Wednesday, April 4, 2012

Mimi ni Msikiti (Nyumba ya Allah)


Sifa njema zote zamstahikia ar-Rahmaan aliyetukuka na shukurani zangu za dhati kwake ar Rahiym kwa kunijaaliya mimi (msikiti) kuwa jengo tukufu hapa ardhini, jambo ambalo limeniwezesha kupata utukufu wa namna yake, kwani kila nikitaja huwa ninataja kwa kuegemeshwa na jina la Mtukufu wa kweli kweli, Allah Subhanahu Wata’ala (nyumba ya Allah).                                                    

Rehma na Amani za Allah zimfikie al-Habibi Musttafa (Salla Llahu’Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) Mbora aliyesali ndani yangu na aliyeniimarisha (mimi msikiti) kwa kila namna ya kuniimarisha kwa kuitikiya wito aliopewa na Mola wangu na wako ar Rahmaan, Qur-an inasema:

إِنَّمَا يَعْمُرُ مَسَاجِدَ اللّهِ مَنْ آمَنَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَأَقَامَ الصَّلاَةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَلَمْ يَخْشَ

                                              إِلاَّ اللّهَ فَعَسَى أُوْلَـئِكَ أَن يَكُونُواْ مِنَ الْمُهْتَدِينَ

   “Hakika wanao amirisha misikiti ya Allah ni wale wanao muamini Allah, na Siku ya Mwisho, na wakashika (wakasimamisha) Sala, na wakatoa Zaka, na wala hawamchi ila Allah. Basi huenda hao wakawa katika waongofu” at Tawbah aya ya 18.

Rehma na Amani za Allah zimfikie al-Habibi Musttafa (Salla Llahu’Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) aliyetowa tangazo la fakhari kwa kusema kuwa miongoni mwa mambo aliyopewa ambalo hakuwahi kupewa Mtume ye yote yule kabla yake ni kujaaliwa ardhi yote kuwa mimi (msikiti), kwa kutangaza:

أعطيت خمسا، لم يعطهن أحد من الأنبياء قبلي: نصرت بالرعب مسيرة شهر، وجعلت لي الأرض مسجدا وطهورا وأيما رجل من أمتي أدركته الصلاة فليصل، وأحلت لي الغنائم، وكان النبي يبعث إلى قومه خاصة، وبعثت إلى الناس كافة، وأعطيت  

                                                                                               الشفاعة)                                                                         .  

“Nimepewa mambo matano; hakuwahi kupewa (mambo hayo) yo yote yule katika Mitume kabla yangu; Nimenusuriwa (nimepewa ushindi kwa njia ya kutiwa maaduwi zangu hofu na woga) na ar Ru’b (woga/khofu) umbali wa mwezi; na imejaaliwa kwangu ardhi kuwa ni msikiti na ni kitwaharisha (kwa tayammam) basi mtu ye yote yule katika umma wangu itakapomkutia sala anatakiwa asali, na nimehalalishiwa ngawira, na alikuwa Mtume akitumwa kwa watu wake tu, nami nimetumwa kwa watu wote duniani” Imepokelewa na Bukhari, Milango ya Misikiti, mlango wa Qawlin Nabiyyi imejaaliwa kwangu ardhi….

 Ayuhal Ahibaa,

 Mgeni wetu mtukufu tuliye jaaliwa kuishi na kukaa naye kwa hamu na shauku kubwa katika masiku yake matukufu ndio ameshaondoka katika majumba yetu, makazini mwetu, maskuli kwetu, mabarazani mwetu, majiyani mwetu, na kadhalika, kwa Amani na Usalama insha Allah. 

 Ndugu yangu katika iman, alipokuwa mgeni mtukufu yu pamoja nawe ulijaaliwa kujenga (kuanzisha/kuasisi), kutengeneza na kuimarisha uhusiano na urafiki mkubwa baina yangu (mimi msikiti) na nafsi yako, uhusianao (urafiki) ambao nilikuwa nikitarajia, na kutegemea kuwa utaendelea kwa kuimarishwa, kuenziwa na kudumishwa hata baada ya mgeni wetu mtukufu kuondoka.

 Ndugu yangu katika iman, mimi(msikiti) nilikuwa nafurahi na ni kawaida yangu kufurahi sana na kuona fakhari na shauku, sifa na raha isiyoelezeka kila ulipokuwa ukinitembelea katika masiku machache na matukufa.  Nilikuwa nahisi raha na shauku kubwa kila unapoingia ndani yangu na kutumia maji yangu, kukaa ndani yangu na kadhalika. Nilikuwa nikijisika vizuri na kujifakharisha na kujitukuza mbele ya majengo yote unayoyatumia katika maisha yako ya kila siku, kwa kuona kuwa mimi (msikiti) ndiye unae nipenda na ni mwenye nafasi kubwa katika nafsi yako (moyo) kulinganisha na majengo yote yaliyopo hapa duniani.

 Ndugu yangu katika iman, ilikuwa ni matarajio yangu makubwa kuona kuwa uhusiano na urafiki wako kwangu hautosimama wala vunjika, bali utaimarishwa kwa kuendelezwa, kuenziwa na kudumishwa, nilikuwa natarajia kuwa mapenzi yako kwangu na nafasi yangu katika moyo wako haitabadilika mara tu baada ya kuondoka mgeni wangu na wako (Ramadhan) mtukufu. Nilikuwa natarajia kuwa utaweza kwa hali na mali kuyathibitishia majengo yote yaliyopo hapa ardhini kuwa, hata kama unapata nafasi ya kuyatembelea na kutumia yaliyomo ndani yake mara kwa mara kila siku, lakini kwa hakika moyo wako umefungamana na mimi (msikiti) na kutarajia kuwa miongoni mwa watu hawa aliowaorodhesha al-Habibu Musttafa (Salla Llahu’Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) wakati aliposema:

 

سبعة يظلهم الله تعالى في ظله يوم لا ظل إلا ظله: إمام عدل، وشاب نشأ في عبادة الله، ورجل قلبه معلق في المساجد، ورجلان تحابا في الله، اجتمعا عليه وتفرقا عليه، ورجل دعته امرأة ذات منصب وجمال، فقال: إني أخاف الله، ورجل تصدق بصدقة، فأخفاها حتى لا تعلم شماله ما تنفق يمينه، ورجل ذكر الله خاليا ففاضت عيناه

 “Watu saba (7) atawafunika na kivuli chake Allah siku itakayo kuwa hakuna kivuli isipokuwa kivuli chake Yeye pekee: Imamu (kiongozi) muadilifu, Kijana aliyekua ndani ya ibada ya Mola wake (katika kumuabudu Allah), Mtu ambae moyo wake umetundikwa katika kuipenda (umefungamana na) misikiti, Watu wawili waliopendana kwa ajili ya Allah, wamekutana (wamekaa pamoja) kwa ajili yake Yeye na wametengana (kuwa mbali mbali) kwa ajili hiyo hiyo, Mtu aliyetakiwa na mwanamke mwenye cheo na uzuri (urembo) wa kuvutia kimapenzi, akamkatalia kwa kumwambia: Hakika mimi namuogopa Allah, Mtu aliyetoa Sadaqah akaificha (kwa siri ya hali ya juu kabisa) hata mkono wake wa kushoto ukawa hauelewi kilichotolewa na mkono wa kulia, na Mtu aliyemkumbuka (amemtaja) Allah hali ya kuwa yu peke yake na macho yake yakatokwa (yakabubujika) machozi ”Imepokelewa na Bukhar, kitabu cha Zakkah, mlango wa as Sadaqah bil Yamiyni.

Ndugu yangu katika iman, ulikuwa huna raha wala utulivu bila ya kunitembelea mimi (msikiti), ulikuwa unatumia wakati wako mwingi ndani yangu, hata wakati mwengine ulikuwa ukila na kulala ndani yangu na kunifadhilisha mbele ya nyumba yako na ahli zako.

 Ndugu yangu katika iman, hali yako ilikuwa kama hiyo au zaidi ya hiyo na wewe na nafsi yako ndio unaielewa zaidi. Hali yako ilinitia tamaa na kuhisi kuwa uhusiano wetu hautopata mchochezi wa kukuchochea na kukutia maneno au fitina kupelekea kuuvunja au kuusimamisha.  Hali yako ilinitia tamaa na kuhisi kuwa urafiki wetu ni wakudumu insha Allah.  Hali yako ilinitia tamaa na kuona kuwa maji yangu na viliomo ndani yangu vitaendelea kutumiwa, jambo ambalo hunihuzunisha na kunifanya niwe na wivu kama hakuna mtumiaji, au kama watumiaji wake ni wachache, au ni wale kwa wale katika miezi yote ya mwaka, na kupatikanwa kwa watumia wa huduma zangu wengi (kama wapangaji) na wapya (kila kinapofunguliwa chuo kikuu cha Ramadhan) kila anapo tutembelea mgeni wetu mtukufu.

 Ndugu yangu katika iman, hivyo ni kweli ulikuwa ukinitembelea kwa kuwa tu palikuwa hapana pa kwenda katika masiku machache na matukufu ya Ramadhan!  Hivyo kweli ulikuwa ukinitembelea kwa kuwa ni pahala pekee penye kunasibiana na mwenye kuishi na kukaa na Ramadhan!  Hivyo ni kweli ulikuwa ukinitembelea bila ya kunielewa mimi ni nani!

 Ndugu yangu katika iman, kama hiyo ndio ilikuwa hali yako, napenda kukueleza na kukuarifu kuwa mimi (msikiti) nilistaajabu sana na kupata huzuni kwa kukuona mara tu baada ya kuondoka mgeni wetu mtukufu (Ramadhan) umenibadilikia ghafla na kujifanya kama kwamba hunijuwi wala hunielewi (sala yako ya ‘Iyd ilikuwa ndio maagano yetu kama uliisali ndani yangu), kama kwamba hujapata kuniona wala kusikia kuhusu mimi hata siku moja katika uhai wako, unajifanya kama vile mimi sio miongoni mwa wenye kustahiki kutembelewa na kupendwa na kuwa na uhusiano wa aina yake na wewe (siku hizi husali ndani yangu –msikiti- ila Ijumaa na wakati mwengi hata hiyo Ijumaa sikuoni habibi), bali kuwa na uhusiano wa karibu zaidi ya nyumba yako.

 Ndugu yangu katika iman, kwa kuiona hali yako yenye kunisikitisha, kunihuzunisha, kunikatisha tamaa na kunifanya nisielewa cha kufanya, nimeonelea ni vyema leo nichukuwe fursa hii ‘adhimu kujitambulisha kwako jambo ambalo natarajia litakupelekea kunielewa na kuweza kukutia hamu na shauku ya kurudisha mahusiano yetu na urafiki wetu uliokuwa katika masiku machache na matukufu ya Ramadhan na kufanya kila uliwezalo katika kuuimarisha uhusiano na urafiki wetu jambo litakalo kupelekea kunipa nafasi katika moyo wako na kurudi kunitembelea ili uweza kuwa miongoni mwa wale walio orodheshwa na al-Habibu Musttafa (Salla Llahu’Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) katika hadithi iliyotangulia.

Ndugu yangu katika iman, mimi (msikiti) ndio jambo la kwanza na la pekee alilolifanya al-Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam), mara tu baada ya kuhama kutoka katika Mji mtukufu wa Makkah na kuhamia Madinah.  Yote ni kwa kuwa mimi ndio msingi madhubuti (pahala) katika kuthibitisha umoja, usawa, nguvu, udugu, mapenzi na kadhalika katika jamii ya kiislamu. 

Ndugu yangu katika iman, Uislamu unahimiza yote haya (usawa, udugu, uadilifu na kadhalika) baina ya waislamu (na wasio), na pahala pa kwanza na mwisho penye uwezo wa kuyathibitisha kivitendo (na sio kimaandishi, kikatiba na kisheria) haya ni ndani yangu (msikitini), kwani humo ndani yangu (msikiti) unatarajiwa kukutana na waislamu wenzako kila siku Saffan Waahidan (safu moja) kama jengo lililo kamatana (mkubwa, mdogo, mweusi, mweupe, tajiri, masikini, kiongozo, raiya, mpemba, mmasai, wepya, wakukuu na kadhalika) huku mukisimama mbele ya Mola wangu na wako. 

Ndugu yangu katika iman, ndani yangu (msikiti) hukusanyika waislamu kupanga na kujifunza mambo mengi yakiwemo Sharia za Allah ili wapate kushikamana nazo kwa ujuzi, elimu na utekelezaji katika maisha yao ya kila siku.  Ndugu yangu katika iman, mimi          (msikiti) ni pahala muhimu, penye kutegemewa na madhubuti pa kuwakusanya wewe na waislamu wenzako katika kupanga, kuandaa, kutafakari na kufanikisha karibu mambo yenu yote (yawe ya hapa duniani au ya baadae kama walivyokuwa wakifanya walio kutangulieni).

Ndugu yangu katika iman, mimi (msikiti) ndio jengo la pekee katika majengo yaliyomo ardhini ambalo kila mwenye kunijenga na akawa anatafuta radhi za Allah katika kunijenga huko, basi Allah atamjengea nyumba ambayo hatoikaa isipokuwa yeye, kwani itajengwa pahala ambapo una uhakika wa kwenda.  Wangapi katika nyinyi mmejenga majumba na maqasr (palaces) ya maajabu, na hamuko tayari kukaliwa na watu wenu (kwa visingizio mbali mbali vikiwemo, washamba wale wataharibu wall papers, watakaa bure mimi napindwa huku, mimi sili vizuri, sivai vizuri, sendi holiday, silali kwa kazi na kadhalika) wachilia mbali kukaa nyinyi wenyewe ambao muko mbali nayo! 

Ndugu yangu katika iman, umejenga qasr lako kwenu wala huna uhakika wa kurudi wachilia mbali kulikaa, huoni bora na vyema ukajenga qasr pahala ambapo una uhakika wa kwenda (sote tutarudi kwa Mola wangu na wako)! Hapa ulipo (duniani) hata uishi miaka elfu kasoro miaka khamsini (950) kuna siku utaondoka kama walivyo ondoka waliokuwa kabla yako wewe na mimi, unalipa fedha nyingi (mapauni, madolari, mayuro, mariyali, madirhamu) upatiwe mhandisi mwenye ujuzi wa hali ya juu katika fani ya uchoraji na ujenzi, huoni bora kumpa kazi hii Mjuzi wa kila kitu akujenge Qasr la aina yake,  al-Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) anasema:

“Aliyejenga msikiti na anatafuta kwa msikiti (ujenzi) huo ridhaa za Allah, basi Allah atamjengea nyumba mfano wake (kama hiyo aliyoijenga) huko Peponi” Imepokelewa na Muslim, Kitabu cha Misikiti na mahala pa sala, mlango ubora wa kujenga Misikiti na kuihimiza.

Ndugu yangu katika iman, wewe si mwenye kunijenga mimi (msikiti), wala si mwenye kuhimiza wengine kufanya hilo, basi habibi hata kuwa katika wenye kunitembelea unashindwa!  Kuondoka kwa mgeni wetu Ramadhan kumekufanya uwe huna hamu wala shauku ya kunitembelea!  Hivyo kweli huelewi kuwa mwenye kunitembelea wakati wo wote ule huwa anafutiwa makosa yake na kunyanyuliwa daraja yake! al-Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) anasema:

“Atakae toka mapema kwenda msikitini na akarudi Allah atamuandalia makazi peponi kila anapoenda au anaporudi” Imepokelewa na Muslim, Kitabu cha Misikiti na mahala pa sala, mlango wa kwenda kwa miguu msikitini kusali kunafuta makosa.

Ndugu yangu katika iman, umewacha kunitembelea mimi (msikiti) baada tu ya kuondoka Ramadhan kwa visingizio mbali mbali, huku ukitembelea majengo yote yaliyoko juu ya ardhi!  Watembelea majengo mengi (maskuli, maosifi, majumba ya kazi, mahoteli, mikahawa, majumba ya jamaa na marafiki na kadhalika kila siku) yaliyo masafa marefu (masaa wawili au matatu) na mbali na nyumba yako (meli au kilo mita 5 na zaidi) kwa kutafuta mahitaji mbali mbali, lakini kwanini uwe unajifunga na kujitundika na mahitaji ya hii dunia tu ambayo utaiondoka bila ya shaka wala wasi wasi na ni ya muda mfupi (ni ya kupita)! Kwanini usijishughulishe pia na kutafuta mahitaji ya kudumu ambayo utayapata au itakuwa wepesi kwako kuyapata au kuyafikiria na kujiandaa nayo ukinitembelea mimi (msikiti)! al-Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) anasema:

“Mwenye malipo zaidi katika sala, ni yule anae kaa mbali zaidi, na anae tembea zaidi mbali kufuata sala, na yule anae isubiri sala mpaka akaisali pamoja na Imamu malipo yake ni makubwa zaidi …” Imepokelewa na Muslim, Kitabu cha Misikiti na mahala pa sala, mlango ubora wa wingi wa hatua za kwenda msikitini, pia al-Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) anasema:

“….. Mmoja wenu atakapo tawadha (kutia udhu) akafanya vizuri (katika udhu wake, akatawadha kama alivyofundisha al-Habibu Musttafa Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) na akaenda msikitini hakuna kilichompeleka isipokuwa sala (sio nikisali msikiti ule nitawaona jamaa wengi, kwani hatuonani, kila mtu yuko busy), basi hatoinua mguu wake kuvuta hatua isipokuwa Allah kwa kila hatua atamuinua daraja na atamuondoshea (atamfutia) kosa mpaka anaingia msikitini na akishaingia msikitini atahesabiwa kuwa yuko katika sala kwa muda wa kuwa sala ndiyo inayomzuia, na Malaika wanamuombea Rehma kwa kubaki mahala pake pale pale aliposali, kwa kusema: Ewe Mola wetu Msamehe, Ewe Mola wetu Mrehemu, Ewe Mola wetu Mkubalie tawbah yake, kwa muda wa kuwa hajahuduthi (haujavunjika/ haujabatilika udhu wake)” Imepokelewa na Muslim, Kitabu cha Misikiti na mahala pa sala, mlango wa fadhila za sala ya jamaa na kusubiri sala.

Ndugu yangu katika iman, hivyo kweli hupendi kuombewa na wenye kukubaliwa maombi yao (Malaika)!  Kwanini umeacha tena basi kwa ghafla tu kunitembelea baada ya kunizoesha na kunitia hamu ya kukuona kila wakati na kila siku na siyo siku ya Ijumaa peke yake! 

Ndugu yangu katika iman, hata hiyo siku unayo nitembelea (siku ya Ijumaa) huwa unanitembelea wakati uutakao wewe (huji mapema ndani yangu, unajileta ili uwahi Rakaa na wakati mwengine hata hiyo Rakaa huiwahi) kwa visingizio vyako mbali mbali (tuko ulaya , nchi za nje huku) na kwa nia mbali mbali (Waswahili, Wazanzibari/Wapemba wote utawapata msikiti fulani, hivyo unakuja kukutana na jamaa zako badala ya kuja kunitembelea mimi na kusali), hivyo kweli ndugu yangu katika iman, huelewi kuwa mimi (msikiti) ni jengo la pekee katika majengo yaliyopo ardhini lenye kutembelewa siku ya Ijumaa na mtembeleaji akawa ni mwenye kutoa Sadaqah! kadiri ya umapema wa wakati utakao nitembelea na kuingia ndani yangu ndio kadiri ya ukubwa na aina ya Sadaqah uitowayo!  Ndugu yangu katika iman, wewe si mwenye kutoa sadaqah wachilia mbali Zakkah, je hutaki kuwa miongoni mwa wenye kuandikwa kuwa ametowa Sadaqah kwa kunitembelea mimi (msikiti) siku ya Ijumaa, al-Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) anasema:

من اغتسل يوم الجمعة غسل الجنابة ثم راح، فكأنما قرب بدنة، ومن راح في الساعة الثانية، فكأنما قرب بقرة، ومن راح في الثالثة، فكأنما قرب كبشا أقرن، ومن راح في الساعة الرابعة، فكأنما قرب دجاجة، ومن راح في الساعة الخامسة، فكأنما قرب                                       بيضة، فإذا خرج الإمام حضرت الملائكة يستمعون الذكر                                                                                             “Mwenye kuoga siku ya Ijumaa kama anavyooga janaba kisha akenda msikiti (katika nyakati za mwanzo mwanzo unakwenda na kuingia msikitini hakuna mtu isipokuwa wewe na mfunguwa mlango, kama vile saa nne za asubuhi), basi atakuwa kama ametoa (sadaqah) Ngamia, na atakae kwenda katika saa ya pili (watu washaanza kuwa kiasi) basi atakuwa kama aliyetoa (sadaqah) Ngo’mbe, na atakae kwenda saa ya tatu basi atakuwa kama ametoa (sadaqah) Kondoo mwenye pembe, na atakae kwenda wakati wa saa ya nne kama ametoa (sadaqah) kuku; na atakae kwenda wakati wa saa ya tano kama ametoa (sadaqah) yai; na Imamu anapojitokeza kwa kutowa khutbah basi (wakati wa kutoa sadaqah huwa umekwisha) wakati huo Malaika wanafika kusikiliza ad-dhikra” Imepokelewa na Bukhari, Kitabu cha Ijumaa, mlango wa fadhila za Ijumaa.

Ndugu yangu katika iman, sio kusudio langu kukuchokesha katika kunisikiliza, lakini hali yako ya kutoendeleza na kuimarisha uhusiano na urafiki wako na mimi (msikiti) uliokuwa wenye nguvu, wenye kila aina ya vivutio na mashirikiano ya hali na mali (hata uliamua kulala ndani yangu katika siku chache za mwisho za Ramadhan) ndio inayoniweka katika hali kama hii, hali ya kujaribu kujitambulisha kwako huenda ukarudisha uhusiano wako kwangu na kufunguwa tena ofisi zako za uwakilishi ndani yangu. 

Ndugu yangu katika iman, mwisho nimeonelea ni vyema nikutambulishe baadhi yangu (misikiti) ambayo ni bora kwa kila mwenye uwezo (kama wewe hapa ulipo) kunitembela kila ukipata wasaa (tafadhali usijifanye kuwa fedha zako zina mipango mengi na zina shughuli nyingi na huna fedha za kunitembelea mimi) kwani fadhila zake ni kubwa usizofikiria kama utawafikishwa kukubaliwa sala zako katika misikiti hiyo.

Ndugu yangu katika iman, umekwenda holiday ngapi ulizojaaliwa, umetembelea miji mingapi na majengo mbali mbali yawe ya historia au ya anasa, yawe na kisasa (millennium-dome) au ya kifakhari (Buckingham palace) na kadhalika, je katika matembezi yako hayo yote uliwahi kutembelea msikiti wo wote ule!  Je hutamani kunitembelea mimi (msikiti) mwenye kupendekezwa kutembelewa katika misikiti ya ardhi hii!  Hutamani kunitembelea mimi (msikiti) wa Makkah (al-Masjidil Haraam) au msikiti wa Madinah au msikiti wa al Aqswa, al-Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) anasema:

"Sala moja katika Msikiti wangu (Madinah) ni bora kuliko Msikiti mwengine kwa mara elfu isipokuwa Msikiti wa Makkah " imepokewa na an Nasaai, kitabu cha Misikiti, mlango wa fadhila za sala katika Masjidil Haraam.

 

Ndugu yangu katika iman, hutamani kunitembelea ukapata malipo kwa Mola wangu na wako na ukapata zawadi za kuchukuwa huko uendako, hutamani kunitembelea mimi (msikiti wa Makkah) niliye wekewa watu kuwa ni jengo la kwanza kwa ibada hapa dunia, Qur-an inasema:

 

                  إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ

“Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka, iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote.” Al-Imran  aya ya  96.

Ndugu yangu katika iman, tumuombe al-Mannan aliyetupa fursa nyengine ya kukutana baada ya kukutaka na kujuana wakati wa Ramadhan, tumuombe atujaaliye tuwe miongoni mwa wale walio fungamana nyoyo zao katika kuipenda misikiti na kuwa katika chama cha watu saba watakaofunikwa na kivuli siku isiyo kuwa na kivuli isipokuwa chake Yeye Subhanah kwa kutujaaliya kila tutokapo msikitini baada ya sala kuwa na hamu ya kuingia tena kwa ajili ya sala nyengine, twamuomba al Qariyb al Mujiyb atujaaliye katika nyoyo zetu kuwa ipo nafasi ya msikiti, atujaaliye tuwe wenye kuijenga, kuisimamia, kuimarisha, kusali ndani yake, kuitunza na kuhimiza wengeni katika hayo.

Twamuomba Mola wetu atusamehe makosa yetu, kwani Yeye ni al-Ghaffar, atukubalie ‘amali zetu na saumu zetu tulizofunga, twamuomba ar Rahmaan atujaaliye tuwe miongoni mwa wenye kuandaliwa makazi peponi kila twendapo na turudiapo misikitini, twamuomba Mwenye kupenda kuombwa al Waahyd al Ahadu As Samad asiye zaa wala asiye zaliwa atujaaliye tuwe wenye kufutiwa makosa yetu kwa kila hatua tuinuayo wakati twendapo msikitini na hakuna kinachotupeleka isipokuwa sala, twamuomba Allah kwa kila hatua zetu atuinuwe daraja na atufutie kosa.

Twamuomba Ar Rahmaan atujaaliye tuwe miongoni mwa wenye kutoa sadaqah siku ya Ijumaa kwa kwenda misikitini mapema, twamuomba aturehemee wazee wetu na waislamu wenzetu wote waliotutangulia mbele ya haki, atuwafikishe katika yote anayoyapenda na kuyaridhia, twamuomba al Hayyu al Qayyumu aliye weka nyumba ya mwanzo kwa ibada iliyo barikiwa na yenye uongofu kwa viumbe atuwafikishe kuwa miongoni mwa watakaojaaliwa kuitembelea nyumba hiyo na kukubaliwa matembezi yao na kila ‘amali zao watazojaaliwa na kuwafikishwa kuzitekeleza wakati  wakiwa katika matembezi hayo matukufu.

Amin ……….Amin………. Amin.


Wassalamu'alaykum Warahmatu Llahi Wabarakaatuh

Ndugu yenu katika iman

Mkusanyaji

Abu Faatimah

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget