Wednesday, April 4, 2012

Madhara ya ulevi kwa binadamu


Madhara ya ulevi kwa binadamu
Madhara ya ulevi kwa binadamu 
 KILA sifa njema anazistahiki Mwenyezi Mungu ambaye amempa heshima mwanadamu na kumfanya kuwa bora kuliko viumbe vingi (1). Na rehema amani zimfikie Mtume Muhammad aliyeletwa akiwa ni rehema kwa viumbe 
Miongoni mwa visa vya kushangaza na kutisha ni hiki: Kijana mmoja, akiwa amelewa, aliingia chumbani kwa mama yake na kumtaka unyumba.Mama alikataa. Kijana alichukua kisu na kumwambia mama yake kuwa: Usiponipa unyumba nitajiua. Mama ilimjia huruma na hivyo akajisalimisha kwa mwanae na kumpa unyumba. 
Baada ya hapo kijana alikwenda kulala chumbani kwake. Ilipofika asubuhi, kijana alihisi kuna jambo amefanya, na hivyo akamwendea mama yake na kumuuliza: Mama, nilifanya nini mimi jana? Mama akajibu: Hukufanya kitu. 
Kijana akamng'ang'nia mama yake amwambie na mwishoe mama akamwambia. Kijana alichukua petroli na kuingia nayo chooni. Alijimwagia na kujichoma moto. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe salama! 
Kijana huyu amefanya makosa makubwa matatu:1.Amekunywa Pombe. 2. Amezini na mama yake. 3.Amejiua. 
Kisa hiki ni miongoni mwa visa vingi vilivyo tokea na vinavyoendelea kutokea. Kwa sababu hii, ndio maana ulevi umeitwa Mama wa Maovu, na hasa hivyo ndivyo ilivyo. 
 
MAANA YA POMBE
Pombe [khamri] ni kila kitu kinacho ifinika akili kwa njia ya ladha na starehe. Mara nyingine pombe huitwa kileo na mara nyingine huitwa vinywaji vya kiroho au alcohol au madawa ya kulevya [mikhadarati] kwa aina zake zote. Kinacho zingatiwa ni maana na makusudio na sio matamshi au herufi. Imekuja katika Hadithi ya Mtume Muhammad, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani, iliyosimuliwa na Abuu- Maalik Al-Ash'ariy kwamba alimsikia Mtume akisema kuwa: "Wallahi [nina'apa kwa Mwenyezi Mungu kuwa] kuna watu katika umma wangu watakunywa pombe na wataiita kwa jina lisilokuwa lake"(2) 
Jihadhari ewe ndugu yangu yasije yakakutatanisha mambo kwa pombe kubadilika jina pale inapoitwa wiski[whisky] au jina jingine. 
Elewa kuwa hiyo ni pombe na ni kileo hata kama jina lake limebadiliwsha"Na kila kinacholewesha ni pombe na kila kinacholewesha ni haramu" (3) 
 
HUKUMU YA KUNYWA POMBE
Kunywa pombe ni haramu, bali ni miongoni mwa madhambi makubwa. Waislamu waliotangulia [Salaf]na waliofuatia [khalaf] wamekubaliana tangu zamani juu ya uharamu huo kwa mujibu wa hoja ²zifuatazo: 
1.Amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika kwamba:"Enyi mlioamini, hakika si vingine isipokuwa kwamba pombe na kamari na masanamu na ramli ni uchafu katika vitendo vya shetani. Hivyo, jiepusheni navyo ili mfanikiwe. Hakika, si vingine isipokuwa kwamba shetani anataka atie kati yenu uadui na chuki katika pombe na kamari na awazuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Je,mmekoma ?" (4)Aya hizi zilitosha kabisa kuwafanya Waislamu waache pombe bali na kuimwaga barabarani. Ewe ndugu yangu Mwislamu, hebu angalia picha hii: Imepokewa kutoka kwa Anas,Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, akisema kuwa: Nilipokuwa natembeza [nagawa] glasi za [pombe] kwa Abu-Talha, Abu-Ubaida Ibn-Aljarraah, Abu-Dujaanah, Muadh bin Jabal na Sahli bin Baidh mpaka vichwa vyao vikawa vinayumba kutokana na [ukali wa pombe ya]mchanganyiko wa tende na kokwa zake, nilimsikia mnadi akisema: Ee! Hakika, pombe imeharamishwa. Amesema Anas kuwa: Kutokana na wito huo, hakuingia wala hakutoka mtu [klabuni] mpaka tukaimwaga pombe na kuvunja mitungi. Baadhi yetu walitawadha na wengine wakaoga kwa Ummu-Sulaim, halafu tukatoka kwenda msikitini na kumkuta 
Mtume anasoma aya hizi: Enyi mlioamini, hakika si vingine isipokuwa kwamba pombe .....(mpaka) ....je , mmekoma ?" (5) 
Ewe ndugu yangu Mwislamu, hivi ndivyo unavyokuwa msimamo wa Mwislamu katika kuitikia amri za Mola wake.Anatakiwa kuitikia haraka, bila ya kusita wala kuchelewa au kungojea. 
Ewe ndugu yangu mpenzi, tutangaze toba kwa Mola wetu na tukariri kama Sahaba, Mwenyezi Mungu awawiye radhi, walivyokuwa wakikariri kusema: "Tumekoma ewe Mola wetu, tumekoma ewe Mola wetu". 
2. Sheria ya Kiislamu imelipiga vita vikali sana ovu hili na kupelekea kuwalaani aina kumi ya watu kuhusiana nalo.Idadi kama hii haukutajwa katika maovu yoyote mengine. Imepokewa kutoka kwa Anas, Mwenyezi Mungu amwiye radhi, akisema kuwa: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amewalaani watu kumi kwa sababu ya ulevi: 1.Mkamua pombe [mtengenezaji]na 2.Anayekamuliwa [anayetengenezewa] na 3. Mnywaji pombe na 4.Anayebeba pombe na 5.Anayepelekewa na 6.Anayenywesha pombe(mhudumu /mfadhili) na 7.Anayeuza pombe na 8.Anayekula thamani yake na 10. Anaye nunuliwa pombe" (6) 
Ewe ndugu yangu, pengine unaweza kujiuliza: Nini maana ya laana? Maana ya laana ni kutengwa na rehema za Mwenyezi Mungu. Je, unaridhia ndugu yangu kutengwa na rehema za Mola wako? Tunamuomba Mwenyezi Mungu atulinde na hilo. 
3. Kwa kulikata ovu hili katika mizizi yake, sheria ya Kiislamu imempangia adhabu mnywaji pombe. Hilo limetajwa katika Hadithi ya Anas, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, anayesimulia kuwa Mtume alipelekewa mtu aliyekunywa pombe na kumchapa kwa bakora mbili viboko arobaini. Pia alifanya hivyo Khalifa Abubakar. Ulipokuja utawala wa Khakifa Umar, aliwashauri Sahaba na Abdulrahman bin Auf alimweleza Umar kuwa adhabu ndogo zaidi ni viboko thamanini (80), na hivyo Umar akaamuru kuwa mnywaji pombe achapwe viboko thamanini (80).(7) 
4. Sheria ya Kiislamu imeharamisha kiwango kichache katika kileo [hata kama hakileweshi], iwapo kiwango kikubwa katika kileo hicho kinalewesha. Sahaba Jabir anasimulia kwamba Mtume amesema kuwa: "Kitu ambacho kingi chake kinalewesha, basi kichache chake ni haramu"(8) 
 
MADHARA YA ULEVI 
Ulevi una athari na madhara mengi ambayo si rahisi kuyataja yote katika kurasa hizi chache. Vitabu na vijarida vimeandikwa na utafiti mwingi umefanywa mashariki na magharibi. Yanayogunduliwa kila wakati yanaonesha wazi hatari ya jambo hili na athari zake mbaya. Haya yanaonesha utukufu wa sheria ya Kiislamu pale ilipoliharamisha ovu hili na kuikata mizizi yake. 
i.Athari ya kwanza na hatari zaidi kwa Mwislamu ni athari katika imani. Maasi yanaathiri imani ya Mwislamu na hivyo imani yake inapungua na moyo wake unakuwa na giza. Iwapo ni hivyo, hebu jiulize: Hali yako itakuwaje iwapo maasi hayo ni katika madhambi makubwa? Aidha jiulize: Hali yako itakuwaje iwapo anayefanya maasi hayo ameahidiwa kupata laana? 
ii. Athari ya pili ya ulevi ni kwa mnywaji mwenyewe. Kileo kina madhara makubwa ya kimwili kwa kila sehemu ya mwili wa mnywaji na kina sumu inayoathiri moja kwa 
moja kwenye mfumo mzima wa mwili. Aidha, madhara ya ulevi yanafika kwenye chembe chembe za mfumo wa ngozi na kwenye viungo vinavyohusika na utengenezaji wa nishati; viungo ambavyo vinapoteza uwezo wake wa kufanya kazi ndani ya saa ishirini na nne (24) tangu kunywa funda la kwanza la pombe. 
Pombe inadhuru hususan moyo ambao baada ya muda unabadilika na kuwa mkusanyiko wa manyavunyavu yaliyokufa, yasiyojikunja na yasiyofanya kazi yake. Hali hii huishia kwenye kushuka kwa mapigo ya moyo na hatimae kifo. Aidha pombe husababisha vidonda vya koo vinavyonuka na ambavyo vinaweza kusababisha kifo baada ya saa ishirini na nne (24) tangu kuanza kwa dalili zake iwapo havitotibiwa haraka. 
Ama uhusiano wa ulevi na ugonjwa wa saratani (cancer) sema upendavyo. Ulevi una uhusiano mkubwa na saratani ya tumbo, saratani ya umio (eusophagus), saratani ya ini (kidney) n.k. Maafa makubwa zaidi ni kudhurika kwa tindikali ya DNA (Deoxyribonucleic Acid); tindikali ya ajabu amabayo ndiyo siri ya uhai na ambayo inabeba sifa za urithi kutoka vizazi na vizazi. Pamoja na hayo kuna magonjwa mengine mengi kama kupumbaa kwa chembe chembe za ubongo, kuvuja damu kwa umio, tumbo, utumbo mwembamba (small intestine), kunyambuka kwa ini, upungufu wa damu, kifua kikuu, vidonda vya mapafu na magonjwa mengine mengi. Mara nyingine mnywaji pombe huwa anapatwa na hali inayojulikana kama Kichaa cha Ulevi ambapo mtu anapoteza kabisa uwezo wa kujidhibiti na hivyo kulazimika kunywa zaidi na zaidi hadi kupoteza fahamu ambapo anaweza azinduke au asizinduke. 
iii. Athari ya tatu ya ulevi ni kwa jamii. Hapa tutatosheka kutaja takwimu za baadhi ya matukio yaliyo sababishwa na ulevi. 
1. Mwaka 1968 theluthi moja (1/3) ya matukio ya kujinyonga au ya kutaka kujinyonga yaliyotokea ulimwenguni yalisababishwa na ulevi. 
2. Mwaka 1980 asilimia themanini na sita (86%) ya makosa ya jinai yakiwemo ya kuua, na asilimia hamsini (50%) ya matukio ya uporaji na kutumia nguvu yalisababishwa na ulevi (WHO). 
3. Mwaka 1976 madhara ya ulevi yalisababisha ajali za barabarani kama ifuatavyo: 
* Nchini Marekani asilimia sitini na saba 67% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi. 
* Nchini Ufaransa asililmia arobaini na sita 46% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi. 
* Nchini Australia asilimia hamsini 50% ya ajali za barabarani zilisababishwa na ulevi. 
4. Matatizo ya kifamilia na ya kikazi. Nadhani kisa kilichotajwa mwanzo wa makala hii kinatosha kuwa ni ushahidi. 
5. Hasara za kiuchumi kwa mtu binafsi na kwa taifa: 
* Hasara za kiuchumi nchini Marekani kwa mwaka ni dola za Kimarekani milioni elfu arobaini na tatu( $43,000,000,000). 
* Hasara za kiuchumi kwa mwaka nchini Australia ni dola milioni elfu moja na mia moja ($1,100,000,000). 
 
HITIMISHO 
Je, katika ulevi kuna faida? Je, inafaa kutumia pombe kama dawa? Mtume, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani, alikwisha yajibu maswali haya pale aliposema kuwa: "Hakika, Mwenyezi Mungu hakufanya dawa yenu katika vitu alivyoviharamisha kwenu" (9) Aidha huyu hapa Taariq bin Suwaid, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, anamuuliza Mtume kuhusu pombe anayoitengeneza kwa ajili ya dawa, na Mtume anamjibu kwa kusema:"Hiyo(pombe ) sio dawa bali ni ugonjwa" (10) 
Ama aya ya Qurani isemayo kuwa "Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema, katika pombe na kamari kuna dhambi kubwa na manufaa kwa watu na dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake" (11) 
Aya hii inamaanisha kwamba katika pombe kuna manufaa. Tunasema kwamba manufaa yaliyotajwa katika aya hii ni ya kiyakinifu (material benefits) kabla ya pombe kuharamishwa. Ama baada ya pombe kuharamishwa haifai kuiuza wala kuinunua achilia mbali kuinywa.Pia pato lake ni haramu. Iwapo Mtume anasema kuwa pombe ni ugonjwa je, sisi tuitumie kama dawa? Sayansi za kisasa zimethibitisha kwamba hakuna faida zozote za kiafya katika pombe bali kinyume chake ni kwamba kuna madhara kama tulivyotangulia kutaja. 
Nataraji kuwa jambo hili tumeliweka wazi. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe sisi na nyinyi uwezo wa kufuata amri zake, kuyaacha aliyotukataza na kukoma aliyotukemea. JE, MMEKOMA? 

REJEA: 
(1) Sura Bani-Israil 17, aya 70. 
(2) Ameipokea Hadithi hii Imam Ahmad na Abudaud. 
(3) Ameipokea Hadithi hii Imam Muslim. 
(4) Sura Al-Maaidah 5, aya 90-91. 
(5) Ameipokea Hadithi hii Imam Muslim. 
(6) Ameipokea Hadithi hii Imam Tirmidhiy na Ibn- Maajah 
(7) Ameipokea Hadithi hii Imam Bukhariy na Muslim. 
(8) Ameipokea Hadithi hii Imam Ahmad, Tirmidhiy na An-Nasai 
(9) Ameipokea Hadithi hii Imam Bayhaqiy 
(10) Ameipokea Hadithi hii Imam Muslim. 
(11) Sura Al-Baqarah 2, aya 219

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget