KITABU:Mchakato wa
Katiba Mpya Maelekezo Kwa Waislamu
JUKWAA LA WAISLAMU LA KURATIBU MCHAKATO WA
MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA
(JUWAKATA)
MUHIMU KWA WAISLAMU WOTE
Yaliyomo.
1.
Ijue JUWAKATA
2.
Maelezo ya awali
3.
Katiba ya nchi ni nini?
4.
Aina za Katiba duniani
5.
Muundo na vipengele vya katiba ya Tanzania
6.
Hatua za mchakato wa kupata katiba mpya
- Tume ya kurekebisha
Katiba
- Bunge la Katiba
- Kura ya Maoni
7.
Kwa nini Waislamu wanashiriki katika mchakato wa katiba?
- Wajibu
wa kupigania haki
- Uislamu
na katiba
- Fiq-hi
na mazingira yaliyopo
- Wajibu
wa Viongozi Waislamu
- Wajibu
wa Wanataaluma Waislamu
- Wajibu
wa Muislamu mmoja mmoja
- Umakini
wetu
8.
Mambo ya kupiganiwa na Waislamu katika katiba mpya.
9.
Hitimisho.
1.
JUWAKATA
JUWAKATA ni Jukwaa la waislamu
la Kuratibu mchakato wa Mabadiliko ya Katiba Tanzania. Chombo hiki kinaundwa na
Jumuiya na Taasisi mbali mbali za Kiislamu sizizopungua 40. Chombo hiki
kilizinduliwa rasmi katika kongamano kubwa lililohudhuriwa na kada mbalimbali
za Masheikh, wanataaluma na viongozi wa Kiislamu lililofanyika Januari 6, 2012
katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam na kuhusisha vyombo
mbalimbali vya habari. Makao makuu ya JUWAKATA ni Dar Es Salaam. JUWAKATA lina mawasiliano ya
karibu na Waislamu wa Tanzania
Visiwani kwa uratibu wa pamoja.
Aidha
azimio la mkutano mkuu wa Jumuiya na Taasisi za kiislamu, limeipa JUWAKATA
idhini ya kushirikiana na muislamu au mwananchi yeyote mwenye malengo ya
kupatikana katiba yenye misingi ya haki na uhuru pasina ubaguzi wa aina yoyote.
- MAELEZO YA AWALI
Nchi
yetu imo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba ya nchi. Wananchi wa Tanzania
wanakabiliwa na jukumu moja la kuhakikisha katiba ijayo itakuwa kwa maslahi ya
watanzania wote na yenye kuzingatia haki na usawa bila kujali kabila, rangi,
dini wala jinsia. Tukio la kuundwa kwa katiba ya nchi ni miongoni mwa matukio
makubwa kabisa katika nchi yoyote ile duniani. Ni kwa sababu hii, mivutano,
ushindani, kupigana vikumbo, mizengwe na mahala pengine vita vya wenyewe kwa
wenyewe hutokea. Ni kwa kutambua ukweli huu, sisi waislamu wa Tanzania, tayari
tumekwisha ipatia ushauri serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na Tume
ya kurekebisha katiba tahadhari ya kuzingatiwa haki na uadilifu katika mchakato
wote wa mabadiliko ya katiba ili katiba iwe kwa faida ya wote na iwe
msingi wa kudumisha amani iliyopo.
- KATIBA YA NCHI NI
NINI?
Katiba
ya nchi ni makubaliano ya wananchi kuhusu haki na wajibu mbali mbali kati
ya dola na raia na jinsi ya mgawanyo wa madaraka na rasilimali za taifa, mfumo
wa utoaji haki na ulinzi na usalama wa nchi.
Kutokana
na ainisho hili la ujumla, makubaliano haya ya katiba yanaweza kuwekwa katika
maandiko au yasiwekwe. Hata hivyo nchi nyingi duniani zinaongozwa kwa katiba
iliyoandikwa. Mara nyingi tumepata kusikia kwamba ‘katiba ndiyo sheria mama
ya nchi’. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, sheria na kanuni mbali mbali
zinazoongoza nchi chimbuko lake
ni katiba.
Katiba
hujumuisha mambo makubwa ya kisheria ambayo huandikwa kwa mukhtasari. Kwa mfano
kipengele kimoja kinacho zuia ubaguzi, kinaweza kukusanya mambo lukuki
yanayohusu ubaguzi wa rangi, jinsia, dini, ukabila, umri, hadhi katika jamii
nk. Kwa muktadha huo Bunge la nchi ndicho chombo kinachoundwa na katiba
kwa madhumuni ya kutunga sheria, kanuni mbali mbali ili kufafanua jinsi ya
kutekeleza vipengele vya katiba husika. Sheria na kanuni ambazo hutungwa na
Bunge, ikiwa zitapingana na katiba ya nchi, sheria hizo huhesabika kuwa ni
batili (yaani null and void).
- AINA ZA KATIBA
DUNIANI
Katiba
zimegawanyika katika mafungu makubwa mawili.
- Katiba za kisekula
na
- Katiba ya Kiislamu.
Katiba
za kisekula zimebeba taswira kubwa mbili:
(a)
Katiba za kidikteta na
(b)
Katiba za kidemokrasia.
Katiba
za kidikteta
ni zile ambazo wananchi hawana kauli juu ya mambo ya uendeshaji wa nchi yao wala hawaruhusiwi
kuchagua wawakilishi wao bali mamlaka na madaraka yote ya nchi yako mikononi
mwa mtu au tabaka la watu wachache.
Katiba
za kidemokrasia
ni ile ambayo wananchi wanashirikishwa katika kuamua nchi yao iendeshwe namna gani na wanashiriki
katika kuiendesha nchi kwa kuchagua wawakilishi wao.
Katiba
ya Kiislamu
– Hii hutokana na Qur’an na Sunnah za Mtume (SWALALLAH ALAYHI WASALLAM) na
Ijmaa ya wanazuoni. Wananchi hulazimika kutii na kutekeleza mipango na ibada
nyingine kwa kadiri ya uwezo walio nao. Watawala wa Kiislamu huongoza na kutoa
hukumu kwa kila jambo kwa kuzingatia mwongozo wa Allah (Subhaanahu Wataala) na
Sunnah za Mtume (SWALALLAH ALAYHI WASALLAM).
5.
MUUNDO NA VIPENGELE VYA KATIBA YA TANZANIA
Muundo
wa dola ya Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya sasa ni wa ushirikishwaji wa
wananchi katika uendeshaji wa nchi kupitia wawakilishi (wabunge, wajumbe wa
baraza la wawakilishi na madiwani). Katiba ya Tanzania ina sehemu kuu kumi (10)
na ibara (152) kuhusu mambo mbali mbali.
Katika
sehemu zake kumi (10) na ibara (vifungu) 152 katiba ina sehemu zinazoeleza
misingi ya katiba, muundo wa dola, mipaka ya nchi, vyama vya siasa, sera ya
nchi, haki za raia na wajibu wao, majukumu ya Serikali, Bunge, Mahakama
nk. Kwa ujumla kutokana na muundo huu wa katiba ya Tanzania,
katiba iliyopo sasa inahesabika kuwa ni miongoni mwa ‘katiba za kidemokrasia’.
6.
HATUA ZA MCHAKATO WA KUPATA KATIBA MPYA
- Kupitishwa kwa
Sheria ya mabadiliko ya Katiba
Hatua
hii ilifikiwa mnamo mwezi wa Novemba, 2011 pale muswada wa Sheria Na. 8 ya
mabadiliko ya katiba, 2011 ulipopitishwa na Bunge. Kisha yalifuata marekebisho
ambayo yalifanyika Januari, 2012. Sheria hii ya mabadiliko ya katiba, ndiyo
inayotumika kuongoza mchakato huu.
Tume
ya kukusanya na kuratibu maoni ndicho chombo chenye dhima ya kushughulikia
sehemu kubwa ya mchakato wa katiba mpya. Chombo hiki chenye wajumbe 30,
Mwenyekiti na Makamu wake, kimeundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa
kushirikiana na rais wa Zanzibar
April 6, 2012. Hatua hii imetanguliwa na ile ya bunge la Jamhuri ya Muungano
kupitisha sheria ya mabadiliko ya katiba The Constitutional Review Act
iliyopitishwa Novemba 18, 2011.
Tume
ya Katiba itakuwa na sekretarieti yake ambayo ndiyo itakuwa mtekelezaji wa
shughuli mbali mbali za tume kiufundi.
- Ukusanyaji maoni
kutoka kwa Wananchi
Tume
itaendesha mikutano (mabaraza) ya hadhara ya ndani na nje, na hata kupokea
maoni kwa njia ya maandishi kwa nchi nzima. Hii ndio kazi ya msingi ya tume
mara baada ya kuundwa na kuapishwa wajumbe wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Baada ya kazi ya kukusanya maoni Tume itaandaa rasimu ya katiba mpya
itakayotokana na maoni iliyoyakusanya.
Baada
ya kukusanya maoni na kuandaa rasimu ya Katiba mpya iliyotokana na maoni
yaliyotolewa, rasimu ya katiba mpya itachapishwa katika vyombo vya habari ili
kutoa fursa kwa wananchi kuthibitisha maoni yao. Baada ya hatua hiyo rasimu ya katiba
mpya itakabidhiwa kwa Rais wa Muungano na Rais wa Zanzibar.
- Rasimu ya katiba
mpya kujadiliwa na bunge maalum la katiba
Baada
ya Rais kuipitia rasimu ndani ya siku 21 tangu akabidhiwe atatangaza Bunge
Maalum la katiba. Bunge hili litaundwa na wajumbe wafuatao:-
- Wabunge wote
wa muungano
- Wajumbe wa
baraza la wawakilishi Zanzibar
na
- Wajumbe 166
kutoka:-
(a)
vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu
(b)
Asasi za kijamii(NGO’s)
(c)
Jumuiya za Dini
(d)
Makundi ya wakulima
(e)
Wafugaji.
(f)
Taasisi za elimu ya juu
(g)
Wafanyakazi
(h)
Makundi mengine yenye maslahi ya pamoja
(i)
Makundi yenye mahitaji maalum
Mwenyekiti
wa Tume ya katiba atasoma rasimu hiyo kwa mara ya kwanza ndani ya bunge maalum
la katiba na kukabidhi jukumu hilo kwa Mwenyekiti wa bunge la katiba ili
ijadiliwe na bunge hilo na hatimaye kuipitisha au kuirejesha ikafanyiwe
marekebisho. Endapo Bunge maalum la katiba litaipitisha rasimu ya katiba hatua
itakayofuata ni kupigiwa kura ya maoni na watanzania wote.
Baada
ya rasimu ya katiba kupitishwa na bunge la katiba itakuwa katiba
iliyopendekezwa na itakabidhiwa kwa Tume ya Taifa ya uchaguzi yaani NEC na Tume
ya uchaguzi Zanzibar ZEC kwa ajili ya kuandaa na kusimamia kura ya maoni, kwa
kupiga kura ya NDIYO au HAPANA. Ikiwa rasimu hiyo itakubaliwa na wananchi wa
bara kwa 50% na visiwani kwa 50%, katiba mpya itakuwa imeundwa, na kwa
matarajio ya serikali katiba hiyo itaanza kutumika Aprili 26, 2014.
7.
KWA NINI WAISLAMU WANASHIRIKI KATIKA MCHAKATO WA KATIBA
Sababu
kubwa ni Wajibu wa waislamu kupigania haki ili kuwa na katiba nzuri inayolinda
haki zetu. Kuwa na katiba inayolinda haki za waislamu kama sehemu ya watanzania
ni njia bora zaidi ya hakikisho la haki katika mfumo wa uendeshaji wa nchi kama
hii inayojiita ya kisekula.
Kwa
mfano katika Katiba iliyopo imechangia kwa kiasi kikubwa kuwaathiri Waislamu
kiimani, kiuchumi na kijamii. Waislamu tumekosa haki ya kuwa na muwakilishi
bungeni, haki ya kuwa na mfumo wetu wa elimu, haki ya kunufaika kwa misaada ya
shirika la kimataifa la waislamu OIC, haki ya usawa katika miliki ya ardhi,
haki ya usawa katika uteuzi wa ngazi mablimbali za uongozi wa nchi, haki ya
kuheshimiwa sheria za kiislamu n.k.
Kutokana
na udhaifu wa kikatiba serikali kupitia amri ya Rais ilizifuta Mahakama
za Kadhi mwaka 1963 na ilipofika mwaka 1971 bunge lilipitisha sheria ya ndoa.
Sheria hii inazidhalilisha sheria za Kiislamu kwa kuhukumiwa na mahakama zisizo
za kiislamu na pia kusimamiwa au kutafsiriwa na wasioziamini (wasiokuwa
waislamu) na kusababisha kutolewa kwa tafsiri potofu.
Mwaka
1992 serikali iliingia mkataba wa maridhiano na Makanisa (MoU) kugharamia
shughuli za kijamii, kiafya na kielimu za Wakristo bila ya kuwasikiliza
waislamu au kutupa fursa kama hiyo sisi waislamu nk.
Aidha
haki za msingi za raia wakiwemo waislamu hutolewa na kuhakikishiwa (guarantee)
na katiba. Kwa katiba iliyopo sasa haki hizo hazipatikani kwa uwazi, uhakika na
kwa haki; na endapo mtu au serikali ikivunja haki hizo ni vigumu mno kuchukua
hatua kwa mfano tokea mauaji ya Mwembechai,1998 hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa
dhidi ya wauaji.
Kwa
mantiki hiyo utaona wajibu wa kupigania mabadiliko ni MUHIMU SANA. Hofu yetu
katika mchakato huu ni je, Tume ya katiba itafanya uadilifu kwa wananchi wote
bila kujali dini? Hofu hiyo si kigezo cha kuturudisha nyuma na kuwaacha
wasiokuwa waislamu kuyasemea yanayowahusu waislamu. Hivyo basi waislamu lazima
tushiriki kuhakikisha uadilifu, haki vinazingatiwa, waislamu wanasikilizwa na
maoni yao yanazingatiwa.
Mtume
Muhammad (SWALALLAH ALAYHI WASALLAM) aliandika waraka wa makubaliano ya namna
ya kuishi kati ya waislamu na jamii mchanganyiko alipofika Madina. Makubaliano
haya kwa sasa yanaitwa katiba. Utaratibu huu ulimuwezesha Mtume (SWALALLAH
ALAYHI WASALLAM) kujenga nguvu ya kusimamisha dola ya kiislamu ndani ya kipindi
cha mpito.
- Mtazamo wa
Wanawazuoni wa Fiq-hi na mazingira yaliyopo
Waislamu
kwa nyakati tofauti ima watakuwa wanaishi katika dola ya Kiislamu (Daarul
Islaami) ama dola kama ya Tanzania ambayo si ya kiislamu. Katika dola ya
Kiislamu, sheria zote za nchi chimbuko lake ni Allah (Subhaanahu Wataala), na
katika dola isiyokuwa ya kiislamu ni kinyume chake. Waislamu tunaishi katika
nchi hizi (Daarul harb) na katiba zake zinatuathiri sana kwa njia moja ama
nyingine.
Kwa
sababu hiyo tunalazimika kushiriki katika kuundwa kwake kwa lengo la kuondoa
kabisa na ikibidi kupunguza madhara yake kwetu na kwa jamii na wala si kwa
lengo la kuipa nguvu mifumo dhidi ya mwongozo wa Allah (Subhaanahu Wataala).
Hapana
shaka Fatwa ya jumuhuri ya wanazuoni wa fiq-h na ile ya Kamati ya Kudumu ya
Fataawa na Uchunguzi ya Saudia, Fatwa ya Al Azhar, Sheikh Al Uthayminyn, Ibn
Jibriin, Nassur ad-Diyn Al-Albany n.k zilizopitisha kuwa inajuzu kwa waislamu
kushiriki katika mambo mbalimbali (kama siasa, chaguzi nk) katika nchi za
kitwaaghuti wanazoishi, zimezingatia hekma ya Qur’an na mafundisho ya Mtume
(SWALALLAH ALAYHI WASALLAM).
- Wajibu kwa viongozi
wa Kiislamu
Kila
jamii hutaraji maelekezo kutoka kwa viongozi wao. Kwa hiyo wajibu wa kwanza kwa
kiongozi wa umma wa waislamu ni kujitambua kwamba waislamu wanamtegemea
awaelekeze jinsi ya kushiriki kwa namna itakayoleta tija kwao na kwa taifa kwa
ujumla.
Ili
kutekeleza jukumu hili, kiongozi wa waislamu anapaswa kujifunza mambo muhimu
kuhusu mchakato huu wa katiba, madai ya waislamu, kura ya maoni na namna
ya kutoa maoni kama kundi jamii.
Kiongozi
pia anapaswa kuwa na ung’amuzi wa nini kinachoendelea katika kijiji, mtaa, mji,
kata, tarafa, wilaya na Mkoa wake kuhusu mchakato wa katiba.
Hawa
ni wahasibu, wanasheria, wanasiasa, wachumi, walimu wa shule na vyuo, mabwana
na mabibi afya, kilimo, mifugo, maafisa ardhi, wathamini, madaktari, wahandisi,wanafunzi
(vyuo na sekondari) na huduma nyingine za jamii, wanategemewa sana kufafanua
mambo ambayo wengine wasio na taaluma kama zao hawana namna ya kuyajua kwa
namna yanavyoweza kuwanufaisha au kuwaathiri vibaya hususan yanapoingizwa ndani
ya katiba. Wajibu wao mwingine ni sawa tu na ule wa viongozi wengine wa
kiislamu kuanzia ngazi za msikiti, kijiji, mtaa, mji, kata, tarafa, wilaya na
Mkoa.
Mbali
na masheikh, wataalamu na viongozi wa kiislamu, kila muislamu anatakiwa awe
macho na kufuatilia ratiba ya Tume ya Katiba ili ashiriki kutoa maoni. Aidha
awe amejiandaa barabara kutoa maoni kwa kuelewa madai yetu ya msingi.
Muislamu
mwanamke au mwanamme anao wajibu wa kuhakikisha elimu na ujumbe huu vinawafikia
wengine ili waweze kushiriki kwenye mchakato wa katiba ili madai yetu
yazingatiwe na kuingizwa kwenye katiba mpya.
Aidha
kwa wale waislamu waliobahatika kuteuliwa katika Tume ya Katiba, na wale
watakaochaguliwa katika bunge la katiba na kwa watakaopata fursa ya kutoa
maoni, wanapaswa kuelewa kuwa wanao wajibu mkubwa zaidi ya ule wa
kitaifa. Yakiwezekana hayo tunaamini kwamba mchakato huu utakuwa na manufaa si
tu kwa waislamu wa Tanzania bali wananchi wote ili kuitunza tunu ya amani
ambayo Allah (Subhaanahu Wataala) ametutunukia watanzania.
- Katika mchakato huu
umakini wetu Unahitajika
Katiba
ni chimbuko la mambo yote ya msingi kwa taifa na kimataifa. Kwa hiyo matakwa
(maoni) halali ya wananchi hutolewa, hukusanywa na kuandikwa kwa mukhtasari mno
ili mambo mengi ya msingi yapate nafasi ya kuingizwa ndani ya katiba.
Hivyo
basi maoni yanapaswa kutolewa kwa mambo ya msingi. Kwa mfano, ni kweli tunataka
vijana wetu wavae mavazi ya stara na tunakereheka sana wanapowaiga wahuni wa
magharibi. Lakini hatuwezi kuiambia tume ya katiba kwamba “maoni yetu tunataka
katiba itamke ni marufuku vijana kuvaa hereni au suruali chini ya makalio” na
mfano wa haya. Maoni kama haya hayatozingatiwa kamwe kwa sababu kanuni na
sheria juu ya mavazi zinapaswa kuwekwa na sheria zingine za bunge, Halmashauri
za miji, Wilaya na Manispaa na si katika katiba ya nchi.
- MAMBO YA KUPIGANIWA
NA WAISLAMU KATIKA KATIBA MPYA
Sehemu
A. MASUALA YA MSINGI KWA WAISLAMU.
i.
UWEPO WA MWENYEZI MUNGU
Hapa
tunapendekeza Katiba mpya itambuwe uwepo wa Mwenyezi Mungu
Ibara
ya 19 (1-3) inatoa uhuru wa imani na dini. Kwa kuwa katiba inatambua uwepo wa
dini basi itambue pia uwepo wa Mwenyezi Mungu isipokuwa tu kwamba kila mtu awe
huru kuamini Mungu kwa mujibu wa imani yake. Ikumbukwe kuwa viapo mbali mbali
hutolewa mahakamani, bungeni na serikalini kwa wabunge, majaji, mahakimu,
watendaji wa serikali n.k. Basi ni busara na uungwana Mungu huyo anayemuombwa
kwa kusema “Ee Mungu nisaidie” uwepo wake utambuliwe katika katiba.
ii.
UBAGUZI WA KIDINI KWA SIKU ZA MAPUMZIKO UFUTWE.
Upendeleo
wa kidini uondolewe. Mfano;- Siku za mapumziko Jumamosi na Jumapili ni siku za
ibada kwa Wakristo. Hivyo ni vyema Ijumaa nayo iwe mapumziko walau nusu siku
ili kuruhusu waislamu nao wawe huru kwa ibada hasa sala ya Ijumaa. Pia
upendeleo wa kidini katika pato la taifa uondolewe. Mifano mkataba wa
Serikali na Makanisa maarufu kama MoU unayoitaka serikali kutoa pato la
taifa na kuipa dini hiyo huku dini nyingine zikinyimwa haifai. Katiba mpya ni
vyema ikapiga marufuku suala kama hilo kutendwa na serikali.
iii.
KATIBA ITAMBUE NA KUIREJESHA (REINSTATE) MAHAKAMA YA KADHI.
Katiba
mpya itambue na iweke utaratibu wa uwepo wa Mahakama ya Kadhi ambayo
itaendeshwa na waislamu wenyewe kama moja ya Mahakama za nchi. Mashauri yote
yanayohusu ndoa, talaka, mirathi, waqf, malezi ya watoto, hibba (zawadi),
wosia, biashara, bima kwa mujibu wa dini ya kiislamu yasikilizwe katika
Mahakama ya Kadhi alimradi mhusika/wahusika ni waislamu.
Pawekwe
kipengele kinachozuia rufaa za Mahakama ya Kadhi kwenda kwenye mahakama za
kawaida. Mahakama ya Kadhi iwe chombo chenye nguvu za dola na ipewe haki
na uwezesahaji wa kifedha kutoka serikalini ili kutekeleza majukumu yake katika
uendeshaji wa kesi.
Ni
dhahiri kuwa baadhi ya sheria za kiislamu ni sheria
halali za nchi hii. Mfano sheria za ndoa na mirathi, sheria hizi hazipati
tafsiri sahihi kutokana na mamlaka zilizopewa jukumu la kuzisimamia kuendeshwa
kinyume na misingi ya dini ya kiislamu kwa asiyekuwa muislamu kuruhusiwa
kutafsiri sheria za kiislamu.
hili
pia linatokana na ujuzi finyu wa utambuzi matumizi ya hukmu za sheria hizi
ambalo ni tatizo katika kusimamia haki zitokanazo na sheria za kiislamu. Kwetu
sisi Waislamu kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria za kiislamu ni tendo la kiibada
na kijamii, na vile vile kuhukumiwa nje ya misingi hiyo ni matendo
yanayoingilia uhuru wetu wa kuabudu.
Hivyo
basi tunataka katiba mpya itambue na iweke utaratibu wa uwepo wa mahakama ya kadhi
mahakama ambayo itaendeshwa kwa mujibu wa sheria za kiislamu katika mambo
yahusuyo waislamu bila ya kuingiliwa na chombo chochote. Hakika hili ni eneo
muhimu na nyeti sana kwa uislamu tunataka tume ya katiba isipuuze kwa namna
yoyote hitajio hili kwa lengo la kulinda amani na kuheshimu imani na uhuru wa
kuabudu kwa waislamu.
Ni
pendekezo letu pia kuwa rufaa za mahakama ya kadhi zishughulikiwe bila ya
kuhusisha mahakama za kawaida.
Tunataka
mtu ambaye amefunga ndoa ya kiislamu au anaishi kama Muislamu na jamii
inamtambua kuwa ni Muislamu iwe ni kigezo cha shauri lake la mirathi na ndoa
kupelekwa katika Mahakama ya Kadhi na siyo ridhaa ya warithi au maoni ya mtu
mwingine.
- iv. ADHABU
YA KIFO KWA MUUAJI IENDELEE KUTAMBULIKA KIKATIBA
Yapo
madai yanayotolewa kutaka adhabu ya kifo ifutwe kwa kuwa eti ni kinyume na haki
za binadamu. Kuondolewa kwa adhabu ya kifo kutaleta hali ngumu kwa jamii na
hasa wanyonge kwa sababu:-
- Mauaji ya raia
wasio na hatia yataongezeka sana.
- Nchi zilizoondoa
adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, bado haikupunguza idadi ya wahalifu
wa makosa ya mauaji. Mfano, Afrika ya kusini waliiondoa na sasa wanajadili
kuirudisha.
- Hoja ya wapinga
adhabu ya kifo kuwa pamoja na adhabu hiyo kuwepo bado mauaji yanaendelea
haina msingi kwani hata wizi na makosa mengine bado yapo japo wezi
wanafungwa na magereza kupanuliwa kila siku. Je, ni busara kuondoa adhabu
dhidi ya wezi kwa kuwa wezi bado wapo? Ni busara kuondoa adhabu dhidi ya
makosa ya barabarani kwa kuwa ajali zinaongezeka?
- Kosa la kuua
linaumiza na linakwenda mbali sana zaidi ya kwa yule aliyeuliwa ndugu yake
hivyo basi muuaji akiendelea kuishi kwa kulishwa na serikali kwa kodi za
waliouliwa ndugu yao kutachochea mauaji na visasi zaidi, tunaamini salama
yake nay a jamii ni muuaji naye kuhukumiwa kuuwawa kuzuia raia
kujichukulia hatua mikononi mwao.
- Hoja ya kwamba
adhabu ya kifo haimpi muuaji nafasi ya kujirekebisha haina mantiki kwani
adhabu si sehemu pekee ya kujirekebisha bali ni hukumu kwa matendo ya mtu
na katazo (detterance) kwa wengine.
- Pia hoja ya kwamba
adhabu ya kifo inamdhalilisha mtuhumiwa nayo haina mantiki kwani hakuna
adhabu ambayo inampa sifa mtuhumiwa; bali adhabu zote mfano kifungo, faini
au viboko zinadhalilisha na ndio maana zikaitwa adhabu na sio pongezi.
- v.
KATIBA ITAMBUE HAKI YA WAISLAMU KUWA NA MFUMO WAO WA ELIMU
Nchi
mbali mbali duniani zinaruhusu watu wa dini mbali mbali kuwa na mfumo wao wa
elimu ili kutoa nafasi ya kufundisha watoto wao imani, mila na desturi zao
alimradi wanaingiza na mitaala ya kiserikali. Afrika ya Kusini, Uingereza,
India na hata Marekani hufanya hivyo.
Waislamu
tumeruhusiwa kuanzisha mashule yetu lakini yanadhibitiwa mitaala, vitabu,
kanuni na sheria mbali mbali na Wizara ya Elimu kiasi kwamba sisi ni waathirika
wakubwa wa kufutiwa mitihani, kuhujumiwa hujuma mbali mbali pamoja na watoto
wetu kuzuiwa kutekeleza dini yao katika shule na vyuo vya serikali. Mfano,
sakata la wanafunzi wa Kiislamu ndanda Mkoani Mtwara kufukuzwa shule kwa
kutekeleza uislamu wao.
Katiba
itamke wazi kuwa wananchi wana uhuru wa kuwa na mfumo wao wa elimu kwa mujibu
wa dini yao. Tayari kuna shule na vyuo (Akademia) vinavyoendeshwa kwa mitaala
ya Uingereza na hata Marekani hapa nchini kwa nini isiruhusiwe waislamu
kuendesha shule na vyuo kwa mitaala yao kama ilivyo kwa Vyuo vyao Vikuu?
Kuendelea kulazimisha mfumo wa elimu wa pamoja ni kukiuka misingi ya haki za
binadamu na uhuru wa mawazo (freedom of opinion).
Sehemu
B. HAKI ZA MSINGI ZA BINADAMU
HAKI
YA UHURU KAMILI WA IBADA NA UWAKILISHI KIDINI.
a)
Katiba itoe haki na uhuru kamili wa kuabudu
Katiba
ya sasa inatoa uhuru wa kuamini na uchaguzi katika mambo ya dini (Ibara 19:
1-3) lakini haitoi uhuru wa kuabudu. Hii inafanya baadhi ya waumini kulalamika
kwamba hawapati uhuru kamili wa kuabudu. Baadhi ya masuala yanayolalamikiwa ni
pamoja na ya akina mama wa kiislamu jeshini, polisi, na baadhi ya ofisi
kutoruhusiwa kuvaa hijab, wanazuiliwa kuswali katika mashule, vyuoni na maeneo
ya serikali nk.
Katika
uhuru wa ibada, sheria za kiislamu ziheshimiwe mfano mirathi, ndoa, talaka,
waqf, biashara, bima n.k. zitambuliwe kikatiba kama sehemu ya ibada yetu. Hii
itafanya Mahakama ya Kadhi iwe na maana kwani sheria zitakazotumika katika
mahakama hizo zitakuwa zinatambuliwa na hivyo haitakuwa rahisi kuziondoa kama
ilivyopata kutokea huko nyuma.
Hili
linajitokeza pale ibada hizi muhimu zinakandamizwa kwa vigezo vya haki za
binadamu vya kimagharibi bila kuzingatia kwamba haki ya kuwa katika dini ni ya
hiyari na kwamba mtu anaingia na kubaki katika dini akijua iko hivyo.
b)
UWAKILISHI WA KIDINI BUNGENI
Katiba
itamke uwepo wa viti maalum vya uwakilisha wa makundi ya dini hasa Waislamu na
wakristo Bungeni. Bunge ndio mhimili wa dola unaowakilisha maoni na matakwa ya
wananchi. Hali ilivyo hivi sasa yanapojitokeza mambo yanayowahusu waislamu na
wanadini wengine bungeni maoni yao hayapati nafasi wala kuzingatiwa.
C
) TUNATAKA UWAKILISHI WA KIDINI KATIKA BARAZA LA MADIWANI
Katiba
itamke kama tulivyopendekeza katika uwakilishi wa Waislamu na wakristo bungeni
kwamba katika serikali za mitaa pia kuwe na uwakilishi kama huo.
d)
SHERIA YA UGAIDI IFUTWE
Katiba
mpya ipige marufuku sheria ya ugaidi ya mwaka 2002 na utungwaji wa sheria kama
hizo zinazopelekea kuvunjwa kwa haki za msingi za binadamu na ambazo
utekelezaji wake unaleta manyanyaso na madhara makubwa kwa Waislamu kama ilivyo
sasa Tanzania.
e)
Haki za Binadamu ziendane na Maadili ya Dini na ya Kitanzania
Tunataka
katiba mpya isiruhusu mambo ya kishetani kama vile ulawiti, ndoa za jinsia
moja, utoaji wa mimba, uhuru wa kupindukia wa mtoto dhidi ya wazazi wake na
mfano wa hayo kuwa ni miongoni mwa haki za binadamu. Zipo kampeni
zinazoshinikizwa na makundi yanayojiita watetezi wa haki za binadamu na hata
baadhi ya nchi za nje kama vile Uingereza kutaka kushinikiza kuingizwa mambo
hayo katika katiba mpya.
f)
Katiba Mpya itoe ainisho sahihi la ndoa na familia
Kutokana
na shinikizo la ushoga dhidi ya nchi yetu ni muhimu katiba itamke wazi maana ya
ndoa. Katiba itamke hivi ‘ndoa ni baina ya mwanaume na wanawake au mwanaume na
mwanamke.
Ndoa
kati ya watu wa jisnia moja zisiruhusiwe na iwe ni kosa la jinai iwapo watu wa
jinsia moja watabainika kuoana au kuishi kama mke na mume ili kulinda maadili
yetu.
g)
Nafasi mbali mbali za uteuzi serikalini na mashirika ya umma zizingatie uwiano
wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu.
Katiba
mpya iweke utaratibu kuwa nafasi zote za uteuzi serikalini na katika idara
zake, uwakala wa asasi za serikali nk zizingatie uwiano ulio sawa baina ya dini
za waislamu na wakristo, ili kuondoa manung’uniko kuwa kuna ubaguzi katika
uteuzi wa nafasi za uongozi serikalini.
Hii
itasaidia kuweka misingi ya usawa katika utumishi wa umma na kuondoa hisia za
udini. Salama ya nchi hii kwa kiasi kikubwa inategemea kuaminiana na
kuheshimiana baina ya dini hizi kuu mbili, hivyo basi uwiano katika uteuzi
ukilindwa kikatiba itakuwa ni kujenga msingi imara wa amani, haki na
kuaminiana.
h)
Urekebishwaji wa vifungu vya haki za binadamu ndani ya katiba
Pia
tunapendekeza kuwepo taratibu makhsusi za urekebishaji wa vifungu vya haki za
binaadamu katika Katiba. Utaratibu wa sasa wa vifungu hivyo kurekebishwa kama
vifungu vingine vya Katiba ni hatari kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa haki
za binaadamu katika maisha yetu.
Vifungu
kama vile vinavyohusiana na haki ya kuishi, kuchagua na kuchaguliwa, kuabudu,
kufanya kazi, kutokubaguliwa, uraia na kumiliki mali visibadilishwe mpaka iwepo
ridhaa ya wananchi kwa njia ya kura (referendum).
Haki
nyingine za Katiba zisibadilishwe mpaka zaidi ya asilimia 75 ya wabunge kutoka
pande zote za Muungano waridhie na pia iwepo haki ya wananchi wasioridhika na mabadiliko
hayo kuyapinga katika Mahakama Kuu ya Katiba ndani ya siku tisini toka
marekebisho hayo yalipofanyika.
Muswada
wowote wa kurekebisha kifungu chochote kinachohusu haki za Binaadamu lazima
usambazwe kwa wananchi kutoa maoni yao ndani ya siku 90 kabla haujasomwa
Bungeni na kisha upigiwe kura ya maoni.
Ili
kulindwa kwa haki za kibinadamu na kuwepo kwa uwazi tunapendekeza sheria zote
kandamizi maarufu kama sheria 40 zilizoorodheshwa na tume ya jaji Nyarali
zifutwe.
Adhabu
ya kifo kwa makosa makubwa kama mauwaji ya makusudi iwepo katika katiba mpya na
iwe ni moja kati ya mambo ambayo hayawezi kubadilishwa bila referandamu (kura
ya maoni).
i)
Mahakama Kuu ya Katiba na haki za binadamu
Tunataka
katiba mpya iruhusu uwepo wa Mahakama Kuu ya Katiba ambayo itapewa uwezo na
nguvu za kisheria wa kutafsiri vipengele mbali mbali vya katiba na pia
kubatilisha sheria yoyote itakayotungwa ambayo inapingana na katiba.
Mahakama
hii pia izuie marekebisho ya Katiba yanayokinzana na misingi ya Katiba yenyewe.
Na ili hili liwe na mantiki, Katiba itamke wazi kwamba baadhi ya vifungu vya
Katiba kama vile vinavyohusu Muundo wa Dola, Muungano, haki za binadamu
makhsusi zinazorekebishika kwa ridhaa ya wananchi ndio utakuwa msingi mkuu wa
katiba na kwamba haiwezi kubadilishwa bila kuwa na ridhaa ya wananchi kupitia
kura ya maoni (referendum).
Pawepo
na Mahakama Kuu ya Katiba ambayo itakuwa na hadhi ya muungano na pia pawe na
Mahakama ya Rufaa ya Katiba ambayo pia itakuwa ya muungano. Mahakama Kuu ya
Tanganyika na Mahakama kuu ya Zanzibar kama ilivyo Mahakama ya Rufaa ya
Tanganyika zisiwe sehemu ya Muungano.
j)
Mahakama za hakimu mkazi
Mahakama
za Hakimu Mkazi zifutwe na badala yake ziwepo Mahakama za Wilaya ambazo
zitaendeshwa na Mahakimu wa Daraja la Pili ambao watakuwa na uzoefu wa kuwa
mahakimu wa mahakama za mwanzo kwa kipindi kisichopungua miaka mitano.
Mfumo
wa sasa hivi wa kuwa na mahakama za wilaya na mahakama za hakimu mkazi ambazo
zinakaribu mamlaka sawa hauna tija. Na pia mfumo wa kuwapa uhakimu mkazi wahitimu
wa chuo wasiokuwa na uzoefu wowote unakwaza utoaji haki. Ni bora mahakimukama
hao wakaanzia mahakama za mwanzo.
k)
Haki ya kumiliki Ardhi
Haki
ya kumiliki Ardhi iwe ni haki ya raia. Mgeni anaweza kuruhusiwa kumiliki ardhi
kwa kushirikiana na mzawa tu na kwa masharti kwamba hamiliki zaidi ya asilimia
45 ya ardhi hiyo ya pamoja na kwamba umiliki wake uwe ni kwa ajili ya uwekezaji
na si makazi.
Pawepo
na ukubwa maalumu wa ardhi mtu mmoja atakubaliwa kumiliki. Zaidi ya hapo raia
awe na haki ya kukodisha ardhi anayoimiliki kwa muda usiozidi miaka kumi na
tano. Hii inakusudia kuondoa uwezekano wa mtu mmoja au kikundi cha watu
kumiliki na kuhodhi eneo kubwa la ardhi na kuacha jamii kubwa ya watanzania
wakikosa haki ya kumiliki ardhi. Ikumbukwe kuwa ardhi haiongezeki bali watu
wanaongezeka.
Mamlaka
ya Raisi ya kutwaa ardhi kwa maslahi ya umma iweke wazi mambo yanayohesabika ni
maslahi ya umma na itoe muda maalum kwa mtu asiyeridhika kukata rufaa dhidi ya
uamuzi wa kutwaliwa ardhi yake katika Mahakama ya Ardhi .
Katiba
ielekeze Sheria za mipango miji zitenge maeneo ya dini (ibada) kwa kuainisha
maeneo ya waislamu, wakristo na dini zingine kama vile majumba ya ibada,
makaburi n.k. na sio kutaja kiujumlajumla “eneo la kidini” kama ilivyo sasa.
Kitendo
cha kutaja kiujumlajumla “Eneo la Kidini” bila kuainisha dini gani kinafanya
makundi ya dini moja kuhodhi maeneo makubwa kuliko makundi mengine na hivyo
kusababisha manung’uniko.
Sehemu
C. MUUNDO WA SERIKALI NA MUUNGANO
i.
Tunapendekeza nchi yetu iwe na serikali tatu, yaani serikali ya Muungano,
serikali ya Tanganyika na serikali ya Zanzibar
Pendekezo
hili linalenga kuturejesha katika dhamira ya uasisi wa Muungano kama
unavyojidhihirisha katika hati ya Muungano ya 1964 ambao ulibainisha wazi
kuwepo kwa muungano wa nchi mbili na serikali tatu. Hili pia linalenga kuondoa
malalamiko ya mara kwa mara ya kila upande kuona unaburuzwa au kuonewa ndani ya
mfumo wa serikali mbili tulionao hivi sasa. Vile vile litatibu kilio cha
Wazanzibari kujiamulia mambo yao na kile cha watanganyika kufutiwa serikali
yao.
Mfumo
wa sasa wa himaya tatu katika serikali mbili una matatizo mengi kiutendaji na
kisiasa hasa katika himaya ya Tanganyika ndani ya serikali ya Jamhuri. Kwa
mfano, nafasi kama ya Waziri Mkuu, Mwanashera Mkuu wa Serikali zinazua utata
kama ni nafasi za muungano au Tanganyika. Maana, hadhi ya Waziri Mkuu
haitambuliki Zanzibar na kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar nako kuna
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pia
wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano chini ya mfumo huu
wanapata nafasi ya kujadili na kutoa maamuzi juu ya masuala ya Wizara za
Tanzania Bara kama vile Wizara ya Elimu wakati wabunge wa Tanzania Bara hawana
nafasi hiyo katika Wizara za Zanzibar.
ii.
Tunapendekeza Urais wa serikali ya muungano uwe ni wa kupokezana kwa Tanganyika
na Zanzibar
Ili
kuondoa manung’uniko kama tulivyoeleza hapo juu sisi waislamu tunaona kwamba
umefika wakati sasa nafasi ya uongozi wa Rais wa Serikali ya Muungano iwe ni ya
kupokezana. Tunataka utaratibu huo sasa uwe rasmi kikatiba.
iii.
Mambo yaliongezwa katika orodha ya mambo ya Muungano yaliyopo katika hati ya
Muungano yajadiliwe upya
Masuala
yatakayokubalika kuwa ya Muungano yasirekebishwe isipokuwa kwa ridhaa ya
wananchi wa sehemu zote za Muungano kwa njia ya kura ya maoni (referéndum). Ili
kulinda maslahi ya Zanzibar kutokana na idadi yao, kura zitazingatia
uwiano wa sehemu mbili za Muungano na sio idadi ya watu.
Katika
masuala yanayoweza kukubalika kama masuala ya Muungano, Katiba ya Jamhuri ya Muungano
na Katiba za Tanganyika na Zanzibar zitamke bayana kwamba iwapo kutakuwa na
ukinzani wowote kati ya Katiba ya Jamhuri na Katiba za Zanzibar na Tanganyika
kuhusiana na masuala ya Muungano, katiba za nchi hizi zitakuwa batili kwa
kiwango cha ukinzani kwenye vifungu husika. Hili litalinda uwezekanao wa kuwepo
migogoro inayotokana na moja kati ya nchi hizi kurekebisha katiba kwa namna
inayoweza kuvuruga sura ya Muungano. Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya hivi
karibuni yanaweza kutoa picha ya uwezekano huu.
iv.
MAHAKAMA NA MUUNGANO
Kwa
maoni yetu, isipokuwa tu kwa masuala yanayohusu tafsiri ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano, Mahakama ibaki kuwa suala lisilo la Muungano. Ili kuweka mfumo mzuri
wa utatuzi wa migogoro ya Katiba, iwepo Mahakama Kuu ya Katiba ambayo
itakuwa na hadhi ya Muungano bila kujali kama ipo Zanzibar au Tanganyika. Pia
iwepo Mahakama ya Rufaa ya Katiba ambayo itasikiliza Rufaa kutokana na
maamuzi ya Mahakama Kuu ya Katiba. Mahakama Kuu ya Rufaa ya Katiba pia iwe na
uwezo wa kusikiliza Rufaa toka Mahakama Kuu za Tanganyika na Zanzibar kwa
maamuzi yanayohusiana na tafsiri ya Katiba za Zanzibar na Tanganyika.
v.
MALIASILI NA MUUNGANO
Kwa
maoni yetu masuala ya madini na mafuta hayana sababu yoyote ya kuwa masuala ya
Muungano. Ni bora yakabaki katika serikali husika ili kuondoa malalamiko kwamba
sehemu moja ya muungano inataka kujinufaisha na maliasili zilizopo katika
sehemu nyingine.
vi)
URAIS WA TANGANYIKA
Tunapendekeza
kwamba Uraisi wa Tanganyika uwe wa kupokezana kuzingatia makundi makubwa ya
kijamii waislamu na wakristo. Kwa muda mrefu katika serikali ya Tanzania, hasa
katika kipindi cha mfumo wa chama kimoja, kumekuwa na kanuni, japo
hazikuandikwa, za kupokezana uraisi kati ya waislamu na wakristo. Utaona kwamba
Raisi wa kwanza alikuwa mkristo, akarithiwa na Raisi wa Pili Mwinyi ambaye ni
muislamu. Mwinyi akarithiwa na Mkapa ambaye ni mkristo naye akarithiwa na
Kikwete ambaye ni muislamu.
Kwa
mazingira yetu ambayo uwiano wa idadi kubwa ya watanzania ni aidha waislamu ama
wakristo na ukizingatia mvutano wa chini chini unaojitokeza kati ya wanadini
hizi kuu mbili nchini kuhusiana na uwakilishi katika dola, ni busara kama mfumo
huu aliotuachia mwalimu ukaendelezwa na ikibidi kulindwa kikatiba. Mfumo
huu pia unaweza kuwa msingi wa kulinda umoja wetu na uvumilivu.
vii.
BARAZA LA MAWAZIRI NA UBUNGE
Tunapendekeza
Baraza la Mawaziri lisitokane na wabunge kama ilivyo sasa. Hii inatokana
na ukweli kuwa mara kwa mara kumetokea mgongano wa kimaslahi kwa mawaziri
kupeleka miradi mingi ya maendeleo katika majimbo yao ili kujijengea uhalali wa
kuchaguliwa tena. Vile vile pendekezo hili linalenga kutenganisha utendaji wa
mihimili miwili ya serikali na bunge. Haileti maana nzuri wabunge kuwa sehemu
ya serikali (executive) kwani ile dhana ya mgawanyo wa madaraka ambayo ni
muhimu katika kuhakikisha utendaji na ufanisi haionekani kuleta tija
inayotegemewa katika mfumo huu tulionao wa mawaziri kuwa sehemu ya bunge.
viii.
SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO
Ili
kutoa nafasi sawa katika pande zote za Muungano, ni bora nafasi ya Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iwe ya kupokezana kati ya
Tanganyika na Zanzíbar.
Aidha
iwapo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano atatoka upande mmoja wa Muungano
basi naibu wake atoke upande wa pili. Katibu wa bunge pia iwapo atatoka upande
mmoja wa Muungano naibu wake atoke upande wa pili wa Muungano.
ix.SPIKA
WA BUNGE LA TANGANYIKA
Katika
serikali ya Tanganyika kwa yale mambo ambayo si ya muungano tunapendekeza bunge
la Tanganyika liwe na spika wake kwa kuzingatia uwiano kama tulivyopendekeza
kwa nafasi ya urais wa Tanganyika au uwepo utaratibu mwingine maalum unaofanana
na huo.
Nafasi
ya katibu wa bunge pia iwe kama katibu ni wa dini moja basi naibu wake awe
kutoka dini nyingine.
x.
WIZARA ZA SERIKALI
Ili
kuleta ufanisi na kumpunguzia Raisi majukumu na madaraka, ni bora muundo na
idadi ya Wizara zikatamkwa moja kwa moja ndani ya Katiba badala ya utaratibu wa
sasa wa wizara na idadi yake kutegemea matashi ya Raisi.
xi.
MAKAMU WA RAISI
Tungependekeza
kama serikali ya Tanganyika itakuwepo, nafasi ya Makamu wa Raisi wa Tanganyika
isiwepo na badala yake pawepo na Raisi na Waziri Mkuu tu. Utaratibu wa sasa wa
kuwa na mgombea mwenza ambaye anakuwa Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano
uondolewe na badala yake kama Raisi anatoka Zanzibar Raisi wa Tanganyika awe
kwa nafasi yake ni Makamu wa Raisi wa Jamhuri na kinyume chake.
Ingawa
kuna uwezekano wa Raisi wa Muungano kutoka chama tofauti na chama cha Raisi wa
upande wa muungano utakaostahili kutoa Makamu wa Raisi, mfumo huu ni mzuri na
wa lazima maana utakuwa umelinda maslahi na uwakilishi wa watu wengi katika
upande wa Muungano unaohusika. Hii pia itawezekana maana serikali ya Muungano
itakuwa inahusika na masuala machache ya muungano wakati masuala mengi
yakishughulikiwa na serikali zinazounda muungano.
xii.
MANAIBU WAZIRI
Tungependekeza
pia nafasi ya Naibu Waziri kwa upande wa serikali ya Tanganyika isiwepo maana
inaongeza gharama bila sababu.Katibu Mkuu wa wizara anatosha.
Kwa
upande wa serikali ya Muungano, nafasi hiyo iwepo ili kuleta uwakilishi sawa
kutoka pande mbili za muungano. Na pale Waziri akitoka upande mmoja wa
muungano, naibu wake atoke upande wa pili wa muungano.
xiii.
SERA RASMI YA NCHI
Tunapendekeza
será ya nchi yetu iwe ni será ya kujenga ustawi wa jamii yaani “welfare
state policy” badala ya será ya ujamaa ambayo kivitendo haipo tena.
Pendekezo hili linazingatia ukweli kuwa sasa nchi yetu ni ya kibepari. Hivyo
basi sisi waislamu tunaona kuwa ni heri sera ya nchi yetu iwe ni kuimarisha
ustawi wa kijamii yaani ili kuifanya serikali iweze kuwajibika zaidi kwa
wananchi kuwawekea ustawi wa maisha yao.
xiv.
BAADHI YA MASHARTI YA KUSAJILI VYAMA VYA SIASA YAONDOLEWE
Kwa
kuwa kila mtu ana uhuru wa kujiunga au kutojiunga na chama chochote cha siasa.
Masharti yafuatayo ya uanzishwaji wa vyama vya siasa yaondolewe:-
- Sharti la kwamba
chama cha siasa lazima kiwe na wanachama kwa Zanzibar na Bara liondolewe
kwani linanyima uhuru na uchaguzi wa kujiunga na wengine kwa ridhaa ya
mtu.
- Sharti la kuwa na
wanachama mikoa 10 bara na 2 zanzibar liondolewe kwani halina mantiki.
Chama kisicho na wanachama kiachwe kife chenyewe kwa kukosa wanachama.
- Vyama vya kidini
viruhusiwe ili wananchi waamue wenyewe katika sanduku la kura. Hili
linawezekana na kuna mifano hai kama vile Ujerumani, Australia,Uingereza,
Canada,DRC Kongo,Denmark,Ufaransa,Italia, Rwanda, Ubelgiji, Afrika ya
Kusini n.k na wala hakuna matatizo yoyote.
xv.
MAMLAKA YA RAISI YAPUNGUZWE
Japo
mamlaka ya kutosha kwa Raisi ni muhimu kwa maslahi ya umma ili kumuwezesha
kutekeleza majukumu yake makubwa kama Mkuu wa Nchi na Dola, ni bora, kwa lengo
la utawala bora na kulinda zaidi maslahi ya umma, madaraka ya Raisi
yakapunguzwa katika maeneo yafuatayo:-
.
Raisi
asiwe na mamlaka ya kuweka watu vizuizini bila ya kufikishwa mahakamani na
Kuhukumiwa
kwa kuthibitishwa shutuma dhidi yake.
.
Mamlaka
ya Raisi ya kusamehe wafungwa yawe ni kwa mujibu wa vigezo maalumu
vinavyotamkwa
na sheria ya Bunge na iwe katika utaratibu ulio wazi.
.
Mamlaka
ya Raisi ya kuunda idara mbalimbali za serikali pamoja na kuteua
wakurugenzi
yatumike kutokana na mapendekezo yatakayotolewa na Kamisheni ya Ajira
na
Idara za Serikali itakayoundwa kutokana na uwiano wa kimakundi ya kijamii.
xvi.
VYOMBO VYA UTEKELEZAJI WA SHERIA, UPELELEZI NA UENDESHAJI WA MASHITAKA
a)
Mkurugenzi wa mashtaka
Mamlaka
ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) yanahitaji kupunguzwa ili kuleta ufanisi na
uwazi zaidi katika mfumo wa utekelezaji wa sheria. Kwa maoni yetu, pale kesi ya
jinai itakapoanzishwa na taasisi nyingine au mtu binafsi, DPP asiwe na uwezo wa
kuidhinisha kesi hiyo kwenda au kutokwenda mahakamani, kuondoa mashitaka
mahakamani wala kuingilia isipokuwa tu kama atatoa sababu za kisheria
zitakazomridhisha hakimu au Jaji anayesikiliza kesi kwamba kuna mwenendo
unaoweza kupelekea haki kutokutendeka.
Katiba
na sheria tulizonazo kwa sasa zimetoa mamlaka makubwa sana kwa Mkurugenzi wa
Mashitaka, kwani kwa mamlaka aliyonayo anao uwezo wa kuingilia au kuifuta kesi
yoyote iliyo mahakamani bila ya kulazimika kutoa sababu yoyote na hakuna
atakayemzuia kufanya hivyo. Hii imeleta maswali na malalamiko mengi kuwa wapo
watu wanaofaidika na mamlaka hayo makubwa ya DPP kutoweza kufikishwa Mahakamani
kwa matendo yao.
b)
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa PCCB
Tunapendekeza
ofisi ya Kikosi cha Kuzuia na Kuondoa Rushwa Tanzania (PCCB) itamkwe ndani ya
Katiba na iwe na mamlaka kamili na huru katika kusimamia sheria ya kuzuia
rushwa bila kuingiliwa na ofisi ya DPP. Utaratibu wa sasa wa baadhi ya makosa
kuhitaji ridhaa ya DPP kabla ya kupelekwa Mahakani yanaleta matatizo
kiutekelezaji na yanapunguza uhuru wa PCCB.
Ni
bora pia, ili kuondoa muingiliano, sheria ya PCCB ijihusishe na makosa makhsusi
ambayo hayatamkwi katika Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code). Na lau baadhi
ya makosa katika Penal Code yanastahili kuwemo katika sheria ya PCCB, sheria ya
Penal Code irekebishwe kuyahamishia makosa hayo katika sheria ya PCCB.
c)
Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa serikali (CAG)
Ili
kuzuia ubadhilifu wa mali za umma ni bora ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
hesabu za Serikali iwe na uwezo wa kutoa ushauri kwa mamlaka zinazohusika na
mashitaka ya kushitakiwa au kumfungulia mashitaka yeyote atakayeonekana kuwa na
makosa kwenye taarifa ya hesabu za serikali. Na endapo vyombo husika vitakataa
ushauri bila kuwa na sababu ya msingi kwa mtizamo wa Mkaguzi Mkuu, Sheria impe
nguvu kulipeleka suala Mahakama Kuu ili iamue kama kuna haja ya kesi hiyo
kufunguliwa.
d)
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Tunapendekeza
utaratibu wa sasa wa Raisi kuunda Tume ya Uchaguzi ubadilishwe badala
yakeiundwe na Chombo cha Kikatiba kitakachokuwa katika muundo unaozingatia
uwiano wa maslahi ya kisiasa na kijamii. Hili litaondoa malalamiko kwamba
Raisi anaunda Tume ya Uchaguzi kwa kuzingatia maslahi ya chama chake.
e)
Muundo wa Tume ya Uchaguzi uwe wa kitaifa kuanzia chini hadi juu
Muundo
wa tume kipande unawafanya viongozi wa Serikali wa Kuteuliwa na Raisi kuwa watendaji
wa misimu wa Tume na hivyo kuzua malalamiko mengi kwamba haifanyi kazi kwa
uhuru.
f)
Matokeo ya Kura za Urais
Katiba
iruhusu matokeo ya Uchaguzi wa Raisi kupingwa katika Mahakama Kuu ya Katiba.
Ili kulinda usalama wa nchi kesi hiyo itapaswa kufunguliwa ndani ya siku kumi
na tano toka matokeo yalipotangazwa na kusikilizwa ndani ya siku thelathini.
Mara
baada ya kesi hiyo kufunguliwa, Katiba itamke kwamba Raisi aliyemaliza muda
wake atakaimu nafasi ya Raisi ili kutoa nafasi kesi kusikilizwa kwa uhuru. Pia
Katiba itamke wazi kwamba, kabla kesi hiyo haijafunguliwa, Mahakama Kuu ya
Katiba itafanya upembuzi wa ushahidi uliopo kuona kama kuna sababu zozote za
msingi za kufunguliwa kwa kesi. Utaratibu wa sasa wa matokeo ya Raisi
yanayotangazwa na tume kuwa uamuzi wa mwisho hata kama kuna malalamiko ya
msingi yanazua wasiwasi kuwa haki haitendeki.
g)
Mgombea Binafsi.
Mgombea
binafsi aruhusiwe katika nafasi zote isipokuwa nafasi ya Raisi. Mfumo wa sasa
unaolazimisha mgombea kuwa na chama cha siasa unawanyima wananchi wasio na
vyama vya siasa kushiriki katika uongozi wa nchi kwa kutumia haki yao ya
kuchagua na kuchaguliwa.
Kwa
upande wa Raisi, mantiki ya kutaka wagombea wawe na vyama vya siasa ni kutoa
nafasi ya kutosha kwa wananchi kutathimini sera vyama vyenye mgombea Urais
ambazo ndizo zitakazotekelezwa na serikali itakayoundwa na Rais atakayeshinda.
Na pia kutoa nafasi kwa Tume ya Uchaguzi kutathimini sifa ya mgombea.
Yawezekana mtu akajitokeza kuwa mgombea Uraisi na akawa na Sera inayopingana na
Katiba na maadili ya nchi. Kuwa na chama cha siasa kutaifanya Tume kuchukulia
kwamba sera za mgombea ni kama zilivyo katika Katiba na Sera ya chama chake.
h)
Mfumo wa serikali za Majimbo urejeshwe
Katiba
isiwe na nafasi za Mkuu wa Mkoa, Wilaya na badala yake kuwe na uongozi wa
majimbo na viongozi wa majimbo hayo watoke katika majimbo hayo na wapigiwe kura
na wananchi wa majimbo husika.
i)
Uhusiano na Jumuiya za Kimataifa Usiwe wa Kibaguzi
Katiba
itamke kuwa Tanzania inaweza kujiunga au kuwa na uhusiano wa kibalozi,
uanachama au vinginevyo na jumuiya yoyote ya kimataifa pasina kujali kama
jumuiya hiyo ni ya kisiasa, kiuchumi, kijamii au za kidini alimradi kufanya
hivyo itathibitika kuwa na maslahi kwa watanzania au sehemu ya watanzania.
Ni
kwa msingi huu waislamu wa Tanzania tunataka Tanzania ijiunge na OIC kama
ambavyo ina uhusiano wa kibalozi na Papa ambaye ni kiongozi wa Dola ya Kidini
ya Vatican ya Kanisa Katoliki.Kama hili la kujiunga na OIC haliwezekani, basi
iwe pia Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania usiwepo kwa sababu ni ubaguzi wa
kidini.
j)
Mali za viongozi zihakikiwe kabla na baada ya kutoa madarakani.
Katiba
iweke utaratibu maalum kwa mali za viongozi kuhakikiwa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa serikali (CAG) wakati wa kuingia madarakani na wakati wa kutoka badala
ya Tume ya Maadili ya Viongozi.
Hii
ni kutokana na ukweli kwamba wajumbe wa Tume ya Maadili wengi wao wanaweza
wasiwe na ujuzi wa kutathmini na kuhakiki mali hivyo atumike CAG. Na iwe ni
kosa la kisheria kukaidi utaratibu huo.
k)
Rasilimali za maeneo husika ziwanufaishe wenyeji wa maeneo husika
Katiba
itamke kiwango ambacho wananchi wa maeneo yenye rasilimali kama vile gesi,
madini n.k wanatakiwa wapatiwe kutoka kwa muwekezaji ili kuzuia kuhamisha mali
kutoka eneo hilo kwenda kwingine au hata nje ya nchi bila wenyeji kunufaika.
l)
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uwe wa Mkataba
Katiba
itamke kuwepo kwa Muungano wa mkataba na mambo yote ya Muungano yaliyoongezwa
kutoka kwenye mkataba wa awali wa mwaka 1964 yapitiwe upya na pande zote
husika.
HITIMISHO
Ndugu
muislamu hii ni sehemu tu ya yale ya msingi kwa waislamu; yako mengine ambayo
yanaweza kuongezwa wakati wa utoaji wa maoni, tafadhali muislamu uwe huru
kuyatoa mbele ya tume alimuradi hayapingani na maoni yetu ya msingi, vinginevyo
pata ushauri zaidi toka kwa jukwaa la katiba la waislamu JUWAKATA:-
Simu
ya M/Kiti wa Jukwaa – 0785 955 859/0715955859
Simu
ya Makamu M/Kiti wa Jukwaa -0784863539
Simu
ya M/Kiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania- 0689378747
Simu
ya Makamu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu – 0715631183
Sisi
waislamu hatupaswi kutofautiana katika mambo ya msingi kwa ajili ya dini yetu.
Tupo wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa, lakini tukiingia msikitini imamu
wetu ni mmoja, hii ni fundisho kuwa sisi ni ummah mmoja. Tetea itikadi yako ya
kisiasa alimuradi haipingani na dini yako. Itikadi ya kisiasa haipaswi kwenda
kinyume na uislamu wako. Tafadhali jitambue na uutambue uislamu wako na uwe
tayari kuutetea popote.
Baada
ya maelekezo haya, tunamuomba kila muislamu sasa kujifunga kibwebwe na kusimama
kutekeleza jukumu lake kwa uwezo wake wote. Nia zetu ni njema katika kushiriki
mchakato wa mabadiliko ya katiba Tanzania na Allah (Subhaanahu Wataala)ni
shahidi wa nia zetu. Tunashiriki ili kuona kwamba katiba inazingatia matakwa
yetu na ya wengine yasiyo na madhara kwetu na haitoi nafasi ya mtu yoyote
kunyanyaswa.
Ni
wazi tutakapo simama na kudai haya tuliyoyasema tutasikia mengi kutoka kwa wale
wote wasioutakia mema Uislamu na waislamu. Wajibu wako wewe Muislamu kuitetea
dini yako kwani kuna ujira mkubwa kesho mbele ya Allah (SW). Hautokuwa na
udhuru wowote utakaposhindwa kusimama kuutetea uislamu ili hali umepewa nafasi
ya kuutetea uislamu wako kupitia mabadiliko ya katiba.
Tumedhulimiwa
kiasi cha kutosha ni wajibu wetu sasa TUSEME TUMECHOSHWA KUDHULUMIWA,
TUNATAKA HAKI ZETU NDANI YA KATIBA MPYA.
TAFADHALI
TIMIZA WAJIBU WAKO
Imeandaliwa
na:
Jukwaa la Waislamu la Kuratibu Mabadiliko ya Katiba Tanzania (Juwakata)
Dar
es Salaam,
Tanzania.