Friday, April 20, 2012

Kisa cha Msikiti wenye jina la ajabu kupita yote Ulimwenguni

Kifuatacho ni kisa kilichoandikwa ndani ya kitabu kiitwacho 'Maajabu katika historia ya utawala wa Al Othmania (Ottoman empire)'.

Mwandishi wa kitabu hicho Ustadh Arukhan Muhammad Ali ameandika yafuatayo;

"Yupo kati yenu aliyewahi kusikia juu ya msikiti wenye jina la ajabu kama hili? Jina la msikti ni (Nishakula mimi).

Basi hili ni jina la msikiti uliopo katika eneo la Fateh katika mji wa Istanbul, na jina lake kwa lugha ya Kiturki ni 'Sanikiy Yadam', na maana yake (Nishakula mimi!), na sababu ya kupewa jina hili la ajabu ni kisa kizuri cha ajabu chenye ibra ndani yake kwa mwenye kuzingatia."

Anaendelea kusema Ustadh Arukhan;

"Katika kijiji hiki alikuwa akiishi mcha Mungu mmoja fakiri jina lake Khayruddin Kajji Afandi. Na sahibu yetu huyu alikuwa kila anapokwenda sokoni akatamani kununua tunda au nyama au haluwa, alikuwa akisema nafsini mwake; "Sanikiy Yadam', (Nishakula mimi!), kisha hanunui tena tunda lile au nyama ile au haluwa ile na badala yake hurudi nyumbani na kuziingiza pesa zenye thamani ya kununulia vitu hivyo ndani ya kisanduku chake na kuzidunduliza kidogo kidogo.

Na baada ya miaka mingi kupita huku akijinyima vyakula vya anasa visivyo vya lazima na kula vyakula vya dharura tu, pesa zile zikaongezeka akaweza kupata thamani ya kujenga msikiti mdogo kijijini pake.

Na kwa vile watu wa kijiji chake wanakijua kisa chake mcha Mungu huyu fakiri na namna alivyoweza kuujenga, wakaupa msikiti wake huo jina la; "Sanikiy Yadam', na maana yake; (Nishakula mimi!)."


Ibra tunayopata katika kisa hiki;

Kiasi gani cha pesa tungeweza kukusanya kwa ajili ya masikini na wenye kuhitaji misaada, na qasri ngapi tugeweza kujijengea huko Peponi Inshaallah, lau kama kila mmoja wetu baada ya kwisha kula, ataweza kujinyima kununua kile kisicho cha dharura, ambavyo ni vingi mno na kutenga thamani ya vitu hivyo kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zake?

Ndugu yangu Muislamu! Mtume wetu mtukufu (SAW) alikuwa mkarimu sana, na katika mwezi huu mtukufu alikuwa mkarimu kupita kiasi. Imepokelewa katika hadithi sahihi kuwa; 'Alikuwa mkarimu kupita upepo uliopelekwa (kwa ajili ya kueneza rehma na baraka kila mahala)'.

Jaribu kuifanyia kazi hadithi hii kwa kutenga kila siku kiasi kidogo tu cha pesa baada ya kuacha kununua baadhi tu ya vile visivyo vya lazima, tena baada ya kwisha kula, kisha kwa pesa hizo uingize furaha ndani ya nyoyo za ndugu zako wenye dhiki na shida ambao ni wengi sana! Na kwa njia hii utaweza kujijengea qasri nyingi huko Peponi – Inshaallah

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget