Tuesday, April 10, 2012

Miujiza ni nini?


Miujiza mbali mbali huwafanya watu wengi warukeruke mara kwa mara toka dini moja kwenda nyingine au dhehebu moja kwenda lingine. 
Baadhi ya wahubiri wamekuwa wakitumia mazingaombwe ya uponyaji kama chambo cha kuwania waumini kwa wingi bila jasho. Lakini je "miujiza" ndio inathibitisha ukweli na usahihi wa dini au dhehebu?

Ili kujibu kwa ufasaha swali hilo, inabidi tuangalie vitu vitatu vifuatavyo: (i) Miujiza ni nini, na kwa nini ipo? (2) Usahihi wa dini au dhehebu ni nini (3) Uhalali wa miujiza inayofanywa na baadhi ya Wakristo. Hapa tuzingatie kuwa, tutazungumzia miujiza ya Wakristo, sio ya Mtume Yesu (a.s.) wala wafuasi wake wa mwanzo. Miujiza ya Mtume Yesu (a.s.) na wafuasi wake wa awali ni halali moja kwa moja na hauna utata wowote. 


Miujiza ni nini? 
Miujiza ni kitendo au tukio lisilo la kawaida kwa mujibu wa maumbile ya kawaida. Zipo sababu mbili tofauti za Mwenyezi Mungu (s.w.) kuruhusu miujiza. Ya kwanza ni kuonyesha nguvu na uwezo wake mkuu ili watu wameuamini yeye pamoja na Mitume, Manabii au watu wake aliowateua kwa makusudi maalum. Tazama kutoka 20:18-20, Yohana 14:1-11 n.k. Sababu ya pili iliyotofauti kabisa na hiyo ya mwanzo ni hii ifuatayo: "Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, "Na tuifuate miungu mingine USIOIJUA, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto; kwa kuwa Bwana Mungu wenu, YU AWAJARIBU, apate kujua kwamba mwampenda Bwana Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote. Tembeeni kwa kumfuata Bwana Mungu wenu, mcheni na kushika maagizo yake, na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye. Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya Bwana Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru Bwana Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako. "(Kumbukumbu la Torati 13:1-5). Hivyo sababu ya pili ni mtihani toka kwa Mwenyezi Mungu ili tuthibitishe utii wetu na kutoyumbayumba tukiona vitu visivyo vya kawaida vikifanywa na watu wanaojiita "watumishi wa Mungu" wakati wanaenda kinyume na Mwenyezi Mungu. 


Usahihi wa Dini 
Usahihi au uhalali wa mhubiri wa Mwenyezi Mungu, unafafanuliwa vizuri na Wanatheolojia. Wanasema, "18:21 Wayahudi walihangaika kubaini Manabii wa kweli na wa uongo (Taz.1 Fal 22; Yer.28). Alama ni hizi, Nabii wa kweli hufuata kiaminifu mafundisho ya Bwana (s.13), tena ukurasa 159). Wakifafanua zaidi wanasema "Alama ya mwalimu wa kweli ni kwamba afundisha yale yaliyopokewa na Mitume. Yohana awaonya wasisadiki hadithi za walimu wa uongo (1 Yoh 2:18 n.k. Tit 3:9; Tim 2:16)" Biblia Takatifu Tabora Uk. 1119. Ili kuwasaidia wale wasomaji wasiotaka kusikia neno "Wanatheolojia" maneno hayo ya wanatheologia ni ufafanuzi wa maneno ya Biblia yafuatayo:" "kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. Yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu". (1 Yohana aya 9-11). 
Hapo tumeona kuwa, mhubiri wa kweli ni yule anayefuata mafundisho sahihi toka kwa Mwenyezi Mungu na Mitume au Manabii wake, kisha akafundisha mafundisho yatokayo kwa Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Mafundisho ya Mwenyezi Mungu ni mengi. Yapo makubwa na madogo. Makubwa hayabadiliki kabisa tangu zamani. 
Mafundisho makuu ni tafsiri ya uungu wa Mwenyezi Mungu (s.w.), kuamini Mitume na Manabii wake, kuamini Malaika zake, kuamini Maandishi yake (vitabu, vyaraka n.k.), kuamini siku ya mwisho (kiyama) na kuamini kuwa, uendeshaji wa dunia, mbingu na vilivyomo (Qadari), uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu (S.W.). Mafundisho madogo yanayobadilika kulingana na mazingira ni kama utekelezaji wa ibada (rituals), sheria ndogondogo, hukumu za makosa n.k. 
Fundisho lililo kuu kuliko yote ni tafsiri ya Mwenyezi Mungu Mwenyewe. Hili ndilo fundisho kuu la kwanza kabisa kuandikwa katika kitabu rasmi cha Mwenyezi Mungu (Torati). "Mungu akanena maneno haya yote akasema.
Mimi ni Bwana, Mungu wako; niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. USIWE NA MIUNGU MINGINE ILA MIMI" (kutoka 20:1-2). Kutokana na uzito wa fundisho hili, kinaitwa kwa Kiebrania "Shema" ((Tazama Kumb. 6:4, na Marko 12:28-20), na wanafundishwa watoto wa Kiebrania waweze kulitamka kabla ya kusema "Baba" na "Mama". "Shema" inaanza na "sikia eeh Israel......". Mitume na Manabii wote kabla ya kufundisha lolote, walihimiza na kusisitiza hilo (Taz. Isaya 45:21-23 n.k. Mtume Yesu (a.s.) naye anasema "Na uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma (Mtume)". (Yohana 17:3). 
Paulo naye akisisitiza upweke wa Mwenyezi Mungu anasema: "Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanaadamu ni mmoja, mwanaadamu Kristo Yesu" (1 Timotheo 2:5). 
Hivyo mhubiri yeyote, ajiite vyovyote atakavyojiita, akifundisha tafsiri ya Mwenyezi Mungu kinyume na hiyo ya Mitume, Manabii na wafuasi wa Manabii (Paulo), atakuwa anafundisha na kufuata miungu migeni. "Kukizuka kati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia, akisema, Na tuifuate miungu mingine usioijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au mwotaji wa ndoto; kwa kuwa Bwana Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zetu zote." (Kumb. 13:1-3). 


Uhalali wa miujiza ya Wakristo 
Kama tulivyokwisha ona, ili miujiza iwe halali yenye kuthibitisha utukufu wa Mwenyezi Mungu (s.w.), lazima mfanya miujiza (Mhubiri) awe mfuasi wa dini yenye mafundisho sahihi ya Mwenyezi Mungu hasa upweke wa Mwenyezi Mungu, na afundishe mafundisho sahihi yanayotokana na vyanzo halali (Mwenyezi Mungu na Mitume wake). 
Ili tujue kama miujiza ya uponyaji inayofanywa na baadhi ya wahubiri wa Kikristo ni halali au la itabidi tuangalie kwa ufupi historia ya fundisho kuu sana la Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa tafsiri ya dini ya Kikristo. Yaani Mungu moja mwenye nafasi tatu, za Mungu Baba (Mwenyezi Mungu), Mungu Mwana (Yesu) na Mungu Roho Mtakatifu. Kabla ya kuona historia hiyo, tuangalie kwanza Mtume Yesu (a.s.) anasemaje kuhusu wafanya miujiza wanaofuata na kufundisha mafundisho potofu Anasema "kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule". (Mathayo 24:24). 
Na kwa wale wahubiri watakaofanya miujiza kwa jina la Yesu ili kuwapotosha watu, anasema "Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. 
Mtawatambua kwa matunda yao (mafundisho). Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti (Mhubiri) mwema huzaa (hufundisha) matunda (mafundisho) mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndipo sasa kwa matunda (mafundisho) yao mtawatambua. 
Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni. Wengi wataniambia siku ile (kiyama), Bwana, Bwana hatukufanya unabii kwa jina lako, na jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendapo maovu (kupotosha watu)" (Mathayo 7:15-23). 
Kwa kuwa Mchungaji A.T. Manoni ameshaeleza kwa ufasaha sana historia ya itikadi ya utatu (Tazama AN-NUUR Na. 158 Uk. 11), mimi nitaeleza kwa ufupi sana. 
Mara baada ya Mtume Yesu (a.s.) kuondoka, Wapagani waliokubali Ukristo walizusha itikadi za Wanikolai (Taz. ufunuo 2:6) ambao waliukubali Ukristo lakini waliendelea na matambiko yao waliyoyapa sura ya Ukristo. Na walikuwepo Wagnostik walioamini kuwa Mwenyezi Mungu (Yahwe) ni Mungu Muumba aitwaye "Demiurgos" (mtenda kazi). Lakini yupo Mungu mwingine mkubwa zaidi yake. Hatimaye waliibuka Waamontanist wafuasi wa Montano aliyekuwa kuhani wa Mungu wa Kipagani "Cybele". 
Hatimaye aliibuka Manes Mmedi na wafuasi wake waitwao Wamanikayo. Yeye alisema ndiye paracretos aliyetabiriwa na Yesu (Yohana 16:7-16). Hayo ni baadhi ya madhehebu ya Wakristo toka Upagani. 
Lakini pia kulikuwepo na madhehebu ya Wakristo wa Kiyahudi ya Ebionites (maskini) na Essene Ebionites (Watawa - Mamonaki) yaliyokuwa yameshika sana torati. 
Ili nifupishe makala hii, naona niachane na hayo madhehebu mengine yaliyokuwa na itikadi ambazo hivi sasa hazipo, niingilie itikadi hii ya utatu iliyodumu hadi sasa. Itikadi ya Mungu Mwenye nafsi tatu haikuanza ghafla kama watu wengi wanavyofikiria. Itikadi hii ilianza kipengele kwa kipengele. Alianzisha rasmi mtakatifu Yustino ajulikanaye sana kwa jina Yustino Shahidi (Justine Martx) aliyeuwawa mwaka 165 B.K. Yeye aliposoma Mithali 8:1-36 hasa aya ya 2-31 alipoyachanganya maneno ya Yohana 1:1-14, akafasiri kuwa, "hekima" ndiye "Neno" na ni sehemu (nafsi) ya Mwenyezi Mungu mmoja. Na kuwa nafasi hiyo ni Yesu. Hivyo neno la Kigiriki "Homo-ousios" yaani Baba ni sawa na Mwana, akimaanisha kuwa Yesu ni Mungu sawa na Mwenyezi Mungu likaanza kufundishwa rasmi. 
Fundisho hilo lilipoanza kukolea, Askofu Paulo wa Samosata wa Antiokia tangu 260-2709 BK, alilipinga vikali. Hatimaye neno "Homo-ousios" lilipigwa marufuku katika mkutano wa kanisa uliofanyika antiokia mwaka 270 BK, japo askofu Paulo alifukuzwa Uaskofu.
 Hata hivyo liliendelea kufundishwa na likaimarika zaidi na zaidi. Hatimaye kasisi (Padre) Ario (Areus) wa Mtaa wa Boucalis katika jimbo la Alexandria (Misri), (aliyezaliwa mwaka 250 BK na kufa 336 BK), alipinga vikali sana neno hilo na akaanzisha dhehebu la Waario. 
Mzozo ulikuwa mkubwa sana hadi ikabidi kaisari (mfalme) Constantino aitishe mkutano mkuu wa kanisa uitwao "first aecumenical council of Nicea" mwaka 325 BK. Katika mkutano huo uliokuwa chini ya mpagani kaisari (Constantino), Shemasi Athanasio (Athanasius) wa Alexandri "alithibitisha" uhalali wa neno. "Homo-ousios".
 Hivyo Padre Ario alifukuzwa kazi na neno hilo likaingizwa rasmi katika imani ya kanisa uitwayo "kredo ya Nikea". Alipokufa kaisari Constantino, alitawala mwanaye aitwaye Constantio. Yeye alikuwa mwario, hivyo mwaka 343 BK katika mkutano uliofanyika Philopopulis baada ya kutokea mzozo Sardica, imani ya Nikea ikakataliwa rasmi. Hapo ikaidhinishwa rasmi imani ya nne ya mkutano wa Antiokia wa mwaka 341 BK ambayo neno "Homo-ousios" liliondolewa. Lakini alipokufa kaisari Valenis mwaka 378 BK, itikadi ya Uungu wa Yesu ilirudishwa kwa nguvu sana na kaisari Theodosio aliyetawala mwaka 378-395 BK. Mwaka 381 BK katika mkutano wa Constantinopol imani ya Nikea ikarudishwa rasmi na kuongezewa Uungu wa Roho Mtakatifu ili kukanusha imani ya Wamekedoniano waliokataa Uungu wa Roho Mtakatifu. Baada ya hapo zilitumika nguvu kubwa za dola ili kufuta. Kisiasa imani nyingine.Kwa ufafanuzi zaidi rejea makala ya uchanguaji A.T. Manoni "Ni mwaka gani Yesu alianza kuitwa Mungu" katika AN-NUUR No. 158 Uk. 11. 
Kama tulivyoona itikadi ya utatu mtakatifu haina uhusiano kabisa na Mwenyezi Mungu, Mitume wake wala wafuasi wa Mitume. Hata maneno katika Mithali 8:22-31, Yohana 1:1-14, Yohanda 20:28), Rumi 89:5, Tito 2:13 n.k., hayathibitishi Uungu wa Yesu bali yanatafsiri yake sahihi ya Kitheologia. Wanatheologia wanajua vizuri sana tafsiri sahihi ya manenmo hayo. Wameamua akujikausha makusudi ili waendelee kuwakaamua Waumini wao, na wanaishi maisha bora bila jasho. Kwa hiyo miujiza inayofanywa na Wakristo kwa jina la Yesu, sio miujiza halali kwani imesemea kwenye mafundisho potofu juu ya Mwenyezi Mungu rejea tena kusoma kumbukumbu la Torati 13:1-5. 
Hivyo japo miujiza hiyo inawasaidia baadhi ya watu kuacha madhambi ya kimwili (kuiba, kuzini, kuua n.k.) na kuwa waongofu (walokole), lakini inawang’ang’aniza watu wafanye dhambi kubwa sana ya kiroho.
 Yaani dhana potofu juu ya Mwenyezi Mungu (s.w.) na kumkataa "Roho Mtakatifu: (Mathayo 12:31-32). Kwa hiyo waongofu hao wanakuwa kama waongofu wa Kiyahudi walioacha madhambi ya kimwili bila kumkubali Mtume Yesu (a.s.). Hivyo wakawa watu wa motoni kuliko hata hao "waliowaokoa". "Ole wenu waandishi na mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu (mlokole), na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanam mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe." (Mathayo 23:15). 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget