Anasema Sh. Sayed Sabeq katika Fiqhil Sunnah;
“Atakayefuatilia aya za Qurani atagundua kuwa Mwenyezi Mungu mara nyingi anaitaja ibada ya Sala kwa kuipambanisha na ibada mbali mbali. Kwa mfano;
Ameipambanisha Sala na Dhikri (kumbusho) aliposema;
“Bila shaka Sala (ikisaliwa vilivyo) humzuiliya (huyo mwenye kusali na) mambo machafu na maouvu, na kwa yakini kumbusho la Mwenyezi Mungu (lililomo ndani ya Sala) ni jambo kubwa kabisa (la kumzuwilia mtu na mabaya)”.
Al Ankabuut – 45
Na akasema;
“Hakika amekwishafaulu aliyejitakasa (na mabaya). Akakumbuka jina la Mola wake na akasali”.
Al Alaa –
Na akasema;
“Basi niabudu na usimamishe Sala kwa kunitaja”.
Ta Ha- 14
Ameipambanisha na Zaka;
“Na shikeni Sala na toeni Zaka”
Al Baqarah – 110
Akaitaja pamoja na Subira;
“Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali”.
Al Baqarah-45
Mwenyezi Mungu pia ameitaja pamoja na ibada ya kuchinja;
“Basi sali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi”.
Kauthar – 2
Na akasema;
“Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu”.
Al An am – 162-163
Mtu hata atende mema ya namna gani, lakini akiwa hasali, au anaposali hamnyenyekei Mola wake, basi matendo yake yote hayo yanapotea bure na anakuwa miongoni mwa waliokula hasara.
Mwenyezi Mungu anasema;
“HAKIKA wamefanikiwa Waumini, Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao,
Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi,
Na ambao wanatoa Zaka,
Na ambao wanazilinda tupu zao,
Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa.
Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.
Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,
Na ambao Sala zao wanazihifadhi.
Hao ndio warithi,
Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo milele.
Al Muuminun – 1-11
Atakayezingatia vizuri mfumo wa aya hizi ataona kuwa Mwenyezi Mungu ameitaja Sala mara mbili. Mara ya mwanzo kwa ajili ya kutufahamisha umuhimu wake na unyenyekevu unaotakiwa ndani yake, na mara ya pili kwa ajili ya kututaka tuihifadhi (tusiiache) pamoja na kutujulisha kuwa ni watu wa aina hiyo tu ndio watakaoirithi Pepo ya Firdausi.
No comments:
Post a Comment