Wednesday, April 4, 2012

KUWA NA ‘IZZ (FAHARI) NA UISLAMU



 

Anasema Allah Subhaanahu Wata’ala katika Quraan Aal Imraan/19

 

                                                                         إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّهِ الإِسْلَـمُ

Bila ya shaka Dini mbele ya Allah ni Uislamu

 

 Na anasema tena katika sura hii aya ya 85

 

                                                      وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الإِسْلَـمِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ   

             

Na anaye tafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake

 

Na anasema Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) katika hadithi sahihi

 

                                             ......     كل مولود يولد على الفطرة

" رواه البخاري  ومسلم

 

“Kila mtoto anaezaliwa huzaliwa katika fitrah ( hali ya uislamu). ……

                                   Imesimuliwa na Bukhari na Muslim

 

Hatuna budi kwanza kumshukuru Allah (Subhaanahu Wata’ala) kwa kutujaalia kuwa waislamu na kwa kutuletea uongofu ndani ya dini hii adhimu ambayo Allah (Subhaanahu Wata’ala) alimtamkia Mtume wake Muhammad (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kwamba tayari dini hii imekamilika na neema zake Allah(Subhaanahu Wata’ala) kutimia na kutupa upendeleo wa kipekee kwa  kutuneemesha na neema hii kubwa ambayo kadri tutakavyomshukuru Allah(Subhaanahu Wata’ala) basi hatutofikia hata thuluthi ya uzito wa neema yenyewe Al Maaidah/3

 

                    الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِى وَرَضِيتُ لَكُمُ الأِسْلاَمَ دِيناً

 

Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe kwenu ndiyo Dini

 

Na bado tutatakiwa kurudi kwake Subhana kila mara kwa kumuomba atupe uwezo wa kuishi katika kuifuata dini hii kikamilifu na mpaka wakati wetu takapofika kuondoka katika dunia basi tunaondoka katika hali ya kuridhiwa  na Allah(Subhaanahu Wata’ala) - Aal Imraan /102

 

                      يأَيُّهَا الَّذِينَ ءَامَنُواْ اتَّقُواْ اللَّهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلاَ تَمُوتُنَّ إِلاَّ وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ   

 

 Enyi mlio amini! Mcheni Allah kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu

 

Hakuna biashara iliyo njema kama kuweka akiba  kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) katika maisha na pia wakati tutakapokufa kwa kuishi katika mfumo sahihi wa dini yetu hii adhimu kwani kigezo hiki kitamtosheleza Allah(Subhaanahu Wata’ala) kuweza kutuokoa sisi na moto na kuwa sababu ya kupelekwa  peponi.

 

Hali halisi ya jamii za waislamu ulimwenguni leo ni kwamba tumekumbwa na kila aina za mitihani tokea fitna miongoni mwetu wenyewe,kufuata matamanio ya nafsi zetu, kuchanganyikiwa katika kujua kipi cha kufuata na kipi cha kuacha, kuacha misingi sahihi ya dini yao kufikia hali kwa muislamu anaeshikamana na dini yake basi huonekana mtu wa maajabu kabisa mbele ya jamii na  muislamu “poa” kuwa ndiyo muislamu msafi.

 

Kila muislamu anatakiwa kwanza awe na fahari ya kuwa muislamu na fahari hii si kwa kujilabu tu kwa maneno yanayotoka kinywani lakini kutahitajika kufanyiwa kazi kwa ikhlaas na hapo ndipo itakapoonekana fahari hii kwenye nyoyo za waislamu, maneno na pia kwenye matendo yao .Baadhi ya mambo yenyewe ni kama yafuatayo:

 

1     IFANYIE KAZI DINI YAKO

 

Kila siku muislamu anapolala hujiuliza nini amefanya kwa ajili ya dini yake kwani katika siku ile kwa ni Uislamu tayari ushatufanyia kila linalopaswa kwa ajili yetu tokea kutuletea Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kutuongoza na kutuonesha njia na kututeremshia Qur’aan ambayo ndiyo katiba yetu na  kupitiwa na hazina ya elimu ya waislamu tokea masahaba, mataabiina na salafun saalih na wengi wengineo waliofanyia kazi dini hii ya Allah(Subhaanahu Wata’ala) kilillahi hadi kutufikia sisi ambao pia tuna wajibu wa kuhakikisha kizazi kijacho kifaidike kama tulivyofaidishwa sisi na kizazi kilichopita. Hili ni jukumu la kila muislamu kuhakikisha kila siku tunaifanyia kazi dini hii kwenye nafsi zetu, ibada zetu, familia zetu, mbele ya marafiki zetu na

 

2     UWE NA MSIMAMO MADHUBUTI KATIKA DINI

 

Kama ananvyosema Allah(Subhaanahu Wata’ala) katika Quraan Al Ahqaaf/13

             

                        إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

Hakika walio sema: Mola wetu ni  Allah; kisha wakatengenea, hawatakuwa na khofu, wala hawatahuzunika

 عن سُفْيَانَ بْنِ عَبْدِ اللهِ  رَضيَ اللهُ عَنْهُ قَال: قُلْتُ: يا رَسُولَ الله، قُلْ لي في الإِسْلاَمِ قَوْلاً، لاَ أَسْأَلُ عَنْهُ أَحَداً غَيْرَكَ. قَال: ((قُلْ: آمَنْتُ باللهِ ثُمَّ اسْتَقِمْ)).

                                                                        رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

Kutoka kwa  Sufyaan Ibn Abdillah Allah amuwie radhi amesema:

Nilisema: Ewe Mjumbe wa Allah niambie kitu kuhusu Uislamu ambacho siwezi kumuuliza mtu yeyote ila wewe.  Akasema Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam)   : Sema;  Nimemuamini Allaah , kisha kuwa mwenye kunyooka na kuwa na msimamo madhubuti katika dini

Imesimuliwa na Muslim.

Mtume Muhammad Salla Allahu 'Alayhi Wasallam  mara kwa mara alikuwa akiomba dua hii:

“ Ewe mwenye kuzigeuza nyoyo udhibiti moyo wangu katika dini yako”

Msimamo huu  ndio  silaha itakayokufanya usiyumbishwe, usichanganywe wala kubabaishwa na pia kutokuwa na khofu,woga wala kuhuzunishwa. Kumbuka kuwa muislamu ni jambo rahisi sana lakini kubaki kwenye msimamo madhubuti kwenye dini ni jambo linalohitaji kufanyiwa kazi  na kuwepo mikakati madhubuti huku tukimuomba Allah(Subhaanahu Wata’ala) atuwafikishe kama anavyotukumbusha Mtume wetu(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam).

 

3     KUWA MKALI MBELE YA MAKAFIRI NA MWENYE HURUMA MBELE YA WAISLAMU

Kama anavyosema Allah(Subhaanahu Wata’ala) katika Suuratul Fat-h /29

 

                          مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّهِ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّآءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَآءُ بَيْنَهُمْ

 

Muhammad ni Mtume wa Allah. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao.

 

 Na anasema tena katika Suuratul Maaidah/54

 

                  فَسَوْفَ يَأْتِى اللَّهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَـفِرِينَ

 

Basi Allah atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa waumini na wenye nguvu juu ya makafiri.

 

Nguvu hizi dhidi ya makafiri zinatakiwa ziwe za hoja ,msimamo ,mapambano na kadhalika.Kwani hakuna mjadala katika mas - ala yote ya kimsingi ya kidini, kupoozana au kuchukuliana kwa lengo la kuwaridhisha makafiri na wasiokuwa waislamu au hata waislamu ambao tayari mitazamo yao ishaelekea mrama..

Tumsikilize Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akitusimulia jinsi muislamu anavyokuwa mbele ya waislamu wenzake:

 

مَثَلُ الْمُؤْمِنِينَ فِي تَوَادِّهِمْ وَتَرَاحُمِهِمْ كَمَثَلِ الْجَسَدِ الْوَاحِدِ، إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى

                                                           لَهُ سَائِرُ الْجَسَدِ بِالْحُمَّى وَالسَّهَر

 

Mfano wa waumini katika kupendana kwao na katika kuoneana huruma kwao ni kama mfano wa kiwiliwili. Kikiugua kiungo kimoja tu basi kiwiliwili kizima kitaugua na kukesha kwa homa.

 

4     ITANGAZE DINI YAKO

Kufanya Daawah ni wajibu katika uislamu Annahl/125

 

                  ادْعُ إِلِى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَـدِلْهُم بِالَّتِى هِىَ أَحْسَنُ

 

Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.

 

Dini ya kiislamu imeweza kufika katika kila pembe ya dunia kwa sababu ya kuwepo waislamu waliojitolea kuifanya kazi hii ya Daawah kuuita ulimwengu kuja katika uislamu.

Suuratu Yuusuf/108

 

   قُلْ هَـذِهِ سَبِيلِى أَدْعُو إِلَى اللَّهِ عَلَى بَصِيرَةٍ أَنَاْ وَمَنِ اتَّبَعَنِى وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَمَآ أَنَاْ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

 

Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Allah kwa kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Allah! Wala mimi si katika washirikina.

 

Mwenye kuwaita watu katika uislamu hutakiwa pia kuitekeleza dini yake kikamilifu  na kufanya mambo mema na huku anajitambulisha bila ya woga wala khofu kwamba yeye ni MUISLAMU. Fussilat /33

                     

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلاً مِّمَّن دَعَآ إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَـلِحاً وَقَالَ إِنَّنِى مِنَ الْمُسْلِمِينَ      

  

Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Allah na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu

                            

Masahaba walikuwa na fahari na uislamu wao hawakuwa watu wa kuogopa lolote na jambo hili ndilo lililowasaidia kuweza kupambana na makafiri na kuwashinda. Tunasoma katika historia jinsi sahaba Abu Dharril Ghifari Allah amuwie radhi alivyodiriki kwenda kujitangazia kwamba yeye ni muislamu mbele ya makafiri licha ya kunasihiwa na Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kwamba asijitangazie. Na hata kipigo alichokipata hakikumfanya kubadilisha uamuzi wake kwani alisema na kesho kama akitakiwa kufanya atakwenda tena kuwatanganzia kama alivyofanya leo. Allahu Akbar! Akaambiwa yatosha ulivyofanya na ujumbe tayari umefika.

Kumbuka wewe ndiye balozi wa uislamu na mwakilishi wa dini hii popote ulipo hivyo kila unalolifanya ikiwa mbele ya hadhara au faragha ,alama za dini yako lazima zionekane kama ukweli, uaminifu, ukarimu, usafi, upole na kadhalika. Kuitangaza dini huwa kwa maneno na vitendo pia. Kwani njia bora katika kuitangaza dini hii kwa wasiokuwa waislamu ni daawah ya vitendo.

 

5     ILINDE DINI YAKO

Anasema Allah (Subhaanahu Wata’ala) katika Suuratu Muhammad/7

                              يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ     

 Enyi mlio amini! Mkimnusuru Allah naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu 

Na anasema katika Suuratul Hajj/40

 

                                      وَلَيَنصُرَنَّ اللَّهُ مَن يَنصُرُهُ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ

Na bila ya shaka Allah humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Allah ni mwenye nguvu mtukufu

  

Uwe tayari kila wakati kuihami na kuilinda na kuwa tayari kujitolea muhanga kwa ajili ya kuhakikisha dini ya Allah(Subhaanahu Wata’ala) inasimama katika ardhi kwa misingi ya haki na uadilifu. Na hapo kupata nusra yake Allah(Subhaanahu Wata’ala) kama ilivyotajwa katika aya.  

 

Ndugu yangu muislamu umeshawahi kuchukua hatua hizi katika maisha yako?

Au kuchukua moja katika hizi kwa ajili ya dini yako?

Kama bado basi haujafika wakati wa kuona fahari kwa dini yako na kuifanyia kazi kwenye moyo,maneno na vitendo vinekane hadharani? Na kama unaendelea basi tuzidi kumuomba Allah atupe ithbati katika nyoyo zetu, subira katika kuikabili  mitihani na azma ya kuendelea na kazi hii inshaallah.

Usione haya kujinadi kama wewe ni muislamu.

Usione taabu kujipamba kwa mavazi ya kiislamu.

Uwe tayari kuilinda dini yako,

Ujenge tabia ya kuitangaza dini yako na kuonesha kwa vitendo mafundisho ya dini yako na hapo ndipo inshaallah kwa taufiq yake Allah(Subhaanahu Wata’ala) tutakuwa kweli na fahari na dini yetu.

 

Wabillahi Tawfiq

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget