Tuesday, April 10, 2012

Umuhimu wa elimu ya awali kwa watoto wadogo


Mwanaadamu yeyote, japo awe haamini kuwa yupo Mwenyezi Mungu na ipo siku moja viumbe wote tutakusanywa mbele yake, hawezi kuridhia kuona mwanawe anapata malezi mabaya kitabia, kiafya n.k. Kutoridhia pekee, hakuwezi kumpatia mwanawe malezi mema anayoyaridhia bila ya kufanya juhudi. 
Moja ya juhudi za kufanikisha kuwa na watoto wenye tabia na afya njema, ni kuwapa Elimu ya Awali yenye mwelekeo sahihi inayotolewa na waalimu waliotayarishwa vyema kwa ajili ya kazi hiyo. 


Hatua za utoaji wa Elimu ya Awali kwa mtoto 
1. Mtoto hupewa Elimu ya Awali kabla ya mimba kutungwa kulingana na Itikadi na jamii ya Wazazi wake. Mfano Nabii Zakariya (a.s.) alipoomba kwa Allah (s.w.) apewe mtoto mwema, alisema" 
"Mola, nipe kutoka kwako mtoto mwema, kwa hakika wewe ni Mwenye kusikia dua." (Qur 3:38). 
Pia Bwana wetu Muhammad (s.a.w.) ametufundisha kusoma dua kabla ya kufanya jimai mke na mume isemayo "Ewe Mwenyezi Mungu! Tuepushe na shari ya shetani (katika Ibada yetu hii), na umuepushe na shari ya shetani yule (mtoto) utakayeturuzuku (kutokana na ibada hii)." 
Mtume (s.a.w.) akasema kwamba, kama atapatikana mtoto kwa tendo hilo, basi Allah (s.w.) atamlinda na kila aina ya shari ya shetani. Hii haina maana kwamba mtoto anayetungiwa mimba bila ya ile dua ya jimai, basi huwa muovu tangu siku ile walipojamiiana wazazi wake kwa kuwa hatopata Hifadhi ya Allah (s.w.) kujikinga na shetani muovu. 
2. Mtoto hupewa Elimu ya Awali akiwa tumboni mwa mamaye. Mfano ni mama yake Maryam (Mke wa Mzee Imran) aliposoma kwenye uja uzito wake yafuatayo: 
"Mola wangu! Kwa hakika mimi nimeweka nadhiri kwako, aliyetumboni mwangu awe wakfu; basi nikubalie dua yangu (nadhiri yangu). Bila shaka wewe ndiye usikiaye na ujuaye." (Qur 3:35) kinyume chake watu wabaya huomba kwa Allah (s.w.) kupata watoto, na wakishapata tu, huwakabidhi kwa vinyamkela, Sharif, n.k. ili wawalee na kuwalinda. Allah (s.w.) amesema: 
"Yeye ndiye aliyekuumbeni katika nafsi moja; na akafanya katika (nafsi) hiyo wake zao, ili (kila mwanamume) apate utulivu kwake (mkewe). Na anapomuingilia hushika mimba (ambayo huwa) nyepesi kutembea nayo (yule mwanamke bila ya uzito).(Hata) anapokuwa mja mzito (mimba pevu inamtaabisha), wote wawili (mke na mume) huwa wanamuomba Mwenyezi Mungu, Mola wao (wakisema): "Kama ukitupa (mtoto) mwema (kamili), tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru. Basi anapowapa (mtoto) (Kiumbe) alichowapa. Lakini Mwenyezi Mungu ametukuka kuliko wale wanaowashirikisha naye." (Qur.7:189-190). 
3. Mtoto hupewa Elimu ya Awali akiwa nyumbani kwa wazazi wake. Mfano ni Mzee Luqman ambaye Allah (s.w.) alimpa Hekima iliyompelekea kumlea mwanawe malezi mema; mzazi huyu alisema: 
"....Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu, maana shirki ndiyo dhuluma kubwa..... 
"Ewe mwanangu! Kwa hakika jambo lolote hata likiwa na uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au mbinguni au katika ardhi, Mwenyezi Mungu atalileta (amlipe aliyelifanya); bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo yaliyofichikana, (na) Mjuzi wa mambo yaliyodhahiri. 
Ewe Mwanangu! Simamisha swala, na amrisha mema, na kataza mabaya, na uwe na subira juu ya yale yatakayokusibu; hakika hayo ni katika mambo yanayoazimiwa. Wala usiwafanyie watu kiburi (kwa kuwaangalia upande na kujitukuza), wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila ajivunaye, ajifakharishaye. 
Na uishike mwendo wa kati na kati, na uteremshe sauti yako; kwa kinyume chake mtoto hujifunza tabia mbaya kwa mzazi wake kwa kutendewa kila atakalo ikiwa ni pamoja na kuangalia sinema za maasi n.k. 
4. Mtoto hupewa Elimu ya Awali katika Kituo cha Malezi. Mfano Mke wa Mzee Imrani alipopata mtoto na kumpa jina Maryam, alimpeleka kwenye Kituo cha Malezi kwa Nabii Zakariya (a.s.) ambaye ndiye alikuwa Mwalimu pekee kwa wakati huo aliyetayarishwa na Allah (s.w.) kwa ajili hiyo. Nabii Zakariyya (a.s.) alitoa huduma kubwa ya malezi kwa Maryam na kila wakati alimzuru ili kulinda usalama wake. Allah (s.w.) amesema:- 
"Basi Mola wake akampokea (yule mtoto mwanamke) kwa kubuli njema, na akamkuza kukua kwema, na akamfanya Zakariya awe Mlezi wake. Kila mara Zakariya alipoingia chumbani (kwake) alikuta nyakula mbele yake. Akasema: "Eve Maryam! Unapata wapi hivi?" Akasema: "Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hesabu." (Qur. 3:37). 
Kinyume chake mtoto akipelekwa kwenye kituo cha malezi kilicho kinyume na Itikadi ya Kiislamu, au kwenye kituo ambacho walezi/Waalimu wake hawakutayarishwa vilivyo, mtoto atafunzwa Itikadi ya Kumkana Allah (s.w.) na kutokuwa na adabu. Hata akikutwa na vitu vya thamani hawezi kuhojiwa alikovipata kama alivyohoji Nabii Zakariya (a.s.), bali pengine na huyo Mlezi? Mwalimu ataomba apewe sehemu ya vitu hivyo, na huo ndiyo huwa mwanzo wa tabia mbaya za kutamani vya watu, kutokuwa na kinaa, na kuanza wizi, ujambazi na umalaya. 


Aina ya vituo vinavyotoa Elimu ya Awali kwa mtoto 
Vituo vinavyotoa Elimu ya Awali kwa watoto ni:- 
1. KINDERGATTGEN: Hii ni Bustani ya Watoto yenye miti mingi na uwanja mpana ambao umewekwa ndani yake michezo mingi ya watoto kama bembea, mizani, miterezo, vigari n.k. ambao kazi yake kubwa ni kuwajenga watoto kielimu. 
2. DAY CARE CENTRE: Hiki ni kituo cha kutoa malezi kwa watoto wadogo wakati wazazi wao wapo kazini au katika shughuli mbalimbali. Hushughulika hasa kutoa:- 
- Lishe kwa watoto 
- usalama kwa watoto, na 
- maadili mema kulingana na jamii. 
3. NURSERY SCHOOL: Hii ni shule ya Malezi ambayo hushughulika na:- 
- Yote yanayofanywa kwenye Day Care Centre 
- Kuwaandaa watoto kwa ajili ya kuanza Elimu ya Msingi. 
4. PRE-SCHOOL: Hii ni shule ya Awali ambayo kazi yake kubwa ni kuwalea na kuwaanda watoto Kielimu. 
Kwa vile Uislamu ndiyo Mfumo (Dini) pekee ulio sahihi wa maisha ya mwanadamu, sisi Waislamu hatuna budi kuwalinda watoto wetu kwa kila hali, dhidi ya athari ya tamaduni zisizo za Kiislamu. 
Kwa kuwa watoto wana sifa ya kunasa upesi mafunzo, yawe mema au mabaya, kwa kuona, kusikia, na kucheza michezo ya aina mbalimbali, ipo haja kubwa ya kuwa na vituo vyetu vya kulelea watoto, na hasa lifanywe kila liwezekanalo ili kila Madrasa iwe ni kituo cha malezi ya watoto wadogo kitakachotoa Elimu ya Awali kwa watoto ambao hawajafikia umri wa kuanza Elimu ya Msingi. Pia yatubidi tuwe na Muhtasari wetu na vitabu vyetu vya kiada, vitakavyofuata na kulinda Itikadi yetu. 
Lengo la Muhtasari huo, liwe ni kumuongoza Mwalimu katika yale yanayohitajiwa kwenye utendaji wa shughuli zake za kuwalea wanafunzi wa Elimu ya Awali ambayo ni:- 
(a) Kuhimiza ukuaji wa watoto kimwili, kiakili, kiroho/kimaadili, kiafya, kijamii/kimazingira na kielimu. 
(b) Kutambua tofauti za ukuaji wa watoto kati ya wale wenye maendeleo ya kawaida katika ukuaji, na wale wenye matatizo katika ukuaji ili iwe rahisi kuweza kuyasaidia makundi yote mawili ipasavyo. 
(c) Kuwaandaa waweze kumudu masomo ya Elimu ya Msingi. 


Kazi ya kufundisha (ualimu) 
Kufundisha ni moja ya kazi ngumu sana duniani, hasa kwa vile inahusika na malezi ya wanadamu hususan watoto. Tofauti iliyopo baina ya watoto, humfanya Mwalimu/Mlezi apambane na upinzani mkubwa katika shughuli zake za kufundisha. 


Tofauti za watoto 
Watoto hutofautiana kwa:- 
1.UMBILE: Wapo warefu, wafupi, wanene, wembamba, weupe, weusi, wang’avu n.k. 
2. TABIA: Wapo wenye huruma, wakatili, wapole, wakali, waongo, wakweli n.k. 
3. UZOEFU KATIKA MAISHA: Wapo wanaoweza kumudu kutawala mazingira yao, wasioweza kumudu kutawala mazingira yao. 
4. KIJAMII: Wapo watoto wa kitajiri, wa kimasikini, kisomi, na wasio wa kisomi. 
5. KIFAMILIA: Wapo wanaolelewa katika familia ya kawaida (yenye mwelekeo unaofanana) inayoundwa na Baba, Mama, na Watoto. Wapo wanaolelewa katika familia mchanganyiko (yenye mielekeo tofauti) inayoundwa na watu mchanganyiko -Baba, Mama, Watoto, Babu, Bibi, Mjomba, Shangazi, Baba na Mama Mkubwa/Mdogo, Ndugu wa hiyari/urafiki/ukabila/kunyonya n.k. 
6. URITHI WA VIZAZI: Wapo wanaorithi tabia za Wazazi wao, na wapo wanaorithi tabia za ndugu/Wazazi wa Wazazi wao. 
Ili Mwalimu aweze angalau kumudu sehemu ya ugumu wa kazi yake hii nzito, anatakiwa afahamu mambo muhimu yafuatayo:- 
Jina la mtoto, Jinsia ya mtoto, wasifu wa ndani wa mtoto, wasifu wa nje wa mtoto, urithi wa mtoto (Asili, Kabila, ukoo), na umri wa mtoto. 
Pia afahamu kuwa mtoto anataka nini, anapendelea nini, anajua nini, na anataka kujifunza nini. 


Kazi ya Mwalimu 
Kazi kubwa ya Mwalimu ni kumsaidia mtoto:- 
(a) Aweze kujifunza maarifa kutokana na mazingira yake. 
(b) Aweze kujifunza jinsi ya kutatua matatizo yake mwenyewe. 
(c) Aweze kujifunza stadi mbalimbali za utendaji. 
(d) Aweze kujifunza namna ya kuuthamini utamaduni na Itikadi ya jamii yake. 
(e) Aweze kujifunza Tabia na Maadili mema. 
(f) Aweze kukuza uwezo wa Lugha na mawasiliano. 


Njia za kujifunza watoto wadogo. 
Watoto wadogo hujifunza kwa vitendo - yaani: Kusikia, kuona na michezo. Hivyo Mwalimu huwaelekeza watoto kutenda, yeye akiwa ni msimamizi, na watoto huwa ni watendaji wakuu. 


Nasaha kwa walimu 
Nawaomba Waalimu wajitahidi kuwa na subira kubwa katika kufanya kazi hii ya kufundisha, kwani ni kazi iliyorithiwa kwa Mitume (a.s.) ambao ndio Waalimu wakubwa waliotumwa na Allah (s.w.) kufundisha jamii zao, wakifuata muhutasari maalum uliotayarishwa na Mwenyewe Allah (s.w.) uliokuwa na vitabu vyake vya kiada viitwavyoVITABU VYA ALLAH (S.W.). Imesimuliwa kwamba, Mtume (s.a.w.) amesema: 
"Hakika nimetumwa ili niwe Mwalimu". Pia amesema, "Hakika nimetumwa ili kuja kukamilisha tabia njema." 
Pia Waalimu msiwe watumwa wa Muhutasari, kwani kufanya hivyo kutawanyima fursa ya kusoma vitu vingi kwa muda mfupi wale watoto wenye uwezo wa kuelewa upesi. Hivyo jaribuni kuwa wabunifu wa kubadilisha mbinu mbalimbali za ufundishaji ili yapatikane mafanikio haraka zaidi. 


Nasaha kwa wazazi 
Pamoja na kuwa Walimu wanatakiwa kuwa na subira nyingi Wazazi ndiyo chanzo kikubwa cha kuwafanya waalimu wasiwe na subira hali inayopelekea wasiweze kufanya kazi zao ipasavyo na kufikia malengo yao. Fahamuni kuwa waalimu ni binadamu kama nyie, na hawana uwezo wa kufanya maajabu, bali hufanya kazi zao za ufundishaji kwa kufuata maelekezo yaliyomo kwenye Muhtasari. Hivyo wazazi acheni tabia mbaya zifuatazo:- 
(a) Kumuhoji Mwalimu: "Kwanini muda mrefu sasa umepita na mwanangu hajafahamu somo fulani? Au hujui kufundisha?" 
(b) Kuwa wabakhili wa kutoa huduma muhimu kwa Walimu zikiwemo Ada n.k. Fahamuni kuwa waalimu huwa hawatumii nguvu katika kazi zao kama fundi seremala n.k., bali hutumia akili nyingi kuandaa somo, kufundisha ni kufanya tathmini ya somo alifundisha. Kwa hiyo mnatakiwa mzitulize akili zao zisiwe na fikra nyingine kwa kuwapa misaada wakati wa shida zao bila ya kuhoji, na kutowapa maneno ya maudhi yatakayompotezea malengo yake. 
(c) Shirikianeni na waalimu kwa kufuata ushauri wanaowapeni ili watoto wenu waweze kuwa na tabia njema, na waweza kuelewa upesi masomo yao.  
 
Na Ustaadh Kupa Pazi Said 

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget