Wednesday, April 4, 2012

Utaratibu wa kuiwajibisha Nafsi.


Pale ambapo nafsi ya mja imejiona kwamba imeelekea kwenye amali chafu zaidi kuliko amali njema basi haina budi nafsi hiyo kuwajibishwa.  Hili ni jukumu la kila mja na nafsi yake ikiwa mja huyu kweli anamuamini Allah (Subhaanahu Wata’ala) na siku ya mwisho.

Utaratibu huu uko aina mbili.

(i)            Kabla ya amali – kitendo

(ii)          Baada ya amali – kitendo

Utaratibu huu umegawika aina mbili kwa mujibu wa aya ya  Al Hashr/18

يأَيُّهَا الَّذِينَ ءَامَنُواْ اتَّقُواْ اللَّهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ وَاتَّقُواْ اللَّهَ إِنَّ

                                                              اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ       

“ Enyi mlio amini! Mcheni (muogopeni) Allah, na kila nafsi iangalie inayo yatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni (muogopeni) Allah. Hakika Allah anazo khabari ya mnayo yatenda.”

Katika aya hii limetajwa neno Taqwa mara mbili  baina ya kauli yake (Subhaanahu Wata’ala)  “ na kila nafsi iangalie inayotanguliza kwa ajili ya kesho” 

Hivyo kumuogopa Allah(Subhaanahu Wata’ala) kabla ya kufanya amali na kurudi tena kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) baada ya kufanya amali ndiyo maana walliyoifahamu wafasiri na tutaielezea kwa kirefu.

(i)           Kuiwajibisha nafsi kabla ya kitendo

Muumini wa kweli, kabla ya kufanya tendo lolote lile ni vyema asite kwa  kulitazama .  Je tendo hili ni zuri au baya?. Hatoi uamuzi mpaka ahakikishe kwamba chaguo lake  kulifanya/kuliacha tendo hilo ni la busara na kumridhisha Allah (Subhaanahu Wata’ala). Chanzo kikuu ni mja kujijua kwanza yeye mwenywe ni nini atende au asitende nini na kwa nini, sambamba na kuijua nafsi yake mbele ya Mola wake na mbele ya viumbe wenzake.

Tukitaka kufuata utaratibu huu hatua kwa hatua ni kama ifuatavyo:-


Hatua ya kwanza: Tathmini

Tathimini kabla ya kuamua kufanya tendo lenyewe je ni zuri kwake na je atapata ujira kwa tendo hili?  Au ni baya kwake na je hatopata dhambi na kumzidishia mzigo?  Akiliona kuwa ni zuri na kuwa na faida nalo binafsi na kwa dini yake na kuko tuendako akhera huenda hatua ya pili.


Hatua ya pili: Ithbati

Baada ya kulifanyia tathmini tendo ni vyema ukapata uthibitisho wa tendo kwa kuiuliza nafsi:

Je! ni vyema kulitenda, kusubiri au kutolitenda?  Ikiwa chaguo ni kutolitenda basi moja kwa moja ajiepushe nalo na aliondoshe kabisa mawazoni.  Ikiwa ni kusubiri kwa kuona labda wakati si muafaka kulitenda jambo hilo basi ni bora awe na uvumilivu na asaa subira hii itamletea kheri nyingi. Na kama ataamua ndiyo ni vizuri kulitenda hapo ataelekea hatua ya tatu.


Hatua ya tatu: Kuwepo Ikhlasi

Hapa tunaangalia kama tendo hili linatendwa kwa nia safi kabisa ya kutaka ridhaa ya Allah (Subhaanahu Wata’ala) na kupata makaazi mema tuendako akhera.  Je mja analifanya kwa nia hiyo au ni kutaka kujionesha tu. Na kama ni kutaka ridhaa ya Allah (Subhaanahu Wata’ala) na baada ya kupitia hii hatua basi aendeleaa kulitekeleza huku akiomba msaada kwake (Subhaanahu Wata’ala) kulifanikisha kwa kheri na kuliepusha na mitihani.  Na kama ni vyenginevyo basi moja kwa moja aachane na tendo hili kwani halitokuwa na faida kwa yeye mwenyewe, wala dini yake na hata huko tuendako akhera. Na hapa tunapata mfano halisi katika utekelezaji wa amali zetu je zinakuwa ada au ibada? . Kwani ikiwa amali imeshageuka na kuwa ada basi moja kwa moja amali hiyo haikufanywa kwa Ikhlasi

Na kukosa ikhlasi ambayo ndiyo roho ya ibada amali hii iko hatarini kutopokelewa na Allah(Subhaanahu Wata’ala). Sasa ikiwa mja amejitathmini mwenyewe ndani ya nafsi yake na kujitambua hivyo basi ana wajibu wa kurudi nafsi yake na kuirekebisha katika mfumo mzima wa utendaji wa amali zake.


Hatua ya nne: Shura/Istikhara

Hatua hii itakuja endapo mja licha ya kupita hatua zote tatu bado ameshindwa kupata uamuzi.  Hapa ataweza kufanya shura na kutafuta ushauri ima kwa waislam wenzake au kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) kwa kufanya Istikhara (kuomba ushauri wa kheri).

(ii)          Kuwajibisha nafsi baada ya kitendo.

Ikiwa mja amekumbushwa kuiwajibisha kabla ya kitendo basi ana wajibu tena na kuirudi nafsi yake baada yake pia.

Nayo imegawika sehemu tatu:-

Sehemu ya kwanza

Kuiwajibisha kwa amali au kitendo kilichofanyika lakini hakikukamilika au kufanywa lakini katika utaratibu uliokuwa na kasoro.

Kila amali itatakiwa ipite katika mambo yafuatayo ili amali hiyo ihesabike kama imefanyika kwa ukamilifu, nayo ni:-

1)    Ikhlasi katika kufanya amali

2)    Taqwa (khofu) kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) na unyenyekevu.

3)    Kigezo/Ruwaza yaani kumfuata Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) katika kuhakikisha kulitenda vilivyo.

4)    Kuwa na matarajio kutoka kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala

Mambo haya ni lazima yatumike katika kutathmini mfumo mzima wa utendaji amali yoyote ile ya kumtii Allah Subhaanahu Wata’ala). Ikiwa mja ataifanyia tathmini amali na kutopatikana moja kati ya mambo haya basi nafsi ina wajibu na kuziangalia dosari zilizopo na kuzirekebisha. . 

Sehemu ya pili.

Kuwajibisha nafsi kwa zile amali ambazo zilikuwa ni vyema zaidi kuachwa kuliko kutendwa.

Hapa panakusudiwa zaidi zile amali zenye utata labda katika uhalali na uharamu wake.Au amali ambazo kufanyika kwake huwa ni makruhu na kadhalika. Kwa sababu ukiziacha na ni halali unakuwa hujafanya kukosa kwani kuacha kufanya halali katika sheria si dhambi lakini ukizifanya na zikawa ni haramu basi tayari uko katika dhimma.

Sehemu ya tatu

Kuwajibisha nafsi katika matendo yote ya mubaha (yale kutoyafanya hupati dhambi).

Je kwa nini aliyafanya na nini alikusudia? Je utendaji huu ulikusudiwa kupata radhi za Allah (Subhaanahu Wata’ala) na mafanikio huko akhera au ilikuwa ni kupata mafanikio ya kidunia tu na hapo kupoteza ile fursa ya kunufaika kwa sababu tu ya nia  aliyoikusudia.

Kuiwajibisha nafsi kwa   mambo ya wajibu.

Ni vyema mja aangalie katika mambo ya wajibu anayoyatekeleza Je aliyatekekleza kikamilifu?. Na kama kuna kasoro na upungufu basi ni wajibu mja kurekebisha dosari iliyokuwepo au kama ni upungufu basi ni kuuondoa ima kwa kuutekeleza wajibu wenyewe kama inavyotakiwa au kurekebisha dosari zake. 

Kama wajibu huo ni sala .  Hivyo, nafsi ijirudi kama haitekelezi ibada hii na kuanza kufanya hivyo haraka iwezekenavyo, na kama kuna dosari katika kuitekeleza basi ni wajibu wa nafsi kuzirekebisha dosari hizo zikiwa kama kutozisali kwa wakati wake au kutosali jamaa msikitini na kadhalika.

Kuiwajibisha nafsi kwa yale yaliyoharamishwa.

 Ukigundua nafsi kama imetenda haya basi haraka iwezekanavyo irudi kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) na kuomba toba na  maghfira. Pia kufanya amali njema ili iweze kuifuta ile amali iliyoharamishwa. Mfano mja amesema uongo, amesengenya basi akijishtukia tu kama ametenda jambo la haramu aombe msamaha kwa mola wake haraka iwezekanavyo. Na kujitahidi kusema ukweli na kuacha kabisa tabia ya kusengenya.Ndivyo Quraan inavyotufundisha Huud/114

وَأَقِمِ الصَّلَوةَ طَرَفَىِ النَّهَارِ وَزُلَفاً مِّنَ الَّيْلِ إِنَّ الْحَسَنَـتِ يُذْهِبْنَ السَّـيِّئَـتِ

                                                     ذِكْرَى لِلذَكِرِينَ  ذلِكَ                               

Na simamisha Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka.

Kutojihimu katika kuiwajibisha nafsi katika kufanya amali. 

Ukigundua nafsi kwamba haikuipa umuhimu jambo ambalo lilistahiki hivyo basi ni wajibu kwa nafsi hiyo kurudi kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) na kuomba msamaha kwa nia safi kabisa. Mfano kila muislamu mwanamme anatakiwa kuzisali sala tano jamaa msikitini,ni vyema aelewe kuwa ipo kasoro katika utekelezaji huu. Sasa ikiwa mja anajiona yumzito kutekeleza jambo hili muhimu atatakiwa kuomba maghfira na kuanza kuitekeleza ibada hii kama inavyotakiwa .

FAIDA /HASARA ZA KUIWAJIBISHA /KUTOIWAJIBISHA NAFSI

FAIDA

HASARA

1

Kuwa tayari kumridhisha Allah (Subhaanahu Wata’ala)

Kufanyika amali isiyokubaliwa na Allah (Subhaanahu Wata’ala)

2

Kuweza kugundua kasoro na kutafuta njia za kuziondoa

Kufanya amali kimakosa

3

Kuweza kuisukuma nafsi kufanya yale isiyoyataka

Kuikubalia nafsi matakwa yake

4

Kujenga uvumilivu

Kushindwa kustahamili

5

Kuwa mkweli kwa nafsi, Allah (Subhaanahu Wata’ala) na watu wengine

Kujidanganya nafsi yako

6

Kuwa karibu na Allah(Subhaanahu Wata’ala)

Kumfanya shetani rafiki.

Kuna faida kubwa sana kwa mja pale anapowajibisha nafsi yake mwenyewe kabla ya kuwajibishwa.

Moja ya faida hizo ni kuweza kugundua na kuzielewa kasoro za nafsi.  Kwani mja asiyezijua kasoro zake mwenyewe huwa vigumu kuweza kuziondoa.

Ibnul Qayyim amesema: “Bila ya shaka kuichukia nafsi kwa ajili ya Allah (Subhaanahu Wata’ala) ni moja katika  tabia za watu wakweli. Hii ni muhimu sana kwani ni ufunguo wa mlango wa unyenyekevu na uvumilivu badala ya kiburi, majivuno na kujiona na hivyo nafsi kuwa safi mbele ya Allah (Subhaanahu Wata’ala).”

Moja kwa moja mja atarudi kwa mola wake huku akiwa na imani kwamba katika mihangaiko yake yote hatoweza kufanikiwa bila ya kupata msamaha, ukarimu na rehma za Allah (Subhaanahu Wata’ala). 


KWA NINI IKHLASI ?

Tumeona katika somo letu la Jihadi dhidi ya nafsi, Ikhlas ni zana moja muhimu ya kuwa nayo kwa kila mwenye kuingia katika kazi hii . Hivyo kwa kumalizia tumeona bora tuigusie  tena ikhlasi. Kwani katika alama za kheri kwa mja ni kutafuta ukamilifu katika maeneo ambayo yana kasoro katika nafsi yake.

Maana ya ikhlasi kilugha  ni kitu safi au utakaso.

Ikhlasi  kisheria ni:

“kuzisafisha amali zisichanganyike na malengo mengine zaidi ya kutaraji radhi za Allah(Subhaanahu Wata’ala).

Katika Quraan ikhlasi imetajwa katika aya nyingi kama

Al Bayyinah/5

                                          وَمَآ أُمِرُواْ إِلاَّ لِيَعْبُدُواْ اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدّينَ


Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Allah kwa kumtakasia Dini

Al An- ‘Aam /162

                                 

              قُلْ إِنَّ صَلاَتِى وَنُسُكِى وَمَحْيَاىَ وَمَمَاتِى للَّهِ رَبِّ الْعَـلَمِينَ                


 Sema: Hakika Sala yangu, na vichinjwa vyangu(katika ibada za hijja), na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allah, Mola  wa viumbe vyote.

Kwa maana hii basi ikhlasi ina mihimili miwili mikuu nayo ni:

1             Amali itayofanyika iwe ni kwa ajili ya Allah(Subhaanahu Wata’ala) pekee na si vyenginevyo.

2             Amali iwafikiane na sheria ya Allah(Subhaanahu Wata’ala) kama ilivyokuja katika kitabu chake Quraan na Sunna za Mtume wake (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam).


DALILI ZA KUWEPO IKHLASI KATIKA AMALI

Allah (Subhaanahu Wata’ala) anasema katika Suuratul qiyaamah /14

                                                              بَلِ الإِنسَـنُ عَلَى نَفْسِهِ بَصِيرَةٌ

Bali binadamu ni shahidi juu ya nafsi yake

                                           

Kwa hivyo mja mwenyewe tayari anaweza kuijua amali aliyoifanya kama aliifanya kwa ikhlasi au laa. Na baadhi yake ni zifuatazo:

A         Mukhlis (mwenye kufanya ikhlaas) hajinasibishi na fadhila, khairaat au neema zozote alizojaaliwa kuwa nazo bali hurudisha fadhila kwake Allah (Subhaanahu Wata’ala) na wala haangalii vipimo na vigezo vya waja katika mfumo mzima wa utendaji amali zake. Kigezo chake ni Allah (Subhaanahu Wata’ala) pekee.

Suuratul Insaan/ 9

                               إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّهِ لاَ نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَآءً وَلاَ شُكُوراً

Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Allah(SUBHAANAHU WATA’ALA). Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.

B         Mukhlis akifanya amali kwa utaratibu unaotakiwa na sheria huwa hana haja ya kutaka kusifiwa au kulaumiwa na waja wenzake.Hubaki kusubiri malipo kutoka kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) na ridhaa yake.

Suuratul Llayl/19-21

وَمَا لاًّحَدٍ عِندَهُ مِن نِّعْمَةٍ تُجْزَى - إِلاَّ ابْتِغَآءَ وَجْهِ رَبِّهِ الاٌّعْلَى –            

                                                                      وَلَسَوْفَ يَرْضَى

Na wala si kwa kuwa yupo yeyote aliye mfanyia hisani ndio anamlipa

Ila ni kutaka radhi ya Mola wake  aliye juu kabisa

Naye atakuja ridhika!

C         Mukhlis siku zote akifanya amali hata kama imekamilika katika idara zote bado hujihisi kuwepo na upungufu fulani kati ya utendaji wake na jinsi anavyotaka Allah(Subhaanahu Wata’ala

D         Mukhlis anapofanya amali isiyohitajika kuonekana mbele ya macho ya watu kisheria basi huificha .Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) anatutajia katika wale watu saba watakaofunikwa na kivuli cha Allah(Subhaanahu Wata’ala) siku ambayo hakutokuwa na kivuli chengine zaidi ya chake kwamba:

ورجل تصدق بصدقة فأخفاها ، حتى لا تعلم شماله ما تنفق يمينه ، ورجل ذكر الله                                                              خالياً ففاضت عيناه "        

“Na mtu atakaetoa sadaka na kuificha hata usijue mkono wake wa kushoto kilichotolewa na mkono wa kulia na mtu aliekaa faragha na kumkumbuka Allah(Subhaanahu Wata’ala) kisha akabubujikwa na machozi”

 Na hapa tuutazame wasia wa Luqmaan kwa mwanawe alipomwambia “ Ikiwa kuidhihirisha (amali) ni wajibu basi jitahidi kuitakasa amali hiyo kwa ajili ya Allah (Subhaanahu Wata’ala) na ikiwa haikulazimilka kuidhihirisha, ,jitahidi kumsafishia Allah(Subhaanahu Wata’ala) kwa kuificha.”

Kwa ufupi hizi ni baadhi tu ya dalili za amali kufanyika kwa ikhlasi au vyenginvyo.

Kufanyika amali kwa ikhlasi hupelekea mja kupata utulivu wa moyo ambao kila wakati humfanya kuitazama tena nia yake kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala). Hali kadhalika kuwa na hisia kwamba kila wakati Allah (Subhaanahu Wata’ala) anamuona na anajua kila kinachojiri ndani ya moyo wake na hivyo kuwa na nadhari na tahadhari kwa kila kitu huku akijikurubisha kwake kwa kuomba kama alivyokuwa akiomba amiirul muuminiin Umar ibn Khattaab(R.A) ; “ Ewe mola ijaalie kila amali yangu kuwa njema na ijaalie mbele yako yenye ikhlasi na wala usiijaalie kwa mtu yeyote, kitu chochote(katika amali zangu)”

Ni haki yake mola kutiiwa, kupendwa, kukumbukwa na kushukuriwa mola ambae ndiye muumba wa nafsi na mfanya atakalo.

Allah wewe ndiye Mola wangu. Umeniumba na mimi ni mja wako, na mimi nitatimiza ahadi yako na waadi wako kiasi niwezavyo. Najikinga kwako kutokana na kila shari uloumba. Nakiri juu ya neema zote ulizonineemesha nazo. Na ninakiri juu ya dhambi zangu. Kwa hivyo nisamehe, kwani hapana mwenye kusamehe madhambi isipokuwa wewe.

Tumuombe Allah (Subhaanahu Wata’ala) atuongoze katika kuzisafisha nafsi zetu, atupe moyo wa subira na uvumilivu katika kupigana jihadi na nafsi zetu, atuongeze imani katika kuzitakasa nafsi zetu na tujikurubishe kwake kwa kufanya kila lenye kumridhisha Allah(Subhaanahu Wata’ala) hata kama nafsi zetu hazitopendezwa, na atuoneshe njia kama alivyutuahidi katika Quraan Al- Ankabuut/69

                وَالَّذِينَ جَـهَدُواْ فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا وَإِنَّ اللَّهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ    

Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Allah yu pamoja na watu wema.

Hakika Allah(Subhaanahu Wata’ala) ni muweza wa hayo.

Wabillahi Tawfiyq.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget