Saturday, April 7, 2012

Mtume (SAW) na haki za binadamu


Katika kifungu hiki cha mkataba wa Mtume na Wakristo wa Najran, licha ya kwamba mtukufu huyo alikuwa tayari amewashinda viongozi wa jamii ya Kikristo wa Najran na kuwathibitishia kwamba dini ya Kiislamu ndiyo ndini ya haki katika tukio la mdahalo (Mubahala) lililojiri kati ya pande hizo mbili, lakini Nabii Muhammad (saw) hakutumia tukio hilo kwa ajili ya kuwataka Wakristo hao wakubali na kuingia kwenye dini ya Kiislamu, bali alitoa ahadi ya kulinda dini, nafsi na mali zao.

Moja ya mambo ambayo Mtume wa Uislamu Muhammad (saw) aliyazingatia na kuyapa kipaumbele siku zote ni haki za watu. Kama ilivyonukuliwa katika mafundisho ya Uislamu, haki za Mwenyezi Mungu zinaweza kusamehewa lakini haki za watu haziwezi kusamehewa isipokuwa kwa ridhaa na msamaha wa walionyang'anywa au kukanyagiwa haki zao.
Hii leo dini ya Kiislamu inayosisitiza juu ya misingi hiyo muhimu inakabiliwa na hujuma na tuhuma za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwamba ni dini inayopuuza haki za binadamu.
Kwa kutumia mikataba na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Mtume (saw) na makundi mbalimbali, makala hii inajaribu kuthibitisha kwamba tangu zama za kale Waislamu wamekuwa wakifanya juhudi za kuheshimu haki za makundi ya waliowachache bali hata za kaumu na makundi yaliyoshindwa katika medani mbalimbali za mapambano. Kwa maneno mengine ni kuwa, Uislamu umekuwa ukifanya kila liwezekanalo kuheshimu haki za binadamu wote.
Historia imehifadhi barua na mikataba 185 ya Mtume Muhammad (saw) na makundi au jamii za watu mbalimbali. Maandishi hayo ambayo yanajumuisha barua, mikataba, wito na ulinganiaji wa mtukufu huyo kwa wafalme, watawala, viongozi wa makabila, miongozo, barua za kutoa dhamana ya amani na kadhalika, yanaakisi picha kamili ya maadili ya kisiasa na kijamii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw). Umuhimu wa maandiko hayo umo katika kudhihirisha misimamo aali ya kisheria na ya kisiasa ya Mtume Muhammad (saw). 
Japokuwa baadhi ya maandiko na barua hizo pia zina miongozo ya kimaadili na hata mafundisho ya teolojia ya Kiislamu, lakini masuala hayo pia yanaangaliwa katika fremu ya maadili ya kisiasa na kijamii ya Mtume Muhammad (saw). Maandiko na barua hizo pia zinadhihirisha tofauti ya barua zilizokuwa zikiandikwa na mtukufu huyo kwa wafalme na viongozi mbalimbali wa dunia ya wakati huo kama barua alizowaandikia viongozi na wafalme wa Kikristo mithili ya Muqawqis wa Misri na Heraclius mfalme wa Byzantine akiashiria aya ya 63 ya Al Imran inayosema: "Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa waola walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu," na pia barua alizowaandikia viongozi wengine kama Khosru Parvez wa Iran ya wakati huo.
Uchunguzi wa kina na uhakiki katika barua na maandiko hayo unaweza kuweka wazi sira na mwenendo wa Mtume Muhammad (saw) katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kijamii na masuala ya sheria na kuwa marejeo ya uandishi wa protokali za kisheria katika ulimwengu wa Kiislamu. Vilevile maandiko na barua hizo zinaweza kuwasilishwa katika jumuiya na taasisi za kisheria na kisiasa za dunia ya sasa hususan nchi zinazodai kustaarabika za Magharibi. Hata hivyo suala hilo linahitajia juhudi kubwa za wasomi na wanafikra wa Kiislamu.
Kwa hakika kuweka wazi kanuni na sheria za haki za binadamu za Kiislamu kwa kuzingatia suna na mwenendo wa Mtume (saw) kunawapa Waislamu uwezo wa kuamiliana vyema zaidi na changamoto mbalimbali za dunia ya sasa na pia kusahihisha sheria na kanuni zinazotawala dunia ya leo.
Ulimwengu wa Kiislamu unahitaji harakati kubwa ya mabadiliko na marekebisho ya kifikra. Harakati hiyo inapaswa kuwa na sifa mbili za uhakiki na utekelezaji. Katika hatua ya awali ulimwengu wa Kiislamu unahitajia wanafikra na wahakiki mahiri wanaoweza kuzama katika turathi kubwa ya dini hii kwa kutumia mbinu za kisasa za uhakiki na kunyambua kanuni za sheria zake. Katika hatua ya pili ulimwengu wa Kiislamu unahitajia weledi na wataalamu wenye uwezo wa kutekeleza kanuni hizo na kuzioanisha na sheria zinazokubalika za haki za binadamu za dunia ya sasa kama Hati ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Hata hivyo kazi hiyo ya kutekeleza na kuoanisha sheria za haki za binadamu za Uislamu na zile zinazotumiwa sasa duniani haina maana ya kubadili na kugeuza sheria na kanuni za Kiislamu kwa maslahi ya kanuni za kibinadamu za dunia ya sasa, la hasha; bali jambo hilo lina maana ya kutayarisha hati kamili ya kimataifa ya haki za binadamu ambayo si tu kwamba inakusanya na kujumuisha pamoja haki na majukumu ya mwanadamu katika uwanja huo, bali pia inatoa mwongozo na kuweka dira ya masuala ya kiroho ya kiumbe huyo katika kutumia haki zake.
Inaonekana kuwa dunia inayozipa thamani zaidi haki za mwanadamu kuliko wajibu na majukumu yake na kutanguliza mbele haki za mwadanamu huku ikifumbia macho wajibu na majukumu ya kiumbe huyo na jamii ya kibinadamu, au kuyapa majukumu na wajibu wake nafasi ya daraja la pili hukabiliwa na madhara na hatari kubwa sawa kabisa na yale yanayozikumba jamii zinazojali wajibu na majukumu ya mwanadamu pekee bila kujali haki za kiumbe huyo. Sheria za Kiislamu zinapima thamani ya haki katika mipaka yake na kamwe hazifumbii macho haki mkabala wa taklifu na wajibu wa mwanadamu au kutoa mhanga wajibu na majukumu yake mkabala wa haki za kiumbe huyo.
Jambo muhimu linalokosolewa na wanafikra na wasomi wa dunia ya sasa kuhusu maudhui ya haki za binadamu ni kwamba wasomi na wananadharia wa haki za kiumbe huyo hawapaswi kujali na kutoa kipaumbele tu kwa suala la “haki za mwanadamu” na kufumbia macho au kupuuza “wajibu na majukumu yake.” Wanafikra hao wanapaswa kuainisha wajibu na majukumu ya mwanadamu sambamba na kuweka wazi haki za kiumbe huyo. Kwani maadamu mwanadamu hajioni kwamba anawajibika na anapaswa kutoa maelezo mbele ya marejeo makhsusi kuhusu matendo na amali zake, hawezi kuelewa kwa undani kuhusu haki zake mwenyewe. Suala la kujua vyema haki linaambatana na kuchunga mipaka, na sharti la kuchunga mipaka na kuwajibika ni kuwa na haki. Wajibu na mipaka hiyo si jambo linalokabiliana na kupambana na haki bali ni wenzo unaomfikisha mwanadamu katika haki zake.
Aya za kitabu kitukufu cha Qur’ani na hadithi za Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu zimeweka wazi zaidi uhakika huo. Hapa tutaashira barua moja tu ya Bwana Mtume (saw) kama mfano wa ukweli huo na jinsi Uislamu unavyojali na kulipa umuhimu suala la haki za binadamu.
Barua hiyo ni ile ya mkataba wa Mtume Muhammad amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake na Wakristo wa Najran. Maandishi ya mkataba huu yameandikwa katika vitabu vya”al Kharaj” cha Abu Yusuf, “al Kharaj” cha Abu Ubaida, “Futuhul Buldan” cha Baladhiri, “Zadul Maad” cha Bin Qayyim, “Imtaa” cha Moqrizi, "Wathaiqus Siyasa al Yamaniyya” cha Muhammad bin Akuu’ Hawali, “Sunan Abi Daud”, “Tarikhul Yaaqubi” na marejeo mengine ya Kiislamu.
Imepokewa kwamba mkataba huo ulitiwa saini katika mwaka wa 9 Hijria baada ya tukio maarufu la Mubahala na mdahalo uliofanyika kati ya Mtume (saw) na Wakristo wa Najran, eneo lililoko katika mpaka wa Hijaz na Yemen. Mkataba huo peke yake ni mfano wa misingi inayotawala maadili ya kisiasa na kisheria ya Mtume wa Uislamu katika kuchunga na kuheshimu haki za binadamu.
Katika mkataba huo Mtume (saw) alikubaliana na Wakristo wa Najran kwamba watatoa jizia kwa ajili ya kulindwa mali na usalama wao. Mkataba huo pia unadhirisha rehma isiyokuwa na kifani, upendo na uadilifu mkubwa wa Kiislamu na dhamana ya haki sawa kwa Wakristo hao. Mfano wa rehma na upendo huo unaonekana katika kifungu cha kwanza cha mkataba huo. Kifungu hicho kinasisitiza kwamba kutokana na kuwa Wakristo wa Najran wameamua kusimamisha mdahalo na kumpa Mtume wa Mwenyezi Mungu hiari kamili ya kutoa hukumu na maamuzi kuhusu mapato, mali na milki zao (watumwa wao), mtukufu huyo anawapa mali na milki hizo zote na atatosheka tu kwa kuchua jizia ambayo si kwa sababu ameshinda, bali kutokana na majukumu yanayotajwa katika vifungu vinavyofuatia vya mkataba huo kwa ajili ya kuwadhaminia usalama wa mali na nafsi zao.
Sehemu muhimu ya mkataba huo unaolinda na kudhamini haki za watu wa Najran inajumuisha vipengee vifuatavyo:
1- Mtume wa Mwenyezi Mungu anaahidi kufidia mali za watu wa Najran zitakazotolewa kwa jeshi la Kiislamu kama amana kwa ajili ya kutumiwa katika kuzima fitina za kieneo iwapo amana hiyo itapatwa na dosari au kuharibiwa. Kipengee cha mkataba huo kinasema: “Wanajran watawaazima Waislamu ngao 30 za vita, farasi 30 na ngamia 30 iwapo kutatokea vita na mapigano huko Yemen, na iwapo amana hizo na mali nyingine zitaharibiwa, wajumbe na wawakilishi wangu watafidia uharibifu huo.”
2- Mtume Muhammad (saw) anatambua rasmi haki za watu wa Najran za kulindwa dini yao, usalama wa nafsi na kuheshimu mali zao. Mtukufu huyo anatoa ahadi ya Mwenyezi Mungu na kukubali kulinda nafsi, mali na dini ya watu wa Najran. Katika kifungu hiki cha mkataba wa Mtume na Wakristo wa Najran, licha ya kwamba mtukufu huyo alikuwa tayari amewashinda viongozi wa jamii ya Kikristo wa Najran na kuwathibitishia kwamba dini ya Kiislamu ndiyo ndini ya haki katika tukio la mdahalo (Mubahala) lililojiri kati ya pande hizo mbili, lakini Nabii Muhammad (saw) hakutumia tukio hilo kwa ajili ya kuwataka Wakristo hao wakubali na kuingia kwenye dini ya Kiislamu, bali alitoa ahadi ya kulinda dini, nafsi na mali zao. Mkataba huo unasema: “Ahadi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake itaheshimiwa katika kulinda mali, nafsi na dini za watu wa Najran na maeneo ya kandokando yake, waliopo na wasiokuwepo hapa, koo zao, maeneo yao ya ibada na kila wanachomiliki.”
3- Mtume (saw) alitambua rasmi haki za makasisi, mapadri na makuhani za kutekeleza kazi zao za kidini na wala hakuwazuia kazi hizo au kuwataka wasimamishe shughuli zao. Mkataba huo unasema: “Kiongozi yoyote wa dini ya Kikristo hataachishwa kazi au kuondolewa katika cheo na nafasi yake.”
4- Sehemu nyingine ya mkataba wa Mtume (saw) na Wakristo wa Najran inabainisha kaida ya kisheria inayowaondolea watu hao wa Najran mzigo wa kulipa fidia ya damu iliyomwagwa katika zama za ujahilia (zama za kabla ya Uislamu). Mkataba huo unasema: "Wanajrani hawatalazimika kulipa fidia ya damu iliyomwagwa katika zama za ujahilia."
5- Mtume wa Uislamu aliwadhaminia Wakristo wa Najran na kuahidi kutekeleza haki ya kimsingi kabisa ya kisiasa ya taifa lolote lile, yaani haki ya kuishi katika ardhi yao na kufaidika na amani na usalama. 
Mkataba huo unasema: "Watu wa Najran hawataondolewa katika ardhi zao, hawatatakiwa kulipa asilimia kumi ya mapato yao na ardhi yao haitavamiwa. Kila mtu anayewadai haki, suala hilo litachunguzwa kwa insafu na uadilifu bila ya wao kudhulumu wala kudhulumiwa."
Mwishoni mwa mkataba huo pametajwa masharti ya kudumishwa na kuimarishwa kwake. 
Japokuwa kidhahiri jambo hilo linaonekana kuwa ni sharti, lakini kimsingi ni sisitizo juu ya umuhimu wa misingi ya kimantiki inayotiliwa mkazo na vitabu vya mbinguni kikiwemo kitabu cha Wakristo wenyewe. 
Sharti hilo linasema: "Tangu sasa na katika siku za usoni kila mtu atakayechukua riba atakuwa ameondoka katika dhamana yangu, na hakuna mtu atakayehukumiwa kwa makosa yaliyofanywa na mtu mwingine."
Katika kipengee hiki Mtume Muhammad (saw) analitaja suala la kutokula riba kuwa ni sharti na kudumishwa na kuendelezwa mkataba huo, na hii si kuwatishwa sharti Wakristo wa Najran kama inavyoweza kudaiwa na badhi ya maorientalist, bali ni kuwarejesha Wakristo hao katika mafundisho ya dini ya Nabii Issa inayokataza maovu kikiwemo kitendo kiovu cha kula riba.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget