Wednesday, April 4, 2012

Kula Haramu - Sababu Ya Kutokubaliwa Du'a Na Ibada Zetu


Kuna mahusiano makubwa kati ya moyo uliosalimika na kufisidika kwake na baina ya chakula cha mja na jinsi anavyokichuma. Kwani ikiwa njia za kukipata chakula zilikuwa za haramu hupelekea mja kula haramu na hapa kufisidika kwa moyo na hatari ya kufisidika kwa moyo ndiyo kuharibika kiwiliwili chote kama anavyosema Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) katika hadithi sahihi iliyosimuliwa na Bukhari a Muslim kwamba:
                                                                                                                                            
أَلا وَإنَّ في الجَسَدِ مُضْغَةً إذَا صَلَحَتْ صَلَحً الْجَسَدُ كُلُّهُ وإذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ    
                                                                                                                    كُلُّهُ، أَلا وَهِيَ الْقَلْب"
……Na hakika katika kiwiliwili kuna kipande cha nyama kikitengenea, kiwiliwili chote kitatengenea, kikiharibika kiwiliwili chote huharibika. Basi jua (kipande hicho cha nyama) ni moyo
Allah (Subhaanahu Wata’ala) ametuhadharisha sana kula haramu ikiwa haramu hii ni mali au haki za watu wengine,au chakula ambacho kimeharamishwa , au rizki tunayoipata kwa njia zisizokuwa za halali n.k
Kwa mja anaejichunga na kuhakikisha kula vilivyo halali basi dua yake huwa karibu kwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) kupokelewa na kukubaliwa . Ama asiejishughulisha na kuzama katika kula haramu basi yeye mwenyewe hujiwekea vizingiti kati ya dua yake na kutakabaliwa kwake.
 عن أبي هُرَيْرَةَ رَضي اللهُ عنه قال: قاَل رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم : "إنَ الله طَيِّبٌ لا يَقْبَلُ إلا طَيِّباً، وإنَّ الله أَمَرَ المُؤمِنينَ بِمَا أَمَرَ به المُرْسَلينَ فقال تعالى: {يا أَيُّها الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيَّباتِ واعمَلُوا صالحاً} [المؤمنون: 51] وقال تعالى: {يا أَيُّها الَّذِينَ آمَنُوا كلُوا مِنْ طَيِّباتِ ما رَزَقْناكُمْ} [البقرة: 172] ثُمَّ ذَكَرَ الرَّجُل يُطِيلُ السَّفَرَ أشْعثَ أَغْبَرَ يَمُدُّ يَدَيْهِ إلى السَّماءِ يا رَبُّ يا رَبُّ، ومَطْعَمُهُ حَرَامٌ، ومَشْربُهُ حَرَامٌ، وغُذِّيَ بالحَرَامِ، فأَنَّى يُسْتَجَابُ لهُ".  
                                                             رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ وَمُسْلِمٌ      
Kutoka kwa Abu Hurayrah(Allah amuwie radhi) :  Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema:
Allah(Subhaanahu Wata’ala) ni mwema na anakubali kilicho chema tu. 
Allah(Subhaanahu Wata’ala) ameamrisha Waislamu kufanya yale aliyowaamrisha Mitume, na akasema "Enyi Mitume Kuleni katika vitu vyema na mfanye yaliyo sawa"(Al Muuminuun 51) .  Na Allah(Subhaanahu Wata’ala) akasema :" Enyi mlioamini kuleni katika vitu vyema ambavyo tumekuruzukuni” (Al baqarah 172) Kisha akataja (kisa cha yule) mtu aliyesafiri safari ndefu, kachafuka na kajaa mavumbi na huku anayanyua mikono yake mbinguni akisema "Ewe    Mola! Ewe Mola! wakati chakula chake cha haramu, na kinywaji chake ni cha haramu, na kivazi chake ni cha haramu, na  amelishwa haramu, je, vipi atajibiwa (dua zake?)
Imesimuliwa na Bukhari na Muslim
Anasema Imaam Ibn Kathir: Kula halali ni sababu ya kukubaliwa dua na ibada kama ilivyo kwa kula haramu ni sababu ya kutokubaliwa dua na ibada.
Na ibn Rajab anasema : Kula, kunywa, kuvaa na kulishwa haramu ni moja katika sababu ya kutokubaliwa dua .
Naam ndugu yangu muislamu ikiwa dua zetu tunaziwekea vizingiti  na vikwazo sisi wenyewe  basi kuna hatari ya ibada zetu pia zikawa na vikwazo na huku tunaabidika bila ya kujiangalia katika mwenendo wetu mzima huku tunasali lakini nguo tulizovaa zimepatikana kwa njia ya haramu, chakula tulichokula (cha kutupa nguvu za kusimama kwa ajili ya ibada) asili yake ni haramu,hata watoto wetu nao tunawalisha haramu, wazazi wetu tunawasaidia katika pesa ambazo tumezipata kwa njia za haramu, tunasaidia mayatima, kujenga misikiti, kuimarisha vyuo kwa pesa zile zile tulizozipata kwa njia ya haramu......
Na hapa sote tuna yakini kabisa kwamba dunia ni pahala pa kupita na kuna “life” nyengine huko akhera tutakaposimama kwa ajili ya hesabu na hapo kujulikana pumba, chua na mchele safi....
Basi haujafika ule wakti wa kuziangalia ibada na dua zetu kwa jicho la huruma kwa nini hazikubaliwi na Allah (Subhaanahu Wata’ala) kwa kujiangalia sisi wenyewe katika nafsi zetu na kile tunachokichuma?
Suuratu Arraad/11
                                                                               إِنَّ اللَّهَ لاَ يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّى يُغَيِّرُواْ مَا بِأَنفُسِهِمْ
Hakika Allah habadilishi (yaliyomo kwenye) kaumu za watu mpaka wajibadilishe wao wenyewe.
Wabillahi Tawfiyq

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget