Friday, April 20, 2012

Adabu za kustanji (Kuchamba)


Kustanji/Kuchamba ni kusafisha na kuondoa najisi iliyotoka katika mojawapo ya tupu {uchi}mbili au zote mbili; tupu ya mbele na ya nyuma kwa kutumia maji twahara au kinachosimama memo/mahala pa maji wakati wa kukosekana maji kama vile mawe, karatasi, kitambaa, majani na kadhalika. Mchambaji ahakikishe amejisafisha vema kiasi cha kutobakia athari ya najisi iliyotoka; ikiwa ni mkojo au mavi.
Kustanji/Kuchamba baada ya kukidhi haja ni WAJIBU/FARADHI kama tutakavyoona katika kauli za Mtume – Rehma na Amani zimshukie – katika maelezo yajayo.

VITU VITUMIKAVYO KATIKA KUSTANJI
Inajuzu/inafaa kustanji (kuchamba) kwa kutumia maji mutlaq (maji halisi) ambayo ndiyo asili katika kujitwahirisha na najisi. Pia inajuzu kustanji kwa kila kitu chenye sifa zifuatazo :
  1. Kigumu (kigogofu)
  2. Chenye Kuparuza (kisichoteleza)
  3. Kinachoweza kuondosha najisi.
Vitu vyenye sifa hizi ni kama mawe, karatasi, kitambaa na kadhalika. Ni vema kustanji, mtu akaanza kwa kutumia mawe/karatasi kisha ndio akamalizia na maji. Kufanya hivyo ni kwa sababu mawe/karatasi huondosha juta (dhati) ya najisi na maji huondosha athari ya najisi bila ya kuchangayika na juta lake. Ikiwa atatumia kimojawapo baina ya mawe/karatasi na maji, basi ni bora akatumia maji kwani ndiyo pekee yenye uwezo wa kuondosha juta (dhati) na athari ya najisi, kinyume na mawe na nduguze {karatasi, kitambaa na kadhalika}.
Imepokelewa kutoka kwa Anas Ibn Maalik – Allah amuwie Radhi – amesema : Mtume wa Allah alikuwa akiingia mahala pa kukidhi haja, mimi na kijana wa rika langu tukimbebea chombo cha maji na fimbo/mkuki mfupi, basi akistanji kwa kutumia maji. Bukhariy na Muslim.
Maelezo : Fimbo/Mkuki ulikuwa ukitumika kama sitara na alama wakati wa kuswali ili mtu asiweze kupita mbele.
Imepokewa na Ibn Masoud – Allah amuwie Radhi – amesema : Mtume – Rehma na Amani zimshukie – alienda kukidhi haja na akaniamrisha nimletee mawe matatu. Al-Bukhariy.
USISTANJI kwa kutumia najisi nyingine iliyo kavu au kitu kilichonajisika tayari kwani huenda kikaizidisha athari ya najisi badala ya kuipunguza. 
Kadhalika ni haramu kustanji kwa kilicho chakula cha binadamu kama vile mkate au chakula cha majini kama vile mifupa. Amesema Bwana Mtume – Allah amshushie Rehma na Amani – "Msistanji kwa (kutumia) kinyesi cha wanyama wala mifupa kwani hiyo (mifupa) ni chakula cha ndugu zenu majini" Tirmidhiy.
ADABU/TARATIBU ZA KUFUATA KATIKA KUKIDHI HAJA NA KUSTANJI (KUCHAMBA)
Sheria imeweka taratibu ambazo muislamu anapaswa kuzichunga na kuzifuata wakati wa kukidhi haja na kustanji. Taratibu hizi tutazigawa katika mafungu/sehemu zifuatazo :

A. ADABU/TARATIBU ZINAZOFUNGAMANA NA MAHALA PA KUKIDHIA HAJA
Imemlazimu mkidhi haja, ajiepushe kukidhi haja katika :
  1. Njia ya watu au mahala wanapokaa, hii ni kutokana na kero na maudhi yatakayowapata. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah amuwie Radhi – kwamba Mtume – Rehma na Amani zimshukie – amesema : "Yaogopeni mambo mawili yaletayo laana" (Maswahaba) wakauliza : Ni yapi mambo mawili hayo ? (Mtume) akajibu : "Ni yule ambaye anajisaidia katika njia ya watu au kivuli chao" Muslim.
  2. Tundu iliyopo ardhini au ufa wa ukuta/kiambaza. Hii ni kwa sababu ya kumlinda na kumuepusha mkidhi haja na madhara yanayoweza kumpata. Kwani anaweza akawamo ndani ya shimo/ufa mdudu mwenye kudhuru kama vile nge au nyoka, huyu akakerwa na haja akaamua kumtokea mtu na kumdhuru. Imepokelewa kutoka kwa Abdillahi ibn Sarjisi, amesema : Amekataza Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – kukojoa katika tundu. Abuu Daawood.
  3. Chini ya mti utoao matunda. Hii ni kwa ajili ya kuyahifadhi na kuyalinda matunda yadondokayo yasipatwe na najisi. Ni mamoja ikiwa matunda hayo yanaliwa au hayaliwi lakini yana manufaa mengine kama dawa.
  4. Maji yaliyotuama (yasiokwenda). Hii ni kutokana na kichefuchefu watumiaji wa maji hayo yakiwa ni mengi yasiyoharibika na najisi na kuyanajisi yakiwa machache na hivyo kuyafanya yasifae kutumika. Imepokelewa kutoka kwa Jabir – Allah amuwie Radhi – kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kwamba (Mtume) amekataza kukojoa katika maji yaliyotuama". Muslim.
Kunya ni aula zaidi kwa kukatazwa

B. ADABU/TARATIBU ZENYE KUFUNGAMANA NA UINGIAJI NA UTOKAJI MAHALA PA KUKIDHI HAJA
Ni Vema kwa mwenye kutaka kukidhi haja, atangulize mguu wake wa kushoto wakati wa kuingia chooni na mguu wa kulia wakati wa kutoka chooni, kama tulivyofundishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kadhalika asiingie na chochote chenye jina la Mwenyezi Mungu au jina lolote tukufu kama vile jina la Mtume au aya ya Qurani Tukufu. Bali imemlazimu muislamu kukivua kitu hicho wakati wa kuingia chooni. Pia imesuniwa kuleta dua wakati wa kuingia chooni. Pia imesuniwa kuleta dua zilizothibiti kutoka kwa Bwana Mtume kabla na baada ya kutoka chooni.
Aseme kabla ya kuingia chooni :
BISMILLAH ALLAHUMMA INNIY AUDHUBIKA MINAL KHUBUTHI WAL-KHABAITH. Al-Bukhariy na Muslim.
Na aseme baada ya kutoka :
GHUFRAANAKA AL-HAMDU LILLAHIL-LADHIY ADH-HABA ANNIYL-ADHA WA-A’AFANIY. Abu Dawood, Al-tirmidhi, Ibn Majah na Al-twabraniy.

C. ADABU/TARATIBU ZIFUNGAMANAZO NA UPANDE WA KUELEKEA WAKATI WA KUKIDHI HAJA :
Ni haramu kwa mwenye kukidhi haja kuelekea Qiblah au kukipa mgongo. Uharamu huu ni iwapo anakidhi haja mwandani, wala hapana chenye kumsitiri wakati wa kukidhi haja yake. Na imeshurutizwa sitara isiwe mbali nae zaidi ya dhiraa tatu za binadamu sawa na sentimeta 150 takriban. Ikiwa jengo analotumia limeandaliwa maalum kwa ajili ya kukidhia haja (chooni), basi si haramu, bali inajuzu kuelekea na kulipa mgongo Qiblah kwa kuwa pana sitara.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Ayyuub Al-Answariy – Allah amuwie Radhi – kutoka kwa Mtume –Rehma na Amani zimshukie – amesema "mnapokwenda chooni msielekee Qiblah wala msikipe mgongo kwa (kukidhi) haja ndogo au kubwa, lakini elekeeni mashariki na magharibi". Al-Bukhariy na Muslim.

D. ADABU/TARATIBU ZINAZOFUNGAMANA NA HALI YA KUKIDHI HAJA :
Ni vema kwa mwenye kukidhi haja akategemea mguu wake wa kushoto na kuusimamisha/kuunyoosha mguu wa kulia, hivi ndivyo anavyotakiwa akae wakati wa kukidhi haja. Hekima ya ukaaji huu ni kuifanya haja itokee kwa wepesi kama vile unavyomimina kilichomo ndani ya chupa kwa kuinamisha upande upande. Kadhalika anatakiwa wakati wa kukidhi haja asiangalie juu, utupu wake wala kile kimtokacho. Pia ni karaha kuzungumza wakati anakidhi haja.
Imepokelewa na Ibn Umar –Allah amuwie Radhi – kwamba mtu mmoja alipita ilhali Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehma na Amani zimshukie – akikidhi haja ndogo, (mtu yule) akamtolea salamu, (Mtume) hakumjibu. Muslim.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said – Allah amuwie Radhi – amesema ; Nimemsikia Mtume – Rehma na Amani zimshukie – akisema : "Wasitoke watu wawili wakaenda kukidhi haja, hali ya kufunua tupu zao huku wakizungumza, hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hulichukia hilo" Abu Dawood na wengineo.
Maelezo : Inakisiwa/Inapimiwa juu ya maneno (mazungumzo) mambo mengine kama vile kula, kunywa na kuchezeachezea utupu (uchi).

Kustanji/kuchamba kwa kutumia mkono wa kushoto : Anatakiwa mwenye kukidhi haja atumie mkono wake wa kushoto kusafisha mahala ilipotokea najisi kwani ni karaha kutumia mkono wa kulia.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Qatadah – Allah amuwie Radhi – kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – amesema : "Anapokojoa mmoja wenu, basi asiishike dhakari yake kwa mkono wa kulia na wala asistanji/asichambe kwa mkono wa kulia".
Kadhalika miongoni mwa adabu, anatakiwa mwenye kukidhi haja mawandani; nje ya jengo lililoandaliwa kwa kukidhia haja (chooni), atafute mahala pa faragha palipo mbali na watu. Watu wasimuone wala kusikia harufu ya choo chake au sauti ya mashuzi yake. Imepokelewa kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa anapotaka kwenda kujisaidia huenda mbali mpaka mtu asiweze kumuona. Abu Dawood na Al-Tirmidhiy.

Vile vile anatakiwa asiisege/asiipandishe nguo yake ikiwa ni shuka/msuli mpaka akurubiapo ardhi, sio anaanza kuvua nje kabla hajaingia ndani. Afanye hivyo kwa ajili ya kuusitiri utupu wake, jambo ambalo limeamrishwa na sheria.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget