Thursday, April 5, 2012

HUKMU YA MWENYE KUACHA KUSALI

HUKMU YA MWENYE KUACHA KUSALI (TAARIKU SALAAT)
Maulamaa wote bila hitilafu yoyote baina yao wamekubaliana kuwa mwenye kuiacha Sala kusudi kwa jeuri na kwa kuikanusha, huyo anakuwa kafiri aliyekwisha toka katika dini ya Kiislam.
Isipokuwa wamehitalifiana juu ya yule mwenye kuiacha kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha na dunia lakini haikanushi na anaamini kuwa ni fardhi juu yake.
Wapo wanaosema hata huyu naye pia anakuwa kafiri aliyekwishatoka katika dini ya Kiislam, na dalili walizoziegemea maulamaa hao ni hadithi za Mtume (SAW) zifuatazo;
“Kutoka kwa Jabir (RA) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Baina ya mtu (kuwa Muislam) na baina ya (kuwa) kafiri, ni kuacha Sala”.
Muslim – Ahmed – Atttirmidhiy na wengineo
Na kutoka kwa Buraida (RA) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Ahadi iliyopo baina yetu na baina yao ni Sala, atakayeacha (kusali) kesha kufuru”.
Ahmed na wengineo
Na kutoka kwa Abdillahi bin Amru bin Al Aas (RA) kuwa Mtume (SAW) siku moja alizungumza juu ya Sala kisha akasema;
“Atakayeisimamisha atakuwa na nuru na dalili na ataokoka siku ya Kiama, ama asiyeisimamisha hatokuwa na nuru wala dalili wala hatookoka, na atakuwa siku ya Kiama pamoja na Qaruni na Firauni na Hamana na Ubaya bin Khalaf”.
Imam Ahmed na Attabarani na wengineo
Katika kuifasiri hadithi hii, anasema mwanachuoni maarufu Ibnul Qayim al Jouzi kuwa;
“Mwenye kuacha Sala huwa ameshuhgulika na mojawapo kati ya yafuatayo; ama atakuwa imemshughulisha mali yake au ufalme wake au cheo chake au biashara zake. Yule aliyeshughulika na mali yake, atafufuliwa pamoja na Qaruni, na aliyeshughulika na ufalme wake, huyo atakuwa pamoja na Firauni, na aliyeshughulika na cheo chake atakuwa pamoja na Hamana na yule aliyeshughulika na biashara zake (akaacha kusali), huyo atakuwa pamoja na Ubaya bin Khalaf”.

Kutoka kwa Abdillahi bin Shaqiq Al Aqliy anasema;
“Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) hawakuwa wakiona amali yoyote nyingine mtu akiiacha anakuwa kafiri isipokuwa Sala”.
Attirmidhiy na Al Hakim

Anasema Ibni Hazm;
“Imepokelewa kutoka kwa Omar bin Khatab na Abdul Rahman bin Auf na Muadh bin Jabal na Abu Huraira na Masahaba wengi (RA) kuwa;
“Atakayeacha kusali (Sala moja tu ya) fardhi kusudi (bila ya udhuru wowote) mpaka wakati wake (Sala hiyo) ukatoka, anakuwa kafiri”.

Hadithi zifuatazo zinaelezea juu ya hukmu ya kuuliwa kwa Taariku ssalaat (Asiyesali);
Kutoka kwa Ibni Abbas (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Heshima ya Uislam na misingi ya dini ni mitatu, juu yake misingi hiyo umejengeka Uislam. Atakayeacha mojawapo anakuwa kafiri na damu yake halali;
Kushuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah,
Na Sala zilizofaradhishwa,
Na Funga ya Ramadhani”.
Abu Yaala
Na kutoka kwa Ibni Omar (Abdillahi bin Omar bin Khattab (Radhiyallahu anhum) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Nimeamrishwa nipigane vita mpaka pashuhudiwe kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na isimamishwe Sala na itolewe Zaka, watakapofanya hivyo, itakingika kwangu damu zao na mali zao ila kwa haki ya Uislam na hesabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka”.
Bukhari na Muslim”

RAI ZA BAADHI YA WANAVYUONI
Anaendela kusema Sayed Sabeq kuwa;
“Kutokana na Aya pamoja na Hadithi zilizotangulia, inatubainikia kuwa Asiyesali ni kafiri na kwamba damu yake ni halali. Hata hivyo baadhi ya maulamaa waliotangulia na wa siku hizi wakiwemo Imam Abu Hanifa na Imam Shafi na Imam Ahmed wanasema kuwa hawi kafiri moja kwa moja, bali anahesabiwa kuwa ni mtu fasiq na anakamatwa na kutubishwa na akikataa kutubu basi maulamaa wote hao wanasema kuwa mtu huyo anahukumiwa kuuliwa.
Anasema Annawawi katika Sharhi Muslim;
“Anakatwa kichwa chake kwa upanga”.

Imam Abu Hanifa anaona kuwa aliyertadi na akastahiki kuhukumiwa kuuliwa ni yule tu anayeikanusha Ibada hiyo ya Sala, lakini yule anayeacha kusali kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha na dunia, huyo si kafiri bali ni fasiq na hukmu yake ni kumhamisha mbali na mji wake, wakiegemea dalili zinazobeba maana kwa ujumla kama vile kauli Yake Subhanahu wa Taala aliposema;
“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe(dhambi ya) kushirikishwa na kitu, lakini Yeye husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye”.
Annisaa - 114
Na hadithi iliyosimuliwa na Abu Huraira kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Kila Mtume ana dua yake inayokubaliwa. Kila Mtume akafanya haraka kuiomba dua yake hiyo. Ama mimi nimeiweka dua yangu kwa ajili ya kuwaombea shafaa ummati wangu siku ya Kiama, ataipata Inshaallah kila aliyekufa na asimshirikishe Mwenyezi Mungu na chochote”.
Na hadithi nyingine za mfano huo.

Maulamaa wengine wakasema kuwa hauliwi mtu kwa ajili ya kutosali, na hawa wameegemeza hoja zao kutokana na hadithi iliyomo ndani ya Bukhari na Muslim isemayo;
“Si halali kumwaga damu ya Muislamu ila kwa mojawapo ya matatu; Mzinzi aliyekwishaoa, nafsi kwa nafsi (aliyeuwa auwawe) na aliyertadi (aliyetoka katika dini) na kujitoa katika jamii ya Kiislam”.
Wanasema kuwa hapa Mtume (SAW) hakumtaja asiyesali kuwa ni miongoni wa waliohalalishwa damu yao. 

MAJADILIANO BAINA YA IMAM SHAFI NA IMAM AHMED
Imepokelewa kuwa Maimam waiwili wakubwa, Imam Shafi na mwanafunzi wake Imam Ahmed bin Hanbal walijadiliana juu ya maudhui haya ya mtu asiyesali, na majadiliano hayo yalikwenda kama ifuatavyo;
Imam Shafi;
“Ewe Ahmed! Unasema kuwa anayeacha kusali anakuwa kafiri?”
Imam Ahmed;
“Ndiyo nasema hivyo”.
Imam Shafi;
“Ikiwa atakuwa kafiri, vipi atarudi katika Uislam?”
Imam Ahmed;
“Kwa kutamka; ‘Ash-hadu an laa ilaaha illa Llah Muhammadan Rasulu Llah”.
Imam Shafi;
“Lakini mtu huyo hajaikanusha shahada hiyo”.
Imam Ahmed;
“Anarudi katika Uislam kwa kusali”.
Imam Shafi;
“Sala ya kafiri haikubaliwi, na kafiri hahesabiwi kuwa ni Muislamu hata kama atasali”.
Imam Ahmed akanyamaza.

TAHAKIKI YA IMAM ASHAUKANI
Anasema Ashaukani kuwa;
Kwa hakika asiyesali ni Kafiri, kwa sababu hadithi zote zilizopokelewa katika maudhui haya zinamwita hivyo (kuwa ni kafiri), na mpaka uliowekwa baina ya mtu anayestahiki kuitwa kafiri na yule asiyestahiki kuitwa kafiri ni ‘Sala’

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget