojali kuadhirika wala kuaibika na mengi mengineyo.

Jinsi nafsi hii iliyojitwika jukumu la kuamrisha maovu inavyotekeleza wajibu wake kwa upeo mkubwa ni jambo lisilohitaji dalili wala uthibitisho kwani tunaliona kila siku katika maisha yetu.

Nafsi hii, si kwamba huamrisha maovu tu bali nayo, humzuia binadamu katika kufanya yale yaliyokuwa mema. Hii pia ni moja katika kazi yake. Nafsi hujiona nzito hasa katika amali njema na kuwa mwepesi mno kwenye amali mbaya. Hujenga hoja aina kwa aina kumfanya mtu asite na kuona uzito kila panapotokea amali za kheri.

Tuchukue mfano wa Sala:

Nafsi inafahamu kwamba sala ni wajibu. Na kutotekeleza wajibu huu ni kuasi na kwenda kinyume na amri ya Allah (Subhaanahu Wata’ala) na mwongozo wa Mtume wake (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam). Hata hivyo itajenga hoja nyingi na nzito za kumvunja mja moyo na kutekeleza ibada hii: sikufundishwa, sijawa tayari, Allah atanisamehe, sitaki kuwa mnafiki kusali leo kesho nikaacha, nitasali vipi wakati bado nnafanya maasi. Hizi ni baadhi tu.

Mfano mwengine ni pale unapoingia mwezi mtukufu wa Ramadhan.Tunaelewa kwamba mashetani hufungiwa sasa inakuwaje bado kuna waja wanafanya maasi ndani ya mwezi mtukufu?. Ni kwa sababu ya nafsi zile chafu, ovu na mbaya ambazo huendelea na kazi ambayo kwa kipindi kile shetani amepumzishwa.

           

Nafsi hii ina shetani kama sahiba wake, huipa tamaa ya mafanikio makubwa na raha zilioje. Huijengea mazingira mazuri ya kufanya maovu na kuzidi kuipa tamaa. 

2             NAFSI INAYOJILAUMU

Nafsi hii imetajwa katika Quraan Suuratul Qiyamah /2

                                               وَلاَ أُقْسِمُ بِالنَّفْسِ اللَّوَّامَةِ

 Na ninaapa kwa nafsi inayojilaumu!

Maulamaa wametofautiana katika tafsiri ya aya hii katika kauli tatu zifuatazo.

A         Hii ni nafsi ya aliyeamini kikweli na hupenda kujilaumu kila inapofanya makosa.

B         Ni nafsi ya kawaida ya mja ambapo mtu mwema anapofanya maasi nafsi yake humlaumu kwa nini amefanya maasi hayo na muovu anapoyakosa maasi hujilaumu kwa kuyakosa.Hapa nafsi inawalaumu wote lakini kwa hali tofauti kwani mja mwema anajilaumu kwa ajili ya kijirekebisha na mja muovu anajilaumu kwa jinsi alivyokosa kufanya uasi.

C         Lawama hii iliyokusudiwa hapa ni kwa siku ya kiama ambapo muovu atajilaumu kwa uovu wake na mwema atajilaumu kwa kuwa na upungufu katika mema yake.Maana hii inaongezewa nuguvu na aya iliyokuja kabla ambapo Allah anaapa kwa siku ya kiama.  Kila mtu hujilaumu kwa matendo yake hasa mabaya, ikiwa ni mengi au kwa kutokuwa na ukamilifu katika kutenda mazuri.

 Hassan Al-Basry anasema “Kila siku muislam huilaumu nafsi yake na kusema mfano wa haya, “Kwa nini ninataka kitu hiki, kwa nini nimefanya kitu hiki, kwani hiki  kizuri kuliko hiki.

Ni nafsi isiyoelewa au yenye kujitoa fahamu kuwa itawajibika kwa matendo yake hivyo hupeleka lawama kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) kwa yale matendo inayoyafanya.  Ni tabia ya baadhi ya waja kakataa kubeba lawama na kuzitupia wahusika wengine na wao kujitoa, hata kama nafsi hizi ndizo ziko makosani. Mfano wa nafsi isiyosali huwa inaelewa kuwa wajibu wake kusali lakini hudiriki kusema kama lau Allah (Subhaanahu Wata’ala) angelitaka nisali ningelisali kwani Allah (Subhaanahu Wata’ala) humuongoa amtakae na kumpotoa amtakae na hii ndio maana potofu ya aya kwa waja hawa.

Nafsi inayojilaumu ni  nafsi inayofahamu  majukumu yake na kuelewa lengo la kuumbwa kwake na huwa tayari kubeba lawama zote kwa kuilaumu nafsi yake mwenyewe kwa kuwa na upungufu katika kumtii Allah (Subhaanahu Wata’ala). Nafsi hii huwa tayari kustahamili, kukosolewa, kuwaidhiwa ikiwa na lengo la kumridhisha Allah (Subhaanahu Wata’ala).  Ni matarajio kuwa nafsi hii haitolaumiwa na Mola hata ikiwa itajilaumu yenyewe kwani iko tayari kubeba na kuridhia yale iliyotanguliza kwa mola wake.

Na nafsi hii ni adhimu kwani inakuwa kwenye kujilaumu daima hata ikiwa katika kumtii Allah(Subhaanahu Wata’ala) ikijihisi kama  bado ina upungufu .

Said ibn Jubayr (Allah amuwie radhi) na Ikrimah (Allah amuwie radhi) pale walipoielezea Nafsi inayojilaumu wamesema, “ni nafsi inaemlaumu sahiba wake ikifanya jambo la shari na pia humlaumu sahiba wake ikifanya jambo la kheri”.(Angalia tafsiri ya Ibn Kathir kwenye aya hii)

Sehemu ya kwanza ya maana hii ni dhahiri.  Sasa vipi nafsi humlaumu sahiba wake ikifanya kheri. Sufiyaan Thauriy anasema, “ hakuna muumini yoyote atakaefanya jambo la kheri isipokuwa nafsi yake itamlaumu kwa nini haikufanya zaidi”

Mfano  mja labda ametoa sadaka Shilingi mia. Nafsi hulaumu vipi mbona ametoa mia wakati hana kitu nyumbani? Na Nafsi hiyo hiyo inaweza kulaumu kwanini ametoa mia badala ya kutoa alfu haoni kama mia ni kidogo? . Maana hii ya pili ndio inayokusudiwa na Said ibn Jubayr na kusisitizwa na Sufiyan Thawriy. Na hii ndio nafsi ya muumini wa kweli kwani mpaka kwenye khairaat (mambo ya kheri) bado inalaumu na kuisisitizia kufanya ziada kwani inaona bado ina upungufu.  

Lakini ile nafsi iliyoridhika na hali yake ikawa haijali lawama za Allah (Subhaanahu Wata’ala) hiyo ndio itakayolaumiwa.

3. NAFSI ILIYO NA UTULIVU

Nafsi hii ni nifsi iliyotulizwa na imani ya kweli na ambayo daima inarudi kwa mola wake huku ikiwa na subira ,uvumilivu haina khofu za kidunia wala huzuni ,hupenda kutubu na kuommba maghfira wakati inajitayarisha na kukutana na mola wake.

Nafsi hii huburudika pale anapotajwa Allah (Subhaanahu Wata’ala). Pia huwa nyepesi kurudisha kwa mola wake kila jambo linalosibu ima kwa kushukuru au kwa kusubiri; jambo hilo liwe zuri au baya . Hii ndio nafsi iliyosifiwa kwa sifa ya utulivu ndani ya Quraan

يأَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ ارْجِعِى إِلَى رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً   فَادْخُلِى فِى عِبَادِى وَادْخُلِى جَنَّتِى

“Ewe roho iliotulia, rudi kwa Mola wako katika hali ya kuwa radhi na kuridhika, ingia pamoja na waja wangu, ingia katika pepo yangu”  Al fajr 27-30

Nafsi hii Qatada anaielezea kwa kusema “Ni roho ya muumini iliyotulizwa na yale aliyoahidi Allah(Subhaanahu Wata’ala). Roho hii imekubali na kusalimu amri kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) wala huwa haina kinyongo wala kulalamika.  Haioni haja ya kufurahi ikipata jambo zuri na wala haioni haja ya kulalama inapopata mitihani kwani tayari inaelewa kwamba kila kitu chake tayari kimeandikwa hata kabla ya kutokea na hata kabla ya yeye kuumbwa, kama ilivyo katika Aqidah (imani) ya muislamu na mafundisho ya Quraan Attawabah/51

 قُل لَّن يُصِيبَنَآ إِلاَّ مَا كَتَبَ اللَّهُ لَنَا هُوَ مَوْلَـنَا وَعَلَى اللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ

Sema: Halitusibu ila alilo tuandikia Allah. Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na Waumini wamtegemee Allah tu!

Amani na utulivu wa nafsi hii unapatikana katika imani, ikhlasi, taqwa, ibada na unyenyekevu. Vitu hivi vinamjengea binadamu mazingira mazuri ya kuwa na uwezo na nguvu dhidi ya nafsi yake na kuipa upendeleo.  Utulivu huu hauruhusu kabisa kupenya kwa mawazo machafu. Haina wasi wasi wala woga kwa yale iliyoyafanya hata ikiwa yasiyomridhisha Mola kwani utulivu huu humfanya ielekee moja kwa moja kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) na kurudi kwake kwa toba na maghfira.

Nafsi iliyotulia kwa kubahatika kuwa na ukumbusho wa kila siku na kuzingatia ukumbusho huo hufahamu fika kwa nini imeumbwa, nini inatakiwa ifanye/itarajie kukabiliana tokea kuzaliwa, kufariki mpaka kufufuliwa

Nafsi hii ina mpenzi wake, Malaika, huisaidia na kuiongoza.  Malaika huipa nafsi hii msukumo katika kutamani yaliyo mazuri na kuweka wazi faida zake na kuitahadharisha na mabaya na athari zake.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget