Wednesday, April 4, 2012

Mirungi katika Uislamu


Abu ‘Abdillaah  
MIRUNGI, QAAT, KHAT, GHAT, GATI, MIRAA, GOMBA, MBAGA, VEVE, MTI, KIJITI, MAJANI, MAUA …
Sample ImageSample ImageSample Image
Mirungi au kama inavyojulikana kama Qaat au Qaadka huko Somalia, na Yemen huitwa au Al-Qaatالقات ; ingawa kwa matamshi ya huko hutamkwa ‘Gaat’, Kadhalika Kenya kulingana na miji yake hujulikana kama; Miraa, Veve, Kijiti, Gomba n.k., na Tanzania ni maarufu kwa majina; Mirungi, Gomba, Gati, Miti, Majani n.k. kulingana na kila eneo na jina lake.
 Mirungi au (Catha edulis) Ni mmea au mti unaoota au kuoteshwa kwa wingi sana huko Ethiopia, Yemen na Kenya.
 Jani hilo ambalo Maulamaa wameeleza kuwa ni Haraam kutafuna kama tutakavyoona mbele ya makala hii, ni jani lenye madhara mengi katika siha ya mwana Aadam na lenye kusababisha mengi katika madhara na maangamizi ya kimaadili na kijamii.
 Matumizi ya mmea huo ambao hakika kwa masikitiko makubwa, yameenea zaidi katika jamii za Kiislam na haswa maeneo ya mijini na zaidi kwa wanaojulikana kama ‘Waswahili.’
 Ingawa neno ‘Waswahili’ asli yake ni neno la Kiarabu ‘Saahil’ ساحل pwani, mwambao na ‘Sawaahiliy’ mkaazi wa pwani au mwambao, ila neno hilo au jina hilo hivi sasa limegeuka kimatumizi na kuashiria zaidi kwa wale watu zaidi wa mtaani, wasiopenda kutumika; kufanya kazi, wasio wakweli, wapenda starehe, wasio na elimu, wazembe n.k. Kwa wasio Waislam wao wanatumia jina hilo kuwaita nalo Waislam, na zaidi wakikusudia sifa hizo tulizozitaja hapo nyuma. Na kadhalika Waislam kadhaa huwaita wenzao hivyo wakimaanisha, wasio na ahadi, wasemao uongo, wasioaminika, wajanja wajanja, wajuaji, na wenye maneno mengi wasioshindika.
Mirungi inakusanya ndani yake alkaloid iitwayo cathinone, amphetamine kama kichangamsho (stimulant) ambayo inasemekana husababisha msisimko, uchangamfu, kuwa na aina ya furaha ya kuwazika –kuhandasika- na huondosha hamu ya kula na kusababisha ukosefu wa usingizi.
 
Mnamo mwaka 1980 WHO (Shirika la Afya Duniani) liliiweka Mirungi katika fungu la madawa ya kulevya ambayo inasababisha nafsi kutawaliwa nayo au kuwa na uraibu (addiction) kwa daraja ya kati hadi ile yenye nguvu.
 
Mti huo umekuwa ukiandamwa na mashirika yenye kupinga madawa ya kulevya kama shirika liitwalo DEA (Drug Enforcement Administration). Shirika hilo katika mwaka 2006 Julai tarehe 26, shirika hilo katika operesheni iliyokuwa ikijulikana kama ‘Somalia Express’ ambayo katika upelelezi wake uliodumu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu ambao ulihusisha wanachama 44 wa kundi lililokuwa likisafirisha tani 25 za Mirungi ambazo zilikuwa na thamani ya Dola milioni 10 za Kimarekani kutoka Somalia kupelekwa Marekani. Shitaka (Kosa) hilo lilihusisha utoroshaji mkubwa kabisa wa Mirungi katika Historia ya Marekani.
 
Biashara hiyo ambayo imeshamiri nchi za Afrika Mashariki ambapo hivi sasa Tanzania imepigwa marufuku, na pia kuenea katika nchi za Ulaya na Marekani. Mirungi imepigwa marufuku katika nchi mbalimbali za Scandinavia, lakini bado inajadiliwa Uingereza kama ni katika kifungu cha madawa ya kulevya au hapana!
 
Ni mmmea ambao umewekewa sheria kali au kupigwa marufuku nchi nyingi duniani.
 
Mirungi imekuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya watu wengi kuanzia Yemen, Ethiopia, Kenya, Tanzania na nchi ambazo watu wa nchi hizi wanaishi. Uingereza ambapo bado ulaji wa Mirungi haujapigwa marufuku; kila siku ndege inateremsha Mirungi kutoka Ethiopia na Kenya kwa wingi, na biashara yake imekuwa na nguvu kwa jamii ya Wasomali, Wayemen, Waethiopia na Watanzania wanaoishi katika nchi hii. Utagundua haraka sehemu au maeneo na nyumba zinazouzwa au kuliwa Mirungi kwa athari za uchafu wa vijiti vya Mirungi na majani yake yanayotupwa ovyo ovyo kila pahali na kuwa kero kubwa kwa wakazi wa jirani wa maeneo hayo na hata Manispaa za maeneo hayo hapa Uingereza.
 
Kadhalika, kwa unafuu wake wa usafirishaji kwa ndege, majani hayo husafirishwa kuelekea sehemu zingine kama Wales, Rome, Amsterdam, Canada, Australia, New Zealand na Marekani.
 
Ulaji wa Mirungi umekuwa ukiongezeka sana katika jamii mbalimbali hususan Yemen, Kenya na Tanzania na haswa walaji wa kiada –wakiwemo wanawake na hata watoto- na kusababisha kuongezeka mahitajio yake. Hii ni kwa sababu Mirungi ni kilevi cha kawaida katika jamii kama ilivyokuwa sigara ni kilevi kikubwa cha jamii ya Ulaya na Marekani hadi hivi karibuni baada ya kampeni za kila siku za kupiga vita. Ni kilewesho na uraibu ambao haujafikia daraja na uzito wa pombe. Haki ya uraibu huu umewatatiza Wanachuoni wengi wa Yemen na jamii zingine kufikia ufumbuzi wa kukata katika kuzima balaa hilo. Hata hivyo, kama tutakavyoona mbele ya makala hii, Wanachuoni wengi wakubwa wa nchi mbalimbali duniani, wameeleza uharamu wake.
 
Kwa kujitetea, walaji Mirungi wanaamini kuwa majani hayo huwapatia nguvu, na uchangamfu na mliwazo wa furaha ‘Handasi au Nakhwa’ kwa lugha yao. “Hakuna Mirungi, hakuna nguvu, na hivyo hakuna kufanya kazi, jimaa, kusoma, au chochote,” hivyo ndivyo wanavyodai.
Pamoja na madhara yake na maonyo makali ya taasisi za tiba na mashirika ya Afya duniani, lakini inaelekea kumalizika matumizi ya Mirungi moja kwa moja, ni jambo linaloonekana litachukua miaka mingi sana na vizazi vingi huko Yemen na hata Afrika Mashariki. Yemen ni nchi ambayo uraibu huo umetawala hadi kufikia watu kulazimika kuwekea ‘nyakati maalumu’ za ulaji.
 
Miaka kadhaa nyuma, Raisi wa nchi hiyo ‘Aliy ‘Abdullaah Swaalih aliwahi kueleza hadharani kuwa naye ni mlaji wa Mirungi lakini mwisho wa wiki; ingawa siku za mbeleni akaja kutangaza hadharani anajaribu kuachana nayo moja kwa moja. Mwaka 2002, wafanyakazi wote wa serikali ambao mwanzoni walikuwa wakila Mirungi kazini, walipigwa marufuku kuila kazini. Lakini leo hii, ulaji umeongezeka sana kuliko ulivyokuwa huko nyuma.
 
Anasema mwandishi maarufu Yemen, ‘Abdul-Kariym Ar-Razihi: “Mirungi (Qaat)… ni kileo cha watu wetu. Ni Imamu wa kijani anayeongoza nchi yetu. Ni ufunguo wa kila kitu na ni makutano ya vikao na minasabati yote ya kijamii. Ni kitu kisichoelezeka kinachoeleza kila kitu”
 
Vitabu kadhaa vimeandikwa na watu wa Magharibi kuhusu uraibu huo unaotisha, watengenezaji vipindi vya Televisheni vya Ulaya wamekuwa wakizuru nchi hiyo kuchukua maisha ya kila siku ya Wayemen ambayo yameeathiriwa kiasi kikubwa na ulaji huo hadi kuonekana watoto wadogo ambao hawajafikia baleghe kuwa ni walaji na wauzaji wakubwa.
 
Hali hii kwa mtazamo wa Kiislam, ikiwa inaashiria jambo, basi inaashiria uporomokaji na uozo wa jamii ya Kiislam na mustaqbali wa kizazi cha jamii hii ya Kiislam.
Historia Yake
Inaaminika kuwa Ethiopia ndio asli yake kuanzia karne ya 15, na ikaenea katika milima ya Afrika Mashariki na Yemen. Ingawa vilevile kuna wanaoamini kuwa ilianzia Yemen katika karne ya 13 kabla ya kuenea hadi Ethiopia na nchi za jirani.
Kutoka Ethiopia na Yemen, mti au mmea huo ulienea sehemu mbalimbali za Arabuni, Somalia, Sudan, Kenya, Tanzania, Uganda. Congo, Malawi, Zimbabwe, Zambia hadi Afrika ya Kusini.
Baadhi hudai kuwa matumizi yake yanarejea miaka ya nyuma sana tokea wakati wa Wamisri wa kale ambao inasemekana walikuwa wakiitumia kama madawa ya jadi kwa baadhi ya magonjwa.
Anaeleza mwandishi wa Kimalaysia ‘Abdullaah bin ‘Abdil-Qaadir kuwa alipokuwa Yemen mwaka 1854, aliona ada na tabia ya utafunaji Mirungi huko Al-Hudaydah. Anaeleza: “Niliona jambo la ajabu katika mji huu –kila mtu anatafuna majani kama mbuzi anavyokula akameza na kisha kucheua kisha hutafuna tena kile alichokicheua. Kuna aina ya tawi, si pana sana kiasi cha urefu wa vidole viwili, ngumu kiasi, watu hutumia aina hii ya tawi au jani na kutia mdomoni na hutumiwa na viambatanishio vingine kuila, tawi hili hutiwa lote mdomoni na kutafunwa. Wanapokuwa wengi na kula kwa pamoja, utaona mabaki ya majani hayo yamerundikana mbele yao. Wanapotema mate, mate yao huwa ya rangi ya kijani. Kisha nikawauliza kuhusu hicho wanachokula: ‘Ni faida gani mnayopata kwa kula majani hayo?’ Wakajibu, ‘Hakuna chochote, ni jambo tulilolizoea lenye kutugharimu ambalo tumekulia nalo’. Wale wanaokula majani haya inawabidi watumie sana mafuta na asali, kwani wasipofanya hivyo wanaweza kuugua. Hayo majani hujulikana kama Kad (Mirungi).”
Wasifu Na Kilimo Chake
Mirungi ni mti unaoota polepole ambao unakuwa kwa urefu wa mita 1.5 hadi mita 20, kutegemea na eneo kijiografia na pia hali ya mvua ya eneo. Likiwa na majani ya kijani yaliyokoza ambayo yana urefu wa sentimeta 5 hadi 10 na upana wa sentimeta 1 hadi 4.
Ina ladha ya uchachu mkali na utamu wa mbali kwa wakati mmoja. Hufungwa katika majani ya migomba ili kuhifadhi ubichi wake. Kawaida huvunwa asubuhi sana na kuuzwa mchana wake au usiku wake, kila inavyokaa sana hupunguza ubora wake kwa walaji na thamani yake. Na kwa sababu walaji wa Tanzania hutegemea zaidi Mirungi kutoka Kenya, huwa hawapati ule ubora unaotakikana kutokana na umbali na kutofika kwa haraka; ingawa walaji wa Arusha hupata haraka zaidi kwa ukaribu wake na Nairobi kuliko wale wa Dar na Zanzibar au miji ya bara ya mbali kama Mwanza na kwengineko.
Kwa hivyo, majani ya Mirungi yanapoanza kukauka, kemikali ile kali ya aina ya cathinone inakauka pia na inabakia ile ambayo sio kali: cathine, na ndio maana mirungi inaposafirishwa inawekwa katika mifuko maalum ya plastiki au kufunikwa na majani ya migomba ya ndizi ili ihifadhike vizuri.
Mirungi ni zao lenye kuwaingizia wakulima Yemen kipato kikubwa na ndio maana wengi wameanza kuacha kilimo cha kahawa, na hutumika asilimia 40 ya matumizi ya maji ya nchi nzima kwa kilimo chake, pamoja na uzalishaji wake kuongezeka kiasi cha asilimia 10 hadi 15 kila mwaka. Matumizi ya maji yamekuwa makubwa kiasi cha hifadhi ya maji ya San’aa mji mkuu wa Yemen kupungua na ikiendelea namna hii basi baada ya miaka kumi tu maji yatakauka na kwa hali hiyo imefikia serikali kugawa maeneo kwa kuwahamisha wakazi wa San’aa kwenda kuishi maeneo ya pwani ya Bahari nyekundu.
  Sample Image
Shamba La Mirungi Huko Yemen
Matumizi ya Mirungi aghlabu hutumika katika maeneo yanayolimwa zaidi na maeneo ya jirani na yale ambayo hufika Mirungi haraka ingali bado mpya mbichi na safi kwa sababu ya mzimuo wake. Kila inavyokaa mzimuo wake na upandishaji wa ‘handasi’/ ‘nakhwa’ yake hupungua.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ya kwamba zaidi ya masaa 14.6 milioni yanapotezwa kila siku katika ulaji wa Mirungi huko Yemen. Ripoti hiyo, iliotolewa katika tovuti ya WHO, inaonyesha ya kwamba asilimia 80 ya watu wazima (male adults) wanatafuna Mirungi kila siku kwa muda wa masaa matatu mpaka manne hadi matano wakati ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wamo pia katika tabia hii yenye hatari.
Mirungi ni kileo kinachotumika sana kama ‘mkusanyiko wa kijamii’ katika maeneo mengi, na huwajumuisha zaidi wanaume ingawa baadhi ya sehemu na kwa miaka ya karibuni wanawake wamevamia sana uraibu huo haswa maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki kama Mombasa, Tanga na Dar-es-Salaam na mji kama Arusha ambao pia umekumbwa na ugonjwa huo kwa vijana wengi wa mjini. Na hupendelewa na madereva wa magari makubwa wanaosafiri safari ndefu, madereva wa abiria na hata wa magari ya kukodishwa kwa kuamini kuwa inawafanya wawe macho na makini. Vilevile hutumiwa na wanafunzi wakiamini kuwa inawafanya wasome muda mrefu na kukesha, kadhalika walinzi wa usiku huona inawasaidia kuwa macho usiku. Na baadhi ya watu hutumia kwa kisingizio cha kukesha kwa ajili ya kufanya ‘Ibaadah za usiku.
Nchi kama Tanzania, imepigwa marufuku lakini serikali kwa kutofuatilia kwa karibu kumefanya kuwe kunaliwa hadharani na bila woga wowote. Hufuatwa sheria pale maaskari wanapotaka kupata chochote kutoka kwa walaji na ni nadra kusikia mla Mirungi katiwa ndani, na akitiwa ndani basi hutolewa mara moja bila kufikishwa mahakamani.
Huko Somalia, waliposhika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na kuleta amani ambayo haikuwahi kuonekana Somalia, Baraza La Juu La Mahkama Ya Kiislam, walipiga marufuku kuliwa mwezi wa Ramadhaan na kusababisha maandamano na upinzani huko Kismayo. Na mwaka huo huo katika mwezi wa Novemba, Kenya ilipiga marufuku ndege kwenda Somalia wakitaja ni sababu za kiusalama, hali ambayo ilisababisha upinzani kutoka kwa walimaji Mirungi. Mbunge wa Ntonyiri, Meru ambayo ndio eneo lenye kutegemewa sana Afrika Mashariki kwa ulimaji wa Mirungi, alieleza kuwa imetengwa ardhi maalum ya kulimia Mirungi, ambapo tani 20 zenye thamani ya Dola Laki 8 ($800, 000) husafirishwa kila siku kuelekea Somalia na hivyo kizuizi cha serikali kitailetea taifa madhara ya kiuchumi na kipato kama hicho kwa siku.
Aina Zake
Alenle (yenye majani mapana mengi, na ni ghali sana) – Yemen, Ethiopia na Kenya
Kangeta – Kenya
Giza (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ndogo) – Kenya
Mbaga (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ya aina duni ambayo aghlabu ni ya bei ya chini -japo kuna baadhi ya mashamba machache sana hutoa aina yenye afadhali- na huliwa na wasiomudu kununua aina za ghali) – Tanzania
Madhara Yake
“Familia nyingi zinateketea, wake kukimbia waume zao, waume kutojali familia zao; hawataki kufanya kazi, jamii kujaa wavivu waombaji, wazazi na wakwe kulea wajukuu wasiongaliwa na wazazi wao, ulaghai na maasi kuzidi, ‘Ibaadah kupuuzwa, uchumi kuporomoka…”
Naam, tukiyaunganisha maneno hayo na tunavyoona hali ya walaji, hakika yana ukweli mtupu usiopingika kwa wanaojua hali hiyo katika jamii.
Tutajaribu kuyaorodhesha madhara mbalimbali yanayosababishwa na ulaji Mirungi.
Madhara Ya Kidini Na Kimaadili
1.     Kupitwa na vipindi vya Swalah au kutokuswali kabisa;
2.     Swawm haikamiliki – katikati ya mchana wa Ramadhaan watu huhangaika kutafuta Mirungi na kucheza bao, keramu, dhumna, kutazama mipira na sinema. Jambo la kwanza baada ya futari, watu huanza kusaga Mirungi. Hakuna Swalah za usiku, hakuna ‘Ibaadah nyingine yoyote, hata Swalah ya Alfajiri huwapita walaji wengi kwa sababu Shaytwaan wa Mirungi huwaambiwa wakalale muda mchache tu kabla ya Swalah ya Alfajiri! Kuamka kwao ni mchana au Alasiri, Ramadhaan inakuwa haina uzito wowote kwa maisha ya mla Mirungi;
3.     Mchanganyiko baina ya wanaume na wanawake;
4.     Uongo – hii ni kawaida kwa wengi ili wafikie malengo ya kupata wakitakacho; ima kudanganya wengine kwa kuwakopa pesa za kununulia Mirungi na kisha hawarejeshi madeni hayo. Na pia wanapokopa husingizia matatizo makubwa waliyonayo wao au jamaa zao kama maradhi, matibabu, ada za shule, n.k. ili waweze kukubaliwa kupata mikopo hiyo. Aghlabu wanapokopa hawasemi ukweli kuwa wanataka pesa za kununulia Mirungi; maana hakuna atakayewakopesha;
5.     Usengenyaji – vikao vingi vya walaji huwa ni mazungumzo ya kidunia, mipira, filamu, kujadili mambo ya siasa, jamii, na kujadili maisha ya watu, maingiliano ya kindoa, na wao kwa wao kutoa siri zao za ndani na kutaja maovu yao waliyowahi kuyafanya;
6.     Uropokaji, uchache wa adabu, ujuaji wa kila kitu, mlaji akiongelea siasa basi hakuna mwanasiasa kama yeye, akija kwenye mpira wa miguu na hususan ligi ya Uingereza, basi hakuna anayeichambua ligi hiyo kama yeye… na mtihani mkubwa na msiba ni kuwa hata mas-ala ya Diyn wao pia ni wataalam wakioongelea Taariykh na kwanini fulani aliuliwa na wangapi waliritadi baada ya Mtume na kwanini fulani walikuwa hawastahiki Ukhalifa walimdhulumu fulani n.k.!!
7.     Upungufu wa hayaa;
8.     Kupoteza muda mkubwa katika vikao hivyo;
9.     Kuomba omba – wengi huwa hawana uwezo wa kununua Mirungi kukidhi mahitaji ya uraibu wao, na hivyo kuwapelekea kuwa waombaji kwa wengine ima wa pesa za kununulia au uombaji wa Mirungi kwa walaji wenzao;
10.            Maasi – baadhi ya vikao vya Mirungi hutawaliwa na kutazamwa sinema za uchi ili kusukumia handasi zao. Hali hiyo ya uchafu wa maadili na kujitumbukiza katika uharamu, huwakutanisha wazee kwa vijana na matokeo kupoteza heshima baina yao, na pia nyumba hizo kupoteza hadhi katika jamii na nyakati nyinginezo kuwatukanisha wake za wenye nyumba hizo kwa machafu yanayoendelea hapo. Baadhi ya nyumba waume wamepoteza wake zao kwa marafiki zao kutokana na maingiliano huru yasiyo na mipaka baina ya wake kwa waume;
11.            Kuharibiwa itikadi zao – mji kama Arusha, vijana wengi wamebadili itikadi zao za Diyn baada ya kujiunga na uraibu huo na kushiriki vikao vyake. Ndani ya vikao hivyo kuna kundi la wakongwe ambao wameweza kuwashawishi vijana kutoka katika itikadi waliyozaliwa nayo na kujiunga na itikadi ya kukufurisha na kulaani Maswahaba na wema waliopita. Imefikia hali ya kusikitisha sana kwa kuona kundi kubwa la watu likiwa limekaa barazani likicheza Dhumna (Domino) na huku Swalah ya Jama’ah ikiadhiniwa, kuqimiwa, na kuswaliwa ubavuni mwao kwenye Msikiti na wala hawana wasiwasi tena wakifanya zogo na kelele na kuzipigisha kete zao kwa nguvu kana kwamba wanashindana na sauti ya Mnadi Swalah. Maskini na wao wanajiona wako sawa kabisa kwenye haki! Na wanapotanabahishwa waache lahwu zao na waende kuswali, husema kuwa wao wanajumuisha Swalah kutokana na Itikadi yao. Ukweli wengi hata kuswali hawaswali;
12.            Haki za kifamilia kukiukwa – haki za kinyumba; waume wanakuwa hawatoa haki zao ima kwa kukesha nje ya nyumba zao, au kwa kudhoofika nguvu zao za kiume na pia kumaliza haraka wanapofanya tendo la ndoa na hivyo kusababisha wake kukosa haki za msingi;
13.            Talaka kuzidi – kwa sababu tulizotaja katika kipengele kilichotangulia, wake wengi hushindwa kuvumilia katika ndoa zao na kuamua kudai talaka;
14.            Haki za watoto hazitekelezeki – kwa kuwa walaji wengi hawafanyi kazi, na wanaofanya kazi hutumia gharama nyingi kwenye ulaji, hivyo hakupatikani matumizi nyumbani au matumizi kubanwa na haki kutotimizwa. Walaji wengine hulelewa watoto wao na wakwe zao au wazazi wao;
15.            Kutoka nje ya ndoa – baadhi ya walaji wanakuwa si waaminifu kwenye ndoa zao, kadhalika baadhi ya wake wanashindwa kuvumilia kuwa wapweke kila mara kwa kuwa waume zao hukesha nje ya nyumba zao, na wakirudi ni usingizi, wakiamka ni kutafuta Mirungi, na hivyo hupelekea wake hao kukosa uvumilivu na kwa kuzidiwa kwao na matamanio yao –na kwa uchache wa Iymaan- kunawapelekea wao kuyahamisha matamanio yao pengine.
16.            Walaji wa uraibu huu hukesha kuorodhesha mambo watakayoyafanya siku ifuatayo, pasi na kuyatekeleza, na kuendelea katika hali hiyo kila mara bila ya mafanikio yoyote.
17.            Wengine husingizia eti wanakesha kwa ajili ya ‘Ibaadah, lakini ni aina gani ya ‘Ibaadah inayofanyika wakati mashavu yametuna kwa kujaa majani hayo?
Madhara Ya Kiafya
Matatizo na madhara ya Mirungi yaligunduliwa mwanzo katika mwaka 1935 na League Of Nations, Mwaka 1970 taasisi ya tiba ikaitenga madhara ya cathinone yanayopatikana katika Mirungi ambayo kikemikali inafanana na amphetamine, na hivyo katika mwaka 1971 ikaorodheshwa na United Nation kuwa ni miongoni mwa madawa ya kulevya.
Bwana mmoja kutoka Canada ajulikanaye kama Mathew Bryden aliyekuwa akifanya kazi na mashirika ya msaada kwa miaka mitatu huko Somalia anasema, “Watumiaji wengi wa Mirungi wamejikuta wakipambana na msisimko wake ili waweze kupata usingizi au hata kufanya kazi kisawasawa. Wanaelekea kwenye pombe au madawa ili kupata mapumziko au kupunguza hali ya wasiwasi. “Hali ilivyo Mogadishu ni watu kutawaliwa na nguvu za Mirungi, madawa au pombe,” Bwana Bryden anaendelea, “Unakuwa umevurugikiwa kabisa. Ima uharibikiwe kikamilifu au upoteze mwelekeo wa hali halisi.”
Utumiaji wa Mirungi husababisha madhara mbalimbali kiafya kama:
1.     Magonjwa ya vidonda vya tumbo (ulcers);
2.     Ukosefu wa haja kubwa (constipation);
3.     Utumiaji wa muda mrefu husababisha kuharibu utendaji kazi wa ini, na pia kusababisha ubadilikaji rangi meno, kudhoofika, na fizi kuuma na harufu ya mdomo;
4.     Upungufu wa msukumo wa kufanya jimaa (sex drive). Na pia kuwahi kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu;
5.     Kupatwa na ugonjwa wa futuru/future/bawasiri/baasili – nyama inayoota kwenye utupu wa nyuma;
6.     Upungufu wa usingizi;
7.     Humpelekea mlaji kutawaliwa nayo (Addiction);
8.     Walaji wengi huvuta na sigara, hata yule aliyekuwa havuti kabla ya kuanza kula Mirungi, hujikuta akizama kwenye uvutaji, na madhara huwa maradufu;
9.     Madhara ambayo bado kinamama walaji Mirungi hawajayagundua ni kwamba mtoto anayezaliwa na mama mlaji Mirungi mara nyingi hukataa kunyonya titi la mama yake kwa sababu ladha ya maziwa inabadilika kwa ajili ya utumiaji wa madawa (pesticides) unaotumiwa na wakulima wa Mirungi kama inavyoeleza utafiti uliofanyika na Chuo Kikuu Cha Aden (Aden University). Utafiti huo unazidi kueleza ya kwamba aina ya madawa yanayotumiwa na wakulima ni zaidi ya 118 (na nyingi katika hizo ni katika zile zilizokatazwa kisheria [illegal pesticides]) na ambazo zinasababisha asilimia 70 ya ugonjwa wa saratani (cancer) huko Yemen.
10.             Utafiti mwengine kule Ethiopia unatueleza ya kuwa mtoto wa mama mwenye kula Mirungi kwa wingi huwa hana uzito wa kawaida wakati wa kuzaliwa.
11.             Ukosefu wa hamu ya kula chakula na mengi mengine.
12.            Madhara Ya Kiuchumi Na Kijamii
13.            Kuwa na taifa la wavivu wapenda starehe wasiotumika;
14.            Jamii ya Kiislamu iliyo chafu kimaadili na isiyosimamisha ‘Ibaadah;
15.            Harakati za kunyanyua uchumi kuwa duni, harakati na juhudi zinazopatikana huwa ni za kuwazika na kutajika tu. Anapokuwa mtu ameshakhazin fundo lake la Mrungi kwenye shavu lake linalovimba kama pulizo kwa kujaa ‘taksima’, hapo atakuwa anatoa mipango na mikakati mizito mizito ya kujenga maghorofa, kuanzisha miradi ya mamilioni…lakini yote ni mipango inayopangwa na ‘Handas’ na ‘Nakhwa’, baada ya kutemwa gomba, mipango yote iliyokuwa ikipangwa huyeyuka na kuwa kama ngano za Alinacha….hapo tena husubiriwa siku ya pili ya kusagwa na mipango yake mingine ya mamilioni ya kuwazika;
16.            Kulala mchana kutwa – kukosekana harakati na michakato ya utafutaji rizki.
17.            Kuzidi kwa omba omba – bila shaka ikiwa watu hulala mchana mzima na hawahangaiki kufanya kazi, kinachotarajiwa ni kuzidi kwa wanyanyua mikono na wainamisha vichwa wanaoongea kwa huzuni kama waliofiwa wakati wanatupa makombora yao ya maombi;
18.            Vijana wa mjini hawataki kuajiriwa – kwa sababu wanajiona ni ma-alwatwan, kwa hiyo –kwa mtazamo wao- haiwezekani kwao kutumwa au kuajiriwa! Matokeo yake uchumi wa wakazi wa mjini kuporomoka na mwisho wake ni wao kukodisha nyumba zao kwa wageni (wanaotoka miji ya mbali) zikawa maduka, na mwisho wake hufikia kuuza hizo nyumba zao ambazo wamerithi kutoka kwa wazee wao waliokuwa wakihangaika na kuchapa kazi;
19.            Huwapelekea baadhi yao kujidunisha na kuwatumikia mabwana wakubwa si kwa lingine ila kwa ajili ya kilo ya Mirungi.
Vituko Na Mikasa Vya Mirungi Na Walaji Mirungi
(Kama inavyoitwa petroli “dhahabu nyeusi,” Mirungi inaitwa na walaji wake “dhahabu ya kijani”).
Matukio yafuatayo hapa chini ni ya kweli yamewahi kutokea na hakuna kilichozidishwa; yanathibitishwa na walaji katika sehemu hizo:
1.     Mmoja wa wasagaji Mirungi alipohandasika alitundika koti lake pale alipo nzi ukutani akidhani ni msumari, na la kushangaza zaidi, ni pindi nzi yule aliporuka kuhamia kwengine, bwana yule alimfuata pale alipotua na kujaribu kutundika koti lake kwa mara ya pili.
2.     Mwengine alijigonga kwenye mti wa stima barabarani na kuuomba msamaha akidhani amemgonga mpita njia mwenzake.
3.     Na kuna tukio la kuhuzunisha huko Arusha na Mombasa, ni pale walipokuwa wakila Mirungi na kutazama sinema chafu, nyumba hiyo ambayo wamebandika Aayah za Qur-aan kwenye kuta –hali ya kuidhalilisha Qur-aan kuifanya ni mapambo na kupoteza lengo la kushushwa kwake-, baada ya kuwa wanatazama maasi yao, mmoja wao akashtuka na kusema ‘AstaghfiruLlaah!!’ na kukimbia kuigeuza ile fremu ya Aayah za Qur-aan kwa sababu aliona ni kuivunjia heshima! Na baada ya kumaliza maasi yao, wakaigeuza fremu ili zile Aayah zirejee kuonekana tena kama awali. Mwengine huko Mombasa alikuwa na gazeti lake la kufunika hizo Aayah pindi anapoanza kutazama balaa hizo, na akimaliza hutoa gazeti hilo ambalo huwa ni kwa kazi hiyo.
4.     Kuna mmoja wa walaji Mirungi alikamatwa huko Arusha na kupelekwa kituoni – kama tulivyosema awali ni tukio la nadra mtu kutiwa ndani kwa kula Mirungi- na wenzake waliposikia, wakamfuata kituoni kumtoa, lakini hawakukumbuka kuwa mashavuni mwao wamejaza taksima ya Mirungi na hali wako kituoni.
5.     Mlaji mmoja baada ya kupata ‘Nakhwa’ iliyomkolea, wakati walipomaliza kikao chao cha Mirungi anliondoka amevaa viatu vya mwengine; alipofika mbele ya safari na kutanabahi, tayari akabaki kwenye tahayuri ya kujiona kuwa atashukiwa kwa wizi na hali ilikuwa ni raha za ‘Nakhwa’.
6.     Dereva mmoja wa Taksi huko Arusha alikuwa amembeba abiria mzungu aliyekuwa akielekea kituo cha ndege cha KIA (Kilimanjaro International Airport) ambacho kipo katikati ya mji wa Arusha na Moshi, kwa kupandwa na ‘Handasi’, alijikuta akikipita kituo hicho na kufika Moshi mjini. Akaanza kuuliza kituo kiko wapi – pamoja na kwamba anakijua kilipo kituo ila ni ulevi wa Mirungi umempoteza-, akaulizwa ‘Kwani wewe umetokea wapi?’ Akajibu, ‘Arusha’, akaambiwa, ‘Mbona kituo umekipita huko nyuma kabla hujaingia Moshi?’…akachanganyikiwa na kuanza kurudi kwa kasi, hata alipofika kituoni, mzungu keshakosa ndege!!
7.     Na huko Australia: Bwana na Bibi McDavitt wa huko Perth (Australia) walipewa “zawadi” ya mmea na rafiki yao wa Kiafrika ili wauoteshe katika bustani yao kubwa nzuri iliyopo mbele ya nyumba yao. Mti ulikuwa mkubwa na mzuri wa kuvutia. Mti ulipokuwa mkubwa kiasi, rafiki yake wa Kiafrika aliomba apunguze (pruning) majani na matawi ya huo mti huo ili uendelee kuwa mkubwa na wa kuvutia. Mtindo huu uliendelea mara kwa mara na kila mara mti unapoanza kuchipua vizuri, yule rafiki Mwafrika akawa anakuja na kuomba kupunguza matawi na majani kama ilivyo kawaida yake. Lakini siku moja, Bwana na Bibi McDavitt walishtuka walipoona watu wengine wa Kiafrika (na sio rafiki yao wa kila siku) wakikata matawi bila ya rukhsa yao. Hapo ndipo walipopatwa na wasiwasi kuhusu mti huo. Na baadaye wakagundua ya kuwa mti huo ni mti wa Mirungi! Wakaamua kuukata.
8.     Na Djibouti: Tani kumi za Mirungi hupelekwa kila siku kwa ndege kutoka Ethiopia kuelekea Djibouti. Katika uwanja wa ndege, hakuna mgeni anayengojewa kwa hamu kama mgeni huyo (Mirungi). Zaidi ya magari 300 yanakuwa tayari kwenye kiwanja cha ndege kumpokea “mgeni” huyo wa thamani. Wafanya biashara wa Mirungi wanaitwa ‘Masultani wa Qaat.’ Ilitokea siku moja watu kushikwa na kiwewe kiwanja cha ndege walipopata habari ya kwamba huenda Mirungi isiwasili siku hiyo kwa sababu fulani fulani. Ilitokea fujo katika nchi na ilikuwa ni siku ya huzuni na watu waligoma kuondoka kiwanja cha ndege. Punde si punde, ndege iliwasili na watu walipopata habari hiyo, basi walikumbatiana kwa furaha na kupeana mikono kama vile ni Siku Kuu (‘Iyd). Djibouti imekataa kupiga marufuku mirungi kwa sababu inaingiza serikalini kila mwaka faida ya dollar 15,000,000 - Kwa hivyo, umefanya mkataba wa Kiserikali baina ya Djibouti na Ethiopia kuhusu kutochelewesha Mirungi hata siku moja.
Hayo ni matukio machache kati ya matukio mengi yasiyo na idadi ambayo kurasa haziwezi kuorodhesha zote. Matukio yanayosemekana Yemen, Ethiopia, Kenya na Somalia yanawezwa kuandikwa vitabu kwa vitabu.
InshaAllaah tutamalizia makala hii kwa kuona namna wanachuoni mbalimbali walivyolieleza tatizo hili na kunyambua hukmu ya Uharamu wake kutoka katika viini vya Shari’ah ya Diyn yetu safi isiyo na nafasi ya uchafu na uraibu wowote wa kiwendawazimu.
Fataawa Za Wanachuoni Kuhusu Mirungi

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashaytwaan (wanamfuata Shaytwaan).  Na Shaytwaan ni mwenye kumkufuru Mola wake.” [Al-Israa: 26-27]
“Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo.” [Al-Baqarah: 125]

“… na anawahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya…” [Al-'Araaf, 7: 157]

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Allaah Anachukia mambo matatu: kusengenya, kuomba na kupoteza pesa.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

Mirungi ni mti mchafu mbaya uliongia katika ardhi ya Waislam, na wameingia katika mitihani baadhi ya Waislam, na unasababisha madhara ya kimali, kimwili, kidini na kiwakati. Vilevile, ulimaji wake husababisha hasara kubwa za kiuchumi kwa sababu ya maji mengi yanayotumika katika ardhi ngumu ambayo inaoteshwewa. Na kwa hivyo, ni HARAAM kulimwa katika ardhi za Waislam, na pia kutafunwa.

Matumizi ya Mirungi yanaingia moja kwa moja katika vileo kwani vinamtoa mlaji katika hali yake ya kawaida na kumbadilisha na kuingia katika hali ya kuishi kwenye fikra za kuwazika na ndoto za aliye macho, vilevile mtu kuwa juu juu amehandasika (kalewa), kadhalika ndani yake kuna kuidhuru mtu afya yake, ubadhirifu wa mali na wakati.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu vinywaji fulani vinavyotengenezwa na asali, mahindi, au shayiri kwa njia ya kuvundikwa au kuchanganywa hadi kugeuka na kuwa pombe. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ufupi na uwazi alijibu,
“Kila chenye kulewesha ni pombe, na kila pombe ni Haraam.” (Muslim)

Na amesema tena Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Kila chenye kulewesha kikiwa kingi, basi japo kichache ni Haraam.” (Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy). Na kwengine, “Kinacholewesha japo ni ndoo nzima, basi hata muonjo (kuinywa kidogo) wake ni Haraam.” (Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy)

Naye ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa amesimama kwenye Minbar ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatangazia,
“Pombe ni chochote chenye kufunika akili” (Al-Bukhaariy Na Muslim)

Wanachuoni mbalimbali wametoa fatwa mbalimbali za kuonyesha uharamu wa utumiaji wa Mirungi.

Zifuatazo ni Fatawa za Wanachuoni mbalimbali, nimechagua Fatwa tatu za Wanachuoni watatu wa nchi tatu maarufu, Saudiyah. Misr na Yemen. Na badala ya kuzikusanya makumi ya Fatwa kutoka Yemen, au maishirini kutoka Saudiyah au kadhaa kutoka Misr, hizi tatu hapa chini zitakuwa zinawakilisha fatwa nyingi za Wanachuoni wakubwa wa nchi hizo:

Mwanachuoni Mkubwa Wa Sa’udiyah Allaamah Ibn Baaz, Aliyekuwa Mufti Wa Sa’udiyah

Alipoulizwa:
‘Wengi katika waraibu wa Mirungi, inapofika wakati wa Swalah basi (kwa wale wanaoswali) hutoa midomoni mwao (Mirungi) na kisha huitema kwenye mifuko ya plastiki kisha huswali. Na baada ya Swalah huichukua kutoka kwenye mfuko na kuila tena, je, Mirungi ni najisi? Na nini hukmu ya mtu mwenye kuswali na hali imo kwenye mdomo wake? Na je, inajuzu kwa yule mwenye kuila akachelewesha Swalah hadi amalize kula, kisha aje kulipa Swalah zake?

Akajibu:

Sina elimu ya chenye kuonyesha kuwa ni najisi, kwani huo ni mti maarufu, na asli kuhusiana na miti na mimea mbalimbali ni kuwa yote ni twahara. Ama utumiaji wake ni HARAAM –kwa kauli sahihi za Wanachuoni- kutokana na madhara yake mengi.

Na inawapasa hao wenye kutumia, wasiitumie kabisa wakati wa Swalah, na wala haijuzu hata kidogo mtu kuchelewesha Swalah kwa ajili hiyo, bali inampasa Muislam aiswali Swalah kwa wakati wake katika Jama’ah pamoja na ndugu zake Waislam Misikitini, kwa kauli yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Atakayesikia Wito wa Swalah (Adhaan) na asiende kuswali, basi hana Swalah ila kwa udhuru.” (Ibn Maajah, Ad-Daara Qutwniy na Al-Haakim kwa Isnaad sahihi)
Na aliulizwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuhusiana na huo ‘udhuru’ ambao umeruhusiwa, akajibu: “Ni khofu au maradhi”’ na matumizi ya Mirungi sio udhuru wa kishari’ah, bali ni jambo la Munkar, na ikiwa mtu atachelewesha Swalah kwa sababu hiyo, basi hiyo itakuwa ni dhambi kubwa sana. Na haifai vilevile kuunganisha Swalah mbili kwa sababu ya Mirungi, kwani huo si udhuru wa kishari’ah unaokubalika…”

Kitabu ‘Fataawa Islaamiyah’ kilichokusanywa na Muhammad Al-Musanad, Juz. 3, uk. 445 – Majmu’ Fataawaa wa Maqalaat Mutanawi’ah, Juz. 23.


Mwanachuoni Wa Misr Yuusuf Al-Qaradhwawiy, Ambaye Ni Mufti Wa Qatar Hivi Sasa

Aliulizwa na muulizaji kutoka Yemen:

Tumekwishafahamu fatwa yenu kuhusiana na sigara, na hukmu kuwa ni Haraam, kutokana na madhara yanayompata mvutaji kwa nafsi yake na mali yake, na kuwa ni aina ya kuua nafsi au kujiua polepole.

Na tunahitaji kujua fatwa ya afa jingine ambalo limeenea kwetu Yemen kutokea siku nyingi, na imeenea kwa watu, inawafanya watoto waonekane kama vijana, na wakubwa waonekane wazee, hata tunaona watu wenye elimu zao (Wanachuoni) na Maqaadhi wanaila na hawaipingi. Tumesoma kuwa kuna Wanachuoni wakubwa wa nchi zingine wameharamisha kuila hii Qaat (Mirungi) na wakakemea wanaoila na wale wenye uraibu huo kutokana na madhara yake na israaf, na Allaah Hapendi wenye kufanya israaf.

Tunaomba maelezo yenye kukinaisha juu ya jambo hili lenye kuwagusa Wayemen. Jazaakum Allaahu khayra

Akajibu:

Ama hukumu ya uvutaji sigara, hakuna shaka kuwa maelezo yote ya kielimu, kitiba za kisasa yamegundua kuwa ina madhara makubwa kwa mtumiaji. Na yanathibitisha yale tuliyoyataja katika fatwa zetu kuhusiana na Uharamu wake afa (janga) hili lenye kuangamiza.

Kadhalika athari mbaya za uvutaji zinazowapata wale wasiovuta ambao wanapata moshi wake na hivyo kuwa hatari zaidi kwao hata kushinda wale wanaovuta.

Uislam unasema, “Hakuna madhara wala kudhuriana.” Yaani ‘usiidhuru nafsi yako wala usidhuru nafsi ya mwenzako’. Na mvutaji sigara huidhuru nafsi yake na huidhuru nafsi ya mwenzake. Na shari’ah imekuja kwa ajili ya kulinda maslahi ya kidharura ya viumbe. Na wameigawa watu wa shari’ah katika sehemu tano, nazo ni: Diyn, Nafsi, Akili, Kizazi na Mali. Na sigara hudhuru maslahi hayo.

Ama kuhusiana na Mirungi, imeingizwa na ‘Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na  Ulevi, Madawa Ya Kulevya na Sigara’ –ambao ulifanyika huko Madiynah chini ya usimamizi wa Chuo cha Kiislam cha Madiynah, miaka kadhaa- kuwa ni mojawapo ya mambo yaliyojumishwa kuwa HAYAFAI na kuingizwa kuwa ni sehemu moja na madawa ya kulevya na sigara.
… Akaendelea Shaykh Qaradhwawiy na kutaja alivyowaona watu Yemen wakila na akaona gharama zinazotumika na wakati unaopotezwa, mwisho akahitimisha fatwa yake kwa kueleza madhara yake ya kiafya, kupoteza wakati, kupoteza pesa, ardhi kutumika vibaya na maji kupotea mengi kwa ulimaji wake.
Kisha akamtaja Shaykh Muhammad Saalim Al-Bayhaaniy na msimamo wake usioyumba na akaelezea fatwa yake ambayo ndani yake kaiharamisha Mirungi katika kitabu chake ‘Iswlaah Al-Mujtama’’


Shaykh Abu Naswr Muhammad Bin ‘Abdillaah Al-Imaam Wa Yemen

Katika fatwa yake ndefu ambayo ni risala nzima, hapa tutaifupisha sana.

Aliulizwa:

Nini hukmu ya Kiislam kuhusu Mirungi; kuliwa, kulimwa, kuiuza, kuinunua na kuitolea zawadi?

Akajibu:

AlhamduliLlaah was Swalaatu was Salaam ‘alaa RasuuliLlaah wa ‘alaa aalihi waswahbihi waman waalaah, amma ba’ad,

Hukmu ya Mirungi kula, kulima, kuuza, kununua na kutolea zawadi yote ni HARAAM kwa dalili na sababu zifuatazo:

1.     Zimekuja Dalili za wazi kuhusiana na ubaya na uchafu wa Mirungi kutoka katika kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ambayo imejengeka katika wadhifa aliotumiwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Na anawahalalishia wao vilivo vizuri na kuwaharamishia vibaya” Kutajwa uharamu wa vitu vibaya na vichafu kwenye Aayah hiyo mkabala na kuhalalishwa vilivo vizuri, ni ishara ya kuonyesha kuwa kila kibaya na kichafu ni HARAAM iwe sawa ni chakula, kinywaji, kuingiliana na mengineyo. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatujulisha katika Aayah hii kuwa Mtume wetu anatuharamishia yale yenye madhara, machafu na mabaya. Na hakutuharamishia Mtume wetu kitu ambacho ni kizuri kwa hali yoyote. Na kuharamishwa jambo, huenda kikawa kwa dhati yake chenyewe au kwa kinginecho, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwenye kula kitokanacho na mti huu, basi asiukaribie Msikiti wetu”, Hadiyth hii imekuja kwa mapokezi mengi. Hapa uharamu umekuja kutokana na harufu mbaya inayotokana na viliwavyo kutokana na mti huo ambavyo ni vitunguu maji na vitunguu thawm, na harufu hiyo huwaudhi watu pamoja na Malaika katika nyumba za Allaah (Misikitini).  Na Mirungi haiepukiki kuwa katika fungu hilo la HARAAM kwa dhati yake au kwa dhati ya kinginecho. Baadhi ya watu wanadai kuwa hakuna Aayah wala Hadiyth inayoelezea kwa uwazi uharamu wa Mirungi, watajibiwa kuwa, Aayah hiyo hapo juu imekusanya moja kwa moja Uharamu wa kila kilicho kibaya, kichafu, chenye madhara. Na kwa uwazi kabisa Allaah Ametaja kilicho kibaya mkabala na kilicho kizuri cha halali. Na Wanachuoni wengi kabisa wametaja Aayah hiyo kuwa inaonyesha wazi uharamu wa Mirungi, na hilo liko wazi.
2.     Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakuna kujidhuru wala kudhuriana (kusababisha madhara)”, Hadiyth hii ambayo imesimuliwa na Maswahaba nane ni hoja nzuri kabisa. Aliposema, “La Dhwarar” hakuna madhara inafafanua kupita kiasi kuliko angesema, “La tadhwuruu” msidhuru, na Hadiyth hii ni msingi wa jumla unaojengea masuala mengi yasiyo na idadi, maana kauli yake “La Dhwarar wala Dhwiraar” maana yake ni msijidhuru nafsi zenu au msijiletee madhara nyinyi wenyewe na wala msidhuru nafsi nyinginezo au msipeleke madhara kwa wengine. Na inafidisha Hadiyth hii kuwa kila chenye kuleta madhara kwa nafsi au kinachopelekea madhara kwa nafsi nyingine ni HARAAM ila tu pale kutakapotokea dalili ya kuonyesha kinyume chake. Na imepokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad na Abu Daawuud na Al-Bayhaqiy na wengineo kutoka kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kila chenye kulewesha.”

Akaendelea Shaykh kuelezea kwa kirefu madhara yake yanayompata mtu binafsi na yale yanayoikumba Taifa zima kutokana na ulaji wake na kilimo na mengine ya kidini, kiafya, kiuchumi, upotezaji wakati na kutopatikana uzalishaji, kuenea umaskini, wizi, rushwa, uongo, kupotea haki za watu na mengi mengineyo.

Akamalizia Shaykh kwa kutaja Wanachuoni wengi walioharamisha Mirungi, miongoni mwao ni:
Shaykh Ahmad bin Hajar Al-Haytamiy katika kitabu chake “Tahdhiyr Ath-Thuqaat Min Aklil Kuftati Wal Qaat”, na Al-Faqiyh Abu Bakr bin Ibraahiym Al-Muqriy Al-Haraaziy Ash-Shaafi’iy katika kitabu chake, “Tahriym Al-Qaat”, na wengineo ni Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aal Shaykh, na Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz, na Shaykh Abul Hasan Mustwafaa bin Ismaa’iyl As-Sulaymaaniy na Maulamaa wengine.
Ama Shaykh Muqbil bin Haadiy Al-Waadi’iy (ambaye ni mwalimu wake), yeye amewafikiana na Fatwa hii. Na kumetungwa vitabu mbalimbali kuharamisha Mirungi ambavyo vimetaja ndani yake madhara na mafaasid yanayopatikana katika ulaji Mirungi, miongoni mwa vitabu hivyo ni, “Kashfu Ash-Shubuhaat ‘An Adhwraaril Qaat” cha Dkt. Ibraahiym bin ‘Abbaas, na kitabu “Al-Qaat” cha Dkt. Al-Marzuuqiy na Dkt. Abu Khutw-wah, na kitabu “Shahaadaatu Ath-Thuqaat ‘Alaa Adhwraaril Qaati” cha Shaykh ‘Aaidhw bin ‘Aliy Mismaar, na kitabu “Al-Qaatu Wal Mujtama’” cha Abu Ibraahiym Atw-Twayriy.
(Mwisho wa kumnukuu)
  
Tunamalizia makala hii ya Mirungi kwa wito kwa walaji wote wamche Allaah na wajiepusha na jambo hilo chafu, baya, lenye madhara makubwa ya kidini, kimwili, kiafya, kimali na kiuchumi, na watumie muda wao huo mkubwa wanaoupoteza kufanya yenye manufaa kwa dunia na Akhira yao. Na wakumbuke wataulizwa siku ya masiku kwa muda wao walioupoteza, na kwa mali yao walivyotumia.

Na wale wanausuhubiana na walaji, wito kwao wajiepushekusuhubiana na watu hao wasije nao kuingia kwenye balaa na afa hilo miongoni mwa maafa makubwa yaliyomo katika jamii ya Kiislam, wakumbuke pia mwenye kusuhubiana na mfua chuma, basi ima akuunguzie nguo yako au akutie harufu mbaya ya moshi wake. Hiyo ni tahadhari tuliyopewa na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa hiyo tuizingatie sana inshaAllaah.

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ajaalie risala hii iwe khaaliswan Liwajhih na iwe na taathira kwa walaji Mirungi na inshaAllaah iwe ndio sababu ya kuachana kwao na uraibu huo.

2 comments:

  1. INTERNATIONAL CONCEPT OF WORK FROM HOME
    Work from home theory is fast gaining popularity because of the freedom and flexibility that comes with it. Since one is not bound by fixed working hours, they can schedule their work at the time when they feel most productive and convenient to them. Women & Men benefit a lot from this concept of work since they can balance their home and work perfectly. People mostly find that in this situation, their productivity is higher and stress levels lower. Those who like isolation and a tranquil work environment also tend to prefer this way of working. Today, with the kind of communication networks available, millions of people worldwide are considering this option.

    Women & Men who want to be independent but cannot afford to leave their responsibilities at home aside will benefit a lot from this concept of work. It makes it easier to maintain a healthy balance between home and work. The family doesn't get neglected and you can get your work done too. You can thus effectively juggle home responsibilities with your career. Working from home is definitely a viable option but it also needs a lot of hard work and discipline. You have to make a time schedule for yourself and stick to it. There will be a time frame of course for any job you take up and you have to fulfill that project within that time frame.

    There are many things that can be done working from home. A few of them is listed below that will give you a general idea about the benefits of this concept.

    Baby-sitting
    This is the most common and highly preferred job that Women & Men like doing. Since in today's competitive world both the parents have to work they need a secure place to leave behind their children who will take care of them and parents can also relax without being worried all the time. In this job you don't require any degree or qualifications. You only have to know how to take care of children. Parents are happy to pay handsome salary and you can also earn a lot without putting too much of an effort.

    Nursery
    For those who have a garden or an open space at your disposal and are also interested in gardening can go for this method of earning money. If given proper time and efforts nursery business can flourish very well and you will earn handsomely. But just as all jobs establishing it will be a bit difficult but the end results are outstanding.

    Freelance
    Freelance can be in different wings. Either you can be a freelance reporter or a freelance photographer. You can also do designing or be in the advertising field doing project on your own. Being independent and working independently will depend on your field of work and the availability of its worth in the market. If you like doing jewellery designing you can do that at home totally independently. You can also work on freelancing as a marketing executive working from home. Wanna know more, email us on workfromhome.otr@gmail.com and we will send you information on how you can actually work as a marketing freelancer.


    Internet related work
    This is a very vast field and here sky is the limit. All you need is a computer and Internet facility. Whatever field you are into work at home is perfect match in the software field. You can match your time according to your convenience and complete whatever projects you get. To learn more about how to work from home, contact us today on workfromhome.otr@gmail.comand our team will get you started on some excellent work from home projects.


    Diet food
    Since now a days Women & Men are more conscious of the food that they eat hence they prefer to have homemade low cal food and if you can start supplying low cal food to various offices then it will be a very good source of income and not too much of efforts. You can hire a few ladies who will help you out and this can be a good business.

    Thus think over this concept and go ahead.

    ReplyDelete
  2. hello,
    Hii ni kuwajulisha wananchi kwa ujumla kuwa Bibi, kiutamaduni matumaini binafsi mkopo wakopeshaji ina kufungua nafasi mpya za fedha kwa kila mtu katika haja ya msaada wowote wa kifedha. Sisi kutoa mkopo saa 2% riba kwa watu binafsi, makampuni na makampuni chini ya sheria wazi na ya kueleweka na hali hiyo. wasiliana nasi leo na e-mail (merithope6@gmail.com)

    ReplyDelete

Twitter Bird Gadget