Wednesday, April 4, 2012

Haki za binadamu katika Uislamu


HAKI za binaadamu ni kauli kuu iliyotanda katika pande nne za dunia. Amerika na nchi nyingi za Ulaya ya Magharibi ndiyo viongozi wa haki hizo. 
Kushiriki kwa nchi hizi hakutuhakikishii kuwa nchi hizi ni safi. Nchi hizi ni chafu kwa saabu zimeshiriki katika ukoloni, mauaji ya kutisha na kueneza au kudumisha mabaya katika jamii mbalimbali bila ya kujakli amri za Mwenyezi Mungu .
 Pia viongozi wake, hivi sasa wamejiweka katika nafasi ya upinzani dhidi ya Muumba wao. Ni bayana kuwa wanaipinga na kuikanusha Akhera na siku ya malipo. Wenye sifa ya namna hi hawawezi hasrani, kusimamia na kutetea haki za binaadamu.


MWENYEZI Mungu ametuumba, hivyo inatosha kusema yeye ndio mjuzi wa haki zetu hapa duniani. Hakusema katika vitabu vyake vitukufu kuwa binaadamu waamue haki zao za kijamii na yeye akajitoa. La hasha. Miongoni mwa vitabu vyake vilivyoweka wazi mambo haya ni Qur'an na ambayo imefafanuliwa katika Sunna za Mtume (s.a.w.). Ebu tuanze.


Haki ya kuishi
Maisha ya mtu ni haki takatifu na utu wa binadamu kimwili na kiroho wakati wa uhai wkae na baada ya kufa kwake kulindwa na sheria, hauwezi kuondoshwa bila kufuata taratibu zinazokubalika kisheria. Kama Mwenyezi Mungu anavyosema: "Ya kwamba atakayemuua mtu bila ya hatia ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya fisadi katika nchi, basi (hukumu yake) ni kama amewaua watu wote, na mwenye kumwacha mtu hai (kumsaidia kuishi) basi (hukumu yake) ni kama amewaacha hai watu wote". (5:32).


Haki ya uhuru
Haki ya mtu kuwa huru ni haki takatifu sawa na haki yake ya kuishi. Hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kuondosha haki hiyo bila ya kufuata taratibu za kisheria. Na Taifa lolote lina haki ya kutetea na kupigania haki ya uhuru wake kama Mtume (s.a.w.) anavyosema yakuwa: "Kila mtoto anazaliwa hali ya kuwa yeye ni huru wa kiasili na kimaumbile". Na kama Mwenyezi Mungu anavyosema: "Na wale wanaolipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, hao hakuna njia ya kulaumiwa. Bali lawama iko juu ya wale wanaodhulumu watu na wakawafanyia jeuri katika nchi (yao) pasipo haki; hao ndio watakaopata adhabu iumizayo". (42:41-42).


Haki ya usawa
Watu wote ni sawa mbele ya sheria, hakuna mtu yeyote aliye bora kwa sababu ya jinsia, kabila, ukoo, rangi, lugha au dini kama Mtume (s.a.w.) alivyosema yakuwa: "Nyinyi nyote mnatokana na Nabii Adamu ambaye ameumbwa kutokana na mchanga". Na kama Mwenyezi Mungu anavyosema yakuwa: "Enyi watu mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili moja; Nabii Adam)". (4:1).
Watu wanatofautiana katika kipato kwa sababu ya kujituma, elimu na kufanya kazi zaidi na kwa bidii kama Mwenyezi Mungu anavyosema yakuwa: "Na (viumbe) wote watakuwa na Daraja (madaraka) na vyeo mbalimbali na tofauti kwa yale waliyoyatenda". 46:19.


Haki ya kudai haki katika vyombo vya sheria
Kila mtu anayo haki ya kudai haki yake yoyote kwenye vyombo vya sheria kama Mwenyezi Mungu anavyosema yakuwa: "Na wahukumu baina yao kwa yale (sheria) aliyoteremsha Mwenyezi Mungu". (5:49)


Haki ya kutendewa uadilifu na vyombo vya sheria
Kutokutenda kosa ndio asili kwa mwanaadamu na mtu yeyote hawezi kuitwa hatiani kwa kosa bila kufuata taratibu za kisheria kama anavyosema Mwenyezi Mungu yakuwa: "Na sisi si wenye kuwaadhibisha (viumbe) mpaka tuwapelekee Mtume (awafahamishe yaliyo ya haki basi wakiyakataa ndipo wanapoangamizwa)". (17:15)


Haki ya kutodhalilishwa
Kila mtu anayo haki ya kutodhalilishwa na kiongozi yoyote au mamlaka yoyote ya dola bila kupatikana na hatia ya kufanya kosa na ushahidi wa nguvu na wa kweli kama Mwenyezi Mungu anavyosema: "Na wale wanaowaudhi (na kuwadhalilisha) waumini wanaume na waumini wanawake pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhambi kubwa na dhambi zilizo dhahiri". (33:58).


Haki ya kutokuteswa
Haifai kwa mtu yeyote au mamlaka yoyote ya dola kumuadhibu na kumtesa mtuhumiwa, mahabusu au mfungwa yeyote bila kufuata misingi ya kibinadamu na heshima ya utu wake ambao unalidnwa na sheria kama Mtume (s.a.w.) anavyosema yakuwa "Mwenyezi Mungu atawaadhibu wale wote ambao wanawaadhibu wenzao hapa duniani".


Haki ya kuheshimiwa
Kila mtu anayo haki ya kuheshimiwa kwa utu wake kama Mwenyezi Mungu anavyosema yakuwa: "Enyi mlioamini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, huenda wakawa bora kuliko wao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao, huenda wakawa bora kuliko wao, wala msitukanane kwa kabila, wala msiitane kwa majina mabaya (ya kejeli)". (49:11). Na kama Mwenyezi Mungu anavyosema ya kuwa: "Na hakika tumewatukuza wanaadamu na tumewapa vya kupanda barani na baharini na tumewaruzuku vitu vizuri na tumewatukuza kuliko wengi katika wale tuliowaumba, kwa utukufu ulio mkubwa (kabisa)". (17:70).


Haki ya ukimbizi
Mtu yeyote bila kujali dini yake, rangi yake au utaifa wake, anayo haki ya ukimbizi kwa kuhofia maisha yake kwa sababu ya vita, mateso au kwa sababu nyingine yoyote inayohatarisha usalama wake. Kama Qur'an tukufu inavyosema katika sura ya 9 aya ya 6. Yakuwa: "Na kama mmoja wa washirikina akikuomba umlinde (ili apate amani ya maisha yake na asikie maneno ya Mwenyezi Mungu) basi mlinde asikie maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha (asipoyakubali usimlazimishe wala usimdhuru, bali) mfikishe mahala pale pa amani; na haya ni kwa ajili ya kuwa hao ni watu wasiojua".


Haki ya jamii ya wachache
Jamii ya watu wachache katika Taifa lolote ina haki kamili na uhuru wa kuabudu na kufuata kanuni za dini zao katika mambo yao ya kifamilia kama Mwenyezi Mungu anavyosema katika Qur'an 5:43: "Na watakuwekaje wewe kuwa hakimu nao wanayo Taurati yenye hukumu za Mwenyezi Mungu? Kisha baada ya hayo wanageuka (unapowahukumu). Na hao si wenye kuamini (lolote, bali tu wanafanya khadaa kwa kutoamini unayowahukumu).


Haki ya kushiriki katika maisha ya umma
Kila mtu anayo haki ya kujua mambo na matukio yanayotokea katika nchi yake na mambo yanayohusu maslahi ya umma, na anayo haki ya kutoa mchango wake kulingana na uwezo wake na kipaji chake, na kila mtu katika Taifa lake anayo haki ya kushika nafasi za kazi mbalimbali za uongozi kwa taratibu, sifa za uongozi bila kujali dini ya mtu, kabila, rangi, lugha au ubaguzi wa aina yoyote.
Wananchi wanayo haki ya kuchagua viongozi wanaoona wanafaa kuongoza bila kulazimishwa, na wanayo haki yakuwawajibisha viongozi ambao watakwenda kinyume na sifa za uongozi kulingana na taratibu zilizowekwa. Kama Mwenyezi Mungu anavyosema katika Qur'an 4:2 yakuwa: "Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri, (yaani msichague cha haramu), kisicho na manufaa (kisicho na sifa nzuri), Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika (yote) hayo ni jukumu kubwa".


Haki ya uhuru wa mawazo na kufikiri
Kila mtu anayo haki ya uhuru wa mawazo na kufikiri na kutoa maoni yake bila ya kulazimishwa na mtu au mamlaka yoyote ya dola bila ya kukiuka sheria na taratibu zilizowekwa na nchi, na kila mtu anayo haki ya kueneza na kusambaza taarifa au habari sahihi ikiwa kufanya hivyo hakutohatarisha amani ya nchi na usalama wa Taifa.
Kama Mwenyezi Mungu anavyosema ya kuwa: "Na linapowafikia jambo lolote la amani au la hofu hulitangaza. Na kama wangali lipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka kwao, wale wanaopeleleza (wanaojua kupima mambo) miongoni mwao wangalijua (kuwa hilo ni jambo la kutangazwa au si la kutangazwa". 4:83.
Uhuru wa mawazo na kufikiri, hairuhusiwi kwa mtu yeyote kwa nia ya kudhalilisha au kukejeli dini na imani za watu wengine kama Qur'an tukufu inavyosema katika sura ya 6 aya ya 108: "Yakuwa wala msiwatukane (wala msiwadhalilishe wala kuwakejeli) wale (wote) ambao wanaabudu, kinyume cha Mwenyezi Mungu, wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri zao bila kujua. Namna hivyo tumewapambia kila watu vitendo vyao. Kisha marejeo kwa Mola wao. Naye atawaambia (yote) waliyokuwa wakiyatenda".


Uhuru wa kuabudu
Kila mtu anayo haki ya kuamini na kuabudu kwa mujibu wa dini yake kama Mwenyezi Mungu anavyosema yakuwa: "Nyinyi mna dini yenu na nami nina dini yangu". (109:6).


Haki ya kutangaza na kueneza dini
Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika kutangaza na kueneza dini yake, yeye peke yake au kushirikiana na waumini wenzake, anayo haki ya kuanzisha taasisi na mashirika ya dini, na anayo haki ya kutumia nyenzo mbalimbali za kueneza dini kama Mwenyezi Mungu anavyosema ya kuwa: "Sema: Hii ndiyo njia yangu; ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa Busara (na ujuzi wa kweli); Mimi (nafanya hivi) na kila wanaonifuata". 12:108.
Vile vile kila mtu anawajibika kuamrisha mema na kukataza mabaya na kutaka jamii kuamrisha utekelezaji wa majukumu haya kwa njia ya kushirikiana kama Mwenyezi Mungu anavyosema katika Qur'an 16:90 ya kuwa: "Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na kufanya hisani, na kuwapa jamaa (na wengineo) na anakataza uchafu, uovu na dhuluma. Anakunasihini ili mpate kufahamu (mfuate)".

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget