Monday, April 9, 2012

Uislamu ulivyoingia Zanzibar

MTUME Muhammad (saw) alifariki mwaka wa 11 Hijiria kwa mwaka 632 wa Kikristo. Makhalifa Waongofu wanne walishika nafasi yake kuongoza umma wa Waislamu. Wakarithi mfumo wa uongozi uliounganisha shughuli za dini na dola. Wakati huo mataifa yaliyokuwa na nguvu kubwa ni dola ya Warumi kwa upande wa Magharibi na Wafursi (persia) kwa upande wa Mashariki.

MTUME Muhammad (saw) aliwahi kuwapelekea risala viongozi wa madola hayo makubwa na mengineyo wakubali Uislamu, na raia wao wanaoamua kufuata Uislamu wasiwatese. Waliojibiza ukafiri, kuwaonea au kuwashambulia Waislamu walipambana na majeshi ya dola ya Kiislamu na watu wa nchi hizo mpya walipofikiwa na neema ya Uislamu na Waislamu wakakaribishwa vyema kama ni wakombozi kutokana na watawala wa zamani walivyowakandamiza.

Mtume (saw) aliwacha dola ya Kiislamu imo vitani na Makhalifa waliendeleza mapambano hayo. Mbali na nchi zilizokuwa karibu na Makka na Madina, Uislamu ulienea Afrika ya Kaskazini. Nchi nyingine kama vile Iran, Afghanistan, India n.k. zikafikiwa na Uislamu.
Katikati ya karne ya 7 A.D. Uislamu ulikuwa tayari umeshafika Ethiopia, Visiwa vya Mediterrean. Alipofariki Sayyidna Uthman bin Affan (ra) eneo la ardhi linalokaliwa na Waislamu lilikuwa na ukubwa ulio karibu sawa na Bara la Ulaya. Kisha Uislamu ukafika nchi za Ulaya kama vile Hispania, pia kwa upande wa Mashariki ya Mbali ukafika Uchina.
Baada ya kumalizika kipindi cha Makhalifa Waongofu kulianza vurugu kubwa. Waislamu wenyewe kwa wenyewe walipigana. Watawala wa Bany Umayya walioshika dola wakayahamisha makao makuu ya dola ya Kiislamu kutoka Madina na kuyaweka Damascus (Syria) 661 AD.
Utamaduni wa sehemu hiyo uliathiriwa sana na Uzungu chini ya dola ya Kirumi na ucha-Mungu haukuwa mkubwa kama Madina na nguvu za kuenea kwa Uislamu zilipungua ingawa hazikusita.
Katika Makhalifa wa Bany Umayya aliyefanikiwa sana kurejesha ucha Mungu na uadilifu, yakafunguka katika dola ya Kiislamu maendeleo mbalimbali ya kiutamaduni kama katika fani ya viwanda na matibabu ni Umar bin Abdu Aziz (817-20 AD) ingawa muda wake ulikuwa mfupi.
Miongoni mwa makundi yaliyozuka na kutofautiana katika kipindi cha Bany Umayya ni kundi dogo la Mashia ambao baadaye walitegemea wanazuoni tofauti na kulifanya kundi hilo la kisiasa kuwa pia ni madhehebu.
Yalikuwepo makundi mengine, lakini wengi waliobaki na ambao walikubaliana na sera za Bany Abbas wakahamisha makao makuu Damascus na kuyaweka Iraq katika mji wa Baghdad, Madinat salaam.
Matokeo ya migongano yote hiyo yakafanya dola ya Kiislamu kuanza kusambaratika, baadhi ya magavana wa majimbo wakajitangazia tawala zao, wakajiita majina mbalimbali kama Makhalfa, Masultani na Maimamu.
Kwa mfano baadaye (karne ya 10 AD) miongoni mwa Mashia kundi la Fatimiyya lilipata nguvu na mali na kufanya Misri makao ya utawala wao. Kwa sababu ya Uislamu lugha ya Kiarabu ikaendea na kuwa muhimu kuliko lugha nyinginezo.
Tumeona kuwa kipindi ambacho ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) ulianza kuenea sana duniani ni pale waliposhika Makhalifa. Dola ya Kiislamu haikufika Afrika Mashariki. Imani iliyopo ni kuwa Uislamu uliletwa katika miji ya Mwambao wa Afrika kupitia misafara iliyokuwepo ya kibiashara na pia kutokana na athari za Waislamu waliotokea nchi za Uarabuni hapo zamani kwa kukimbia vurugu au wimbi la mabadiliko kama tulivyogusia.
Waislamu hao wa mwanzo waliokimbia huko kufika kwao katika mwambao wa Afrika, kuenezwa katika hadithi kdhaa zinazotaja baadhi ya makundi, ingawa hakuna uhakika kama ni makundi hayo yaliyotajwa, mengineyo au yote kwa pamoja walihusika na kufikisha ujumbe wa Nabii Muhammad (saw) katika miji ya Waswahili.
Hadithi moja inasema kuwa katika karne ya 7 AD wakati Sayyidna Umar bin Khattab (ra) ni Khalifa, alitoa ujumbe wa watu wa Syria kufika Mwambao wa Afrika ya Mashariki kutangaza Uislamu.
Hadithi nyingine ni ya kundi la wakimbizi wakati wa Khalifa Abdul Malik Marwan (685 - 707 AD) ambaye alimtuma Gavana wake aliyekuwa Hijaz (na baadaye Iraq), al Hajjaj Ibn Yusuf kuingia Oman na kutuliza fujo iliyokuwepo katika nchi hiyo baadhi ya walioshindwa wakakimbilia Afrika ni Said na Suleiman wa kabila la Julanda ambao inasemekana hasa walitoka mji wa Kufa Haijulikani mji hasa waliofikia Mogadishu (Somalia), Malindi (Kenya) au wapi. Haijulikani kama athari za kuja kwao miji ya Waswahili zilisaidia kusilimisha wenyeji.
Kuna kisa cha mfalme wa Qanbalu kilichoandikwa na Buzurg Ibn Shahriyah katika kitabu chake alichokiita "maajabu ya India". Qanbalu ulikuwa mji mmojawapo uliokuwepo zamani katika kisiwa kimoja Mwambao wa Afrika ya Mashariki kuanzia katikati ya karne ya 8 AD na ambao ulitembelewa sana katika karne ya 10 na majahazi kutoka Oman kwa shughuli za kibiashara.
Kisa cha huyo mfalme wa Qanbalu ni kutekwa nyara katika nchi yake na wafanyabiashara ambao walikuwa Waislamu na kumuuza katika mji wa Baghdad.
Huko akauzwa tena kwa mtu mwingine na kwenda Basra ambako alijifunza Uislamu. Akakimbia na kujiunga na msafara wa watu waliokuwa wakienda Makka kuhiji akiwa ni mchukuzi wao.
Akafundishwa kuhiji na alipomaliza akafuata msafara ulioelekea Misri ambako alifuata ukingo wa mto Nile na hatimaye akafuata msafara ulioelekea Afrika Mashariki na kurejea katika ufalme wake akiwa Muislamu na akasilimisha watu wake.
Ameeleza kuwa kabla yake yeye, hakupata mtu yeyote katika Biladi Zanj neema aliyofadhiliwa na Mwenyezi Mungu kujua dini ya haki, kufahamu kusali, kufunga, kuhiji na kujua haramu na halali.
Kwa ushahidi wa maelezo ya mfalme huyo wa Qanbalu inaonyesha kuwa hadi kufikia 922 AD (mwanzoni mwa karne ya 10 AD) Uislamu ulikuwa bado haujafika katika miji yote yoyote ya Mwambao wa Afrika ya Mashariki.
Amma mpaka sasa ushahidi madhubuti kuthibitisha kuwa Uislamu ulifika Afrika ya Mashariki mnamo karne ya 7 AD kama inavyoelezwa katika hadithi hizo haujaptikana.
Lakini mtaalamu mmoja wa mambo ya kale (Aathari-l-Kadim) aliyefanya utafiti eneo moja la mji wa kale katika Mwambao linaloitwa Shanga, miongoni mwa visiwa vya Lamu, katika kufukua kwake sehemu yenye gofu la Msikiti aligundua kuwa mahala hapo hapo palikuwa na Misikiti kabla katika vipindi mbalimbali vilivyopita.
Amedai kuwa jengo la awali ambalo lilijengwa kwa udongo mwisho wa karne ya 8 AD huenda lilikuwa ni Msikiti ambao utakuwa ndio wa mwanzo katika sehemu hiyo.
Ushahidi kuwa majengo yaliyofuatia mahala hapo yalikuwa ni Misikiti. Jengo lililofuatia, pia ni la udongo ambalo lilionekana kuwa ni la karne ya 9 AD halina shaka kuwa lilikuwa Msikiti na mnamo karne ya 10 AD ufundi wa kujenga kwa mawe ulipoanza kwenye miji ya Mwambao, Msikiti wa wakati huo ukatiwa jiwe.

KWAHIYO, mimi naona kuwa kwa mujibu wa ushahidi wa utafiti wa mambo ya kale, karne ya tisa ndio tarehe mapema kabisa ya kuanza kusilimu watu wa Afrika ya Mashariki, karne ya 10 wenyeji wa Pwani waliingia katika Uislamu kwa makundi. 
Mabaki ya misingi ya baadhi ya Misikiti ya jiwe iliyojengwa katika karne ya 10 imegunduliwa kwenye baadhi ya maeneo ya miji ya kale katika visiwa vya Zanzibar – Unguja Ukuu Kaepwani (Mkoa wa Kusini Unguja) na Mtambwe Mkuu (Mkoa wa Kusini Pemba). 
Ilikuweko biashara kubwa baina ya miji hii ya kale ya visiwa vya Zanzibar na miji muhimu ya Kiislamu ya wakati huo katika nchi za Kiarabu, kama vile Iraq na Misri. Kwa mfano watafiti wa mambo ya kale wamegundua katika viunga hivyo vya miji ya kale pesa za dhahabu zenye Kalimatu Tawhid kwa maandishi ya Kiarabu na majina ya makhalifa waliozitengeneza mwahala kama Damascus na Sur na nyingine zilitengenezwa na Wafalme wa Fatimiyya (Misri). 
Kadhalika kuingia karne ya 11 AD watawala wa kienyeji katika miji ihyo ya Mwambao wa Afrika ya Mashariki pia walitengenezesha pesa zao ambazo zilikuwa za fedha, pia zikiwa na maandishi ya Kiarabu ambayo kama tulivyotangulia kusema ndio iliyokuwa lugha muhimu kwa Waislamu kuanzia wakati huo. Pesa hizo zina majina ya hao watawala na vibwagizo vyenye kusifu imani yao katika Uislamu. 
Karne ya 11 AD wakimbizi na wafanyabiashara waliendelea kufika Mwambo. Wengine walioa na baadhi wakiamua kuishi moja kwa moja katika miji ya Waswahili. Hadithi moja ya wakati huu, ni ya watu wa Zaidiya ambao walifikia katika miji ya bandari za Somali na walipopingwa kutokana na imani ya Ushia pengine walikimbilia sehemu za bara. 
Athari yao haijulikani. Lakini hadithi nyingine muhimu sana inayohusu kipindi hiki ni ya ndugu 7 waliotoka mji wa Al Hassa (Lacar) ambao kutokana na masimulizi hayo walitawanyika katika miji (Tanzania) na baba yao akaishi Anzuani (Comoro). 
Kwa kusambaa kwake ukoo huu wa watu wa Persia, inawezekana ndio baadaye baadhi ya Washahili wa Mwambao wakajihusisha na kizazi chao, na kudai asili inayotokana na Washirazi. 
Inaelekea ukoo huu pia ni wa Shia, labda kundi hili lilitofautiana kidogo tu katika itikadi na kundi la Zaidia. Inaaminiwa ukoo huo ulishika ngazi ya utawala katika baadhi ya miji. 
Msikiti mkongwe wa Kizimkazi Dimbani (Mkoa wa Kusini Unguja) ni kumbukumbu muhimu sana katika historia ya Uislamu Zanzibar na Afrika ya Mashariki kwa jumla. 
Limo jiwe lililojengwa mihrabu ndani ya Msikiti huu lililoandikwa kwa nakshi za herufi za Kufi ambalo linaeleza Msikiti huo mwanzo ulijengwa mwaka 500 Hijiria (1107 AD) na jiwe jingine linaonyesha tarehe ya kujengwa tena katika karne ya 18 AD. Wakati huo katika Kisiwa cha Unguja, Kizimkazi ilikuwa ni mji wa bandari muhimu ya kuwasiliana na nchi za nje, kama vile bandari za Persia, lakini mji wa kale wa Unguja Ukuu ulishahamwa. 
Msikiti wa Kizimkazi ni uthibitisho usio na wasiwasi kuwa katika kipindi cha mwisho wa karne ya 11 AD kuingia karne ya 12 AD Zanzibaar tayari ilikuwa na Waislamu wengi. Hata hivyo, pengine walikuwepo watu ambao bado hawakusilimu. Ushahidi uliokuwepo katika kijisiwa kidogo cha Mtambwe Mkuu, umeonyesha kuwa mnamo karne ya 11 AD kulikuwa na baadhi ya watu waliozikwa ambao hawakuwa wa miji ya Afrika ya Mashariki, walikuwa ni wafuasi wa madhehebu ya Sunii/Shafii. 
Karne ya 12 AD mambo huenda yalikuwa tofauti. Ilianza awamu iliyoendelea hadi karne ya 14 AD ambapo kwenye miji mingi kariub karibu watu wote walikuwa tayari ni Waislamu. Kwamba watawala walikuwa ni Waislamu tunaweza kuona hata kwenye pesa za shaba zilizotengenezwa na watawala wa Zanzibar katika enzi hizo au kipindi cha mbele kidogo. 
Majina ya baadhi ya watawala ni kama vile Al-Hussein bn Ahmad, I-shaq bn Hassan na Al-Hassan bn Ali. Hata hivyo, kipindi hiki kilianza na migogoro ya kidini. Katika kisiwa cha Unguja shughuli za mji na utawala zilikuwa Tumbatu. 
Kisiwa hiki kidogo kaskazini magharibi ya kisiwa kikubwa cha Zanzibar katika eneo la kusini, Jongowe Makutani hadi leo yamehifadhika magofu mengi ya nyumba za huo mji, visima na Misikiti. 
Msikiti Mkuu wa Ijumaa haukuwa na mfano wake kwa ukubwa wakati huo katika Mwambao mzima wa Afrika ya Mashariki. Enzi hizo Tumbatu ilitembelewa na msafiri maarufu wa Kiarabu Yakuti ( Mwaka 1220 AD) alikuta watu wake ni Waislamu na akaeleza kuwa mji huo ndio makao ya mfalme wa Zanj. Utafiti wa mambo ya kale uliofanywa huko umethibitisha ukubwa wa mji huo na kuweko kwa Waislamu wengi. 
Baadhi ya miji ya Mwambao ilikumbwa na mizozo mikubwa ya kimadhehebu, tukizingatia kuja kwa makundi hayo ya imani za Kishia na hata ya Kiibadhi. Yakuti pia alieleza Pemba kulikuwa na mtawala mwenye asili ya Waarabu wa mji wa Kufa ambao wakati huo ulikuwa kituo muhimu cha Waislamu wa itikadi za Shia. 
Kuna waraka ulioandikwa na Muislamu wa madhehebu ya Ibadhi mwisho kabisa ya karne ya 12 AD unaoeleza mpango wa kuwatoa watu wa Kilwa Kisiwani katika madhehebu ya Sunni, wafuate madhehebu ya Ibadhi. Na kama maelezo yaliyoandikwa baadaye na Ibn Mujawwir yameeleweka ndivyo, watu wa Kilwa wakawa Maibadhi kabla ya mwaka 630 Hijiria (1232 AD). 
Na hadithi ya mwisho ambayo tunaitaja ni ya wageni waliofika miji ya Pwani na ambao wenyeji waliwaita Wadebuli (Unguja) au Wadiba (Pemba). Inaaminiwa watu hawa walikuwa Waislamu kwani katika masimulizi wanahusishwa na ujenzi wa baadhi ya visima vya mwanzo vya ndoo katika visima vya Zanzibar na hata baadhi ya Misikiti ambayo sasa imekuwa magofu. 
Asili ya watu hawa haikuhifadhiwa, wako waliofikiria watu hao watu hao walikuwa Wahindi au Waarabu. 
Wanahistoria wamebahatisha kutaja miji inayofanana na jina lao, kama vile Daybul, bandari ya Sindh (India) ambayo ilikuwa chini ya magavana wenye asili ya Kiarabu karne ya 7 hadi karne ya 13 AD. 
Bandari hiyo pia ilikuwa maarufu kwa kutumiwa na watu waliokuwa majangili wa vyombo vya baharini. Wengine wamewahusisha watu hao wa visiwa vya Diba (Maldive) ambako wenyeji wake walisilimu mnamo karne ya 12 AD. Athari ya watu hawa haikuwa kusilimisha kwani wakati huo wenyeji wa Mwambao wa Afrika ya Mashariki walikwa tayari ni Waislamu. 
Watu wa karne ya 15 AD wametuachia magofu mengi ya Misikiti na makaburi katika miji yao. Mnamo katikati ya karne ya 15 AD kwa mujibu tarehe ya Kilwa (Kilwa Chronicle) mtawala wa kienyeji Zanzibar alikuwa Sultan Al Hassan bin Abubakar. 
Ama karne mbili zilizofuatia, 16-17 zilikuwa kipindi cha hofu na wasi wasi mkubwa kwa Waislamu katika miji yote ya Mwambao kwa sababu ya Wareno waliofika wakti huo ambao waliwanyang’anya Waislamu mali zao na kudai mali nyingi kama kodi, waliopinga, miji yao iliangamizwa na Wareno. Hayo yalitokea kwa mji wa Zanzibar. Wareno sio tu walitaka utajiri, walinuia kuupiga vita Uislamu. 
Hayo ni pamoja na kujaribu kuwashawishi watawala wa kienyeji kubadili dini na kufuata imani ya Kikristo, ambayo ilikuwa ya madhehebu ya Augustinia. 
Haya yamehifadhiwa katika vitabu vya historia. Kwa mfano, yalimfia mfalme Muislamu wa mji wa Kilwa walipomwendea Pedro Alvares Cabral mwaka 1500 na Don Fransisco mwaka 1503 AD. Ingawa Wareno hawakufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwatoa wenyeji katika imani ya Kiislamu, misafara ya kibiashara ilizuilika, kwa hali hiyo, hali ya maisha ya Waislamu zikateremka. 
Misafara ya kibiashara pia ilikuwa na watu waliokwenda huku na kule kutafuta na kufundisha elimu za dini, wote wakaepuka kusafiri. Misikiti haikuendelea kujengwa katika kipindi hicho, baadhi ya viunga vya miji vilihamwa na Misikiti ikawa magofu na kuporomoka kabisa. Hatimaye Wareno walipigwa vita na kuondoshwa kwa msaada wa kijeshi kutoka ufalme wa Oman. 
Katika karne ya 18 AD hali ilirejea kuwa ya kawaida, ujenzi mpya ukaanza pamoja na jitihada za kutafuta na kuendeleza elimu ya dini. 
Walimu wa dini walikuja kutoka nchi za Kiarabu, hasa Masheikh wa Kisunni kutoka nchi za kusini ya Bara Arabu, baadhi yao wakiwa ni wafanyabiashara. 
Pia wakati huo kulikuwa na wimbi la kufufua misingi ya dini lilitokea miji ya Makka na Madina ambako kulikuweko na Masheikh waliopinga Taqlid na kudai kuwa mambo yote katika diin yawe na dailili katika Qur’an na Sunnah. 
Maarufu katika hao ni Sheikh Muhammad Abdulwahab (1703 – 1792 AD). Kadhalika huu ulikuwa wakati wa kuanza kwa biashara na nchi za Ulaya ambayo baadaye mfalme Said bin Sultan aliiendeleza. 
Karne ya 19 AD elimu za maarifa ya Uislamu ziliendelea. Watawala wa kifalme kutoka Oman ambao walikuwa wa madhehebu ya Ibadhi walishughulikia dola na biashara hawakuingilia itikadi za Kisunni na Masunni hawakuingilia watu walioitakidi Ushia. 
Zanzibar ilikuwa sana kiuchumi na kisiasa ilidhibiti karibu mwambao wote na kufanywa kituo kikuu cha biashara yote ya nje hasa mali kutoka bara. 
Wanazuoni wa miji ya Mwambao walitembeleana kubadilishana elimu na kufanya biashara, walitunga vitabu na kufungua madarasa kubwa kubwa kufundisha elimu ya dini, wengine walikwenda nje kusomesha kama vile Uganda na kwingineko. 
Kwa hivyo, Zanzibar ikawa pia ni chemchem ya dini. Miji iliyokuwa na Waislamu wengi na dini kuwa na nguvu zaidi, kama Zanzibar, Waislamu wakafikia hatua ya kufuata sharia chache katika Uislamu, zinazohusu ndoa na mirathi na watawala wakiwateua makadhi kushughulikia hayo. Unguja Makadhi wa Kisunni ndio waliokuwa wengi na Pemba Makadhi wa Kiibadhi ndio waliokuwa wengi. 
Hali ya Zanzibar kibiashara na kiutamaduni iliwavutia sana Wazungu na walikaribishwa na mfalme wa Kioman. Walifuatana na Misheni zao za Kikristo. 
Hali ya Zanzibar ikazilea Misheni hizo kwa hali ya Mabara ilivyokuwa, haikuwa rahisi Misheni kuanzia huko. Kwa vile Uislamu ushamiri sana Zanzibar, Wamisheni pia walifurahia fursa ya kuanza harakati zao Zanzibar kuendeza Ukristo, kwa matumaini kuwa wakifanikiwa kubadilisha imani ya Kiislamu Zanzibar itakuwa ni rahisi kuifanya jamii nzima ya Mwambao kuwa ya Wakristo. 
Mada hii ya shughuli za Wamisheni itaelezwa zaidi, hapa la muhimu nikuwa Wazungu hatimaye walichukua hatamu za dola (ukoloni) wakashika kisu mpini, ikawa Waislamu wameshika kwenye makali. 
Khatima ya jamii ya Waislamu Zanzibar ikawa katika mikono ya Waingereza. Hal nzima ikabadilika. Elimu zilizoanzishwa na vituo vya Wamisheni na huduma za afya ikawa ni vya lazima katika hali hiyo mpya. 
Hadi kufikia karne ya 20 ikafifia elimu pamoja na utamaduni wa Kiislamu, Waislamu wakadharauliwa pamoja na dini yao

Watu wa karne ya 15 AD wametuachia magofu mengi ya Misikiti na makaburi katika miji yao. Mnamo katikati ya karne ya 15 AD kwa mujibu tarehe ya Kilwa (Kilwa Chronicle) mtawala wa kienyeji Zanzibar alikuwa Sultan Al Hassan bin Abubakar.  
Ama karne mbili zilizofuatia, 16-17 zilikuwa kipindi cha hofu na wasi wasi mkubwa kwa Waislamu katika miji yote ya Mwambao kwa sababu ya Wareno waliofika wakti huo ambao waliwanyang’anya Waislamu mali zao na kudai mali nyingi kama kodi, waliopinga, miji yao iliangamizwa na Wareno. Hayo yalitokea kwa mji wa Zanzibar. Wareno sio tu walitaka utajiri, walinuia kuupiga vita Uislamu. 
Hayo ni pamoja na kujaribu kuwashawishi watawala wa kienyeji kubadili dini na kufuata imani ya Kikristo, ambayo ilikuwa ya madhehebu ya Augustinia. 
Haya yamehifadhiwa katika vitabu vya historia. Kwa mfano, yalimfia mfalme Muislamu wa mji wa Kilwa walipomwendea Pedro Alvares Cabral mwaka 1500 na Don Fransisco mwaka 1503 AD. Ingawa Wareno hawakufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwatoa wenyeji katika imani ya Kiislamu, misafara ya kibiashara ilizuilika, kwa hali hiyo, hali ya maisha ya Waislamu zikateremka. 
Misafara ya kibiashara pia ilikuwa na watu waliokwenda huku na kule kutafuta na kufundisha elimu za dini, wote wakaepuka kusafiri. Misikiti haikuendelea kujengwa katika kipindi hicho, baadhi ya viunga vya miji vilihamwa na Misikiti ikawa magofu na kuporomoka kabisa. Hatimaye Wareno walipigwa vita na kuondoshwa kwa msaada wa kijeshi kutoka ufalme wa Oman. 
Katika karne ya 18 AD hali ilirejea kuwa ya kawaida, ujenzi mpya ukaanza pamoja na jitihada za kutafuta na kuendeleza elimu ya dini.

Walimu wa dini walikuja kutoka nchi za Kiarabu, hasa Masheikh wa Kisunni kutoka nchi za kusini ya Bara Arabu, baadhi yao wakiwa ni wafanyabiashara. 
Pia wakati huo kulikuwa na wimbi la kufufua misingi ya dini lilitokea miji ya Makka na Madina ambako kulikuweko na Masheikh waliopinga Taqlid na kudai kuwa mambo yote katika diin yawe na dailili katika Qur’an na Sunnah. 
Maarufu katika hao ni Sheikh Muhammad Abdulwahab (1703 – 1792 AD). Kadhalika huu ulikuwa wakati wa kuanza kwa biashara na nchi za Ulaya ambayo baadaye mfalme Said bin Sultan aliiendeleza. 
Karne ya 19 AD elimu za maarifa ya Uislamu ziliendelea. Watawala wa kifalme kutoka Oman ambao walikuwa wa madhehebu ya Ibadhi walishughulikia dola na biashara hawakuingilia itikadi za Kisunni na Masunni hawakuingilia watu walioitakidi Ushia.

Zanzibar ilikuwa sana kiuchumi na kisiasa ilidhibiti karibu mwambao wote na kufanywa kituo kikuu cha biashara yote ya nje hasa mali kutoka bara. 
Wanazuoni wa miji ya Mwambao walitembeleana kubadilishana elimu na kufanya biashara, walitunga vitabu na kufungua madarasa kubwa kubwa kufundisha elimu ya dini, wengine walikwenda nje kusomesha kama vile Uganda na kwingineko.

Kwa hivyo, Zanzibar ikawa pia ni chemchem ya dini. Miji iliyokuwa na Waislamu wengi na dini kuwa na nguvu zaidi, kama Zanzibar, Waislamu wakafikia hatua ya kufuata sharia chache katika Uislamu, zinazohusu ndoa na mirathi na watawala wakiwateua makadhi kushughulikia hayo. Unguja Makadhi wa Kisunni ndio waliokuwa wengi na Pemba Makadhi wa Kiibadhi ndio waliokuwa wengi. 
Hali ya Zanzibar kibiashara na kiutamaduni iliwavutia sana Wazungu na walikaribishwa na mfalme wa Kioman. Walifuatana na Misheni zao za Kikristo.

Hali ya Zanzibar ikazilea Misheni hizo kwa hali ya Mabara ilivyokuwa, haikuwa rahisi Misheni kuanzia huko. Kwa vile Uislamu ushamiri sana Zanzibar, Wamisheni pia walifurahia fursa ya kuanza harakati zao Zanzibar kuendeleza Ukristo, kwa matumaini kuwa wakifanikiwa kubadilisha imani ya Kiislamu Zanzibar itakuwa ni rahisi kuifanya jamii nzima ya Mwambao kuwa ya Wakristo.

Mada hii ya shughuli za Wamisheni itaelezwa zaidi, hapa la muhimu nikuwa Wazungu hatimaye walichukua hatamu za dola (ukoloni) wakashika kisu mpini, ikawa Waislamu wameshika kwenye makali. 
Khatima ya jamii ya Waislamu Zanzibar ikawa katika mikono ya Waingereza. Hal nzima ikabadilika. Elimu zilizoanzishwa na vituo vya Wamisheni na huduma za afya ikawa ni vya lazima katika hali hiyo mpya.

Hadi kufikia karne ya 20 ikafifia elimu pamoja na utamaduni wa Kiislamu, Waislamu wakadharauliwa pamoja na dini yao.

Kutoka gazeti la An nuur

No comments:

Post a Comment

Twitter Bird Gadget