Tuesday, April 10, 2012

Aina za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu


1. KUSENGENYA 
Kusengenya ni tabia ambayo inachukiwa na sheria machukio yote, na akili iliyosalimika inaighadhibikia tabia hii ghadhabu zote, na jamii iliyo nadhifu ina ikataa tabia hii, nayo ni maradhi ya kijamii ambayo hatari yake ni kubwa na athari zake ni zenye kuangamiza. 
Na Qur’an tukufu imempigia mfano msengenyaji mfano wa mtu mbaya (au mnyama mbaya) amemvamia ndugu yake binadamu baada ya kuja kwake akaanza kuung’afua ule mzoga wake na kuitafuna nyama yake na anaviponda, viungo vyake. Na huu mfano binadamu anauchukia na anaukimbia mfano huo lakini pamoja na hayo analiingia jambo hili la kusengenyana analikumbatia. 
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:- 
"Je! mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa? La, hampendi; (basi na haya msiyapende)" (HUJURAT - 12). 
Na kutokana na Hadithi za Mtume (s.a.w.) tunapata ufafanuzi wa hii aya ya Qur’an na athari zinazopangika kutokana na kusengenya katika dunia na akhera. 
Imepokewa kutoka kwa Abii Hurairat (r.a.) ya kwamba Mtume (s.a.w.) amesema: "Kila Muislamu juu ya Muislamu ni haramu damu yake na heshima yake na mali yake." 
Imepokewa na Muslim na Tirmidhy. Na msengenyaji anamuudhi ndugu yake Muislamu katika, heshima yake kwa kuwa heshima ya mtu ni sehemu ya sifa yake njema au sehemu ya sifa yake mbaya. 
Na imekuja katika hadithi iliyopokewa na Bukhari na Muslim:- 
"Na wasisengenyane baadhi yenu juu ya baadhi yenu na muwe waja wa Mwenyezi Mungu ndugu." 
Na imepokewa kutoka kwa Aisha (R.A.) amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwaambia maswahaba wake. "Je! mnaifahamu riba kubwa zaidi ya riba?" Wakasema Mwenyezi Mungu na Mtume wake anajua, akasema, "Hakika riba kubwa zaidi ya riba mbele ya Mwenyezi Mungu ni kuhalalisha heshima ya mtu Muislamu", kisha akasema Mtume (a.s.w.). 
"Na wale wanaowaudhi Waislamu wanaume na Waislamu wanawake pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizodhahiri." (Ah-zaab - 58). Imepokewa na Abuu Yaa’la. 
Na imepokewa kutoka kwa Anas (R.A.) kuwa amesema: Amesema Mtume (s.a.w.)! "Pindi nilipopandishwa Miiraja niliwapita watu waliokuwa na makucha ya shaba wakijiparura nyuso zao na vifua vyao, nikasema; ni nani hawa ewe Jibril?" Akasema, hawa ni wale ambao wanakula nyama za watu na wanatubia (wanaangukia) ndani ya heshima zao (za watu) "Yaani wanaowasengenya watu. Imepokewa na Abuu Dawud. 
Na imepokewa kutoka kwa Jabir (R.A.) amesema: Tulikuwa pamoja na Nabii (s.a.w., ikatokea harufu inayonuka, akasema Mtume (s.a.w.) mnafahamu ni harufu gani hii? Hii ni harufu ya wale ambao wanawasengenya waumini. Imepokewa na Ahmad. 
Na hadithi inaelekeza kushabihishwa harufu ya kusengenya na harufu inayonuka ili kuupa taswira kwa sura ambayo inaendana nayo. Na walikuwa maswahaba (R.A.) wakikutana kwa bashasha wala hawasengenyani na wanaliona hilo (la kutosengenyana) ni katika matendo bora zaidi na wanaona kusengenyana ni katika tabia za watu wanafiki. 
Na wakasema baadhi yao; tuliwakuta walio tutangulia na wao walikuwa hawaoni kama ibada ipo katika swaumu na swala tu lakini ibada ni kujizuia kuziingilia heshima za watu pia. 
Na akasema Ibnu Abbas (R.A.), pindi ukitaka kuzisema aibu za nduguyo basi zikumbuke aibu zako kwanza. 
Maana ya Kusengenya: 
Imepokewa kutoka kwa Abii Hurairat (R.A.) ya kwamba Mtume (s.a.w.) amesema: Je! mnafahamu ni nini kusengenya? Wakasema, Mwenyezi Mungu na Mtume wake anajua; akasema; kumtaja ndugu yako kwa yale anayoyachukia", pakasemwa; Je! unaonaje ikiwa yapo kwake hayo niyasemayo? Akasema: ikiwa yapo kwake hayo uyasemayo basi utakuwa umemsengenya, na ikiwa hayapo kwake hayo usemayo basi utakuwa umemsingizia uongo". Imepokewa na Muslim. 
Kutokanana hadithi hii wametufahamisha Maulamaa maana ya kusengenya na wakatuwekea mipaka ili iwe wazi katika kichwa cha kila Muislamu, wakasema katika kupambanua neno kusengenya kuwa ni "kumtaja ndugu yako Muislamu kwa lile litakalomchukiza, pindi akilisikia, sawa sawa ukiwa umemtaja kutokana na upungufu katika mwili wake au nasaba yake au tabia yake au matendo yake au dini yake au dunia yake mpaka katika nguo zake au nyumba yake au kipando chake. 
Ama kumtaja kutokana na upungufu katika mwili wake ni kama kusema; kipofu, makengeza, upara, mweusi sana, mfupi, mrefu n.k. (isipokuwa kwa nia ya kutambulisha). 
Ama katika nasabu:- ni kama kusema huyu yu katika familia duni, masikini, yenye kudharauliwa, dhaifu n.k. 
Ama katika tabia ni kama kusema, ana tabia mbaya, au anajivuna, ana kibri, mwenye kujionyesha, mwoga, mzembe n.k. 
Ama katika dini yake ni kama kusema, mwizi, muongo, mlevi, mdhulumaji, hatoi zaka, hawatii wazazi wake n.k. 
Ama katika dunia yake ni kama kusema, mlafi, hana adabu, analala sana, haheshimu watu, hajali matatizo ya wenzie n.k. 
Ama katika nguo zake; chafu, zinabana, mamikono marefu n.k. 
Ama katika nyumba yake mbaya, mjengo wa kizamani n.k. 
Ama katika kipando chake gari lake bovu, baya, n.k. 
Na mengineyo ambayo yanaweza kumchukiza ndugu yako pindi akiyasikia basi ni katika kusengenya. 
Na kusengenya kama kunavyokuwa kwa maneno yaliyo wazi, kunakuwa vile vile kwa kufahamisha upungufu wa nduguyo Muislamu kwa vitendo mfano kusema, kuashiria, kukonyeza, kuandika na kumuigiza msengenywaji, yote haya yatahesabika ni kusengenya maadamu itafahamika kutokana na hayo upungufu wa msengenywaji. 
Na pia ni katika kusengenya mfano mtu akitajwa mbele yako kisha ukasema, "Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuepusha kutokana na ubakhili’ au "Ninajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kula mali za watu’, pindi atakapofahamu msikilizaji upungufu wa mtu alotajwa mwenye sifa hizo (ubakhili, kula mali za watun..) bali hii inakuwa ni zaidi ya kusengenya kwamba ni aina ya riaa, kwa kuwa mzungumzaji anadhihirisha upungufu wa mtu mwingine kwa kuwazuga kuwa yeye ni mtu mzuri. 
Na mfano wa kusengenya ni kama vile mwandishi kuandika (kutaja) katika kitabu kundi la watu bila kuwataja majina kama kusema: Kundi la watu wanaofanya hivi na hivi ni wanafiki au waongo, pindi likiwa linafahamika kundi hilo. 
Na kauli nzito ni kwamba kusengenya haiwi ila kwa mtu asiyekuwepo, basi haitakuwa ni kusengenya bali ni kumtukana na kumshutumu.


Na. Ramla

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget