Sala ni ibada ya pekee ambayo mja analazimika kuitimiza anapokuwa katika mazingira ya aina yoyote. Anapokuwa safarini, wakati wa hofu, anapokuwa mgonjwa na hata anapokuwa vitani.
Mwenyezi Mungu anasema;
“Zilindeni Sala, na khasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).
Ikiwa mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapo kuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyo kufunzeni yale mliyo kuwa hamyajui”.
Al Baqarah – 238-239
Na akasema
“Na unapo kuwa pamoja nao (vitani), ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo maliza sijida zao, basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo halijasali, lisali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio kufuru wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni SALA kama dasturi. Kwani hakika SALA kwa Waumini ni FARADHI iliyo wekewa nyakati maalumu”.
Annisaa – 102-103
Mwenyezi Mungu amewakemea sana wale wanaojaribu kuipuuza ibada hii tukufu na kufuata matamanio ya nafsi zao.
Mwenyezi Mungu akasema;
“Lakini wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha SALA, na wakafuata matamanio. Basi watakuja kupata malipo ya ubaya”.
Maryam – 59
Na akasema
“Basi, ole wao wanao sali,
Ambao wanapuuza Sala zao”.
Maaun – 4-5
Kutokana na umuhimu wa ibada hii, Nabii Ibrahim (AS) alimuomba Mola wake amjaalie yeye na vizazi vyake wawe wenye kuishika.
Mwenyezi Mungu anasema juu ya Dua ya Nabii Ibrahim;
“Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu”.
Ibrahim – 40
Katika aya nyingine Mwenyezi Mungu amesema;
“Lakini wakitubu na wakasimamisha Sala na wakatoka Zaka basi iacheni njia yao (waacheni huru), hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu”.
Suratut Tawba – 5
Na maana yake ni asiytubu na akakataa kusimamisha Sala na akakataa kutoa Zaka asiachwe huru.
Na katika Sura hiyo hiyo ya Attawba aya ya 11 Mwenyezi Mungu anasema;
“Kama wakitubu na wakasimamisha Sala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini”.
Na kinyume chake ni kuwa; Yule asiyetubu na akakataa kusimamisha Sala na akakataa kutoka Zaka, basi huyo si ndugu yetu katika dini.
No comments:
Post a Comment