Mwenendo mbaya wa polisi na vyombo vya usalama vya Marekani dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo umeendelea kukinzana na madai ya serikali ya Washington kuhusu masuala ya haki za binadamu na uhuru wa kijamii. Wakati alipochukua madaraka ya nchi miaka kadhaa iliyopita Rais Barack Obama wa Marekani aliahidi kufanya mabadiliko katika siasa za nchi hiyo kuhusu namna ya kuamiliana na Waislamu.
Hata hivyo vitendo na mwenendo wa vyombo vya dola dhidi ya Waislamu wa Marekani unaonesha kinyume kabisa na madai ya kiongozi huyo. Kwa kutilia maanani ukweli huo kundi moja la Waislamu wa mji wa Detroit katika jimbo la Michigan ambao wamekuwa wakipekuliwa wakiwa uchi na vyombo vya usalama vya serikali kwa sababu tu ya itikadi zao za Kiislamu wamewasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo ikiwemo Polisi ya Federali FBI.
Mashtaka hayo ya Waislamu wa Detroit dhidi ya serikali ya Marekani ni faili jipya la kesi zinazohusiana na mwenendo mbaya na wa kikatili wa vyombo vya dola dhidi ya Waislamu nchini humo.
Mashtaka hayo yalipelekwa mahakamani na Baraza la Uhusiano wa Uislamu na Marekani (CAIR). Mwaka jana pia baraza hilo liliwasilisha mashtaka kama hayo ya kunyanyaswa Waislamu na kudhalilishwa katika Idara ya Haki za Kiraia ya Wizara ya Usalama wa Ndani, lakini mashtaka hayo yalipuuzwa na kutupiliwa mbali.
Mashtaka hayo yamewasilishwa mahakamani baada ya wanaume wanne wa Kiislamu akiwemo Imam wa msikiti mkuu wa jimbo la Michigan kupekuliwa wakiwa uchi na kuvunjiwa heshima kwa masaa kadhaa na vyombo vya polisi ya Marekani. Mashtaka hayo yanasisitiza kuwa mwenendo huo unawadhalilisha Waislamu na kutambuliwa kimakosa kuwa ni tishio la usalama.
Inaonekana kuwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria dhidi ya Waislamu vilivyoshadidi nchini Marekani baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, sasa vimeshika sura mpya na kasi zaidi.
Katika miaka ya hivi karibuni polisi na vyombo vya ujasusi na upelelezi vya Marekani vimekuwa vikinasa sauti na mazungumzo ya simu, kusoma baruapepe za Waislamu wa Marekani kwa kutumia sheria ya Partiotic. Kisingizio kinachotumiwa na vyombo hivyo ni eti kuzuia uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi ya Waislamu. La kuchekecha ni kuwa serikali ya Barack Obama imeunga mkono vitendo hivyo vinavyokiuka mipaka ya mtu binasfsi.
Vitendo haramu kama hivyo ikiwa ni pamoja na kasi ya wimbi la propaganda chafu za vyombo vya habari vya Marekani dhidi ya Uislamu na kampeni ya kuwatisha watu kuhusu Waislamu, vimezusha anga chafu na ya uhasama dhidi ya raia wafuasi wa dini tukufu ya Kiislamu katika nchi hiyo inayodai ni kinara wa demokrasia na haki za binadamu.
Takwimu zilizotolewa na taasisi ya uchunguzi wa maoni ya Gallup Agosti mwaka 20011 zinaonesha kuwa asilimia 48 ya Waislamu wanaoishi Marekani wanasema wamekumbwa na vitendo vya kubaguliwa kwa sababu ya mbari au imani zao za kidini nchini humo.
Kwa ujumla vita na propaganda chafu dhidi ya Uislamu nchini Marekani zinafanyika sambamba na vitendo vya kuwazushia urongo Waislamu, kuvunjia heshima matukufu yao, propaganda chafu za kuchafua sura ya Uislamu na wafuasi wake na ubaguzi wa aina mbalimbali. Hata hivyo inastaajabisha kuwa licha ya vitimbi hivyo vyote, dini ya Kiislamu imeendelea kuenea kwa kasi kubwa huko Marekani na barani Ulaya na kila mwaka kunashuhudiwa idadi kubwa zaidi ya watu wanaosilimu na kukubali mafundisho ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.
No comments:
Post a Comment