Friday, June 8, 2012

Mkono nyuma ya vurugu zanzibar


uamsho
Vurugu zilizotokea karibuni na kuchukuwa siku kadhaa ndani ya Zanzibar  zilizopelekea kuchomwa baadhi ya makanisa, kufungwa barabara, kuchomwa kwa baadhi ya maduka ya ulevi (baa) na kusitisha kwa kiasi fulani shughuli za kiuchumi na kijamii kiasi cha kulifanya Jeshi la Polisi kutawanya watu kwa mabomu ya machozi na kufanya doria sehemu kubwa ya mji zilipangwa na kuratibiwa kwa malengo maalum na kuna mkono mrefu nyuma yake.
Kabla ya kuelezea malengo na mkono nyuma ya vurugu hili, amma mkono wa ndani au mkono wa nje. Kwanza, tuangalie baadhi ya viashiria vinavyodhihirisha kwamba vurugu hizi ni mchezo wa kuigiza:
Kwanza, Jumuiya ya Uamsho ni rafiki mkubwa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na Raisi wa Zanzibar, kiasi cha Jumuiya hiyo kuandaa dua maalumu kuiombea dua serikali hiyo na Raisi wake.
Pili, licha ya Uamsho kufanya mihadhara yake viwanjani, lakini pia imekuwa ikitumia misikiti kwa harakati zake mbali mbali katika vugu vugu hili. Kama vile dua na itikafu. Mmoja katika msikiti mkubwa unaotumika kwa harakati zake ni Msikiti Munawwara Kidongo chekundu. Msikiti ambao uko katika mikono ya serikali.
Tatu, mihadhara ya Jumuiya ya Uamsho inayotoa kauli kali dhidi ya muungano na  kuhamasisha watu wawe tayari hata kufa kutetea nchi yao imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu kwa baraka zote za Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Na Serikali iliwapatia kibali cha miezi sita kufanya mahubiri hayo. Kwa jina la kutoa elimu ya uraia.
 Nne, idara ya serikali ya Waqfu ambayo ndio yenye dhamana ya kuratibu masuala ya dini ya Kiislamu yakiwemo mahubiri ya Kiislamu hususan viwanjani ililamika kuhusu mihadhara hiyo na kutaka kuisitisha lakini inaonekana ilishindikana.
Tano, Waziri dhamana katika Ofisi ya Makamo wa Pili wa Raisi Zanzibar, bwana Mohammed Aboud awali alitoa taarifa ya kujikosha serikali na kutangaza kusitisha mihadhara hiyo. Hali iliyopelekea baadhi ya wakuu wa mikoa hususan Pemba kutangaza kuzuia mihadhara hiyo katika maeneo yao, lakini mihadhara iliendelea kama kawaida, kana kwamba inaonekana waliagizwa na serikali kuu waachie mihadhara hiyo iendelee.
Sita, Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar pamoja na wakereketwa muhafidhina wa CCM walionekana kukerwa na mihadhara hiyo pamoja na matamko makali dhidi ya muungano yanayotolewa katika mihadhara hiyo, na walianzisha kampeni maalumu kwa kushirikiana na wakereketwa wenye nguvu kama Borafya Silima na Mbaraka Shamte kwa lengo la kujibu na kukabiliana na wimbi la mihadhara hiyo, huku wakijigamba kwamba watakwenda  sambamba na Jumuiya ya Uamsho, kwa kuwafuata kila mahali inapofanyika mihadhara yao kuvunja na kubomoa athari yao. Cha kushangaza! si muda mrefu Jumuiya hiyo ya CCM na wakereketwa wake pia waliacha kampeni yao, kana kwamba walitakiwa wasitishe.
Saba, siku ya Jumamosi Mei 26 yalipofanywa maandamano na Uamsho yalifanywa bila ya kibali na yalipewa ulinzi kamili na jeshi la Polisi bila ya kudhuriwa wala kukamatwa viongozi wala waandamanaji na hawakupata pingamizi yoyote.
Nane, kitendo na mazingira ya kumkamata kwa kumnyakuwa Ustadh Mussa Juma ambae hakuwa mstari wa mbele sana kama wengine katika mihadhara wala katika maandamano kilifanywa akiwa msikitini ili kiguse hisia za Waumini. Ikikusudiwa  kuchochea fujo na kupatikana uhalali wa vurugu, na ili  ipatikane fursa ya kuongeza vitendo vya vurugu zaidi, kama kuchoma makanisa ili kukuza ukubwa wa vurugu na kuonekana kuna mgogoro na tatizo kubwa ndani ya Zanzibar. Kazi ya kuchoma makanisa yumkin kwa kiasi kikubwa walipewa wakereketwa wa kundi la vijana muhafidhina wa CCM wa maskani. Wakioneshwa kwamba lengo la mkakati huo ni kuimaliza Uamsho. Vijana hawa wa CCM kama walivyo Uamsho ni wenye jazba wasiokuwa na upeo wa mambo wala uchambuzi wa kisiasa, kwa hivyo wakalibeba jukumu hilo bila ya kurudi nyuma. Ilhali lengo kuu la mkakati huo wa kuchoma makanisa ni kukuza ukubwa wa vurugu na kuonekana kuweko kiwango kikubwa cha mgogoro.
Tisa, namna Polisi walivyokabiliana na tukio lenyewe pia ni usanii wa wazi. Kwanza, Kamishna wa Polisi Zanzibar alitamka wazi kwamba viongozi waliochochea vurugu watakamatwa kwa gharama yoyote. Cha kushangaza! Hakukuwa na kiongozi yoyote wa mstari wa mbele aliyekamatwa au kufanywa msako mkali kama tulivyozoea. Pia namna Polisi walivyokuwa kwenye vurugu hili, hakuna kiudhati aliyejeruhiwa au kuuwawa kama tulivyozoea namna Polisi wa hapa wanapokabiliana kwa ukali wa kuruka mipaka na vurugu hususan zenye kufungamana na siasa.
Hivi ni baadhi ya viashiria kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inaelewa fika kila kinachotendeka na kukibariki kuanzia vugu vugu la mihadhara ya Uamsho hadi kuripuka vurugu.
Nani nyuma ya vurugu hili, na nini malengo yake?
Hapa kuna misukumo miwili mikubwa. Msukumo wa ndani na msukumo wa nje. Kwa upande wa ndani, vurugu hizi ni shinikizo la baadhi ya wanasiasa wakubwa wa CCM Zanzibar wakiungwa mkono na baadhi ya wanasiasa wa CUF Zanzibar wanaofungamana kwa uzalendo wao wa ‘uzanzibari’. Japo kwamba CUF nyuma ya pazia inaonekana kupinga vuguvugu hili, kwa kuwa ajenda ya vuguvugu la Uamsho ni kuvunja kabisaa.. Muungano, ilhali sera ya CUF ni kuwepo serikali tatu. Lakini kimsingi CUF imeshakufa na imebaki kuwa tawi la CCM. Na zaidi hakuna matumaini kisiasa kwa CUF kupata serikali ya Muungano kuweza kutekeleza sera yake hiyo. Kwa hivyo, sera yake juu ya Muungano na sera nyenginezo zinabakia kuwa nadharia tu. Hivyo si ajabu CUF Zanzibar kwa hisia zao za kizalendo wakadandia mkondo wa vugu vugu hili. Lakini kutokana na nafasi za wanasiasa hao katika serikali na katika vyama vyao na kulinda maslahi yao binafsi wanakosa ujasiri wa kuonekana wazi wazi. Aidha, wale waliomo ndani ya CCM nao hawana ushujaa katika vikao vyao halali vya chama kutoa duku duku lao kiudhati kuhusu Muungano, zaidi ya kusema ‘ndio nakubaliana’ na kuahidi ‘kulinda Muungano’. Kwa hivyo, kundi hili wamehisi watumie fursa ya kuyadandia majukwaa ya dini ya Kiislamu. Kwa kuwa wakaazi wa Zanzibar kiasili wana hisia ya dini yao ya kiislamu, ili kuweza kuvutia watu na wafuasi wengi zaidi katika vugu vugu hili bila ya kuzingatia chama chochote. Pia kauli mbiu inayotumika na Uamsho ya kutaka kura ya maoni juu ya mustakbali wa Muungano imetumika ili ionekane kuwa kinyume kabisa na vyama vyote vya kisiasa vilivyopo. Lengo ni kuonesha na kupeleka ujumbe kwa CCM taifa na serikali yake ya Muungano kwamba hali si shwari tena kutoka kwa raia wenyewe wa Zanzibar.  Ili kwa haraka matatizo mbali mbali yanaotokamana na Muungano yakiwemo suala la uchimbaji na umiliki wa mafuta yatatuliwe kabla hali haijawa ya kutisha zaidi!. Kimsingi Raisi wa sasa wa Zanzibar si mtu shupavu kama alivyokuwa Dk. Salmin Amour kuweza kuwa na misimamao mikali ya kizalendo. Lakini yumkin waliomzunguuka wameweza kufanikiwa kumchochea kuhusu maslahi ya Zanzibar hususan katika suala la uchimbaji wa mafuta ambao ni mtaji mwanana kisiasa. Ikumbukwe kwamba suala la uchimbaji wa mafuta ya Zanzibar limekuwa na mjadala mkali miongoni mwa wanasiasa na wananchi jumla, kiasi cha kuweza kuwaunganisha wanasiasa wa Zanzibar na raia jumla kuunga mkono vugu vugu la Uamsho, kwa lengo la kuzidisha shinikizo kwa Serikali ya Muungano kulitazama upya. Inawezekana pia kwa kiasi kikubwa katika vugu vugu hili kumuhusisha raisi mstaafu aliemaliza muhula wake. Katika zama zake, aliyekuwa Waziri wake wa Nishati (Mansour) alikuwa akitamka waziwazi kwa maneno makali kuhusu uchimbaji wa mafuta na gesi ya Zanzibar kwamba utabakia kuwa milki ya Zanzibar. Kitu ambacho ni kinyume na mawafikiano ya Muungano. Waziri Mansour alidiriki kutoa kauli hizo kali ilhali Raisi Amani si kwa nafasi yake ya uraisi, wala Unaibu Mwenyekiti wa CCM hakuthubutu kumchukulia hatua za kumzuia wala kumuadhibu. Pamoja na hayo Raisi huyu mstaafu ana shauku kubwa ya kumtakasa baba yake kwamba alikuwa na nia safi juu ya suala la Muungano.Kampeni ambayo inapata nguvu vya kutosha kila uchao. Kinyume na alivyokuwa akichukuliwa huko awali kwamba ni msaliti aliyeuza Zanzibar kwa Tanganyika. Pamoja na sababu hiyo pia wimbi hili ni ujanja wa kujificha kufeli kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kinyume na matarajio ya raia.
Msukumo wa nje.
Kwa upande mwengine wa msukumo wa nje. Vuguvugu hili linatokamana na Marekani. Ukizingatia kwa makini kauli ya balozi wa Marekani ndani ya Tanzania Alfonso E. Lenhardt, baada ya vurugu hili alitamka: “Tunatambua umuhimu wa kuwepo mjadala wenye nguvu ndani ya umma, na tunahamasisha wadau wote kuuendeleza kwa utaratibu wa amani na kidemokrasia”.
http://www.afriquejet.com/tanzania-us-envoy-calls-for-calm-after-riots-rock-zanzibar-island
 Akikusudia wahusika na wadau wa qadhia hii waketi na walimalize jambo hili kidemokrasia na kwa maridhiano. Katika kauli hii kunadhihirika kiashiria cha mkono wa dola hiyo. Marekani inaelewa fika sera ya Muungano ya CCM kwamba ni serikali mbili kuelekea serikali moja, sasa iweje waketi kujadili qadhia hii na wahusika wengine? Marekani ndio msimamizi kwa kiasi kikubwa wa Afrika Mashariki baada ya kumnyan’ganya bwana wa asili wa ngome hii yaani Uingereza. Licha ya Marekani kufanikiwa kujenga himaya na ushawishi mkubwa Afrika ya Mashariki, bado inakabiliwa na upinzani mkubwa na changamoto kadhaa kutoka bwana huyo wa asili wa eneo hili (Uingereza). Hili hudhihirika katika upinzani mkubwa wa vyama vyao ndani ya nchi hizi. Kwa mfano, Chama cha ODM nchini Kenya chini ya Odinga ni chama cha Marekani, ilhali chama cha PNU cha Kibaki kiko chini ya Uingereza. Marekani ilikabiliwa na hali ngumu sana katika uchaguzi uliopita ndani ya Kenya kutokana na ujanja wa kisiasa wa Uingereza. Hadi ikalazimika kugawana ngawira na keki ya Kenya na mwenzake Uingereza. Hali hiyo mpaka sasa ni tofauti na Tanzania. Licha ya Uingereza kwa kupitia Chadema kuota mizizi, bado chama cha CCM ambacho ni chama cha Marekani kinaendelea kushikilia hatamu ndani ya Serikali ya Muungano. Na Marekani imefanikiwa kufanya mkakati kabambe wa kumakinisha athari yake ndani ya Zanzibar na kumkatisha tamaa kabisa Uingereza kwa kuunganisha chama chake kilichokuwa uwanjani CCM na chama chake cha akiba/reserve (CUF). Hata hivyo, Marekani imejifunza kutoka siasa za Kenya, lau haikuwa makini zaidi ndani ya Tanzania, amma itafika mahala ipoteze kabisa ushawishi wake na maslahi yake au italazimika kugawana ngawira na Uingereza. Hali itakayomugharimu kupungua athari yake au kupoteza kabisa nguvu, maslahi na ushawishi wake katika nchi hii. Kwa hivyo, hali inavyoendelea Tanzania kwa Chama cha Muingereza (Chadema) kinachoungwa mkono pia na Jumuiya ya Ulaya hususan Ujerumani, kinaonekana kila siku kumakinika na kupata watu wengi ndani ya Tanzania hususan Bara, kiasi cha hata baadhi ya vigogo wa chama cha CCM, ambao bila ya shaka wanaounga mkono Uingereza kutishia kutoka CCM na kuingia ndani ya Chadema. Hali hiyo inaifanya Marekani kutokuwa na raha juu ya mwenendo wa siasa za Tanzania ikiwemo Zanzibar. Kwa hivyo, vuguvugu hili la Uamsho Zanzibar ni mchezo wa Marekani kupitia CCM kiujanja, kwa kutumia  baadhi ya vikundi vya Kiislamu ndani ya Zanzibar, amma kwa kujijua au kwa kutojijuwa kutokana na kukosa kwao uweledi mpana wa kisiasa na fikra thabiti ya Kiislamu. Marekani imejifunza kwamba baadhi ya vikundi vya Kiislamu ndani ya Tanzania hufanya kazi nzuri ya kufikia malengo yake ikiwemo kukiokoa chama chake cha CCM kinapokuwa katika shimo la maangamizi kwa kubanwa koo na Chadema. Kama ilivyodhihirika katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga. Wakati huo takriban vikundi vingi vya Kiislamu vililitumia tukio la kuvuliwa mtandio Mkuu wa Wilaya Fatma Kimario na wakereketwa wa Chadema kama ni ushahidi wa chama hicho kuwa ni adui wa Waislamu. Huku vikundi hivyo hivyo vya Kiislamu vilijitia upofu wa tukio kubwa ovu lililofanywa na CCM wakati huo huo, kufanya dua ya pamoja baina ya Waislamu na Wakiristo kuwaombea waathirika wa ajali ya Mv. Spice Zanzibar. Unapoyapima matukio mawili haya yaliyotokea wakati mmoja kwa mujibu wa ‘hukmu za Kiislamu’ licha ya kuwa yote ni maovu, lakini la CCM ni ovu zaidi. Sasa iweje vikundi hivi kwa hili la CCM vibakie kimya cha mfu?  Na kwa upande wa baadhi ya vikundi vilivyopo Zanzibar vilifanya kazi nzuri kwa gharama ndogo wakati wa kupiga kampeni ya Marekani ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.
Katika vugu vugu hili linaloendelea la Uamsho Marekani hailengi tu, kuunda serikali tatu katika Muungano, bali ikiwezekana, lakini kwa njia za busara kuiondoa kabisa Zanzibar katika Muungano. Japo kwamba si jambo jepesi, litakalogharimu Zanzibar gharama za mambo ya ubalozi na mengineyo pia kugharimu Tanganyika kulitangaza upya kimataifa dola lao jipya. Na lau haitowezekana Marekani inadhamiria walau kuweka serikali tatu kwa lengo la kuumega muungano kidogo kidogo mpaka kuuhitimisha kabisa. Kwa sababu, kuitoa Zanzibar katika Muungano ni jambo la usalama na utulivu zaidi kwa maslahi ya Marekani ya uchimbaji wa mafuta ya Zanzibar hata kuliko kuwapo serikali tatu. Na pia salama kwake amma ikiwa Bara kinatawala chama chake cha CCM au kikishinda chama cha Uingereza (Chadema). Utaona, japo kwamba sera ya Uingereza (Chadema) kidhahiri katika suala la Muungano ni serikali tatu, lakini inawezekana huo ni mtego tu wa Uingereza ambao Marekani inaonekana kuung’amua. Yumkin, lau Chadema kinapata ushindi Tanganyika, Uingereza inaweza ikaigeuza ghafla sera hiyo kiasi cha kuirejesha tena Zanzibar katika mikono ya Uingereza kutokana na kuwepo rasilmali ya mafuta. Karibuni Mbunge mwenye nguvu wa Chadema Zitto Kabwe alikaririwa akisema kwamba masuala ya mafuta na gesi hayakupaswa kuwa katika mambo ya Muungano. Kauli hiyo ya kijanja ni dhihirisho ya kukita siasa za Muingereza ndani ya Chadema. Siasa ‘za unachosema kinyume na unachoamini na kukitendea kazi’.
 Marekani na maafisa wa juu wa CCM wanajua kinachoendelea katika vuguvugu la Uamsho na vurugu zilizojiri, wanajaribu kuonesha kwa ufundi sana kwamba hili ni suala linalotokamana na wazanzibari wenyewe bila ya mkono wa nje, kama lilivyoonyeshwa suala la muwafaka baina ya ‘Karume na Seif’ lililopelekea kuzaliwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Dhamira ya kuonesha hivyo ni kuwafanya muhafidhina ndani ya CCM waweze kuikubali hali hiyo kidogo kidogo na kuanza kulainika kidogo kidogo tayari kwa mabadiliko.
Kwa ufupi, Marekani inalenga kwa mkakati wa vuguvugu la Uamsho kama mbinu ya kufikia kujihifadhi na kujilinda dhidi ya Uingereza, pia ipate kuikomba kwa raha, salama na utulivu rasilmali ya mafuta ndani ya Zanzibar. Huku Marekani akijifanya kijanja kuwaridhisha wazanzibari kwamba wanajitawalia mambo yao wenyewe kikamilifu nje ya Muungano, dhana iliyojaa ndani ya vifua vyao.
Matarajio
Baada ya vurugu hili Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa mkali mdomoni, lakini laini kivitendo kwa Uamsho, viongozi wake na vurugu lililotokea. Tayari ZBC (Shirika la Utangazaji Zanzibar) katika Tv wanaonesha picha za matokeo ya vurugu hili, na hitimisho la kipindi hicho humalizia: ‘iliyopita si ndwele tugange ijayo’ Pia mihadhara itabanwa kidogo, na hatimae kuruhusiwa kama kawaida. Baadhi ya kesi zilizofunguliwa dhidi ya walioleta vurugu zitafutwa na kufa kifo cha kawaida, serikali italipa gharama za uharibifu wa makanisa na mali nyenginezo, na Marekani kiufundi kidogo kidogo itahamasisha mabadiliko ili kuandaa mazingira ya kufikia lengo lake. Na viongozi wa juu wa CCM wataonekana kukemea qadhia hii kijanja kwa ukali, kana kwamba hawana habari ya kinachoendelea.
Hitimisho
Kwa hakika, kuchanganyikiwa kwa ndugu zetu katika umma kunatupa moyo wa fedheha na masikitiko makubwa. Lau ingekuwa aibu ya kifamilia tu tungeinyamazia mambo yakesha! Lakini kwa kuwa tunabeba qadhia ya umma, hulazimika tuuonye na kuuonesha njia. Katika mwezi kama huu wa Rajab mwaka 1342 Hijri sawa na mwanzoni mwa mwezi wa Machi mwaka 1924 miladi, ndio wakati waliodiriki makafiri kwa uadui mkubwa kuimaliza dola ya mwisho ya Kiislamu (Khilafah Uthmania). Miongoni mwa silaha ya hatari waliyoitumia makafiri hao kufikia lengo hilo ni fikra hii wanayoishadidia leo Uamsho, fikra ya ubaguzi/ aswabia. Fikra ya watu kujifunga, kujilabu na kujitukuza kwa mujibu wa maeneo yao wanayoishi au walipozaliwa, badala ya kujinasibu kama sehemu ya umma mtukufu wa Kiislamu ulioenea duniani kote. Hatimae, Waarabu wakaona wana mambo yao kama Waarabu, na Waturuki kama Waturuki. Haikumalizia hapo, katika Waturuki wakajitukuza wengine kundi la Wakurdi, na Waarabu nao ardhi zao zikakatwa vijinchi telee…. hadi nyengine ni aibu hata kuziita nchi kamwe! Lau Umma wetu ungejifunga vilivyo na hukmu za Kiislamu na manhaj sahihi ya Kiislamu usingeweza kamwe kuingia ndani ya mtego kama hii ya makafiri.
Tunamuomba Allah Ta’ala katika mwezi huu mtukufu wa Rajab ainue ufahamu wa umma wetu ujifunge kidhati na manhaj ya Mtume wetu (SAAW) katika kuleta mageuzi ya kweli ili tuweze kurejesha tena izza/nguvu yetu kwa kurejesha tena dola yetu ya Kiislamu ya Khilafah Rashidah kama alivyobashiri kipenzi chetu SAAW.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget