Wednesday, April 4, 2012

Tunazingatia Matukio Yanayotokea Ulimwenguni?


 Sample Image

Lilipojitokeza tukio la moshi/ wingu, ukungu lililotanda katika sehemu za Ulaya (Volcanic ash) na kuzuia safari za ndege kwa muda na Mashirika mengi ya ndege kusikitika kwa kula hasara je kama ni Waislamu tuliwahi kufikiria kama moshi/ukungu huu ndio mojawapo katika zile alama za kiama ambazo Mtume wetu Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam alituelezea? Au tulichukulia tu kama ni mojawapo ya mambo ya kawaida kutokea?

Hii inawezekana kwa sababu ya jinsi matukio yanavyoripotiwa katika vyombi vya habari vya nchi ambazo hazina fikra kama wlivyo Waislamu.

 

Tujikumbushe Hadithi ya Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam alipowakuta baadhi ya Masahaba wakiulizana kuhusu siku ya kiama na Mtume akawauliza Masahaba : “Ni jambo gani mnazungumzia?”. Wakasema: “Tunazungumzia siku ya  kiama.” Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam akasema: “Hakitokuja mpaka mzione ishara kumi.” Na akaelezea kuja kwa moshi (ukungu), Dajjaal,  kutokea kwa mnyama, kutoka Jua kutoka magharibi, kuteremshwa kwa Isa mwana wa Maryam, kuja kwa Yaajuj na Maajuj, kuzama kwa ardhi katika maeneo matatu moja mashariki, moja magharibi na moja katika bara arabu na kisha moto utaunguza kuanzia Yemen na kuwafanya watu wakusanyike katika sehemu ya mkusanyiko.  Muslim

 

Hadithi hii inatupa picha ya kuweza kujua alama za siku ya kiama ila katika dunia hii ya leo vipi kama ni Waislamu matukio yanayojitokeza huwa tunayachukulia katika mtazamo upi kwani katika ulimwengu uliopo hakuna tena jambo geni kwani kila kitu kikitokea kinatekwa na vyombo vya habari huku kila kimoja kikiwa na ajenda yake kukitangazia.

 

Tumeweza kutanabahi kwamba alama hizi zitakuja na kuondoka na wengi miongoni mwetu tutazichukulia kama ni jambo la kawaida. Ila tukumbuke kitu kimoja muhimu kwamba tayari alama hizi tumeshapewa taarifa nazo takriban karne 14 zilizopita na hatutokuwa tena na taarifa nyengine kutoka kwa Allah Subhaanahu Wata’ala au Mtume wake Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam bali ni wajibu wetu kama ni Waislamu yanapotokea matukio kama haya tuyaangalie kwa mujibu wa dini yetu na  kuweza kuyaweka katika mizani je ndiyo mojawapo wa zile alama tulizoambiwa?

Tusije tukawa tumeshamezwa na kasumba ya michezo ya Sinema inayobeba majina makubwa ya siku ya siku na hivyo akili zetu kujengewa dhana nyengine juu ya siku ambayo haitomfaa mtu mali wala watoto siku ambayo mtu atamkimbia ndugu yake na baba yake na mama yake pamoja na mke wake na mtoto wake kwani kila mmoja siku hiyo atakuwa na jambo linalomshughulisha.

Simaanishi moshi huu ni mojawapo wa alama hizo bali najaribu tu kuwazindua Waislamu wenzangu kwamba yanapotokea matukio kama haya tujaribu kuyapima kama ni miongoni mwa zile alama za siku ya kiama tulizokwisha tanabahishwa nazo ili tuweze kuzingatia.

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget