Friday, April 20, 2012

Ndoa haramu..

Katika zama za ujahilia kabla ya kuja Uislamu ndoa nyingi zilikuwa zikifanyika ambazo hazikufuata sheria alizohukumu Mwenyezi Mungu S.W.T. zifuatwe. Na kwa sababu hizo ndio maana ulipokuja Uislamu Mtume wetu S.A.W. aliwakataza Waislamu wa zama zake. Na zifuatazo hapo chini ni ndoa ambazo Mtume S.A.W. kazikataza kabisa kwa sababu ni kinyume na sheria ya Kiislamu nazo ni:-

1. NDOA YA MUT`A.
Ndoa ya Mut`a (المتعة) ni ndoa ya haramu na batili iliyokuwa maarufu sana katika zama za ujahilia kabla ya kuja Uislamu. Ulipokuja Uislamu uliruhusu kwenye baadhi ya vita tu kwa dharura. Lakini baada ya hapo ukaharamisha mpaka siku ya Kiyama. Kwani ndoa ya aina hii haina talaka, wala mwanamke kukaa eda na wala kurithiana. Nayo inatokea kwa mapatano kati ya mume na mke kuwa wataoana kisha wataishi kwa muda fulani na kwa kiasi fulani cha mahari baadaye wataachana. Na ndoa ya namna hii inaitwa kwa Kiarabu, “Mut`a,” na kwa Kiswahili, “Kuoa kwa muda mfupi.” Na Mtume S.A.W. aliikataza ndoa ya aina hii na akawapigia marufuku Waislamu wote tokea katika zama za vita vya Kheibar ikiwa ni pamoja na kula nyama ya punda wa kufugwa majumbani. Kama ilivyothibiti katika Hadithi iliyopokelewa na Seyyidna Ali bin Abi Twaalib R.A.A. na waliyokubaliana Wanavyuoni wote, “
‘‘أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى عَنْ مُتْعَةِ النِّسَاءِ وَعَنْ لُحُومِ الْحُمُرِ الأهْلِيَّةِ زَمَنَ خَيْبَرَ’’
Maana yake, “Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amekataza ndoa ya mut`a (muda mfupi) na (kula) nyama ya punda wa (kufugwa) majumbani (tokea) katika zama za vita vya Kheibar.”

2. NDOA YA KUOZANA MADADA AU MABINTI.
Ndoa ya aina hii inatokea wakati mtu anapomshurutishia mtu mwingine kwa kumwambiya, “Niozeshe dada yako nami nikuozesha dada yangu,” au kusema, “Niozeshe binti yako nami nikuozesha binti yangu,” bila ya kutoa mahari nayo ni ndoa ya haramu. Na kwa lugha ya Kiarabu inaitwa, “Shighaar.” Na jambo linalosababisha kubatilisha ndoa ya aina hii ni msemo na msimamo. Kwani inakuwa kama vile kila mmoja wao anasema, “Ndoa yako haifungiki na binti yangu mpaka kwanza mimi nifunge ndoa na binti yako,” ambapo haiwezekani kabisa kwa sababu nani kati yao atakaeanza kufunga ndoa? Na yule atakaeanza kufunga ndoa basi mwingine hapati kuoa! Na ikiwa wameoana mume na mke basi watakuwa wamekwenda kinyume na sheria aliyokuja nayo Mtume wetu S.A.W. kwa hivyo lazima waachanishwe mume na mke. Na ikiwa mume kawahi kumuingilia mkewe basi mke kaharamika na hapo inakuwa lazima watenganishwe wasikutane kabisa. Mtume S.A.W. kaikataza kabisa ndoa ya aina hii ya kushurutishana kuozana madada au mabinti bila ya mahari. Na uthibitisho huu umekuja katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na Muslim, “

‘‘نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنِ الشِّغَارِ ، وَالشِّغَارُ أَنْ يَقُولَ الرَّجُلُ لِلرَّجُلِ : زَوِّجْنِي ابْنَتَكَ وَأُزَوِّجُكَ ابْنَتِي ، أَوْ زَوِّجْنِي أُخْتَكَ وَأُزَوِّجُكَ أُخْتِي’’
Maana yake, “Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amekataza ndoa ya mwanamume kumwambiya mwanamume (mwingine): “Niozeshe binti yako nami nikuozeshe binti yangu.” Au “Niozeshe dada yako nami nikuozeshe dada yangu.”

Na pia Hadithi nyingine iliyopokelewa na Ibn `Umar R.A.A. na kutolewa na Muslim, “

‘‘أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى عَنِ الشِّغَارِ وَالشِّغَارُ أَنْ يُزَوِّجَ الرَّجُلُ ابْنَتَهُ عَلَى أَنْ يُزَوِّجَهُ ابْنَتَهُ وَلَيْسَ بَيْنَهُمَا صَدَاقٌ’’
Maana yake, “Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amekataza ndoa ya mwanamume kumuozesha binti yake ili naye amuozeshe binti yake (au dada yake) na baina yao bila ya mahari.”

3. NDOA YA MWANAMKE ALIEACHWA TALAKA TATU.
Ndoa ya aina hii inatokea wakati mume wa kwanza anayeitwa kwa Kiarabu Muhallal (mwenye kuhalalishiwa) anapopanga kwamba mkewe alieachwa kwa talaka tatu aolewe na mume mwingine anayeitwa kwa Kiarabu Muhallil (mwenye kuhalalisha) kwa muda fulani na kwa mahari fulani kisha mke aachike ili apate kurejea kwa Muhallal. Ndoa ya namna hii ya kupanga kwa mipango ya hila haijuzu katika sheria ya Kiislamu, ila ikiwa mke yule ataolewa na mwanamume mwingine kwa khiari yake na aachike kwa ridhaa yake au mume yule yamfike mauti. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Baqarah aya ya 230, “

فَإِنْ طَلَّقَهَا فَلا تَحِلُّ لَهُ مِنْ بَعْدُ حَتَّى تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ…
Maana yake, “Na kama amempa talaka (ya tatu) basi (mwanamke huyo) si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine…” 

Na wote wawili Muhallal na Muhallil wanalaaniwa na Mwenyezi Mungu S.W.T.. Kwa kauli ya Mtume wetu S.A.W. na uthibitisho umekuja katika Hadithi iliyopokelewa na Seyyidna Ali bin Abi Twaalib R.A.A. na kutolewa na Abu Daud, “

‘‘أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : لَعَنَ اللَّهُ الْمُحَلِّلَ وَالْمُحَلَّلَ لَهُ’’
Maana yake, “Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. kasema “Mwenyezi Mungu amemlaani anayehalalisha na anayehalalishiwa (katika ndoa za haramu).” 

4. NDOA YA MTU KATIKA IHRAAM.
Ndoa ya aina hii inatokea wakati Mwislamu anapotaka kuoa naye kahirimu kwa ajili ya Hija au Umra. Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Sayyidna `Uthmaan bin `Affaan R.A.A. na iliyotolewa na Muslim,“

‘‘لا يَنْكِحُ الْمُحْرِمُ وَلا يُنْكَحُ وَلا يَخْطُبُ’’
Maana yake, “Haowi aliyehirimu na wala haozeshwi na wala hachumbii.”

5. NDOA KATIKA EDA.
Mwenyezi Mungu S.W.T. amemkataza mwanamume Mwislamu kumuoa mwanamke wa Kiislamu wakati anapokuwa katika eda ya talaka au eda ya kifo cha mumewe kwani ndoa ya namna hizi mbili ni haramu, mwanamke anaruhusiwa kuolewa na mwanamume mwingine wakati kakamilisha eda yake. Kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu S.W.T., kasema katika Suratil Baqarah aya ya 235, “

…وَلا تَعْزِمُوا عُقْدَةَ النِّكَاحِ حَتَّى يَبْلُغَ الْكِتَابُ أَجَلَهُ…
Maana yake, “…Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka muda ulioandikwa (katika eda) ufike mwisho wake...” 

6. NDOA BILA YA WALII.
Kwa sheria ya Kiislamu haimfalii mwanamume Mwislamu kumuoa mwanamke wa Kiislamu bila ya idhini ya walii wake, kwani ndoa ya namna hii ni batili kwa sababu ya kupungua nguzo katika nguzo za ndoa. Kwa kauli ya Mtume S.A.W. katika Hadithi iliyotolewa na L-Bukhari, Muslim, Nnasaai, Ibn Majaah, Haakim na Ibn Habbaan, “

‘‘لا نِكَاحَ إِلا بِوَلِيٍّ’’
Maana yake, “Hapana ndoa ila kwa walii (wake).”

7. NDOA YA MWANAMKE MUSHRIKA.
Mwenyezi Mungu S.W.T. amemharamishia mwanamume Mwislamu kuoa mwanamke Mushrika (anayeabudu masanamu), wala Majusia (anayeabudu moto), wala Saabia (anayeabudu nyota), wala Budhia na wala Burhamia. Na vile vile imeharamishwa kwa mwanamke wa Kiislamu kuolewa na mwanamume Mushrik (anayeabudu masanamu). Kama alivyokataza Mwenyezi Mungu S.W.T., kasema katika Suratil Baqarah aya ya 221, “
وَلا تَنكِحُوا الْمُشْرِكَاتِ حَتَّى يُؤْمِنَّ…
Maana yake, “Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini …” 

Na hekima ya kukatazwa kuwaoa wanawake wa aina hii ni kwa sababu hizi: Mume na mke wanategemewa kuishi wote wawili kwa pamoja na kuwa na mapenzi na huruma. Na makusudio haya hayawezi kuja kwani kila mmoja wao humchukia mwenziwe kwa kule kuwa kila mmoja wao ana ibada tofauti zisizolingana sawa kwa tabia, mila, sheria na desturi. Na ikiwa ndio hivyo, basi maisha ya mume na mke hayawezi kuendelea kwa muda mrefu na wala kuwa imara na mwishowe huvunjika. Na wanawake wenye dini za aina hii kutokana na dini zao haziharamishi kama vile: Khiana, zina, wala haziamrishi mema na wala kukataza mabaya na mengi mengineo. 

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget