Mwenyezi Mungu S.W.T. kawaumba Majini kwa lengo lile lile alilowaumbia binadamu, yaani kwa ajili ya ibada yake. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Surat Dh-Dhariyaat aya ya 56, “
]وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالإِنسَ إِلاَّ لِيَعْبُدُون[
Maana yake, “Sikuwaumba Majini na watu ila wapate kuniabudu.”
Na kama vile binadamu alivyokalifishwa kufuata amri na kuacha makatazo ya Mwenyezi Mungu ndivyo hivyo na Majini pia, na wao wanahisabiwa na watalipwa kwa vitendo vyao. Kati yao yule atakae muasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake S.A.W. ataadhibiwa na kuingizwa Motoni, na yule atakayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake S.A.W. atalipwa mema na kuingizwa Peponi.
Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil An`aam aya ya 128 mpaka 130, “
]وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا يَامَعْشَرَ الْجِنِّ قَدْ اسْتَكْثَرْتُمْ مِنْ الإنسِ وَقَالَ أَوْلِيَاؤُهُمْ مِنْ الإنسِ رَبَّنَا اسْتَمْتَعَ بَعْضُنَا بِبَعْضٍ وَبَلَغْنَا أَجَلَنَا الَّذِي أَجَّلْتَ لَنَا قَالَ النَّارُ مَثْوَاكُمْ خَالِدِينَ فِيهَا إِلاَّ مَا شَاءَ اللَّهُ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ * وَكَذَلِكَ نُوَلِّي بَعْضَ الظَّالِمِينَ بَعْضًا بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ * يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالإنسِ أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِنْكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَذَا قَالُوا شَهِدْنَا عَلَى أَنفُسِنَا وَغَرَّتْهُمْ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَشَهِدُوا عَلَى أَنفُسِهِمْ أَنَّهُمْ كَانُوا كَافِرِينَ[
Maana yake, “Na (wakumbushe) siku atakapowakusanya wote, (awaambie) “Enyi makundi ya Majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanadamu.” Na marafiki zao katika wanadamu (watawagombania) waseme: “Mola wetu! Tulinufaishana sisi na wao. Na tumefikia muda wetu uliotuwekea.” Basi (Mungu) atasema: “Moto ndio makazi yenu, mtakaa humo milele ila apende Mwenyezi Mungu (kuwarehemu); hakika Mola wako ni Mwenye hekima na Mwenye kujua. Na vivi hivi tunawatia mapenzi baadhi ya madhalimu juu ya wengine (wakapiganiana) kwa sababu ya yale waliokuwa wakiyachuma (kwa pamoja). “(Siku ya Kiyama wataambiwa): “Enyi makundi ya Majini na wanadamu! Jee, hawajakukujieni Mitume miongoni mwenu kukubainishieni Aya Zangu na kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii ya leo?” Nao watasema “Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu (kuwa sisi wabaya)” Na yaliwadanganya maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa makafiri.”
Katika aya hizi kuna dalili zilizo wazi ya kuwa Majini pia wamefikishiwa ujumbe wa dini ya Mwenyezi Mungu na kwamba amewaendea mjumbe wa kuwahadharisha.
Naye ni Mtume S.A.W. Na kwa vile wao pia wanahisabiwa basi wote katika wao watakaoasi wataadhibiwa katika Moto wa Jahannam. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil A`araaf aya ya 38, “
]قَالَ ادْخُلُوا فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِكُمْ مِنْ الْجِنِّ وَالإِنسِ فِي النَّارِ…[
Maana yake, “Atasema (Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama awaambie): “Ingieni Motoni pamoja na umma zilizopita kabla yenu; za Majini na Watu…” Na pia kasema katika Suratil A`araaf aya ya 179, “
]وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِنْ الْجِنِّ وَالإِنسِ…[
Maana yake, “..Na tumeiumbia Moto wa Jahannam Majini wengi na Watu.” Na pia kasema katika Suratis Sajda aya ya 13, “
]لأَمْلأَنَّ جَهَنَّمَ مِنْ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ[
Maana yake, “Kwa yakini Nitaijaza Jahannam kwa wote hawa; Majini na Watu (ambao ni wabaya).” Na kama vile Majini waasi wataadhibiwa basi na wale Majini Waislamu waliosimama katika haki watalipwa ujira mwema na kuingizwa Peponi.
Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema Suratir Rahmaan aya ya 46 mpaka 47, “
]وَلِمَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ جَنَّتَانِ * فَبِأَيِّ آلاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ[
Maana yake, “Na mwenye kuogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake atapata mabustani (Pepo) mbili. Basi nyinyi viumbe namna mbili (binadamu na Majini) ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha (kuwa si kweli) ?” Na khutuba hapa ya Wanadamu na Majini ni kwa sababu maneno yaliyo katika Sura na katika aya iliyopita ni Mwenyezi Mungu kumhakikishia Jini Mwislamu kuwa ataingia Peponi.
MTUME MUHAMMAD (S.A.W.) ALIWEZA KUONANA NA MAJINI NA KUWAFUNDISHA DINI YA KIISLAMU.
Mwenyezi Mungu S.W.T. ametuhakikishia wazi kuwa ujumbe aliopewa Mtume S.A.W. ulikuwa kwa Wanadamu na Majini pia. Na katika Qurani na Hadithi za Mtume S.A.W. kuna dalili zilizo wazi zinazoyakinisha kuwa Mtume S.A.W. alikuwa akikutana nao na kuwafundisha dini. Na hata wakati mwingine Majini walikuwa wakitoa majibu mazuri zaidi kuliko Binadamu kwenye masuala ya dini. Na mfano ni wakati waliposomewa Suratir Rahmaan. Hadithi iliyopokelewa na Jaabir bin Abdallah R.A.A. na iliyotolewa na Ttirmidhi kasema, “Wakati ambapo Mtume S.A.W. alipowasomea Majini Suratir Rahmaan, “
لَقَدْ قَرَأْتُهَا ‘‘يعني سُورَةَ الرَّحْمَنِ’’ عَلَى الْجِنِّ …، فَكَانُوا أَحْسَنَ مَرْدُودًا مِنْكُمْ ، كُنْتُ كُلَّمَا أَتَيْتُ عَلَى قَوْلِهِ ]فَبِأَيِّ آلاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ[ قَالُوا: لا بِشَيْءٍ مِنْ نِعَمِكَ رَبَّنَا نُكَذِّبُ ، فَلَكَ الحمد
Maana yake, “Hakika nimewasomea Majini (yaani Suratir Rahmaan)…wamejibu vizuri zaidi kuliko nyinyi. Kila nilipofikia kauli Yake (Mwenyezi Mungu S.W.T.) “Fabiayyi A-alaai Rabikumaa Tukadhibaan.) Maana yake, “Basi ipi katika neema za Mola wenu ambayo mnayoikanusha kuwa si kweli?” (Basi Majini) walijibu “Laa bishaay Min Niamika Rabbana Nukadhibu, Falakal Hamdu.” Maana yake, “Hakuna neema yoyote katika neema Zako Mola wetu tunayoikadhibisha, bali tunashukuru.” Na Mtume S.A.W. alipowasomea Wanadamu hawakujibu chochote, akawaambia, “Ndugu zenu wa Ki-Jini wamejibu jawabu nzuri waliposikia haya.” Na dalili nyingine kuwa Mtume S.AW. pia alikuwa ametumwa kwao ni kisa cha baadhi ya Majini ambao baada ya kuisikiliza Qurani waliiamini na wakarejea kwao na kuanza kuwaita wenzao kwenye dini ya Kiislamu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu kasema katika Suratil Ahqaaf aya ya 29 mpaka 32, “
]وَإِذْ صَرَفْنَا إِلَيْكَ نَفَرًا مِنْ الْجِنِّ يَسْتَمِعُونَ الْقُرْآنَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوا أَنْصِتُوا فَلَمَّا قُضِيَ وَلَّوْا إِلَى قَوْمِهِمْ مُنْذِرِينَ * قَالُوا يَا قَوْمَنَا إِنَّا سَمِعْنَا كِتَابًا أُنْزِلَ مِنْ بَعْدِ مُوسَى مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيْهِ يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ وَإِلَى طَرِيقٍ مُسْتَقِيمٍ * يَا قَوْمَنَا أَجِيبُوا دَاعِي اللَّهِ وَآمِنُوا بِهِ يَغْفِرْ لَكُمْ مِنْ ذُنُوبِكُمْ وَيُجِرْكُمْ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ * وَمَنْ لا يُجِبْ دَاعِي اللَّهِ فَلَيْسَ بِمُعْجِزٍ فِي الأرْضِ وَلَيْسَ لَهُ مِنْ دُونِهِ أَولِيَاءُ أُوْلَئِكَ فِي ضَلالٍ مُبِينٍ[
Maana yake, “Na (wakumbushe) wakati tulipowaleta kundi la Majini kuja kwako kusikiliza Qurani. Basi walipoihudhuria walisema (kuambiana): “Nyamazeni! (Msikilize maneno ya Mwenyezi Mungu)” Na ilipokwisha somwa walirudi kwa jamaa zao kwenda kuwaonya. Wakasema “Enyi watu wetu! Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremshwa baada ya (Nabii) Musa, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake na kinachoongoza kwenye haki na kwenye njia iliyonyooka. Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mlingani, (Muitaji) wa Mwenyezi Mungu na muaminini, atakusameheni (Mwenyezi Mungu) dhambi zenu na atakukingeni na adhabu iumizayo.
Na wasiomuitikia Muitaji wa Mwenyezi Mungu, basi hao hawatamshinda (asiwapate) hapa katika ardhi, wala hawatakuwa na walinzi mbele Yake. Hao wamo katika upotofu ulio dhahiri.”
Na kisa kingine ni cha Majini waliosikia Qurani kutoka kwa Mtume S.A.W wakati alipokuwa akiwasalisha Masahaba wake Sala ya Alfajiri. Na hii ilikuwa bila ya yeye kuwa na habari mpaka Mwenyezi Mungu S.W.T. alipomjulisha. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Jin aya ya 1 na ya 2, “
]قُلْ أُوحِيَ إِلَيَّ أَنَّهُ اسْتَمَعَ نَفَرٌ مِنْ الْجِنِّ فَقَالُوا إِنَّا سَمِعْنَا قُرْآنًا عَجَبًا * يَهْدِي إِلَى الرُّشْدِ فَآمَنَّا بِهِ وَلَنْ نُشْرِكَ بِرَبِّنَا أَحَدًا[
Maana yake, “Sema: “Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la Majini lilisikiliza (Qurani) likasema: “Hakika sisi tumesikia Qurani ya ajabu. Inaongoza katika uwongofu; kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote tena na Mola wetu.”
Makala haya yametolewa katika kitabu changu kiitwacho, "Hakika ya Majini."
No comments:
Post a Comment