Thursday, June 28, 2012

Kupotoshwa Idadi ya Waislamu ni Changamoto kwa Waislamu!



  • Ni ipi ajenda ya walioficha na kupotosha  idadi yaWaislamu?
  • Waislamu himizaneni kushiriki kwa wingi katika sensa ijayo 
  Na Ahmed Hussein
Hila dhidi ya idadi ya Waislamu katika koloni la Tanganyika zilianza siku nyingi. Hili ndilo koloni lililobeba idadi kubwa ya Waislamu katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Idadi hii ilionekana kuwakera wakoloni na washirika wao wa kimeshari. Itakumbukwa kuwa Wakoloni walibuni mkakati wa kushamirisha miradi ya ufugaji wa nguruwe ili kuwafukuza Waislamu katika maeneo yao.
Hujuma za kitakwimu dhidi ya idadi ya Waislamu Tanzania ni za miaka kama si miongo mingi. Idadi ya Waislamu nchini ilianza kugubikwa na wingu jeusi hata kabla ya uhuru. Kwa makusudi, mamlaka za hesabu za watu ziliondosha utambulisho wa kidini katika sensa bila sababu za wazi.

Kumbe ukweli uliokuwa umefichwa ni kwamba idadi ya Waislamu ilikuwa kubwa kuliko ya makundi mengine. Ukubwa wa idadi ya Waislamu ulitofautiana mno na uwakilishi wao katika maeneo ya elimu hasa kuanzia ngazi ya sekondari, na katika nyadhifa za utumishi wa umma na madaraka serikalini.
Swali ambalo lilikuwa likiogopwa kitakwimu ni kwamba laiti sensa ingefichua idadi kubwa ya Waislamu nchini, hoja ya msingi ingekuwa hii; kwa nini kielimu na kimadaraka Waislamu walikuwa wachache?
Wabunifu wa Mfumo uliojengwa kwa misingi ya dhuluma dhidi ya kundi la Waislamu katika jamii ya Watanzania waling’amua kuwa mikakati yao ya kuwapunja Waislamu taaluma na madaraka ingefichuka kirahisi kama sensa ingeonesha idadi kubwa ya Waislamu nchini.

Hivyo, kwa maslahi ya mkakati huo wa dhuluma, ilibidi wafiche Idadi ya makundi ya dini ili umma usije kuhoji mbona katika daftari la sensa Waislamu ndio wengi lakini katika nafasi za elimu, utumishi na madaraka ni wachache?
Wakati vigezo vya sensa vya Umoja wa Mataifa vinajumuisha utambulisho wa dini, Tanzania licha ya kuwa mwanachama wa Umoja huo, ikakiuka utaratibu huo wa kuweka wazi hesabu za watu wa makundi ya dini. Kwa bahati mbaya, mwamko kwa Waislamu ulikuwa bado mdogo au hafifu juu ya ajenda ya kuondosha utambulisho wa dini katika sensa za Kitaifa, hivyo, jambo hilo halikupigiwa sana kelele.

Laiti ingetosha kuwa, Idadi za Watu wa makundi ya dini hazifahamiki kwa sababu hazijumlishwi kupata wastani katika daftari la sensa, huenda kila mmoja angeamini kuwa uamuzi huo ulikuwa wa kizalendo.
Lakini ajabu ambayo imeonekana Kitaifa na Kimataifa ni kwamba, taasisi kadha wa kadha zimekuwa zikitoa au kutumia takwimu zinazoonesha kuwa kundi la Wakristo ndilo linalounda jamii kubwa ya Watanzania likifuatiwa na lile la Waislamu!
Hiyo ni kusudi ya wabunifu au tuseme waasisi wa mfumo kandamizi uliohujumu nafasi ya Waislamu kielimu na kiutumishi katika nyadhifa za juu na madaraka. Kwa nini walifanya kusudi hiyo? Kwa sababu walitaka jamii na dunia iamini kuwa uchache wa Waislamu katika maeneo hayo ni matokeo ya uchache wa idadi ya jumla!

Hiyo pia ingetoa picha ya jumla kuwa uchache wa Waislamu unaooneshwa na takwimu bandia ndio sababu ya uchache wao kielimu na kimadaraka. Au pia uchache wao kielimu na kimadaraka ni ushahidi wa idadi yao ndogo katika jamii ya Watanzania.
Hivyo, kama yalivyo makundi mengine madogo ya jamii, uwakilishi mdogo wa Waislamu katika maeneo muhimu ya nchi unaakisi “udogo” wa jamii yao

Waliofanya kusudi hiyo ya kupotosha takwimu walikuwa na uhakika wa kuteka asilimia 100 ya saikolojia ya walimwengu juu ya uwiano pogo wa kielimu na kimadaraka baina ya watu wa makundi ya dini iwapo sensa ingeficha utambulisho wa dini ili isijulikane Waislamu wako wangapi Tanzania.
Kwa upande mwingine, upotoshaji wa takwimu kuwa Wakristo ndio wengi nchini ulilenga, pamoja na mambo mengine, kuhalalisha dhulumu ya kimfumo dhidi ya Waislamu katika maeneo ya elimu na ajira za utumishi wa umma hasahasa katika ngazi za juu. Kwamba, wingi wa Wakristo katika maeneo hayo ni matokeo ya ukubwa wa idadi yao kulinganisha na makundi mengine ya jamii.

Ni hoja nyepesi kung’amulika kwamba kama wasingetoa takwimu za kuonesha kuwa Wakristo ndio wengi nchini, wabunifu na waasisi wa mfumo kandamizi wa kidini kwa misingi ya kisiasa wangeyajibu vipi maswali haya; ‘mbona Waislamu ni wachache katika maeneo hayo? Je wingi wa Wakristo mashuleni, vyuoni na madarakani umetokana na nini?
Mwanzo, ilidaiwa kuwa mfumo wa Kikoloni uliwabana Waislamu kielimu kwa sharti la kuritadi ili wapewe elimu, sawa kabisa, mtu angekubali kuwa katika miaka ya awali ya uhuru nafasi za madaraka zingejazwa na Wakristo waliopendelewa kielimu na mkoloni.
Lakini hoja ambayo ingewashinda Wabunifu wa mfumo wa dhuluma ni kwamba mbona hata baada ya uhuru Waislamu wameendelea kuwa wachache katika nyanja za elimu? Kama nyuma kulikuwa na sharti la kubatizwa, je baada ya uhuru sharti hilo lilikuwepo? Lakini bado hilo nalo lingesutwa na idadi ya watoto wa Kiislamu katika shule za msingi.
Waislamu waliandikisha watoto wao kwa wingi katika ngazi ya msingi nchini kote. Sasa, swali lingekomaa zaidi, kwa nini Waislamu waendelee kuwa wachache hata baada ya miaka mingi ya uhuru? Ni wazi mfumo wa dhuluma ungebainika kirahisi.

Ndio maana waasisi wake wakawa makini na sensa ya Taifa ili wajenge hoja ya jumla kuwa Waislamu ni wachache katika nyanja za elimu na madaraka kwa sababu jamii yao ni ndogo kama zilivyo jamii za watu wa makundi mengine madogo.
Na Wakristo ni wengi kwa sababu wao ndio wanaounda asilimia kubwa ya Watanzania. Angalau kwa kuficha takwimu za Waislamu walijiridhisha kuwa dhuluma waliyowafanyia Waislamu ingehalalika kwa mdadisi au mtafiti yeyote yule ambaye angetaka kuhoji kwa nini Waislamu ni wachache madarakani?

Mfano ambao ungetia nguvu dai hilo ni ule wa nchi nyingine jirani kwamba huko Wakristo ndio wengi madarakani kwa sababu jamii ya Waislamu ni ndogo kwa idadi. Jitihada za kuficha takwimu za Waislamu katika sensa ya Taifa, zilikuwa na ajenda ya kutoa picha ya Kimataifa kuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki Kanisa ndilo lenye wafuasi wengi katika nchi zote.
Hivyo, isishangaze kuona Waislamu wachache wakiwa madarakani Tanzania kwani hali ndiyo hiyo hiyo katika nchi jirani za eneo hilo. Kwa kweli, dunia imehadaika sana kwa hila hii. Sehemu kubwa ya watu duniani wakiwemo baadhi ya Watanzania wanaamini kuwa ukiondoa Zanzibar, Waislamu, Tanzania bara, ni wachache kulinganisha na Wakristo.

Tangu hapo, Tanzania ni Taifa la Kikatoliki kwa kauli ya Mwalimu Nyerere. Ili kujenga picha ya kuhalalisha Ukatoliki lazima, kimsingi, upotoshe takwimu za Waislamu ili idadi ya Wakristo ionekane kubwa na hivyo inafaa kuwa Jimbo la Vatikani.
Ingekuwa rahisi kutumia takwimu sahihi za Wakristo na Waislamu wa Kenya kuhalalisha himaya ya Kanisa kwa sababu ni kweli idadi ya Wakristo kule ni kubwa. Lakini isingeliwezekana kujenga himaya ya Ukatoliki kwa kutumia takwimu sahihi za sensa ya Taifa ya Tanzania kwani ingeonesha idadi kubwa ya Waislamu.

Kwa sababu hiyo, mkakati ukawa ni kuficha na kupotosha takwimu. Kuficha kuna maana ya kuondosha utambulisho wa dini katika sensa, na kupotosha kuna maana ya kusambaza takwimu bandia za idadi ya watu wa makundi ya dini. Hebu tazama jedwali hili
                    
s/no

Nchi

Idadi ya Waislamu


Idadi kwa asilimia

Makadirio hadi 2030

Makadirio kwa asilimia

43
*TANZANIA*
“13, 450, 000”?
 ‘29.9’
“19, 463, 000”?
 25.8













Katika jedwali ambalo niliwahi kuchapisha katika makala iliyohusu upotosha wa takwimu za idadi ya Waislamu Tanzania, Tanzania iliorodheshwa katika nafasi ya 43 kama kinavyoonesha kipande cha jedwali hilo hapo juu. Jedwali hilo linaonesha kuwa eti idadi ya sasa ya Waislamu ni milioni 13, 450, 000 sawa na asilimia 29.9 ya Watu wote Tanzania!

Kana kwamba upotoshaji huo haukutosha, jedwali hilo likaonesha makadirio yaliyofanywa na taasisi za Kimataifa kwa kushirikiana na mtandao usiofahamika kuwa eti hadi utakapofika mwaka 2030 yaani miaka 28 ijayo kuanzia sasa, idadi ya Waislamu Tanzania itakuwa ni milioni 19, 463,000 sawa na asilimia 25.8 ya idadi ya watu wote Tanzania.
Niliandika na kuchapisha jedwali hilo kwa minajili ya kuwaandaa Waislamu kisaikolojia na kimkakati kwamba waitumie sensa ijayo
kusahihisha upotoshaji huo. 

Na jambo la kung’ang’ania ni kwamba sensa hiyo ya Mwezi Agosti mwaka huu lazima ijumuishe utambulisho wa kidini.
Hiyo ikiwa na maana kuwa lazima daftari liwe na kipengele cha dini ya mtu anayehesabiwa. Kwa bahati nzuri, Umoja wa Mataifa ndio umeweka kigezo hicho, na Tanzania ni mwanachama wake, hivyo isidhaniwe kuwa kudai kigezo hicho ni ‘udini’.
Ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya Waislamu walioitolea maoni makala yangu ile walipuuza umuhimu wa sensa kwa madai kuwa ‘Uislamu haujali idadi ya watu’ bali unajali waumini. Hii si dalili nzuri kwani ‘uumini ni daraja’ na Uislamu ni utambulisho.
Maadam mtu katoa shahada ya kumkubali Mwenyezi Mungu na Mtume, hebu tumuhesabu kuwa ‘amesilimu’ kama inavyosema Qur’an. Tusimpime kwa daraja la uumini ambalo chujio lake kali pengine linaweza kubakisha watu wawili au watatu kwa ile mizani hasa ya uchaMungu.

Huenda mimi na msomaji tusiwemo katika daraja hilo japo tunaswali na kufunga. Naomba tuamini kuwa “sensa ya Waumini” ni tofauti kabisa na “sensa ya Waislamu”. Kwa hiyo, tusisitize sensa ya Waislamu katika daftari la sensa ambayo itawajumuisha Waislamu wote bila kujali daraja zao za imani.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget