“Nilikuwa na masuali mengi sana ndani ya nafsi yangu juu ya dini yangu ya Ukristo, lakini sikuweza kupata majibu ya kuniridhisha, nikaamua kujiunga na shule ya upadri ili niweze kusoma na kuijuwa vizuri. Nikasoma mpaka nikafikia cheo cha Upadri, nikawa mlinganiaji mkubwa wa dini yangu, na pia baba yangu alikuwa mlinganiaji wa dini ya ukristo juu ya kuwa biashara yetu kubwa ilikuwa ni kuuza vyombo vya muziki ambavyo sehemu kubwa ya vyombo hivyo tulikuwa tukiyauzia makanisa.
Nilikuwa nikiuchukia sana Uislamu na Waislamu na hii inatokana na sura mbaya niliyokuwa nayo juu ya Uislamu kuwa wao ni watu wasiokuwa na imani juu ya Mwenyezi Mungu, wenye kuliabudu sanduku jeusi liliopo jangwani na kwamba ni watu wajinga, magaidi wenye kuua kila asiyefuata dini yao.
Lakini alipokuja kuishi nyumbani kwetu Muislamu mmoja kutoka nchi ya Misri kwa muda wa miezi miwili, nilibahatika kugundua mengi juu ya Uislamu na hii ilitokana na maisha na nidhamu yake mtu huyo, na baada ya kujadiliana naye tuligundua mambo mengi mepya juu ya Uislamu hatukuwa tukiyafahamu hapo mwanzo
Siku moja baba yangu aliniambia kuwa atakuja mtu mmoja kutoka nchi ya Misri na kwamba huenda tukafanya naye biashara ya ala za muziki, jambo lililonifurahisha sana kwani tukifanikiwa biashara yetu itaenea na kufika hadi nchi ile kubwa ya Pyramids (Misri). Kisha baba yangu akaniambia: “Lakini sina budi kukuambia kuwa mtu huyo atakayekuja niMuislamu na ni mfanya biashara maarufu.”
Nikamuuliza huku nikiwa nimeudhika sana: “Muislamu! Hapana, siwezi kukubali kuzungumza naye”
Baba yangu akaniambia: “Huna budi kukubali.”
Nikajibu: “La abadan siwezi kukubali.”
Baba yangu akashikilia kuwa lazima nimpokee vizuri Muislamu huyo kutoka nchi ya Misri, na mimi nilikubali kwa sababu nilikuwa naishi katika nyumba yake asije akanifukuza.
Hata hivyo, siku aliyowasili mgeni huyo nilikwenda kumpokea nikiwa nimevaa kofia yenye msalaba mkubwa na kidani chenye msalaba na pia nilifunga msalaba mkubwa juu ya mkanda wangu huku nikiwa nimebeba Biblia mkononi mwangu.
Nilikwenda kumpokea nikiwa hali hiyo, na jambo la mwanzo nililofanya baada ya kuonana naye ni kuishambulia dini ya Kiislamu pamoja na Waislamu kama nilivyokuwa nikiijuwa mimi kutokana na sura mbaya niliyokuwa nayo. Na wakati wote huo yeye alikuwa mtulivu sana akipokea kwa utulivu mkubwa maneno yangu yaliyojaa hamasa na ghadhabu.
Tulipowasili nyumbani, baba yangu akamkaribisha vizuri na kumtaka afikie nyumbani kwetu na kukaa hapo kwa muda, na nyumbani kwetu tulikuwa tukiishi mimi na mke wangu na baba yangu.
Mmisri yule akakubali kuwa mgeni wetu na wakati ule pia tulikuwa na mgeni mwengine aliyekuwa Mkristo mwenye kufuata madhehebu ya Kikatholiki
Idadi yetu ikawa watu watano. Wane kati yetu ni walinganiaji wa dini ya Kikristo, mimi na baba yangu tulikuwa wafuasi wa madhehebu ya Kiprotestanti na yule Mkristo mgeni wetu alikuwa akifuata madhehebu ya Kikatoliki, na mke wangu pia alikuwa mlinganiaji mwenye kufuata madhehebu ya chuki yaliyokuwa karibu sana na itikadi za Kiyahudi (Zionist). Baba yangu aliisoma Injili tokea alipokuwa na umri mdogo akawa mlinganiaji maarufu. Yule askofu wa Kikatoliki alikuwa na ujuzi mkubwa baada ya kufanya kazi ya kulingania katika bara zote mbili za Amerika (Amerika ya kusini ya Kaskazini) kwa muda wa miaka 12, na mke wangu alikuwa akifuata madhehebu ya ‘Burinjin’ yenye kuunga mkono itikadi za Kiyahudi, na mimi binafsi nilidurusu Injili pamoja na madhehebu mbali mbali ya Kikristo na kupata shahada ya ‘Doctorate’ katika elimu ya itikadi za Kikristo.
Tukawa sisi Wakristo kila mmoja wetu anayo Biblia yake yenye kuhitalifiana na ya wenzake, tunakaa tukiwa tumeizunguka meza ya duara na kujadiliana juu ya hitilafu zilizokuwepo katika itikadi za Kikristo na hitilafu zilizokuwepo katika Biblia zetu tofauti huku yule Muislamu akistaajabu juu ya khitilafu za Biblia zetu. Na wakati ule baba yangu alikuwa na Biblia ya Mfalme James na mimi nilikuwa na Biblia ya Revised Edition inayosema kuwa ndani ya Biblia ya Mfalme James mna makosa mengi na dhambi kubwa kubwa, na hii ndiyo sababu iliyowafanya Wakristo baada ya kuona makosa mengi yaliyomo iliwabidi kukiandika upya na kusahihisha yale waliyoona kuwa ni makosa makubwa. Na Biblia ya tatu aliyonayo mke wangu ni copy ya mlinganiaji wa siku hizi aitawe James Swagart, na kinachochekesha ni kuwa James Swagart huyu alipokuwa akijadiliana na Sheikh Ahmed Deedat mbele ya watu alisema: “Mimi sina elimu ya Biblia!!” Inakuwaje basi mtu aandike Biblia kamili kwa jina lake wakati hana elimu ya Biblia, kisha adai kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu.
Yule askofu wa Kikatholiki, yeye anayo Biblia nyengine yenye milango 73, wakati Biblia niliyonayo mimi ina milango 66, na Biblia zote hizo zinahitilafiana hata yaliyomo ndani yake na hitilafu hizo ni kubwa na nyingi sana.
Tukamuuliza yule Muislamu kutoka Misri ambaye jina lake lilikuwa Muhammad: “Zipo Qurani ngapi kwenu zenye kuhitalifiana?”
Akanijibu: “Sisi hatuna isipokuwa Qurani moja tu nayo ni ile ile iliyoteremshwa kwa lugha ya Kiarabu na wala haijabadilishwa wala kuongezwa hata herufi moja ndani yake tokea ilipoteremshwa miaka 1400 iliyopita.”
Na yule askofu wa Kikatoliki alikuwa haamini mengi yaliyomo ndani ya Biblia yake, jambo lililomfanya awe na ugomvi mkubwa na viongozi wa Kanisa lake, kwani juu ya kuwa ni mlinganiaji wa Kanisa hilo kiasi cha miaka 12 hivi sasa, lakini hakuwa akiamini mengi katika mambo ya itikadi yaliyo muhimu sana.
Na baba yangu alikuwa akiamini kuwa Biblia hizi zimeandikwa na watu na kwamba si wahyi utokao kwa Mwenyezi Mungu, isipokuwa wameandika wakidhani kuwa huo ni wahyi utokao kwa Mwenyezi Mungu. Na mke wangu pia alikuwa akiamini kuwa katika Biblia yake mna makosa mengi sana, isipokuwa yeye pia alikuwa akiona kuwa asili ya maneno yaliyomo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu.
Ama mimi sikuwa nikiayasadiki mengi yaliyomo ndani ya Biblia zetu, kwani nilikuwa nikiona kuwa maneno yake yanagongana na hayakubaliani, na miongoni mwa mambo hayo nilikuwa siku zote nikijiuliza nafsi yangu na nikiwauliza wengine pia kuwa itakuwaje Mwenyezi Mungu awe mmoja kisha wakati huo huo awe watatu? Na niliwahi kuwauliza Maaskofu wakubwa, tena mashuhuri ulimwenguni wakati ule, wakanipa majibu yasiyokubalika akilini. Nikawauliza vipi nitaweza kuwa mlinganiaji na kuwafundisha watu kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na wakati huo huo ni watatu, kisha niwafanye waamini wakati mimi mwenyewe sijaamini.
Wengine wakaniambia: “Usiwabainishie watu, wewe waambie tu kuwa jambo hili ni katika yale ambayo mtu analazimika kuamini bila ya kuuliza”. Na wengine wakaniambia:"Unaweza kuwaambia watu kuwa Utatu wa Mwenyezi Mungu ni mfano wa tunda la tufaha, juu ya kuwa ni moja lakini nje yake mna ganda na ndani yake mna nyama na kokwa.”Nikawaambia: ‘Mfano huu hauwezi kupigiwa Mwenyezi Mungu, kwani ndani ya tufaha mna kokwa nyingi kwa hivyo miungu inaweza kuwa mingi, na pia huenda ndani yake akawepo mdudu, na kwa njia hiyo miungu itaongezeka, na huenda tufaa likaoza na mimi simpendi mungu wa aina hiyo.”
Na wengine wakanipigia mfano wa mtu na mkewe na mwanawe, nikawaambia kuwa mke anaweza kuwa na mimba na idadi ikaongezeka, na anaweza kutalikiwa kisha miungu ikafarikiana, na anaweza kufa mmoja wao na mimi sipendi mungu wa aina hiyo.
Sijapata hata siku moja kuamini juu ya Utatu wa Mwenyezi Mungu na wala sijapata kumuona mwenye kuweza kumshawishi mwenye akili zake akaamini hayo tokea nilipozaliwa nikabatizwa na hatimaye nikawa Padri na mlinganiaji.
Hata hivyo tulipokuwa sisi Wakristo wane tumekaa kuizunguka meza yetu nyumbani tukijadiliana, tulikuwa tukijaribu kumuita Muislamu huyu katika Ukristo, lakini yeye alikuwa akitujibu kuwa yeye atakubali kutufuata ikiwa tunayo yaliyo bora kuliko yaliyomo katika dini yake. Tukamuambia: “Bila shaka yamo mengi.”
Muislamu akasema: “Mimi nipo tayari kama mtaweza kunipa uthibitisho na dalili ya maneno yenu.”
Nikamuambia: “Dini kwetu haina uhusiano na dalili wala akili, bali unatakiwa lazima usalimu amri na kuyakubali yote unayoambiwa. Itakuwaje sasa wewe unataka tukupe uthibitisho na dalili?”
Muislamu akasema: “Lakini Uislamu ni dini ya Itikadi na uthibitisho na dalili na akili na Wahyi utokao mbinguni.”
Nikamuambia: “Ikiwa kwenu mnategemea uthibitisho na dalili basi mimi ningependa kufaidika na kusoma kutoka kwako.” Na tulipoanza kujadiliana juu ya Utatu, kila mmoja wetu akatoa Biblia yake na kuanza kusoma, lakini hatukuweza kupata dalili yoyote iliyo wazi. Kisha tukamuuliza Muhammad: “Nini itikadi yenu juu ya Mwenyezi Mungu katika Uislamu?” Akasema:
1- قُلْ هُوَ اللهُ أَحَدٌ
2- اللهُ الصَّمَدُ
3- لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ
4- وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ".
|
1. Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.
2. Mwenyezi Mungu Mkusudiwa.
3. Hakuzaa wala hakuzaliwa.
4. Wala hana anaye fanana naye hata mmoja
|
ِAlisoma kwa Kiarabu kisha akatufasiria, na sauti yake pale alipokuwa akisoma kwa lugha ya Kiarabu iliingia ndani ya moyo wangu na hata hivi sasa kama kwamba bado inaendelea kuingia sikioni mwangu na bado ningali ninaikumbuka. Ama kuhusu tafisiri yake; sijapata kuona maneno yaliyo wazi na bora, tena yenye nguvu na kufahamika na kukubalika akilini yenye kubeba maana yote kwa ukamilifu kupita hayo.
Tukio hili kwetu lilikuwa mfano wa mshangao mkubwa uliotuamsha katika usingizi wetu na kughafilika kwetu tuliokuwa tukiishi ndani yake pamoja na upotovu.
Yule askofu wa Kikatoliki akamuomba Muhammad ampeleke msikitini ili apate kuona namna Waislamu wanavyoswali, akaenda naye mara mbili katika mojawapo ya makao ya Jumuiya ya Kiislamu, na huko akaona namna Waislamu wanavyotawadha na kuswali, kisha akarudi nyumbani. Na sisi tukamuuliza yule Askofu: “Muziki gani wanapiga Waislamu katika Swala zao?”
Akasema: “Hawapigi muziki kabisa.”
Tukasema kwa mshangao: “Wanamuabudu Mola wao na kuswali bila ya muziki!?”
Askofu akasema: “Ndiyo, na mimi natamka: ( أشهد أن لا إله إلا الله وأن محمدًا رسول الله) Nashuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.”
Tukamuuliza: “Kwa nini ukasilimu, wewe unayo hakika juu ya haya unayotenda?”
Nilimuuliza hayo huku mimi mwenye naungulika moyoni mwangu nikitamani kuwa ningelislimu kabla yake ili asiwe bora kupita mimi.
Kisha baba yangu akasilimu, na mimi na mke wangu tukapanda juu nyumbani kwetu, na mke wangu akaniambia: “Nadhani uhusiani ulio baina yetu hautoweza tena kuendelea.”
Nikamuuliza: “Kwa nini! Unadhani kuwa na mimi pia nimeingia katika dini ya Kiislamu?”
Akaniambia: “Si hivyo, bali mimi ndiye nitakayeingia katika dini ya Kiislamu.”
Nikamuambia: “Kusema kweli hata mimi pia nataka kusilimu.”
Nikatoka nje ya nyumba yetu na kusujudu huku nikielekea kibla, nikasema: “Mola wangu niongoze.” Nikauhisi moyo wangu kuufungukia Uislamu, kisha nikaingia nyumbani nakuwajulisha kuwa nishasilimu.
Kuingia kwetu katika dini ya Kiislamu kunatokana na neema kubwa iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu, kisha kutokana na mwenenedo na tabia njema ya yule Muislamu aliyekuwa mlinganiaji mwema mwenye tabia njema. Upo msemo kwetu usemao: “Usiniambie, bali nionyeshe"
Ushuhuda huu ilitolewa na Yusuf Estes
CLICK HAPA http://www.facebook.com/pages/Yusuf-Estes/9209579703 KUMPATA KATIKA FACEBOOK
CLICK HAPA http://www.facebook.com/pages/Yusuf-Estes/9209579703 KUMPATA KATIKA FACEBOOK
No comments:
Post a Comment