Saturday, May 19, 2012

Huu Muungano vipi?


Wazanzibar wengi wameonyesha kutaka serikali tatu, wakati viongozi wa Bara wamekuwa waking’ang’ania mfumo wa sasa wa serikali mbili.

Watu wenye busara wanatambua kwamba kuna Wazanzibar ambao hawautaki muungano huu katika hali yoyote, na pia kuna Watanganyika ambao pia hawautaki muungano huu katika sura yoyote.

Hiyo ndiyo hali halisi, kwani hakuna mtu aliyewahi  kuwahesabu watu wasioutaka muungano huu, wala kuwahesabu wanaoutaka.

Watu pekee wanaofahamika wazi kuutetea muungano huu  ni viongozi walioko madarakani Tanzania  Bara na Visiwani Zanzibar.  Huutetea muungano huo kwa sababu wanazozijua wao!

Ikumbukwe kwamba muungano huu unaohusisha wapatao milioni 42 wa Bara na milioni moja tu wa Visiwani.  Kwa miaka yote muungano huu 48 umeijengea Zanzibar woga wa kumezwa na ndiyo maana katika muda wote huo imepigana hadi kupata wimbo wake wa taifa, bendera yake, katiba yake na kadhalika.
Wazanzibar bado wanapigania uanachama Umoja wa Mataifa (UNO), Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Jumuia ya Kimataifa ya Waislam (IOC), Shirikisho la Soka Afrika (Caf), na kadhalika.

Kwa nini wanafanya hivyo?  Wanataka utambulisho wa Zanzibar na historia yake viendelee duniani.
Si hivyo tu, limejitokeza suala la mafuta kuwemo eneo la baharini Zanzibar ambayo Wazanzibar wanasema ni mali yao pekee.  Pia kuna tatizo  la rais wao kutokuwa na madaraka katika serikali ya muungano na kutokuwa makamu wa jamhuri ya muungano.

Yote hayo na mengine, hayajapewa utatuzi, watawala wakiamini kwamba watu watayasahau.
Mambo hayo hayasahauliki!

Mwaka 1985, bunge la Tanzania chini ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM)  lilipitisha azimio la kuanzishwa kwa muungano wa serikali tatu, lakini  Mwalimu Julius Nyerere alikuja na sababu zake na kulizima azimio hilo!

Kwa heshima na woga waliokuwa nao kwa Nyerere, wabunge wakanyamaza!

Ndivyo Watanzania walivyokuwa.  Kuzungumzia muungano ulivyokuwa, hasa enzi za Nyerere, lilikuwa kosa la jinai.  Hivyo watu waliendelea kukaa kimya si kwa kuupenda sana muungano, bali kwa kuogopa kuukosoa wasije wakawaudhi watawala!

Hivi leo, Wazanzibar, hususani vijana, wanaamini sababu zilizounda muungano mwaka 1964 leo hii hazipo tena, hivyo wanataka Zanzibar iendelee na historia na utamaduni wake bila kuihusisha Tanganyika.

Hali hii ni tofauti na kauli za  watawala wanaotaka kuzima hisia hizo  kwa visingizio kwamba “muungano ni tunu kutoka kwa Mungu” na hivyo usijadiliwe katika mchakato wa kupata katiba mpya.

Muungano huu haukutoka kwa Mungu.  Ulianzishwa hapahapa duniani na Nyerere na Karume, ‘full stop’!

Ifahamike wazi kwamba muungano ni kitu cha hiari, si cha kulazimisha au kulazimishwa.

Hilo liko wazi kwa watu wenye busara.

Mwalimu Nyerere na Karume hawakuwa malaika kwamba walichokipitisha hakijadiliwi.  Vilevile, muungano  si Biblia wala Koran, vitu ambavyo havihojiwi na waumini wake kuhusu uhalali wake.

Wakati wa kuamua hatima ya muungano huu ni sasa.  Mjadala wa katiba mpya ijayo ulijadili hili bila kujali kauli za wanasiasa ambao hujifanya wana busara zote mikononi mwao.

Wazanzibar ambao wamekuwa wakiulalamikia zaidi muungano huu kuliko Watanganyika, wapewe fursa ya kuulizwa iwapo wanautaka au la.

Kama wanautaka waseme uwe wa aina gani, na kama wanaukataa hakuna haja ya kuendelea na muungano usiotakiwa upande mmoja.

Muungano uvunjike na maisha yaendelee kama yalivyokuwa kabla ya Aprili 26, 1964.
Mbona majirani zetu wa Kenya, Malawi, Zambia, Msumbiji, na kadhalika tunaishi nao kwa kuheshimiana na kupendana wakati hatuna muungano nao?

Muungano ni kitu chema, lakini kisilazimishwe kwa ajili ya kumwogopa marehemu  Nyerere na Karume!

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget