Ibnul Qayyim ametaja mambo mane ambayo yataweza kumsaidia sana mja ikiwa atayafuata na kuweza kushindana na nafsi yake kwa msaada wa Allah (Subhaanahu Wata’ala).
(a) Kuiwajibisha nafsi
Nafsi ya mja huharibika kwa sababu ya kuachwa tu bila ya kuwajibishwa. Ni wachache ambao hutafuta muda na kuzifikiria nafsi zao. Mja hujiuliza: Nini nimekusudia kutumia neno fulani. Je vipi ule ushauri nilioutoa katika kuwaamrisha watu wema na kuwakataza mabaya. Je maneno niliyoyatamka yalikuwa kwa ajili ya Allah? Au kwa ajili ya kuonekana kama msemaji mzuri tu? Nini nnataka kwenye matendo yangu, ikiwa ni sala, zaka, saumu na nini ninataraji kutoka kwenye matendo yangu haya. Je nnataraji radhi za Allah(Subhaanahu Wata’ala na malipo au ni kujionesha tu?
Ni muhimu kuiwajibisha nafsi kwake kila neno, tendo na hata wakati wa mapumziko. Takriban ni kwa kila jambo ambalo mja analifanya je ana matarajio gani nalo na kwa nini analifanya. Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) anasema :
الكيس من دان نفسه، وعمل لما بعد الموت، والعاجز من أتبع نفسه
هواها، وتمنى على الله
رواه البيهقي والترمذي وابن ماج
‘Mtu mwenye akili ni yule anaedhibiti nafsi yake (anawajibisha) na kutenda (kujiandaa) kwa yale yatakayokuja baada ya mauti na Ajizi ni yule anaefuata matamanio ya nafsi yake na huku anatamani kwa Allah ’
Al bayhaqiy, Attirmidhiy na Ibn Majah
Maneno haya ya busara yanatosha kuwa ukumbusho wa kila nafsi ya mja kuiwajibisha hasa kwa kuzingatia yatakayokuja baada ya mja atakapoondoka katika ulimwengu huu. Kila tendo au jambo atakalolifanya mja anapaSubhaanahu Wata’alaa kuliangalia kwa mtazamo huu je! Litakuwa na faida na mimi nikishakufa? Litanisaidia huko niendako au litaniumbua?
Kutoka kwa Imam Ahmad : Umar Ibnul Khattaab(R.A) amesema:
" حاسبوا أنفسكم قبل أن تحاسبوا ، وزنوا أعمالكم قبل أن توزنوا ، فإن أهون عليكم في
اليوم الحساب غدًا أن تحاسبوا أنفسكم
(رواه الترمذي)
.
“Ziwajibisheni nafsi zenu kabla hazijawajibishwa na zipimeni amali zenu kabla hazijapimwa kwani itakuwa rahisi kwenu kuwajibishwa kesho (akhera) tuendako endapo nyinyi wenyewe mtaziwajibisha leo…..”
Attirmidhiy
Hapa nafsi pia inaweza kujiuliza kama imewahi kumuomba Allah(Subhaanahu Wata’ala) kuikinga na moto ?, imewahi kumshukuru Allah(Subhaanahu Wata’ala) kwa neema alizomjaalia?, imewahi kughadhibika kwa ajili ya Allah(Subhaanahu Wata’ala)? Imetekeleza sala za ziada (Sunna) kwa ajili ya kujipendekeza kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala)? Imeweza kujiepusha na kibri na kujiona? na mengi mengineyo na huku ndiko kuifanyia nafsi muhasaba .
Ni nafsi ngapi zinawaongoza waja kwenye gharika? Nafsi huingiwa na kiza kinene mpaka kushindwa kabisa kudhibitika na huku mja anazidi kupotea na kula hasara kwa kutokuwa kiongozi wa nafsi yake na badala yake kuwa mfuasi limbukeni. Mja anatakiwa awe kiongozi, mtawala, dikteta, fashisti wa nafsi ili aweze kuidhibiti kwani nafsi haitaki demokrasia wala nasaha kwani ukiipa shubiri inachukuwa pima. Ukiifungulia mlango huu ndio unaipa nafasi ikuendee kinyume.
Ianze kazi hii ndugu yangu Muislamu, kwani imani inapungua na nafsi inadhoofika kwa wingi wa kupambana na matamanio ya dunia pamoja na mitihani mbali mbali, na utakapoiacha nafsi bila kuiwaidhi na kuirudi, basi itaachana na wewe na kupotea. Na ni wewe peke yako unayeweza kuiokoa.
Rudi haraka kwa Mola wako usije ukaingia katika wale Allah(Subhaanahu Wata’ala) anaosema juu yao; Al Kahf / 28
وَلاَ تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا
" Na wala usiwatii wale ambao tumezighafilisha nyoyo zao wakafuata matamanio yao, na mambo yao yakawa yamepita mipaka."
(b) Kutoikubalia nafsi matakwa yake.
Kuidhibiti nafsi kunahitaji mja kwenda dhidi ya kila inaloamrisha. Kumbuka nafsi huamrisha maovu. Njia pekee ni kutoruhusu matakwa na matamanio yakuvae na kukuchanganya. Pale nafsi unapoikubalia kila inachokitamani; unaipa nafsi murua wa kukutawala.Annaaziaat /40-41
فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِىَ الْمَأْوَى وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَى
Na yule mwenye kuogopa kusimamishwa mbele ya mola wake na akaikataza nafsi na matamanio (yake) basi hakika pepo ndiyo makaazi yake.
Kuweza kuidhibiti nafsi na matamanio yake si jambo rahisi na linahitaji msukumo wa hali ya juu. Msukumo huu upo katika kujizuia kula mpaka kuvimbiana au kufanya israfu, kuyadhibiti macho yasighurike na dunia zaidi kwa kutamani kila inachokiona, kuchanganyika na makundi yasiyo na mwelekeo na mengi mengineyo.
Mtume Muhammad (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) anasema katika hadithi iliyotolewa na Abu Dharr Allah amuwie radhi
أفضل الجهاد أن يجاهد الرجل نفسه وهواه
رواه الديلمي وغيره
“Jihadi iliyo bora ni pale mja anakapopigana na nafsi yake na matamanio yake”
Imesimuliwa na Addaylami na wengineo
Na sheikh Albani anasema ni sahihi ( assilsila Assahiha 1496)
Yote hayo na mengineyo yataweza kufanyika endapo mja atakuwa tayari kushindana nayo kwa yale yaliyokuwa yanaenda kinyume na matakwa ya nafsi yake. Kwa mfano kama mja amejiona ni mpenda kula basi na aitumie fursa ya kufunga. Kuna funga nyingi za sunna ambazo zitaisadia nafsi kudhibitiwa na papo papo kupata thawabu. Hali kadhalika fursa ya kusimama usiku kwa kusali tahajjud humzuia mja kuuendekeza usingizi na pia kupata thawabu kwa ibada hii adhimu. Sala za usiku na funga wakati wa mchana ni baadhi tu ya silaha madhubuti za kupigana na nafsi mpaka isalimu amri.
MATAMANIO | KINGA | FAIDA |
Kula kusikokuwa na mpaka | Funga za Sunna | Kutekeleza Sunna, Afya na nafsi kutoyumba |
Kulala kusikokuwa na kiasi | Sala za usiku | Kutekeleza sunna na nafsi kudhibitiwa |
Maongezi yasiyokuwa na maana | kunyamaza | Kuwa mtu wa busara |
Kutazama yasiyo na maana | Kuinamisha macho | Kutii amri ya Allah (Subhaanahu Wata’ala) na Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) |
Riyaa | Kuwa na ikhlasi | Kuwa radhi na Allah na Allah kukuridhia |
Kujisahau kumkumbuka Allah (Subhaanahu Wata’ala) ni moja katika mikakati ya shetani dhidi ya mja. Huisahaulisha nafsi katika dhikri (kumtaja Allah) kwani shetani anaelewa kwamba dhikri ndiyo ngome iliyomshinda kuivunja. Hivyo hufanya mbinu zote kuisahaulisha nafsi na kuiweka mbali katika kumkumbuka Allah (Subhaanahu Wata’ala).Arraad/28
الَّذِينَ ءَامَنُواْ وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُمْ بِذِكْرِ اللَّهِ أَلاَ بِذِكْرِ اللَّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ
Wale walio amini na zikatulia nyoyo zao kwa kumkumbuka Allah. Hakika kwa kumkumbuka Allah ndio nyoyo hutulia!
Ndio maana Allah (Subhaanahu Wata’ala) pamoja na Mtume wake Muhammad (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) wametuwekea mpangilio madhubuti wa kumkumbuka kwa dua tofauti. Kwa mfano kuna dua za asubuhi, jioni, kuingia na kutoka nyumbani, wakati wa kulala na kuamka, kuvaa nguo, kuanza na kumaliza kula na kadhalika. Hata pale mja anapoingia chooni basi kuna dua za kujikinga na anapotoka za kumshukuru.
Kila mja anaelewa vyema nafsi yake na kitu gani inahitaji na kukitamani. Hivyo ni muhimu kuiwekea vikwazo ili kuonesha kwamba si kila ikitamanicho nafsi hupata. Lakini hali halisi ni kwamba watu wengi wamekuwa wakarimu mno wa nafsi kwa kila inachokitaka na hata isichokitaka.
(c) Kuipa subira nafsi katika kumtii Allah (Subhaanahu Wata’ala)
Subira ni silaha ambayo kila mwenye kupigana na nafsi anatakiwa ajilazimishe kuwa nayo.
Kuipa subira nafsi katika kumtii Allah (Subhaanahu Wata’ala) ni jambo linalohitaji kutazamwa vizuri kwani nafsi, kwa mfano, hukimbia baadhi ya ibada kwa sababu ni miongoni mwa vitu isivyovitaka. Mja hutokwa na hamu ya kufanya ibada na badala yake kujiona mzito kila tendo la ibada linapobidi.
Moja katika mambo hayo ni uvivu. Uvivu katika kutekeleza sala, kutoa zakka na hata funga. Mja anaweza kuacha tu kusali huku akielewa ni wajibu kwake na kukataa kutoa zaka licha ya kuwa na uwezo na hapa nafsi huchekelea kwani tayari imepata lengo lake. Wakati nafsi inajua kwamba sala ni fardhi inayojirudia mara tano kila siku na hivyo kutakikana subira na uvumilivu katika kuitekeleza kama anavyotubainishia Allah (Subhaanahu Wata’ala) katika Al baqarah /45
وَاسْتَعِينُواْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلَوةِ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلاَّ عَلَى الْخَـشِعِينَ
Na jisaidieni katika kusubiri na kwa kusali kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu.
Kushindana na nafsi ni kama mfano wa vita vyovyote vile. Ndani yake kuna majaribu na mitihani aina kwa aina. Pale ambapo wakati wa sala umewadia ndio kuna mchezo mzuri kwenye TV na huko tayari kuukosa. Unapotaka kutoa Zakka unakumbuka nyumba zulia linataka kubadilishwa n.k . Unataka kusali sala za usiku unakumbushwa kuna mechi kali utaikosa au kama ni mfanya kazi wa usiku (night shift) hivyo tayari muda huo huna tena..
Allah anatukumbusha katika Quraan Al – imraan
وَإِن تَصْبِرُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ ذلِكَ مِنْ عَزْمِ الاٍّمُورِ
Lau kama mngelisubiri na kumuogopa Allah hakika hayo ni katika mambo makubwa ya kuazimia mtu kuyafanya.
Ndiyo maana mja anao uwezo na haja ya kufunga sunna lakini hatofanya hivyo kwani nafsi yake inamsuta. Mwengine anafunga sunna bila ya kuwa na haja ya kufanya hivyo kwani nafsi yake ameiweza. Kwani matendo ya sunna ni kuitika wito wa Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na kujipendekeza kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) kwa kufanya ziada ya iliyoamrishwa.
Hivyo, subira ni lazima ziende sambamba na matendo ya ibada ili kupata daraja ya juu ya uvumilivu kama alivyoyaeleza hayo Sheikhul Islam Ibn Taymiyah na Ibnul Qayyim.Wanasema:
“Bila ya shaka kuwa na subira katika kutii hupatikana kwa kutekeleza tendo la utiifu na kulilinda na kulidumisha (katika kutekeleza)”
Uthibitisho huu tunauona ndani ya Quraan Al Maarij 23 na 34.
الَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلاَتِهِمْ دَآئِمُونَ
Ambao wanadumisha Sala zao
وَالَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلاَتِهِمْ يُحَافِظُونَ
Na ambao wanazihifadhi Sala zao.
Hata hivyo, ni wachache miongoni mwetu wanaweza kufanya. Kwani nafsi zetu baada ya muda tu huchoshwa na ibada na kutokuwa tena na hamu ya kuifanya mara nyengine. Licha ya Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kutukumbusha pale aliposema:
“Amali iliyo bora kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) ni ile inayodumu hata kama ni kidogo.”
Ndio maana Mtume Muhammad (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akamuasa Abdullah bin Umar (Allah amuwie radhi) pale alipomwambia:
“Usiwe kama fulani alikuwa akisimama (kwa kusali) usiku kisha akaacha”
Subira na uvumilivu katika kutekeleza amali za kumtii Allah (Subhaanahu Wata’ala) ni nguzo muhimu ya kuweza kuidhibiti nafsi na kuzidumisha amali zenyewe ni mwongozo ambao kila nafsi ikifuata asaa itajikuta iko chini ya amri za mja badala ya kuwa juu yake.
Allah (Subhaanahu Wata’ala) anasema katika Quraan Muhammad / 31
وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّى نَعْلَمَ الْمُجَـهِدِينَ مِنكُمْ وَالصَّـبِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَـرَكُمْ
“Na bila ya shaka tutakujaribuni mpaka tuwadhihirishe wapiganao Jihadi katika nyinyi na wanao subiri. Nasi tutazifanyia mtihani khabari zenu.”
( d ) Kuipa subira katika kujiepusha na kumuasi Allah(Subhaanahu Wata’ala)
Hii ina maana mja anaiwajibisha nafsi yake na kuhakikisha kwamba iko mbali sana na maasi kwani vishawishi na vijisababu vya hayo ni vingi. Na Kama katika moja ya hadithi za Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) zinabainisha jinsi pepo ilivyajaa mambo yenye kuchukiza na jinsi moto ulivyojaa mambo yenye kutamanisha . Sasa ikiwa subira na uvumilivu havipo katika kujiepusha na matamanio ya nafsi basi nafsi ya mja huwa karibu sana na moto
Moja ya sababu hizo ni ujana. Vijana kike kwa kiume wanafahamika vyema kupenda raha na anasa za huu ulimwengu au kama usemi wa kiSubhaanahu Wata’alaahili wako kwenye baleghe changa na baleghe hii hutumiwa kama leseni ya kufanya maasi na vijana.
Vishawishi kama tulivyosema ni vingi na rahisi kuvitaja vyote lakini nafsi tayari Allah (Subhaanahu Wata’ala) aliipa uwezo wa kutambua ovu na jema kama anavyosema katika As Shamsi/ 7-8 :
فَأَلْهَمَهَا فُجُورَهَا وَتَقْوَاهَا وَنَفْسٍ وَمَا سَوَّاهَا
Na kwa nafsi na aliyeitengeneza ,Kisha akifahamisha uovu wake na wema wake.
Mifano hii michache
KISHAWISHI | DAWA | KINGA | BADALA |
Kutanga tanga kwa macho | Kuinamisha macho | Waja kujistiri kujiepusha na sehemu zenye hatari za macho | Kutazama yenye faida, mihadhara, michezo yenye mafundisho ya kiislamu n.k |
Kusikiliza | Kuacha kusikiliza yasiyo na maana | Kujiepusha na vikao vibaya | Kusikiliza yenye manufaa Quran, mawaidha, kasida n.k |
Tamaa na uchu | Kuacha kutamani | kukinai | Kushukuru kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) kwa kila tulichojaaliwa |
Mdomo | Kutoongea yasiyo na maana | Kama hakuna la maana kunyamaza | Kuongea mambo ya kheri na faida |
Usingizi | Kulala kiasi | Kuhakikisha kusali sala za isha na alfajiri jamaa | Kusimama usiku kwa ibada |
Mlo | Kula kiasi | Funga za sunna | Kula chakula cha roho,mawaidha, darsa na pia kula ikihitajika tu. |
No comments:
Post a Comment